Header Ads

MEJA JENERALI MARWA:KAMANDA ALIYEONGOZA VITA YA IDI AMIN


Na Happiness Katabazi

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ndilo lenye dhamana ya kuhakikisha ulinzi na usalama wa nchi na mipaka yake.

Kwa mantiki hiyo inapotokea nchi yetu haielewani na majirani au kujitengenezea maadui wa nje, ni JWTZ lililo na jukumu zito la kuhakikisha linapambana kikamilifu dhidi ya maaduni hao.

Hii inaweza kumaanisha ama kuingia vitani kikamilifu au kufanya operesheni maalumu kwa ajili ya kutokomeza hali ya wasiwasi ili nchi isiingie katika vita kamili.Katika hili twaweza kutoa mfano jinsi JWTZ walivyofanya kazi mwaka 1978/1979 dhidi ya majeshi ya adui Idi Amin Dada wa Uganda.

JWTZ katika vita walifanya kazi iliyotukuka kiasi kwamba sitarajii itakuja kusahaulika miongoni mwa Watanzania na katika historia ya nchi hii. Naam! JWTZ walitimiza wajibu wa kuhakikisha kwamba taifa letu linakuwa usalama.

Sifa hizo kwa jeshi letu hazikuja hivi hivi, bali zililetwa na askari waliotoa maisha yao kwa ajili ya taifa letu, na miongoni mwa watu hao ni marehemu Meja Jenerali mstaafu Michael Mwita Marwa (78).

Kwa wale wanaofuatilia kwa karibu shughuli zifanywazo na JWTZ na historia ya jeshi hilo, jina hilo haliwi geni masikioni mwao.

Meja Jenerali Marwa ni mmoja wa makamanda mashuhuru wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania aliyeongoza majeshi kuteka miji ya Masaka na Entebbe wakati wa Vita ya Kagera.

Marwa maarufu kwa jina la ‘Kambale’ , wakati wa vita alikuwa mmoja wa makamanda waasisi wa kutegemewa wa JWTZ. Hivi karibuni alipelekwa Kenya na Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu kabla ya kufikwa na mauti.

Meja Jenerali Marwa atakumbukwa pamoja na wengine kwa mchango wake alioutoa wakati wa Vita ya Kagera yaani ‘Operesheni Chakaza”. Kwa nyakati tofauti aliongoza Brigedi za 207 na 208 na kutoa kipigo kikali kwa majeshi ya Idi Amin na kufanikisha kuiteka miji ya Masaka na Entebbe.

Mara baada ya Vita ya Kagera, Meja Jenerali Marwa aliteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali jeshini na serikali ikiwamo Kamanda wa Divisheni ya 20 Tabora (1979), Mkuu wa Mkoa wa Singida (1983-1993) wadhifa alioendelea nao hata baada ya kustaafu utumishi jeshini Januari 1, 1990.

Marwa aliyetumikia JWTZ kwa uadilifu mkubwa kwa miaka 36, miezi mitatu na siku 21, alizaliwa Januari 1, 1930 katika Kijiji cha Mogabiri, Wilayani Tarime, mkoani Mara. Alijiunga na jeshi la kikoloni la King’s African Rifles (KAR) mwaka 1953 baada ya kuhitimu elimu ya msingi.

Akiwa jeshini, alijiendeleza kielimu na aliteuliwa kuhudhuria kozi ya maofisa Uingereza mwaka 1962 na baada ya kuhitimu na kurejea nchini, alihudhuria kozi nyingine ikiwamo ya ukamanda wa platuni, kamanda kombania na mafunzo ya siasa katika Chuo cha Chama Kivukoni, Dar es Salaam, mwaka 1970. Pia aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Moja ya sifa ambazo Meja Jenerali Marwa ameacha jeshini ni ujenzi wa kambi na mabwalo. Alisimamia kikamilifu ujenzi wa bwalo la maofisa wa JWTZ lililopo Migombani, Zanzibar akiwa Mkuu wa Brigedi ya Nyuki. Sehemu hii hadi sasa inaitwa Kwa Marwa.

Kwa kutambua na kuthamini mchango wake katika kulinda taifa, Rais na Amiri Jeshi Mkuu alimtunukia medali nane ikiwamo medali ya Vita, Kagera, Uhuru, Jamhuri, Muungano, Miaka 20 ya JWTZ, Utumishi wa Muda Mrefu na Utumishi uliotukuka Tanzania.

Alipanda vyeo jeshini kwa ngazi akianzia na cheo cha askari. Baada ya uhuru mwaka 1961 alipewa kamisheni na kuwa Ofisa wa cheo cha Luteni Usu. Mtiririko wa kupanda vyeo kama ofisa ni kama ifuatavyo: Julai 28, 1962 alipandishwa cheo na kuwa Luteni.

Februari 1, 1964 alipandishwa cheo na kuwa Kapteni, Machi 28, 1965 alipandishwa cheo na kuwa Meja, Januari 1, 1967 na Juni 19, 1973 tarehe ambayo alikuwa akikumbuka siku yake ya kuzaliwa, alipandishwa cheo cha Luteni Kanali. Februari 12, 1974 alipandishwa tena cheo na kuwa Brigedia Jenerali.

Hakuishia hapo kwani Januari 10, 1979 alipandishwa cheo na kuwa Meja Jenerali, cheo alichodumu nacho hadi alipostaafu jeshi.

Meja Jenerali Marwa alifariki dunia Januari 7, mwaka huu, katika hospitali ya Med-Clinic Heart, Pretoria, Afrika Kusini. Mwili wake ulirejeshwa nchini Januari 9 na juzi uliagwa na mamia ya wakazi wa Dar es Salaam walioongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Makamanda wenzake wastaafu walijitokeza kutoa heshima zao za mwisho kwa mpendwa wao huyo na kisha mwili wake ulisafirishwa jana jioni kwenda kijijini kwake Mogabiri, wilayani Tarime, mkoani Mara na amezikwa leo kwa heshima zote za kijeshi.

Meja Jenerali Marwa atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa ndani na nje ya jeshi. Alionyesha njia ambayo bila shaka askari wa jeshi hili watazifuata kwa vitendo.

Bwana alitoa na Bwana alitwaa, jina la Bwana libarikiwe na upumzike kwa amani.

*0755312859
katabazihappy@yahoo.com
http://www.katabazihappy@yahoo.com/

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi,Januari 11,2007.

3 comments:

Unknown said...

Nilazima jeshi kama jeshi liheshimiwe.

Emma tall said...

R.I.P BABA

Unknown said...

R.i.p general kambale

Powered by Blogger.