TUACHANE NA UMBUMBUMBU HUU WA SHERIA
Na Happiness Katabazi
IBARA ya 107A.(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inasema “ Mamlaka ya yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Mahakama.
Wakati Ibara ya 107B ya Katiba hiyo inasema; “ Katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia tu masharti ya Katiba nay ale ya sheria za nchi.
Ieleweke wazi pindi mahakama inapotoa maamuzi yake ni lazima maamuzi yale yaheshimiwe na yatekelezwe na endapo maamuzi yale hayatatekelezwa,mahakama inaweza kutoa amri ya kumwadhibu mhusika ambaye ambeye ameidharau amri hiyo ya mahakama.Na upande mmoja katika kesi ambao unaona haujaridhishwa na maamuzi ya mahakama ya ngazi fulani basi upande huo unaruhusiwa kukata rufaa katika mahakama za juu.
Nimelazimika kutumia nukuu hiyo ya ibara za Katiba na maelezo hayo kwasababu makala yangu ya leo itajadili mwenendo usiopendeza unaozidi kufanywa na baadhi ya wananchi wenzetu hususani baadhi ya wanasiasa na wafuasi wao ambao wamekuwa na kasumba ya kutoa maoni yao yanayo lenga kukashfu hukumu mbalimbali zinazotolewa na mahakama bila ya kutoa ushahidi mbadala ili mahakama na umma uweze kufahamu kweli hukumu hizo zilizotolewa na mahakama zetu zinakasoro, ama zilikuwa na lengo la kupendelea upande mmoja na kuumiza upande mwingine.
Kwa sisi baadhi ya waumini wa sheria na tunaofutilia baadhi ya mashauri mbalimbali yalipo katika mahakama zetu kwa kuudhuria kesi hizo mahakamani, tungali tukikumbuka Agosti 2009, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa nchini, Salum Masati alitoa hukumu ya kesi ya mauaji ya watu wanne iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi(ACP), Abdallah Zombe na wenzake tisa, ambapo aliwaachilia huru washtakiwa hao kwa maelezo kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri ni dhaifu na akaliagiza jeshi la polisi likawatafute wauaji wa watu hao.
Itakumbukwa kuwa baada ya kutolewa hukumu hiyo wananchi mbalimbali wakiwemo wanaharakati,vyombo vya habari walitoa maoni yao wakiishutumu wazi wazi mahakama na kuonyesha hawakuridhika na hukumu hiyo na kwamba Zombe alistahili kuhukumiwa kunyongwa.
Lakini kwa kuwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ambayo kwasasa inaongozwa na Dk.Elizer Feleshi ina uweledi wa masuala ya kisheria na ndiyo imepewa jukumu la kuendesha kesi za jinai mahakamani, baada ya hukumu hiyo kutolewa ilikaa chini na kuisoma nakala hiyo ya hukumu bila kubwatuka mitaani na hatimaye ikafikia uamuzi wa kukata rufaa kwa kufuata taratibu zote za kisheria licha hadi sasa rufaa hiyo bado haijaanza kusikilizwa.
Mfano mwingi hai ni ile hukumu iliyotolewa mwaka 2010 ya rufaa ya kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa katika Mahakama ya Rufaa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Mchungaji Christopha Mtikila, ambapo Jaji Mkuu Mstaafu Agustino Ramadhani ambaye alikuwa akisaidiwa na jopo la majaji sita wa mahakama rufaa, walitengua hukumu ilitolewa na Mahakama Kuu mwaka 2004 ambayo iliruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi kuanzia ngazi ya Ubunge na Urais.
Nayo hukumu hii ilizusha gumzo katika jamii yetu kwani baadhi ya makundi mbalimbali ya kijamii,wanasiasa na sisi waandishi wahabari walitoa maoni yao hadharani kutokufurahishwa na hukumu hiyo na wengine walisema majaji hao ni wasaliti ‘Yuda eskari yoti’ wa watanzania na kwamba hukumu hiyo waliiandika kutokana na maelekezo waliyopewa na serikali kwani serikali haitaki mgombea binafsi.
Na waliokuwa wakipinga hukumu hii hata siku moja hawajawahi kumtafuta Mtikila kumpatia hata nauli ili iwe inaweza kumuwezesha kwenda kuudhulia kesi hiyo mahakamani au kumchangia fedha Mtikila ili aweze kumlipa wakili wake Mpare Mpoki. na wengine walikuwa wakimwita Mtikila ni mwendawazimu.
Na mfano mwingine ni hukumu iliyotolewa Aprili 5 mwaka huu, ya kesi ya kupinga ubunge wa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini(Chadema),Godbless Lema ambayo ilifunguliwa na wapiga kura watatu wa jimbo hilo akiwemo Happy Kivuyo na Mussa Mkanga katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Jaji Gabriel Rwakibarila akisoma hukumu yake alisema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili ameridhika na ushahidi ulitolewa na walalamikaji na kwamba anamtia hatiani Lema kwa madai yaliyokuwa yanamkabili Lema yakiwemo ya kumtolea maneno ya kumdhalilisha na kumkashifu aliyekuwa mgombea wa CCM,Dk.Batrida Buliani na kwa maana hiyo anatengua ubunge wake na kwamba wadaiwa wanayo haki ya kukata rufaa.
Kama ilivyoada baada ya hukumu hiyo kutolewa tumeshuhudia kupitia vyombo vya habari vikimnukuu Lema,wafuasi wake na baadhi ya viongozi wengine wa Chadema wakitoa maoni yao kuhusu hukumu hiyo ambayo hata bado hawajaisoma kwasababu hawajapatiwa nakala yake, wakitoa maneno ya kuikashfu mahakama kuwa hukumu hiyo ni maelekezo toka Ikulu na kwamba hukumu hiyo ni mbaya itasababisha wananchi waanze kuondoa imani na mahakama zetu.
Kwa mifano ya hukumu hizo na maoni hayo ya watu walizipinga hukumu hizo huku wengi waliozipinga hukumu hizo hawajapata fursa ya kuzisoma nakala za hukumu hilo, ni wazi wananchi hao kabla ya hukumu hizo kutolewa tayari walikuwa na hukumu zao vichwani mwao kitendo ambacho kipingana na Ibara hizo mbili za katiba ambazo zimezitaja hapo juu.
Binafsi sijaisoma nakala hiyo ya hukumu ili kujua Jaji Rwakibarila alitumia vigezo gani vya kisheria hadi akafikia uamuzi huo, na kwa sababu mimi ni muumini wa sheria katu siwezi kuwa na jeuri ya kutolea maoni kuhusu hukumu hiyo kwasababu sijaisoma .
Ndiyo maana kimsingi makala yangu ya leo haitajadili kilichomo kwenye nakala ya hukumu ya Lema, la hasha nitajadili tabia hiyo ya baadhi ya wananchi wenzetu ambao wamekuwa vinara wakutoa maoni yao ambayo yanatoa hitimisho la ama kumshutumu jaji au hakimu aliyetoa hukumu ya kesi fulani ambayo hukumu hiyo haijawafulahisha na mahakama kwa ujumla.
Tuwaulize hawa wananchi wenzetu ambao tumewashuhudia wakisema hukumu ya Lema ilipangwa na Ikulu, mara viongozi wa CCM bila kuisoma hukumu ile hivi wana akili timamu?
Na kama wana akili timamu ni kwanini wanashindwa kuheshimu matakwa ya ibara hizo za Katiba nilizozitaja hapo juu?Hivi wanafahamu kuwa kauli hizo wanazozitoa kuhusu hukumu hiyo ya Lema kuwa hukumu hiyo ya Lema kuwa ilivuja kabla haijasomwa, jaji alipewa maelekezo na Rais Jakata Kikwete,viongozi wa CCM, zinaweza kuwaingiza matatani pindi vyombo vya dola vikiamua kuwakamata wale wote walitoa kauli za aina hiyo na kuwafikisha mahakamani kwa makosa ya jinai ili waende kuithibitishia mahakama ukweli wa madai hayo wanayoyasema kupitia vyombo vya habari?
Maana ni sisi wenyewe Watanzania tumeridhia nchi yetu ingozwe kwa utawala wa sheria,sasa ni kwanini leo hii miongoni mwetu hatutaki kuzitii na kuziheshimu sheria hizo?
Nyie wenzetu ambao baada ya hukumu ya Lema kutolewa ndiyo mmeibuka na kusema mahakama imemuonea Lema kwasababu ushahidi uliotolewa kwa maoni yenu hautoshi kutengua ubunge wa Lema, ni nani amewapa mamlaka hayo ya kimahakama ya kutoa hukumu katika kesi hiyo?
Kama mnafikiri mlikuwa na ushahidi mzito ambao mlikuwa mkitembea nao mifukoni mwenu kuhusu kesi hiyo ya mpendwa wenu, na kama kweli mlikuwa mnataka Lema ashinde kesi hiyo, ni kwanini basi kipindi kile kesi hiyo inataka kuanza hamkufuata Lema na kumuomba awaweke kwenye orodha ya mashahidi wake ili nanyie mpande kizimbani mtoe ushahidi ambao mwisho wa siku labda ungeweza kuishawishi mahakama imuone Lema hana hatia?
Kama mnasema hukumu ile ilivuja mapema kabla ya kusomwa, mbona nyie mnaosema hivyo na nyie hamkuitisha mkutano na vyombo vya habari au kwenye uongozi wa mahakama kulisema hilo mapema ?Na kama hukumu hiyo ilivujishwa mapema mbona hakuna hata mmoja aliyejitokeza adharani kabla ya jaji Rwakibarila kusoma hukumu yake kutuonyesha hukumu hiyo anayodai imevuja ili tumwamini?
Mbona hao wanaotueleza hukumu hiyo ilivuja mapema,ndiyo hao hao wanatuambia kuwa wanasubiri waipate nakala ya hukumu iliyotolewa na Jaji Rwakibarila waisome ndiyo waone kama wanaweza kukata rufaa au la?
Mbona hivi karibuni tu Mbunge wa Ilemela(Chadema), Hynesi Kiwia alishinda kesi ya kupinga matokeo ya yalimtangaza yeye kuwa mbunge, iliyokuwa imefunguliwa na wanachama wawili wa CCM, katika Mahakama Kuu ya Mwanza.
Kabla ya hapo baada ya uchaguzi wa mwaka 2005, aliyekuwa mbunge wa Karatu(Chadema), Dk,Wilbroad Slaa alishinda kesi ya kupinga ubunge wake iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo kupitia CCM, Patric Tsere katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, na Jaji Robert Makaramba alitupilia mbali kesi hiyo iliyofunguliwa na Tsere na kuamuru Dk.Slaa aendelee kuwa mbunge, mbona hatukusikia hao wanaoilalamikia hukumu ya Lema, wakipiga kelele kupinga hukumu hizo hadharani na kumwaga machozi hadharani kwenye Televisheni kama sio unafiki na ujuha uliokubuhu nini?
Na mbaya zaidi wanaofanya mchezo huo wa hatari ni wasomi na ni watu wazima na watoto majumbani wanasikilizwa na kutazamwa na baadhi ya wananchi wanaziamini kauli zao,jambo ambalo nasema ni hatari kwa ustawi wa utawala sheria hapa nchini na kuushushia heshima mhimili wa mahakama kwa namna moja ama nyingine vitendo hivyo vinaingilia uhuru wa mahakama ambao umeitolewa kwenye Ibara 107 B ya Katiba.
Wakati umefika sasa kwa Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman na timu yake ya mahakama kuamka usingizini na kutetea heshima ya mhimili wa mahakama kwani endapo wataruhusu vitendo hivyo vinavyofanywa na baadhi ya wananchi wenzetu basi wajiandae kuona siku wananchi ambao hatafurahishwa na hukumu kadhaa wakivamia mahakama au majaji na mahakimu na kuwapiga kizimbani.
Hisia kwamba hukumu hiyo ilipangwa bila kutupatia ushahidi waliopanga hukumu hiyo ni wakinanani na ni kwanini watu hao waitie mikono kwenye hiyo tu na si kwenye kesi nyingine kamwe haitamsaidia Lema,hivyo ni vyema basi Lema kama anaona ipo haja ya kukata rufaa akaae chini na wakili wake wakate rufaa na kama hawaoni haja ya kukata rufaa basi wasikate rufaa kuliko hivi sasa kunukuliwa akitoa maneno ya aina hiyo ambayo si moja ya mambo yaliyokuwa yakilalamikiwa kwenye kesi yake kwani mwomba rufaa anakata rufaa utakiwa kutoa sababu za kukatia rufaa hukumu iliyotolewa na mahakama ya chini na siyo porojo na hisia za barabarani.
Nimalizie kwa kumpa pole na kumuasa Godbles Lema na hao wanaojifanya wamepatwa na uchungu kutokana na hukumu hiyo ya kesi , kuwa makini na kauli zao wanazozitoa mara baada ya hukumu hiyo kutolewa kwasababu serikali inaweza kuwachukulia hatua.
Na Lema naomba ukumbuke kuwa wewe bado unakabiliwa na kesi mbili za jinai hapo hapo jijini Arusha, sasa unapotoa kauli kama hizo ambazo ni wazi zinaupaka matope mhimili huo wa mahakama ambao ni wenyewe pekee ndiyo umepewa mamlaka ya kutoa haki katika mashauri mbalimbali hapa nchini, ulipaswa utafakari kabla ya kutoa kauli kama hizo kwasababu kesi hizo zinaendelea kusikilizwa na mhimili huo huo ambao wewe na wafuasi wako mnaushutumu kuwa unatoa hukumu kwa kupewa maelekezo na Ikulu.Lema kumbuka wahenga walisema ‘ usidharau mkunga wakati uzazi ungalipo”.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
0714 774494
Chanzo:www.katabazihappy.blogspot.com, Aprili 16 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment