Header Ads

Dk.Slaa-Serikali inatekeleza changamoto za wapinzani?

Na Happiness Katabazi

MIAKA 15 sasa tangu Tanzania iruhusu mfumo wa vyama vingi, ambao wataalamu wa masuala ya kisiasa wanakiri kuwa umeleta changamoto kwa chama kilichopo madarakani mbali na wananchi kuwa huru kutoa maoni yao, lakini changamoto nyingine iliyotokana na mfumo huo ni uanzishwaji wa taasisi ambazo zimekuwa msaada kwa wananchi. Wakati imetimia miaka 15, ni utamaduni wetu kutafakari na kutathimini kule tulikotoka na hali ya sasa ikoje hususani kwa kuangalia mabadiliko na changamoto zilizoko. Katika mahojiana na Mwandishi Wetu HAPPINESS KATABAZI, Mbunge wa Karatu na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, anaelezea hali ya demokrasia ya vyama vingi nchini.

Swali: Je, ndani ya Bunge kuna mabadiliko gani tangu mfumo wa vyama vingi uanzishwe hapa nchini mwaka 1992?

Jibu: Kwanza lazima tukiri kwamba idadi ya wabunge wa upinzani ni ndogo.
Wabunge wa upinzani wapo 45 kati ya wabunge 320. Wabunge wa CHADEMA ni 11 kati ya hao 45 wa upinzani.
Lakini uchache si hoja japo maamuzi bungeni yanafanyika kwa kura na hivyo yote yanapitishwa kwa wingi wa wabunge wa CCM hata kama maamuzi hayo hayana maslahi kwa taifa.
Hasa suala la ongezeko la kodi na ushuru wa mafuta ambalo ni dhahiri kabisa halina maslahi kwa wananchi wa kawaida na kwa vyovyote ongezeko hilo litapandisha gharama ya maisha, hoja ambayo iliungwa mkono na wabunge wote wa CCM.
Pamoja na hali hiyo, kambi ya upinzani imetoa changamoto nyingi ndani ya Bunge.
Watanzania sasa wana nafasi ya kujua hali halisi ya mambo yalivyo katika uendeshaji wa nchi yao.
Hata wabunge wa chama tawala wakifungwa mdomo, wabunge wa kambi ya upinzani hakuna wa kuwafunga mdomo, watapasua mabomu tu.
Mfano, tuhuma za ubadhirifu ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambazo Gavana wa benki hiyo, Daudi Balali anauhusishwa, kwa mara ya kwanza sasa wananchi wa nchi hii wamejua kwamba ndani ya chombo kikubwa kama BoT kuna shutuma nzito kama hizo.
Aidha, Watanzania wamejua sasa kwamba kuna uwezekano wa kutengeneza bajeti mbadala kutoka kwenye rasilimali ya nchi yetu kama madini, misitu, uvuvi ambao kwa mara ya kwanza kambi ya upinzani imeonyesha kwamba taifa linaweza kupata sh trilioni 8 ikilinganishwa na sh trilioni 6 za serikali bila kuongeza mzigo wa ushuru na kodi kwa mwananchi wa kawaida.
Aidha, kutokana na rasilimali hizo, tungeweza kuwekeza zaidi kwenye huduma za jamii kama elimu ambayo tungeweza kuifanya kuwa bure hadi chuo kikuu, matibabu na yakalipiwa na serikali kikamilifu bila ya kumbughudhi mwananchi.

Swali: Unafikiri mchanganuo wa hoja za wabunge wa kambi ya upinzani zimeleta changamoto ndani ya Bunge?

Jibu: Siyo siri, tena mchanganuo wa hoja za kambi ya upinzani zimeleta changamoto ndani ya Bunge na zinaendelea kuleta changamoto wa utajiri wa mawazo, ambazo serikali ikizizingatia zitaleta unafuu kwa wananchi wa taifa hili kwa ujumla.
Kwa kuwa wapinzani hawawezi kufungwa midomo, serikali hivi sasa hailali tena, inajiandaa vizuri zaidi kwa maovu yanayoibuliwa na wapinzani ambayo wanayafanyia pamoja na uchache wao.
Naweza kusema ni sawa na mbwa mdogo ambaye kwa kupiga kelele tu, mwenye nyumba ataamka na kuchukua hatua za kulinda nyumba na mali zake.
Sasa kama wananchi hamtaamka baada ya kuamshwa na mbwa mdogo ili msaidiane naye kulinda rasilimali za nchi yenu, ipo siku mtajuta.

Swali: Manufaa na malengo ya mfumo wa vyama vingi nini?

Jibu: Lengo la msingi la vyama vingi vya siasa ni kushindanisha sera na ilani za vyama lengo likiwa ni kumnufaisha mwananchi apate kuchagua chama chenye sera bora.
Sura ya kwanza ya manufaa ya mfumo wa vyama vingi, ni kwamba umeleta utajirisho wa mawazo ambao huwezi kupata kwenye chama kimoja.
Hata kama vyama hivi havishiki madaraka kwa kuwa chama kimoja tu ndiyo kinatakiwa kiingie Ikulu, lakini kwa kuwa utajirisho huo si wa chama peke yake bali ni kwa wananchi wote, chama kina jukumu la kuchapisha na kutangaza sera zake, na mwisho wa hayo yote anayenufaika ni mwananchi.
Kwa hiyo, chama kinachotawala kinatakiwa kiwe na masikio ya kusikiliza sera za vyama vilivyoshindwa kutwaa madaraka na kisha izichukue na kuzifanyia kazi kwa maslahi ya wananchi wote bila kujali itikadi za vyama vyao.
Kwa mfano mwaka 1992, ukiona sera ya kwanza kabisa ya CHADEMA ilisema jengo la Chimwaga lililopo Dodoma ligeuzwe kuwa Chuo Kikuu kwa kuwa mji huo kuwa makao makuu ya nchi ni ngumu na badala yake ugeuzwe na uwe mji wa kitaaluma.
Nchi zilizoendelea kama Uingereza, kuna mji mmoja umekuwa kwa sababu serikali ya nchi hiyo ilitenga mji huo kuwa wa kitaaluma na kujengwa maduka makubwa ya kuuza bidhaa mbalimbali.
Serikali yetu ilikalia kimya sera hiyo hadi hivi sasa ndiyo imekubali jengo la Chimwaga liwe chuo kikuu, kwa hiyo jambo hili ni la kihistoria na kama serikali ingetekeleza tangu mwanzo hiyo sera yetu, mkoa huo hivi sasa ungekuwa mbali kimaendeleo.
Hivyo wananchi wanaweza kuangalia ushindani wa sera za vyama katika uchaguzi wa mwaka 2000, Serikali ya CCM ilikuwa inasema elimu ya msingi inalipiwa na wazazi, lakini vyama vya upinzani viliibuka na sera kwamba huwezi kumsomesha mtoto kwa kutegemea mchango wa wazazi ambao wengi wanaishi chini ya dola moja kwa siku na tulipendekeza elimu ya msingi itolewe bure.
Ilipotimu mwaka 2001, serikali ilipokea hayo mawazo na kuanza kutekeleza licha ya kuwa Ilani ya CCM ilikuwa haisemi kwamba watoto wasome bure na mara moja ikafuta UPE, ikapunguza ada na sasa taifa libeba mzigo wa gharama za wanafunzi.
Badala ya mzazi mmoja kuchangia, wanachangishwa wanajamii kwa kuchangia ujenzi wa madarasa.
Sasa huu ni utajirisho uliotokana na vyama vingi. Chama makini kinapaswa kuchukua sera za vyama vingine na si chama tawala tu ndiyo kichukue sera nzuri, la hasha, hata vyama ambavyo havijashika dola.
Asilimia 95 ya Watanzania wanaishi chini ya dola moja na hizi ni takwimu za serikali. Sasa taifa linapokuwa na idadi hiyo ya maskini kisha unawawekea kodi nyingi, hatuoni kwamba anakandamizwa mwananchi hapo?
Sasa kwa upande wa ilani za vyama vya upinzani, vilipunguza kodi za kichwa, kodi za usumbufu katika Jimbo la Hai, Karatu, Bariadi Mashariki na Kigoma, majimbo haya yanaongozwa na wabunge wa vyama vya upinzani.
Hata hivyo Julai 2002, serikali ilitangaza rasmi kufuta kodi zote za kichwa na usumbufu.
Hivyo hapa utabaini kwamba wapinzani baada ya kupunguza kodi hizo, serikali ikazifuta kabisa kwa hiyo, bila kuwepo ushindani katika hili la kodi serikali isingezifuta.
Hata hivyo, dhana ya vyama kuingia Ikulu katika utendaji, hili si muhimu kwa wananchi, mwananchi anachoangalia atapata faida gani. Na kitu kitakachomwondoa madarakani aliyepo madarakani, ni jinsi atakavyotekeleza yale aliyoyaahidi.
Sasa utekelezaji ni yale aliyobuni kiongozi anayeongoza na sera na ilani ya chama chake.
Sura ya pili ya mfumo huu, ukichukulia miaka 40 iliyopita iliyokuwa chini ya mfumo wa chama kimoja uhuru wa mawazo uliminywa kwa kiwango kikubwa.
Taifa lilitawaliwa na hofu kubwa hadi kwenye mfumo wa vyama vingi ulipoanza. Leo hii Watanzania tunaweza kutembea kifua mbele kwamba kwa kiasi kikubwa hofu imeondoka.
Lakini kwanini imeondoka? Imeondoka kwa sababu sisi wanachama wa vyama vingi hatuogopi, tunawatangulia wananchi katika kuonyesha njia kuondoa hofu.
Na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wamefunguliwa kesi nyingi za kubambikizwa.
Hadi vituo vya polisi, mahakama vimekuwa sebule za nyumba za viongozi wa vyama vya upinzani.
Watanzania watakumbuka Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo katika kampeni yeye na wafuasi wake walipigwa mabomu na marungu na kisha kuangukia kwenye mitaro kwa ajili ya kufanya maandamano na mkutano wa amani.
Sasa leo hii hayo yote yatabaki kuwa ni historia kwa kuwa hivi sasa tupo huru kufanya mikutano ya hadhara kwa kutoa taarifa tu kwa polisi, si kuomba tena kibali kwa Mkuu wa Wilaya yeyote na polisi anawajibika kutoa ulinzi kwa sababu wapinzani na wafuasi wa vyama vyao hivyo ni sehemu ya jamii.
Hakika ni mabadiliko makubwa sana na mtu atakayebeza vyama vya upinzani havijaleta mabadiliko tangu vianzishwe, basi mtu huyo atakuwa ni hayawani.
Nenda kwenye utawala bora, watendaji wa vijiji na wa kata enzi hizo waligeuka miungu watu, wananchi walipigwa kwa kukosa fedha za kuchangia mbio za Mwenge, wakaporwa mali zao na viongozi hao.
Hivi ninavyosema, manyanyaso hayo yamepungua, hasa jimbo ninaloliongoza la Karatu, na sehemu nyingine kama Bariadi Mashariki, Tarime na Kigoma.
Katika miaka hiyo ya nyuma, watendaji wa vijiji walikuwa wanakwenda kwa wanavijiji wanataka ng’ombe kinguvu na mwanakijiji akikataa kutoa anabambikiwa kesi za mauaji ambazo hazina dhamana. Kwa sababu upinzani umeimarisha utawala bora, watu hawanyamazi wanaongea yanayowakera, kwa hiyo haya nayo ni mabadiliko ya msingi.
Uhuru wa magazeti baada ya mfumo wa vyama vingi vya siasa kuanzishwa umepanuka, leo magazeti, redio na televisheni ni nyingi sana.
Zamani tulikuwa tunasikiliza habari zinazohusu nchi yetu kupitia BBC ya Uingereza na Deutschewelle ya Ujerumani.
Sisi kama CHADEMA tupo mstari wa mbele tangu kuanzishwa mfumo huu, hasa uchaguzi wa mwaka 1995, baada ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi, chama chetu kiliingia bungeni na kutumia nafasi yetu nje ya Bunge.
Kazi tuliyoifanya, matokeo yake CHADEMA ilikubalika kwa wananchi na hatimaye kupata halmashauri tatu za Hai, Karatu na Kigoma. Na katika maeneo hayo, kulifanya CCM kuwa chama cha upinzani jambo ambalo ni mabadiliko kama ilivyokuwa miaka 40 iliyopita ya enzi ya mfumo wa chama kimoja.
Kazi ya maendeleo iliyofanyika Karatu, wananchi walikichagua tena CHADEMA kwa sababu kilileta maendeleo.
Mwaka 2000 Karatu ilikuwa na sekondari moja iliyokuwa imejengwa kwa nguvu za wananchi.
“Leo Karatu inakamilisha sekondari 22… wakati Serikali ya CCM inazungumzia ujenzi wa sekondari katika kata, chama chetu Karatu kimeishamaliza ujenzi wa sekondari katika kila kata,” anasema.
Wakati leo serikali inazungumzia ujenzi wa zahanati kwenye kata, mpango ambao haujaanza, Karatu mwaka 2001 imetekeleza ujenzi wa zahanati katika vijiiji kwa mujibu wa sera ya chama chetu.
Kimsingi serikali tumeionyesha njia katika mambo mengi na inatufuata. Ndiyo manufaa ya ushindani na mfumo wa vyama vingi.
Vivyo hivyo vjiiji vya Karatu karibu vyote vinapata mradi wa maji na kimsingi si kwa mkono wa serikali na isipokuwa vijiji 10 kati ya 45 ndani ya jimbo hilo vinapata maji toka mradi wa Benki ya Dunia (WB).
Nasisitiza haya ni matokeo ya kushindanisha, Karatu haisubiri serikali, tunatafuta kwa njia zetu na ndiyo maana tangu nimeingia bungeni sijawai kuiomba serikali inijengee zahanati wala shule, ila serikali kuu inaposaidia pale ni jukumu lake.
Leo hii mbunge anasimama analialia na kuomba serikali imjengee shule, anapewa jibu na wizara husika arudi kwenye halmashauri yake jambo ambalo ni tusi, kana kwamba mbunge amekurupuka kutoa ombi hilo bila kupitia au kuwasiliana na halmashauri yake.
Sasa kulialia huko hakuwezi kutokea kwa mbunge toka kambi ya upinzani, kwa sababu anajua kabisa anachokitaka kwa serikali.
Ni wajibu wa Serikali Kuu kutekeleza mahitaji ya wananchi wa jimbo husika kwa kuwa wananchi hao ni sehemu ya walipa kodi wa nchi hii.
Na hali ya kulialia ufanywa na wabunge wengi wa CCM kutokana na mfumo wa chama chao ulivyo.

0755 312 859
katabazihappy@yahoo.com
www.katabazihappy.blogspot.com
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima,Jumatano Julai 18,2007

1 comment:

Anonymous said...

Nam!
Huyo ni Katibu Mkuu Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)!

Siyo siri Katibu na Mbunge huyu ana hekima na busara isiyo kifani! Haya yanadhihilishwa na mienendo ya uongozi wake katika CHADEMA, Jimbo lake, Bungeni na Taifa kwa Ujumla wake!

Wabunge wa Vyama vya Upinzani ni moto usio wa kuotea karibu! Ni wachache lakini Mahili barabara! Hakika kazi yao tunaishuhudia kila leo nje na ndani ya Bunge. Nawatia shime kwa kazi zao za uwakilishi wa wananchi wote wapenda Demokrasia katika Nchi hii Tanzania!

Historia inaonyesha mabadiliko na mafanikio makubwa katika kile ninacho kiita ukuaji wa Demokrasia ya Vyama vingi nchini tangu kuanzishwa kwake 1992.

Heko na kila raheri wanachi, wanachama, viongozi wa vyama vya Upinzani Tanzania!

Powered by Blogger.