Header Ads

KESI YA RICHMOND HAINA MLALAMIKAJI-WAKILI

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa utetezi katika kesi ya kashfa ya Kampuni ya kuzalisha umeme ya Richmond, inayomkabili Naeema Adam Gile katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, umecharuka na kudai kuwa kitendo cha upande wa mashitaka kutokuwa na jalada la uchunguzi wa kesi hiyo kwa takriban mwaka mmoja sasa ni sawa na kesi hiyo haina mlalamikaji.


Dai hilo lilitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Waliawande Lema na wakili wa utetezi, Zakhe Katto, muda mfupi baada ya wakili wa serikali, Beatrice Mpangala kuiambia tena mahakama kwamba upande wa mashitaka hauna jalada hilo, kwani bado lipo Jeshi la Polisi.

“Mheshimiwa hakimu mara kwa mara kesi hii inakuja kutajwa na upande wa mashitaka unakuwa ukidai upelelezi haujakamilika na leo umedai hauna jalada la uchunguzi …kama upande wa mashitaka ulivyoiambia mahakama hii kwamba hauna jarada hilo, basi ni wazi kesi inayomkabili mteja wangu haina mlalamikaji,” alidai wakili Katto.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Lema, aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 21 mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na kuamuru upande wa mashitaka siku hiyo uje kuieleza mahakama hatua ya upelelezi umefikia wapi na pia waje na jalada hilo.

Gile ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea, Alex Mgongolwa na Zakhe Katto, alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Januari 14, mwaka jana, na tangu wakati huo kesi hiyo imekuwa ikiahirishwa kwa kile kinachodaiwa kutokamamilika kwa upelelezi.

Januari 14, mwaka jana , ilidaiwa mahakamani hapo na Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface kuwa mshitakiwa huyo anakabiliwa na mashitaka matano ambayo aliyatenda kwa nyakati tofauti.

Wakili Boniface alidai kuwa, Machi 13, 2006, Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa na dhamira ya kutenda kosa, alighushi hati ya nguvu ya kisheria (power of attorney) inayoonyesha imetolewa na Hamed Gile, ambaye ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, kwamba amemruhusu kufanya shughuli za kampuni hiyo hapa nchini.

Alidai kwamba, shitaka la pili ni kutoa taarifa za uongo, kuwa Machi 20 mwaka 2006, katika eneo la Ubungo, Umeme Park, Barabara ya Morogoro, mshitakiwa alitoa hati hiyo ya nguvu ya kisheria inayomuidhinisha yeye kwamba ameruhusiwa kufanya kazi ya kampuni hiyo ya Marekani hapa nchini.

Aliendelea kudai kuwa, shitaka la tatu linalomkabili mtuhumiwa huyo ni kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa umma na kwamba Julai 20, 2004 eneo la Ubungo, Umeme Park, alitoa taarifa ya uongo kwa wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Shirika la Umeme (TANESCO), kwamba Richmond LLC ya Texas, Marekani, ina uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 100 kwa Tanzania ili wajumbe wa bodi hiyo waweze kumpendekeza kupewa tenda ya kutoa huduma hiyo.

Katika shitaka la nne, Boniface alidai Juni, 2006 jijini Dar es Salaam, mshitakiwa alitoa taarifa za uongo kwa wajumbe wa timu ya majadiliano ya serikali, kuwa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, ina uwezo wa kuzalisha umeme kwa kiwango hicho ili apewe tenda hiyo.

Wakili Boniface alidai shitaka la tano ni kwamba Julai, 2006, ambapo mshitakiwa akifahamu na kwa ulaghai, alitoa hati ya nguvu ya kisheria iliyotolewa Machi 3, mwaka huo iliyokuwa ikimuonyesha kuwa ameruhusiwa na Mwenyekiti wa Kampuni ya Richmond, Hemed Gile, kufanya kazi za kampuni hiyo hapa nchini.

Gile amefikishwa mahakamani ikiwa ni takriban mwaka mmoja sasa baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kuachia ngazi baada ya Tume Teule ya Bunge kubaini kuwa alihusika katika mchakato wa utoaji zabuni kwa Richmond.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi,Februali 11 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.