Header Ads

KIKWETE ANAPONZWA NA WASAIDIZI WAKE



Na Happiness Katabazi

MWANASESERE ni sanamu inayotumiwa na watoto kwa kuchezea. Kwa mtoto mwanasesere anawakilisha kitu halisi. Katika uhalisia mwanasesere ni hali kwa uanasesere wake lakini kwa kweli si kile hasa anachokiwakilisha.

Kwa mfano, mwanaserere mwenye umbo la simba, atabakia kuwa mwanasesere na si simba halisi.Nimeanza makala yangu na mfano huu nikiamini kuwa utasaidia kufikisha ujumbe wangu kwa watu wa marika yote.

Nitazungumzia tabia isiyopendeza inayoanza kuota mizizi kwa baadhi ya watendaji wa serikali na wasaidizi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Inaonekana kuwa Rais Kikwete amekuwa akidanganywa katika taarifa anazopewa na wasaidizi wake na hata watendaji wa serikali. Kwa bahati nzuri na kwa sababu anawaamini, taarifa hizo amekuwa akizitumia anapozungumza na wananchi na kuwataka waziamini, wakati wananchi wengi wanajua kuwa taarifa hizo si sahihi.

Hili ni moja ya sababu zilizompunguzia umaarufu wake yeye binafsi na serikali yake kwa mwaka mmoja uliopita kama jinsi ripoti ya Taasisi ya Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) katika utafiti wake ilivyoeleza.

Kwa mujibu wa kumbukumbu zangu, Rais Kikwete alianza kutofautiana na wananchi katika hotuba yake aliyoitoa mkoani Mwanza mapema mwaka jana, aliposema wakazi wa mkoa huo hawali mabaki ya samaki – kule Jiji la Miamba wanaojulikana kama mapanki - na kwamba hakukuwa na wasichana ‘wanaojiuza’ mkoani humo.

Rais Kikwete aliyatamka hayo baada ya mtunzi wa filamu ya ‘Darwin’s Nightmare’, raia wa Australia, Hubert Sauper, kutengeneza filamu iliyokuwa ikionyesha jinsi wananchi wanavyoishi katika lindi la umasikini huku rasilimali yao - samaki - ikiwanufaisha wawekezaji kutoka nje.

Katika filamu hiyo, mtunzi alionyesha jinsi wananchi hao masikini wanavyopona kwa kula mabaki ya samaki.

Katika hili, Rais Kikwete alipingwa kwa ushahidi. Wananchi waliikosoa kauli yake hii na vyombo vya habari viliandika vikithibitisha kuwa yaliyokuwa katika filamu ya ‘Darwin’s Nightmare’ yalikuwa ya kweli.

Katika hali ya kushangaza serikali iliibuka na kutumia nguvu nyingi na fedha za walipa kodi kutengeza tovuti ya kupinga maudhui yaliyokuwa kwenye filamu hiyo.

Hata hivyo, haikufanikiwa sana kwa sababu mapanki yamebaki kuwa kitoweo muhimu kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa na Sauper anaendelea kuwa mkweli kuliko Rais Kikwete kuhusu ulaji mapanki.

Ingawa Rais Kikwete ni kiongozi mwenye sifa ya pekee ya kujua zaidi matatizo ya wananchi wake kutokana na staili ya maisha yake wakati akiwa waziri ya kujichanganya zaidi na watu wa kawaida, akiwa rais sifa hiyo hana, anawategemea zaidi wasaidizi wake kumpa taarifa za hali ya maisha ya watu wake.

Hivyo, waliomwandalia taarifa hiyo kwamba Mwanza hawali mapanki walimdanganya na kumuabisha mbele ya wananchi wake na jumuiya ya kimataifa inayoufahamu ukweli huu. Nilidhani alipaswa kuwafuta kazi wasaidizi hawa mara moja kutokana na kumpotosha.

Mwaka jana huo huo, Rais Kikwete alijikuta katika tukio jingine la aibu baada ya picha yake kuchapishwa katika vyombo vya habari ikimwonyesha akiwa anapokea hundi kutoka kwa maofisa wa juu wa Benki ya Dunia.







Katika picha hiyo, Rais Kikwete akiwa ndani ya mavazi nadhifu na uso wake ukiwa umepambwa na tabasamu, alionekana akipokea hundi ambayo kiasi cha fedha kilichoandikwa kwa maneno kilikuwa tofauti na kile kilichoandikwa kwa tarakimu.





Hundi hiyo iliandikwa kiasi cha fedha kwa maneno, dola za Kimarekani laki mbili ilhali katika tarakimu iliandikwa dola 300,000. Wakati Rais akipokea hundi hiyo na kupigwa picha na waandishi wa habari, wasaidizi wake lukuki walikuwapo.





Hawa ni watu wanaoaminika kuwa makini, lakini katika hilo la hundi umakini wao uliyeyuka. Rais akawa amepokea hundi yenye shaka kwa kila hali.





Maswali yaliibuka baada ya Rais Kikwete kuonekana katika vyombo vya habari akiwa amekamata hundi hiyo. Wapo waliohoji kama maofisa wa Benki ya Dunia waliamua kumdhalilisha Rais wetu ili ionekane kuwa ni kiongozi anayeweza kupokea chochote kile ilimradi tu kinahusu fedha. Na wengine walibaki wakihoji umakini wa wasaidizi wa Rais.





Tukio hili liliibua hisia kwamba viongozi wa serikali hawako makini na hata udhaifu ulioko kwenye mikataba mbalimbali inayolitia hasara taifa inatokana na umakini mdogo wa viongozi wetu.




Nami niliamini hivyo na kulingana na tukio lenyewe, sidhani kama yupo anayeweza kupingana na imani hii. Hilo nalo lilipita.





Lakini siku chache kabla ya mwisho wa mwaka 2007, alijikuta akiingia tena katika mtego ule ule wa kupewa taarifa za uongo na yeye kutoa tamko ambalo baadaye lilikuja thibitika kuwa si la kweli.





Safari hii Rais Kikwete alikutana uso kwa uso na mahujaji waliokuwa wamekwama Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, baada ya mahujaji hao kukosa ndege ya kuwapeleke Makka kwa ibada ya Hijja.





Rais Kikwete alifika uwanjani hapo akiwa njiani kwenda zake Marekani. Akawakuta mahujaji waliokata tamaa wakiwa uwanjani hapo, hawajui safari yao itakuwa lini licha ya kulipa fedha kwa ajili ya safari hiyo.





Tunaambiwa kwamba Rais alipowahoji wasaidizi wake alitaarifiwa kwamba tayari kuna ndege imeandaliwa kwa ajili ya kuwasafirisha mahujaji hao. Katika kumsadikisha hilo baadhi ya mahujaji walichukuliwa na kupakizwa kwenye ndege kuonyesha kama kwamba wako tayari kwa safari.





Ilikuwa kama sarakasi. Mheshimiwa akapata moyo, akawafuata kuwaaga huku akiwatakia safari njema ya Hijja. Akaigeukia ndege iliyokuwa imepangwa kumpelekea Marekani, akapaa.





Kituko! Alipoondoka tu, mahujaji waliopakizwa kwenye ndege kwa ajili ya safari wakateremshwa. Kisa? Eti ndege hiyo iligundulika kuwa na hitilafu! Si rahisi kuamini, lakini hivyo ndivyo ilivyokuwa.





Rais Kikwete kwa mara nyingine akawa ameingizwa katika mtego wa kusema uongo, kwamba alikwenda kuwaaga mahujaji hao baada ya kudanganywa kuwa safari imeiva, naye akadanganyika na kuwaaga mahujaji. Hiki ni kitendo cha aibu kwa Rais wetu.





Kwa kumbukumbu ya matukio haya yaliyotokea mwaka jana, nadhani Rais Kikwete ana kila sababu ya kuipanga upya safu ya wasaidizi wake ili kuondokana na aibu ya kutoa kauli zenye utata kila mara kwa wapiga kura wake.





Naamini Rais Kikwete anaweza kusahihisha hali hii kutokana na rekodi yake kiutendeji na kutovumilia watumishi wazembe. Watumishi wanaomwangusha mbele ya wananchi wake.




Kwa matendo yote haya hatuoni kwamba Mheshimiwa Rais wetu anageuzwa mwanasesere?





Wito wangu kwa Rais Kikwete ni kwamba naye awe anajiridhisha kwanza na hotuba anazoandaliwa kabla ya yeye kwenda kuzisoma hadharani, kwa sababu mifano hiyo hai imetuonyesha wazi baadhi ya watendaji wake ambao aliwaamini akawapa dhamana ya kumsaidia si makini.





Wanachokifanya ni kumfurahisha Rais lakini kumbe wanampoteza na kumwingiza mkenge kama watoto wa mjini wasemavyo.





Mungu ibariki afrika, mungu inusuru Tanzania





Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Januari 6, 2007


No comments:

Powered by Blogger.