Header Ads

BABU SEYA,PAPII WAKWAMA TENA



*Mahakama ya Rufaa yawatupa jela maisha
*Yawaachia huru wawili, Chichi na Mashine
*Wapunguziwa mashitaka kutoka 23 hadi 5
*Watu wahoji; nani alileta sheria duniani?

Na Happiness Katabazi

MWANAMUZI mahiri wa muziki wa dansi nchini, Nguza Viking (Babu Seya) na mwanaye Papii Kocha wameshindwa kujinasua kwenye hukumu ya kifungo cha maisha jela.

Mahakama ya Rufaa Tanzania jana ilikazia hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, lakini iliwaachia huru watoto wawili wa Babu Seya ambao ni Nguza Mbangu (Mashine) na Francis Nguza (Chichi).

Pia imeyatupilia mbali mashitaka 18 kati ya 23 yaliyokuwa yakiwakabili warufani hao kwa maelezo kuwa hayatambuliki katika sheria za nchi.

Licha ya kuwafunga wawili na kuwaachia wawili wengine, hukumu hiyo ilileta simanzi, majonzi, vilio, kwiki na huzuni miongoni mwa watu waliofurika katika maakama hiyo kusikiliza hukumu hiyo jana. Miongoni mwa makumi ya watu waliokuwa mahakamani hapo ni baadhi ya wanamuziki raia wa Kongo.

Akisoma hukumu hiyo kwa niaba ya Jaji Natalia Kimaro, Salum Massati na Mbarouk Mbarouk, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Neema Chusi alisema kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyotumika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mahakama Kuu kuwatia hatiani washitakiwa hao, warufani walikuwa wakikabiliwa na makosa 23 ya kubaka na kuwalawiti watoto kumi wa Shule ya Msingi Mashujaa ya jijini Dar es Salaam.

Alisema baada ya jopo hilo la majaji kusikiliza na kuchambua kwa kina ushahidi uliotolewa, walibaini kuwa mashitaka 18 ya kulawiti ambayo walitiwa nayo hatiani hayatambuliki kisheria nchini; wakayafuta.

“Jopo hili baada ya kuipitia sheria namba 4 ya makosa ya kujamiana ya mwaka 1998 imebaini sheria hiyo haiyatambui makosa ya kushirikiana kulawiti, bali sheria hiyo inatambua makosa ya ubakaji. Kwa sababu hiyo mahakama hii inafutia warufani mashitaka hayo 18.

“Hivyo warufani wanabakiwa na mashitaka matano ya kubaka, na kwa mujibu wa ushahidi uliokwishatolewa, jopo hili limeridhika nao, hivyo kuwatia hatiani Nguza Viking na Papi Kocha, na kuwahukumu kifugo cha maisha jela,” alisema.

Hata hivyo, Naibu Msajili alisema ushahidi huo umeshindwa kuthibitisha tuhuma dhidi ya Nguza Mashine na Francis Mbangu, hivyo mahakama inawaachia huru.

Baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Francis aliangua kilio kwa sauti ya juu kizimbani, hali iliyosababisha warufani wenzake, ndugu, jamaa na baadhi ya wananchi waliokuwa wakifuatilia kesi hiyo kukimbilia kizimbani kuungana naye kulia.

Hali hiyo ilizua simanzi kwa baadhi ya watu, huku wengine wakisikika wakijiuliza, “ni nani aliyeleta sheria duniani?”

Hata hivyo, warufani wote walichukuliwa na askari magereza na kurudishwa gerezani, ili walioachiwa wakafuate taratibu za makabidhiano na uongozi wa magereza.

Baada ya hukumu hiyo, wakili wa warufani hao, Mabere Marando, alisema mahakama hiyo ndiyo ya mwisho, hivyo fursa pekee wanayoweza kuipata ni msamaha wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa madaraka aliyopewa.

“Kwa tafsiri ya hukumu hii, tumeshinda nusu, na nusu tumeshindwa; kwani mahakama imewafutia wateja wangu mashitaka 18 kati ya 23 na iwaachia warufani wawili na kuwatia hatiani wawili.

“Kwa kweli nasema kwa niaba yao tumeipokea kwa mikono miwili hukumu hii, kwani tumeshinda nusu na nusu tumeshindwa,” alisema Marando huku akipewa mkono wa pongezi na wananchi mbalimbali.

Januari 3 mwaka huu, jopo hilo la majaji watatu likiongozwa na Natalia Kimaro lilisikiliza rufaa hiyo kwa siku moja, na mawakili wa rufani waliomba mahakama iwaachilie huru warufani hao, wakisema hukumu hiyo imejaa dosari nyingi za kisheria.

Mawakili hao, Marando na Hamidu Mbwezeleni, walidai kesi hiyo ilikuwa ni ya kupangwa na kwamba hawajawahi kuona hukumu ya hovyo ya aina hiyo tangu waanze kufanya kazi ya uwakili kwa zaidi ya miaka 30.

Januari 27 mwaka 2005, aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Thomas Mihayo ambaye kwa sasa amestaafu, alitupilia mbali rufaa yao iliyokuwa ikipinga hukumu iliyotolewa na aliyekuwa Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Addy Lyamuya aliyewatia hatiani kwa makosa 23, Juni 25 mwaka 2004.

Waomba rufani hao walikuwa wakikabiliwa na makosa 10 ya kubaka watoto wa kike wenye umri kati ya miaka sita na minane na mengine 11 ya kulawiti watoto wa kike wenye umri kama huo. Walidaiwa kutenda makosa hayo kati ya Aprili na Oktoba mwaka 2003, eneo la Sinza kwa Remmy, Dar es Salaam.

Katika kesi hiyo, Mwalimu wa Shule ya Msingi Mashujaa, Sigirinda Ligomboka, ambaye alishitakiwa kwa makosa mawili ya kumsaidia Babu Seya kutenda makosa hayo kwa kuwaruhusu baadhi ya watoto hao kutoka madarasani, aliachiwa huru na Mahakama ya Kisutu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Februali 12 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.