Header Ads

WAZIRI WA ZAMANI KORTINI KWA UDANGANYIFU

Na Happiness Katabazi ALIYEKUWA Waziri mwandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa awamu tofauti Arcado Ntagazwa(65) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kwa kosa moja tu la kujipatia kofia,fulana zenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 74.9 kwa njia ya udanganyifu. Mbali na Ntagazwa washtakiwa wengine ni Senetor Mirelya (60) na Webhale Ntagazwa ambao wanatetewa na wakili wa kujitegemea Alex Mgongolwa. Wakili wa Serikali Ladslaus Komanya mbele ya Hakimu Mkazi Liad Shamshama alidai kuwa Oktoba 22 mwaka 2009 huko Msasani Mikoroshini washtakiwa hao kwania ovu walijipatia fulana 5000 na kofia 5000 zenye jumla ya thamani ya Shilingi milioni 74.9 toka kwa Noel Sevele kwa makubaliano kuwa wangemlipa Sevele kiasi hicho cha fedha katika kipindi cha mwezi mmoja tangu walipochukua vifaa hivyo lakini hata hivyo walishindwa kumlipa na washtakiwa walikana shtaka na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Washtakiwa hao walikana shtaka hilo na Hakimu Mshamsha alisema kosa linalowakabili washtakiwa lina dhamana na kwamba atatoa dhamana kwa kufuata matakwa ya kifungu cha 145(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, ambapo kifungu hicho kinamtaka kila mshtakiwa atoe nusu ya kiasi cha fedha au kuwasilisha hati ya mali isiyoamishika yenye nusu ya thamani ya kiasi cha fedha anachotuhumiwa nacho. Hakimu Shamshama alisema kwa kuwa katika kesi hiyo washtakiwa wapo watatu kwa hiyo kiasi cha sh milioni 74.9 kitagawanywa nusu yake na hivyo kila mshtakiwa atatatiwa awasilishe fedha tasilimu au kuwasilisha hati ya mali isiyoamishika yenye thamani ya Sh milioni 12 na wadhamini wawili ambao wanavitambulisho vinavyotambulika na kwamba watasaini bondi ya Sh milioni tano kila mmoja na kwamba hawataruhusiwa kutoka nje ya mkoa bila ruhusa ya mahakama. Hata hivyo ni Arcado Ntagazwa na Webhale Ntagazwa ndiyo waliopata dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana na mshtakiwa wa kwanza Mirelya alishindwa kutimiza mashatri ya dhamana na hivyo akapelekwa gerezani na kesi hiyo ikaairishwa hadi Mei 2 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa. Ntagazwa ambaye kwa sasa ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), kabla ya kujiunga na chama hicho miaka minne iliyopita, akitokea chama cha Mapinduzi (CCM).Akiwa mwanachama wa CCM, aliwahi kuteuliwa na rais wa Serikali ya awamu ya pili na ya tatu, Ally Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa kushika nyadhifa za uwaziri katika wizara mbalimbali hadi ilipofika mwanzoni mwa mwaka 2006, Rais Jakaya Kikwete alipounda baraza lake jipya la mawaziri na kuamuacha nje ya baraza hilo. Ntagazwa ambaye aliwahi kuwa mbunge wa muda mrefu wa Jimbo la Mhambwe kwa tiketi ya CCM, hadi sasa nakumbukwa kwa msemo wake mmoja maarufu aliowahi kuutoa bungeni akiwa Waziri Nchi ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira alisema ‘Ipo siku wajukuu zetu watafukua makaburi yetu wachunguze ubongo wetu kama tulikuwa na akili timamu’. Ntagazwa alitoa msemo huo kutokana na kutoridhishwa na baadhi ya maamuzi yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya watendaji waliopewa dhamana. Wakati huo huo; Raia wa Mali , Albeto Mardes jana alifikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Devota Kisoka kwa kosa kuingiza dawa za kulevya Tanzania zenye uzito wa gramu 12777 ambazo zina thamani ya Shilingi milioni 57.8 aina ya Heroin. Wakili wa Serikali Ester Kyala alidai kuwa mshtakiwa huyo ambaye anaishi Guine Bisau Aprili 15 mwaka huu, alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julias Nyerere akiwa na dawa hizo za kulevya ambazo ni kinyume na kifungu 16(1) b (1) cha Sheria ya Kuzuia uingizwaji wa Dawa za Kulevya ya mwaka 2002 na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Hakimu Kisoka alisema kwa kuwa kosa hilo halina dhamana kwa mujibu wa sheria na kwamba mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kwamba mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, mshtakiwa huyo hatatakiwa kusema chochote na hivyo akaamuru apelekwe gerezani hadi hadi Mei 7 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa. Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Aprili 24 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.