Tendwa:Sheria ya kuungana ni kikwazo
JULAI mosi mwaka huu, Tanzania imetimiza miaka 15 tangu ianzishe mfumo wa vyama vingi vya siasa. Katika mahojihano na Mwandishi Wetu Happiness Katabazi, Msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa, anaeleza kwa mapana historia, changamoto na mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa mfumo huo.
Swali: Tunaomba utueleze kwa mapana historia ya mfumo wa vyama vingi.
Jibu: Mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini ulianza rasmi Julai mosi, 1992, kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992.
Lakini kabla ya hapo, kulikuwa na vuguvugu la wanajamii la kuleta msukumo wa kutaka mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Msukumo huo uliungwa mkono na mabadiliko ya kiulimwengu ya kisiasa, hasa kuanguka kwa dola za Kisoshalisti (dola la Ulaya Mashariki) iliyokuwa ikiongozwa na Urusi ambao ndiyo walikuwa na siasa za Usoshalisti (Ujamaa).
Sasa kuanguka kwa dola hizi ndio kulifanya jumuiya za Ulaya Mashariki kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi.
Mabadiliko hayo ya nchi za Ulaya, yaliungwa mkono na nguvu ya soko huria (free economic) ambapo nchi zilikuwa na uwezo wa kuuza na kununua badala ya uchumi kuwa hodhi ya serikali.
Kwa hiyo mambo yote haya yalileta mabadiliko yakaingia kwenye mfumo wa vyama vingi. Hivyo uamuzi wa Tanzania kujiunga na mfumo huu si wa kushangaza.
Na muda mfupi baada ya mfumo huo kuanzishwa nchini, taasisi nyingi zilituma maombi ya kutaka kuanzishwa kwa vyama vya siasa kwa mujibu wa sheria.
Hadi mwaka 1993, kulikuwa na maombi 51 ya usajili, lakini kutokana na mchujo uliofanyika kwa mujibu wa sheria, ni vyama 13 vilikubaliwa.
Vyama hivi 13 vilianza kushiriki chaguzi ndogo mwaka 1994, kama za nafasi ya ubunge, udiwani endapo tu wabunge au madiwani walikuwa wamefariki au wamepoteza sifa za kuendelea kushika nyadhifa hizo.
Kwa hiyo mwaka 1995 ndipo ulipofanyika uchaguzi mkuu wa kwanza ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Swali: Hali ya kisiasa wakati huo ilikuwaje?
Jibu: Kulikuwa na hali ya vuguvugu la kutaka kutoka katika mfumo wa chama kimoja na nifananishe vuguvugu hilo lilikuwa sawa na ndege au wanyama waliokuwa wamefungiwa sehemu moja, sasa wanataka kufunguliwa wakimbie.
Kimsingi, dira na mwelekeo wa mfumo wa vyama vingi havikuwapo wakati huo mwaka 1995.
Kwa mfano, sheria ilikuwapo na ilikuwa imerekebishwa, lakini wananchi hawakupata nafasi ya uelewa kwamba sheria hiyo ilikuwa imesema nini na hawakupata nafasi ya kupata elimu ya uraia kuhusu mfumo wa vyama vingi na matokeo yake vyama vingi vya siasa vilitoka na hoja ya sheria 40 zilizotamkwa kuwa ni mbovu na kandamizi na Tume ya Jaji Francis Nyalali.
Na hii ikageuka kuwa hoja ya kampeni katika uchaguzi wa mwaka 1995. Kimsingi katika kipindi hicho hali ya kisiasa ilikuwa inatafuta mwelekeo kama maji yanavyotafuta mkondo wa kutokea.
Ili kukidhi matakwa ya mfumo huo, katika uchaguzi wa 1995, vyama vilipata fedha kwa ajili ya kampeni toka serikalini.
Sasa baadhi ya wabunge na madiwani hawakufanya kampeni kama ilivyokusudiwa, kwa hiyo walikuwa wakiganga njaa na hakukuwa na marejesho ya fedha hizo serikalini.
Tunaweza kusema kipindi hicho wale waliokuwa na dhamira ya kisiasa walifanikiwa. Kivipi? Kulikuwa na uwakilishi mkubwa wa upinzani bungeni na vile vile madiwani wengi kwa kuwa halmashauri nyingine ziliongozwa na wapinzani na halmashauri zilizoongozwa na wapinzani wakati huo ni Bariadi, Karatu na Kigoma.
Swali: Baada ya uchaguzi wa mwaka 1995 nini kilitokea?
Jibu: Vyama vilitulia, hakukuwa na vuguvugu kama lilivyokuwa awali, vyama vilivyoshindwa uchaguzi vilitafakari nini cha kufanya kwa sababu mfumo wa vyama vingi ulishaanza.
Kwa hiyo utaona vyama vingi viliingia kwenye uchaguzi huo vikashindwa kukamata dola.
Kwa hiyo mwaka 1996-2000, kikawa kipindi cha mtawanyiko wa wanachama toka chama kimoja hadi kingine na pia kilikuwa ni kipindi cha migogoro ndani ya vyama vya siasa ama kwa kukosa uongozi au hata kugombea ruzuku ambayo ilikuwa ikigombewa sana.
Pia kilikuwa kipindi cha vyama kujizatiti, na kujijenga upya. Mfano ni kipindi ambacho viongozi kama Augustine Mrema alitoka chama cha NCCR-Mageuzi na kwenda Tanzania Labour Party (TLP).
Ni kipindi ambacho vijana walichukua uongozi wa juu kama Mwenyekiti wa sasa wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia.Vyama vilikuwa na sifa kama CHADEMA vilivyopwaya kipindi cha nyuma, lakini pia kilikuwa ni kipindi cha kujiimarisha.
Vyama vikongwe kama UMD baada ya viongozi wake wa juu kuondoka, kama Abdallah Fundikira na kujiunga na CCM, vililala usingizi. Kwa ujumla hakikuwa kipindi cha mikikimikiki na hekaheka kama ilivyokuwa mwaka 1995.
Swali: Uchaguzi wa pili ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 2000, ulikuwaje kwa upande wa Tanzania Bara?
Jibu: Ulikuwa ni uchaguzi wa pili wa vyama vingi. Kipindi hiki serikali haikutoa ruzuku kwa vyama, kwa sababu sheria ya vyama vingi Namba 5 ya mwaka 1992 ilifanyiwa marekebisho na kuweka vigezo vya chama kufanikiwa kupata ruzuku.
Baadhi ya vigezo ni chama lazima kishinde uchaguzi ngazi ya diwani na ubunge au chama kupata asilimia 5 katika kura zilizopigwa kitaifa.
Japokuwa vyama vyote 13 vilishiriki katika uchaguzi, lakini kampeni zilidorora kwa kuwa hawakuweza kufika katika maeneo yote waliyokusudia na matokeo yake ni kwamba, vyama havikupata uwakilishi mkubwa ndani ya Bunge na serikali za mitaa dhidi ya CCM.
Pia kilikuwa ni kipindi ambacho wabunge waliofanikiwa katika chama tawala (CCM), ni wale waliotoka vyama vya upinzani.
Kwa hiyo vyama vingi vya upinzani vilikosa wagombea wenye uwezo wa kufanya kampeni na wale wachache waliopata ubunge kwa kupitia vyama vya upinzani, walienguliwa toka CCM baada ya kufanyika kwa kura za maoni ndani ya chama hicho.
Na hawa walikuwa wasemaji wazuri sana wa kambi ya upinzani ndani ya Bunge.
Swali: Uchaguzi wa pili ndani ya mfumo wa vyama vingi mwaka 2000, kwa upande wa Zanzibar, ulikuwaje?
Jibu: Ni kipindi ambapo Chama cha Wananchi (CUF) kilikuwa na mategemeo makubwa ya kushinda, hasa upande wa kiti cha urais, lakini CCM ilipata ushindi ambapo Rais Abeid Amani Karume, alianza kipindi chake cha kwanza cha urais.
Katika kipindi hiki, kulikuwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa ambapo matokeo yake kulitokea vurugu za Januari 26, 2001 ambapo matokeo yake watu kadhaa walipoteza maisha yao.
Huu ulikuwa ni mwendelezo wa mgogoro wa kisiasa Zanzibar uliotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 1995.
Kipindi hiki kwa ujumla kilikuwa ni cha mgongano wa kiitikadi baina ya vyama vya CCM na CUF. Lakini pia ni kipindi cha maelewano baada ya makubaliano (policatal diolog) yaliyojengwa na utashi wa kisiasa.
CCM na CUF vikaungwa mkono na wanajamii na vyama vingine vya siasa ili kuleta mwafaka na hali bora ya kisiasa Zanzibar.
Mazungumzo haya yalichukua takribani miezi sita na Oktoba 21 mwaka 2001, vyama vya CCM na CUF viliwekeana saini na kuwa mwafaka wa makubaliano ya kisiasa hapa nchini.
Hiki ni kipindi cha ukomavu wa kisiasa ulioanza kujitokeza nchini kwa vyama vinavyogongana kuwa na mazungumzo na kuelewana bila kutafuta msaada wa usuluishi nje ya nchi.
Swali: Tueleze kipindi cha mwaka 2000-2005 vuguvugu la kisiasa lilikuwaje?
Jibu: Vyama vya siasa viliongezeka toka 13 hadi 18 na vyama viwili kupoteza usajili wa kudumu ambavyo ni PONA na TPP, vilivyofutwa kwa kukiuka matakwa ya sheria. Huu ni wakati ambapo demokrasia ilionekana kukomaa katika nchi yetu.
Kwa upande wa CCM, kilikuwa ni kipindi cha kujizatiti ili kuendelea kushika uongozi na kilikuwa ni kipindi cha mwisho wa serikali ya awamu ya tatu kushika uongozi.
Kwa kufuata dhana ya muungano wa vyama vya siasa Kenya na kuunda NARC, baadhi ya vyama vya siasa hapa Tanzania wanajaribu kuunda muungano wa kisiasa, lakini masharti yanawashinda kwa sababu sheria ya vyama vya siasa ya hapa nchini haiwaruhusu kuungana bila kupoteza sifa za vyama vyao.
Dhamana yao pia haikuwa ya kisiasa japo kuwa wangeweza kushirikiana katika chaguzi za serikali za mitaa na baadaye uchaguzi mkuu 2005.
Swali: Uchaguzi wa mwaka 2005 umewafundisha nini Watanzania na vyama vya siasa kwa ujumla?
Jibu: Uchaguzi huu ulikuwa ni kipimo cha sheria ya uchaguzi ya mwaka 1992 na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo imefanyiwa marekebisho mara kadhaa, hasa eneo lililofanyiwa marekebisho ni la mgombea mwenza.
Uchaguzi huu japo ulikwenda vizuri, lakini ulifikwa na kasoro kutokana na kifo cha mgombea mwenza wa CHADEMA, ambacho kilitokea siku tatu kabla ya kupiga kura. Hali hii ilifanya uchaguzi kuahirishwa kwa siku 51 na vyama vya siasa viliathirika kifedha na kupungukiwa na ari ya kufanya kampeni.
Serikali nayo ilipungukiwa na fedha kibajeti kwa ajili ya kununulia vifaa, usafiri wa vifaa vya kupigia kura nk. Baada ya uchaguzi CCM ilipata ushindi kwa asilimia 80.28.
Chama cha CUF japokuwa kilipata ushindi mkubwa Tanzania visiwani, lakini Tanzania bara haikupata hata kiti kimoja cha ubunge, viti vyote vya ubunge vilipatikana Zanzibar na hasa Pemba vilikopatikana viti 17 na Unguja Mji Mkongwe kilipatikana kiti kimoja.
CHADEMA kilifuatia kwa ushindi wa viti vitano vya ubunge na UDP na TLP vilipata kiti kimoja kimoja.
Huu haukuwa ushindi mzuri kwa vyama vya upinzani, ni matokeo ya mambo yaliyotokea katika uchaguzi wa mwaka 2000, kwa hiyo vyama havikuwa vimejizatiti kisiasa.
Na hivyo uchaguzi wa mwaka 2005 ulikuwa ni fundisho kwa vyama vya upinzani. Ni vyema sasa wakajipanga vizuri na wawafikie wananchi wengi waliopo vijijini kwa kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanaishi vijijini.
Swali: Hadi hivi sasa Tanzania ina vyama vingapi vya siasa ambavyo vina usajili wa kudumu?
Jibu: Hadi sasa Tanzania ina jumla ya vyama vya siasa 18 ambavyo vina usajili wa kudumu.
Vyama hivyo ni Chama cha Mapinduzi (CCM), National Convention for Construction and Reform (NCCR-Mageuzi), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), The Civic United Front (CUF), Union for Multiparty Democracy (UMD), National League for Democracy (NLD) na United People’s Democratic Party (UPDP).
Vingine ni National Reconstruction Alliance (NRA), Tanzania Democratic Alliance (TADEA), Tanzania Labour Party (TLP), United Democratic Party (UDP) na Demokrasia Makini (MAKINI).
Pia kuna The Forum for Restoration of Democracy (FORD), Chama cha Haki na Ustawi (CHAUSTA), Democratic Party (DP), Progressive Party of Tanzania (PPT-Maendeleo), Jahazi Asilia na Sauti ya Umma (SAU).
Licha ya kuwa na vyama hivyo, ofisi yangu ipo mbioni kuifuta FORD, kwa kuwa imekiuka katiba yake yenyewe, sheria ya vyama vingi ya mwaka 1992 na cha kustaajabisha hadi hivi tunavyozungumza chama hicho hakijafanya uchaguzi wa ndani.
Swali: Tueleze hali ya kisiasa kwa ujumla hivi sasa Tanzania bara na visiwani ikoje?
Jibu: Kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano ni nzuri. Vyama vya siasa hivi sasa vimekuwa na mwelekeo mzuri kiitikadi.
Migongano na migogoro ya kisiasa ndani ya vyama imepungua, vyama hivi sasa vimejiimarisha kiuongozi na vingi vimeishafanya chaguzi ndani ya vyama vyao na vingine vinajiandaa kufanya chaguzi ndani ya vyama vyao, ikiwemo CCM.
Hivi sasa vyama ya upinzani, vimejenga uhusiano wa kushirikiana kwa nia ya kuungana na hapo baadaye kidemokrasia. Hakika hili ni jambo jema kwa vyama hivi kuwa na mawazo ya pamoja, mwelekeo na mtazamo wa pamoja.
Ila tatizo lililopo ni sheria ya vyama vingi ya mwaka 1992, ambayo hairuhusu vyama kuungana, lakini sheria hiyo hiyo inaruhusu vyama hivyo kushirikiana katika kampeni. mfano chama kimoja kumuunga mkono mgombea wa chama kingine.
Nakiri sheria hii ni tatizo, lakini ofisi yangu ilikwishapeleka mapendekezo serikalini ya kutaka sheria hiyo ifanyiwe marekebisho licha ya kwamba hadi sasa bado marekebisho hayajafanyika.
Swali: Mfumo wa vyama vingi vya siasa umetuletea nini Watanzania?
Jibu: Hakuna ubishi, mfumo wa vyama vingi umetutoa katika mgando wa chama kimoja, ambao ulikuwa hautoi nafasi ya wenye kero kukosoa serikali na kuweka hoja mbadala.
Hivi sasa wananchi wana mwamko mkubwa katika masuala mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Leo hii Bunge si chombo tena cha utekelezaji wa matakwa ya chama kama ilivyokuwa awali.
Sasa hivi Bunge ni chombo chenye nguvu ya kuielekeza serikali nini cha kufanya ili kukidhi matakwa ya wananchi. Hapo awali Bunge lilikuwa likifuata maelekezo ya chama. Dhamana kubwa ilikuwa watu wote walikuwa ni wanachama wa CCM kwa hiyo ilikuwa ni demokrasia ya chama kimoja.
Leo hii wananchi hata bila kupitia Bunge wanaweza kutoa maoni yao kupitia taasisi mbalimbali kutokana na uhuru wa kutoa mawazo yao. Hakika ni jambo la kujipongeza.
Serikali nayo inakubali kukosolewa na kufanya marekebisho ili kukidhi matakwa ya wananchi. CCM nayo inakubali kukosolewa na kujikosoa ili iweze kuendelea kubaki madarakani kwa kuheshimu na kufuata sheria.
Ukilinganisha mfumo wa vyama vingi vya siasa na ule wa chama kimoja, ukiweka kwenye mizani utaona mfumo wa vyama vingi ni mzuri na umeleta fikra za kimapinduzi na maendeleo makubwa katika taifa letu.
0755 312 859
katabazihappy@yahoo.com
www.katabazihappy.blogspot.com
Chanzo:Tanzania Daima Jumatano Julai 18,2007
1 comment:
Safi sana Happy!
Maswali yameenda kozi! Na muulizwaji leo naona hakupendelea, nampa bigup kubwa. Watanzania wote tukianza kujenga msitakabali wa uhuru wa kutoa maoni, ushauri na kukubali kukosolewa ama kwa hakika tutapiga hatua japo moja mbili mbele! Tutafika!
Nakupongeza sana kwa juhudi zako katika kukidhi haja na kiu ya wanzalendo wote. Mungu akujaze juhudi na maarifa!
Post a Comment