Header Ads

MWAHALISI ALUTA CONTINUA

Na Happiness Katabazi

UBAYA ni kama kutu, kutu inayoharibu chuma huota kwenye chuma chenyewe. Na ndivyo ubaya uotavyo ndani ya moyo wa binadamu na kuuharibu.

Nimelazimika kutumia msemo huo kwani mada yangu ya leo nitakayoichambua inaenda kabisa na maana nzima ya msemo huo.

Mada hiyo inahusu tukio la kishenzi lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo watu wasiyofahamika walivamia katika ofisi za gazeti la Mwanahalisi na Mseto na kuwajeruhiwa kwa mapanga na kuwamwagia tindikali usoni wanahabari mahiri nchini Saed Kubenea na Ndimara Tegambwage.

Siku zote ubaya ni mbaya na ubaya haufanywi na wanyama bali ufanywa na binadamu wenywe ambao binadamu hao kutokana na akili zao kuwa finyu ufikiri kwamba mungu ni wao peke yao na wanasahau kwamba ipo siku nao ubaya huo utawarudia ikiwezekana mara dufu.

Ubaya uliofanywa dhidi ya wanahabari wenzetu endapo hautakomeshwa ipo siku utaota mizizi katika mioyo ya binadamu wa jamii yetu na hatimaye tutaanza kuumiza wenye kwa wenyewe.

Tukio hilo hakika ni la kwanza tangu nchi yetu ilipopata uhuru mwaka 1961 na hakika limeweka historia mbaya ndani na nje ya nchi kwani kila kukicha viongozi wetu wamekuwa wakitamba Tanzania ina uhuru wa habari lakini cha kushanga kama si kustaajabisha tambo hizo tayari zimeanza kuingiwa na dosari.

Dosari hizo hasa hasa zimeanza kujitokeza katika kipindi cha serikali ya awamu ya nne muda mfupi kabla ya kuingia madarakani na hadi ilivyoingia.

Baadhi ya viongozi wa awamu nne ambao katika mchakato wa kumtafuta mgombea urais kupitia chama chao cha CCM, hakuna kificho kundi maarufu la wanamtandao’ ambalo linaelezwa lilikuwa likimunga mkono Rais Jakaya Kikwete, lilikuwa mstari wa mbele kununua baadhi ya waandishi wa habari waandamizi toka vyombo mbalimbali vya habari ili viweze kuwaandika kwa mazuri na kuficha maovu yao.

Waliokuwa wakifuatilia mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, walibaini hilo kwani kundi la Mtandao liliwaweka kwapani wanahabari wakiwemo baadhi ya wahariri kwa kuwapatia safari za ndani na nje ya nchi,fedha na hata kuwaidi vyeo vya ukuu wa mkoa, wilaya na ubalozi na hadi sasa baadhi ya wanahabari hao wanaendelea kutumiwa na wanasiasa wa kundi hilo kwa maslahi yao na si jamii tena wala maadili ya taaluma ya uandishi inavyotaka.

Waanahabari ambao walikataa kugeuzwa vibaraka wa kundi hilo, walionekana kuwa ni maadui na kusakamwa sambamba na kutishiwa usalama wao na wengine walifukuzwa kazi kutokana na misimamo yao.

Baada ya jamii kugundua uzandiki huu, ilianza kuwalaumu wanahabari hao sambamba na kuwaanika majina yao kwenye tovuti mbalimbali hali iliyosababisha vibaraka hao heshima yao kuporomoka kwenye jamii ya wanahabari.

Nalazimika kusema hali hiyo ilisaidia kidogo kwani hata mbwembwe na ngebe walizokuwa nazo awali wanahabari hao ambao nao wakalewa ujinga na kujiita nao ‘wanamtandao’ hivi sasa zimekwisha kwani kwenye mijumuiko ya wanahabari makini wamekuwa wakionekana kwa nadra na hivyo vyeo waliyoaidiwa wengi wao wametoswa.

Baada ya wanahabari na wadau wa habari kugundua njama ya wanahabari hawa vibaraka waliamua kusimama kidete kwa kuanza kupambana na vibaraka hawa ambapo walianza kuandika ukweli kuhusu mwenendo wa serikali ya awamu ya nne na viongozi wake sambamba na kuikosoa na hatimaye hivi sasa wamefanikiwa kuwazidi nguvu vibaraka hao.

Na kutokana na mapambano hayo, serikali ikaondoka kwenye lindi la ulevi wa sifa za ushindi wa Tsunami na hatimaye imeanza kuchapa kazi kwa uwezo wake licha katika nyanja nyinge utendaji umekuwa ukizolota na hiyo yote imesababishwa na changamoto mbalimbali zinazotolewa na vyombo mbalimbali vya habari uhuru.

Licha vyombo hivyo vya habari uhuru kuipa changamoto serikali, baadhi ya viongozi wa juu wa serikali ambao kila kukichwa wanataka wasifiwe kama ‘mabibi harusi’ huku jamii inawafahamu kuwa ni wachafu ,wamekuwa wakitoa maelekezo katika taasisi za serikali zisitoe matangazo kwa magazeti hayo likiwemo gazeti la Tanzania Daima, Mwanahalisi ,kwa sababu magazeti haya yamekuwa yakiandika habari zisowasifia.

Ukiona kiongozi wa serikali amefikia hatua hiyo, ama anatumwa na kiongozi wanchi au ameamua kufanya hivyo kwa matakwa yake kwa kutumia wadhifa wake, ujue kabisa kiongozi huyo hanatofauti na madikteta kwani Dikteta anakasumba ya kutotaka kukosolewa na kupokea changamoto na kwa bahati nzuri kwa hapa kuna viongozi wa aina hiyo na wanafanywa mchezo huo ,tunawajua ,wanajijua tena wamepewa dhamana ya kutuongoza.

Nimeeleza hilo ili wadau wa habari watambue kwamba uhuru wa habari pia unapigwa vita na baadhi ya viongozi wa juu wa serikali tuliyoiweka madarakani, na hali hii aikubaliki hata kidogo kwani hatuwezi kuona mambo yanaenda mlama kisha tukae kimya kwani tutakuwa hatuitendei haki jamii na siku wa siku tuje kulaumiwa.

Ukibaraka uliokuwa ukifanywa na unaendelea kufanywa na wanahabari wenzetu ambao wanaelimu kubwa tu, naweza kusema ni mianya ambayo inawapa fursa mabazazi wasiyopenda kuona uhuru wa habari ukiendelea kukua hapa nchini , kutuangamiza kirahisi.

Kwani endapo wanahabari wote wakifanyakazi yao kwakuzingatia matakwa ya taaluma zao bila kujikomba kwa wanasiasa,wafanyabishara, viongozi wa juu wa serikali ,kamwe hakutakuwa na kundi la watu watakaothubutu kuchezea wanahabari wala kutikisa uhuru wa habari.

Ni sisi wenyewe kwa njaa zetu ambazo tumeamua ‘kuzifungulia feni’tumekuwa mstari wa mbele kulamba viatu vya viongozi na kuchomana wenyewe kwa wenyewe kwa hao mabazazi.Hatuna umoja wa kweli miongoni wetu, wengi wetu tumetanguliza maslahi binafsi mbele kuliko ya taifa.

Ni sisi miongoni mwetu tumekuwa tukitumiwa na baadhi ya watu ili kuhujumiana kwa kubambikiana habari ili ikiichapisha gazeti lake lishitakiwe au kufungiwa. Ni sisi si tumekuwa tukio siri tumekuwa tukivujisha siri za vyumba vyetu vya habari kwa mabazazi.

Wanahabari wamekuwa wamoja wakati wa kipindi cha uchaguzi kikikiwa kimemalizika , ila umoja huo uenda likizo pindi mchakato wa uchaguzi mkuu unapoanza kwani kipindi hiki waandishi vibaraka ugeuka kuwa ni kipindi cha neema na mavuno kwao.

Hivyo katika kipindi hiki cha majonzi kutokana na yaliyowakumba wanahabari wenzetu , tukae chini tufikiri kwamba ukibaraka siyo chanzo cha kuzika uhuru wa habari?.Miongoni mwetu kujirahisha kwetu kwa wakubwa na kuchomana wenyewe kwa wenye kwa mabazazi siyo sababu inayosababisha sisi kutishwa,kujeruhiwa na hata kutaka kutolewa uhai na watu hao?

Kila mmoja wetu akiacha unafki na kuyatafakari hayo kwa kina naamini atakubali kwamba mapungufu hayo yanatoa mianya kwa ‘mabazazi’ wasiotaka kukosolewa kutudhuru kwa urahisi na kuangamiza uhuru wa habari ambao sisi kama wanataaluma ndiyo tunatakiwa tuwe wa mstari wa mbele kuutetea na kuusimamia.

Lakini nawataka wale wote ambao hawataki kuguswa na kalamu zetu basi wajirekebishe ,waache ufisadi na na wachape kazi, wasifikiri kututisha na kujeruhi ni dawa, hiyo siyo dawa kwani hata wakifanikiwa kutoa uhai miongoni mwetu bado, watazaliwa watu wengine ambao nao watakuwa na fikra za kimapinduzi na wataendeleza kazi iliyokwishaanza kufanywa na watu wa taifa hili tangu lilipopata uhuru wake.

Na mtambue kwamba wanao sisi tunawaokoa kwa hoja nikiwemo mimi, siyo maadui wa taifa hili bali tunalitakia mema taifa na viongozi wake ila hao wanaowasifia na kuwajaza ujinga kila kukicha hawawatakii mema kwani wanawageuza ‘wanasesere’ machoni kwa jamii, wanachokitaka kutoka kwenu ni msaada unaowanufaisha matumbo na familia zao na si jamii.

Nikiligeukia jeshi la polisi ambalo limetuaidi kuwa limeunda timu ya uchunguzi kuchunguza waliosika na tukio hilo la uvamizi, nataka nimwambie IGP-Said Mwema kwamba tunaomba uhakikishe vijana wako wanawakamata watu sahihi waliohusika na tukio hilo na si vinginevyo.

Kwani endapo watawakamata watu wasiyohusika sisi kama wanahabari ambao miongoni mwetu ni mahiri kabisa katika kuandika habari za uchunguzi ambazo zinahusu serikali, majeshi yetu na ambazo zimekuwa zikichapishwa magazetini, na baada ya kuchapishwa habari hizo taasisi hizo zimekuwa zikishindwa kuzikanusha kutoka na habari hizo kujaa ukweli.

Hivyo sisi wanahabari ni askari kasoro magandwa,na endapo vijana wako watafanya ujanjaujanja ili kutaka kufunika- kombe mwanaharu apite- tutajua na tukijua tutauanika ujanja huo kwenye vyombo vyetu vya habari .

Jambo litashusha adhi na heshima ya Jeshi la Polisi ambalo kwa muda mfupi tangu uanze kuliongoza ,limeanza kurejesha heshima na matumaini kwa jamii kwani siyo siri lilikuwa limepoteza sifa, heshima kutokana na baadhi ya askari wake waliokuwa wamekubuhu kwa rushwa,kubambikia raia kesi na wengine kujihusisha na uharifu wa kutumia silaha.

Nimalizie kwa kuwapa salamu hao mahalamia ambao wamefanikiwa kuwajeruhi mpiganaji Kubenea na Ndimara, ni hivi wapiganaji wengine bado wapo ndani na nje ya nchi licha wapiganaji hao ni wachache ukilinganisha na idadi ya mafisadi lakini tunawaakikishia kwamba tutaendelea kupigania maslahi ya walio wengi, kuandika na kusema ukweli bila kumhofia mtu yoyote kwani tuliumbwa siku moja na tutakufa siku moja.

Na rejeeni msemo huu ambao uwapa moyo wa ujasiri wapigania haki wote,unasema hivi “Makalio ya chungu hayaogopi moto kwani yakiogopa moto ugali hautaiva’.Hivyo haturidi nyuma,tunasonga mbele na wala hatuogopi vitisho vyenu na kwa tafsiri rahisi ya msemo huo, wanahabari tukiogopa kufichua uovu, jamii na serikali kwa ujumla itakwenda mlama.

Enyi mnaotuma watu kutufanyia uharamia mkae mkijua ipo siku hizo fedha zinazowatia uchizi na hayo madaraka mnayolingia ipo siku mungu atawanyang’anya atawapatia wengine.

Naamini katika dunia hii sote tunapita na tuendako atukujui na kila mtu aliyepo hapa duniani, mungu anajua amemleta kwa makusudi gani hivyo hila na ubaya ufanywao na binadamu dhidi ya binadamu wenzao ipo siku mungu atawaadhibu.

Namalizia kwa kuungana na wadau wenzangu wa habari kulaani tukio hilo .Na kuwataka wadau wa habari wenzangu kuacha ubinafsi na kutanguliza maslahi ya taifa mbele naamini tutawashinda manyang’au haulitakii mema taifa hili kwani wanatumia fedha na madaraka yao kutaka kuua uhuru wa habari ambapo tuna fahamu kwamba taifa ambalo uhuru wake wa habari umekufa ni taifa ambalo shughuli zake za maendeleo zinadolola.Nyie manyang’au wa Tanzania hatutaki mtufikishe huko na kamwe hatutakubali mtufikishe kwa hali yoyote ile.

Mungu ibariki Afrika, Mungu inusuru Tanzania
0755312859:katabazihappy@yahoo.com:www.katabazihappy.blogspot.com

No comments:

Powered by Blogger.