Header Ads

KESI YA LIYUMBA:NAIBU GAVANA AIBUA MAMBO MAZITO

Na Happiness Katabazi

NAIBU Gavana wa Benki Kuu (BoT), Juma Reli (54), ameshindwa kuithibitishia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuhusu hasara iliyopatikana katika mradi wa ujenzi wa minara pacha kwa sababu hadi sasa ripoti ya mwisho ya matumuzi ya fedha za mradi huo haijakamilika.

Sambamba na hilo, katika hali isiyotarajiwa, upande wa mashitaka katika kesi hiyo umesema unakusudia kupunguza idadi ya mashahidi wake kutoka 15.

Naibu Gavana huyo ambaye ni shahidi wa nane wa upande wa mashitaka katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221, alitoa maelezo hayo jana mbele ya kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi, Edson Mkasimongwa, Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa baada ya wakili wa utetezi, Majura Magafu na Hudson Ndusyepo kutaka ufafanuzi.

Kesi hiyo ya matumizi mabaya katika ofisi ya umma inamkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa benki hiyo, Amatus Liyumba,.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano baina ya mawakili wa utetezi na shahidi huyo:

Wakili: Lini umeajiriwa BoT?

Shahidi: Niliteuliwa kuwa Naibu Gavana Februari 2005 na ndipo nilipoanza rasmi kufanya kazi katika BoT.

Wakili: Unajua mradi huu wa ujenzi wa minara pacha ulianza lini?

Shahidi: Sikumbuki sawa sawa.

Wakili: Utakubaliana nami kimsingi wakati unaanza kufanya kazi hapo, mradi huo ulikuwa umefikia hatua za mwisho?

Shahidi: Ni kweli mradi niliukuta katikati.

Wakili: Utakubaliana na mimi hayo mabadiliko ya nyongeza yanazolalamikiwa na upande wa mashitaka, hilo zoezi lilikuwa limeishapita?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Ni mabadiliko ya nyongeza katika mradi huo yalifanyika wakati wewe upo BoT, unayajua?

Shahidi: Mradi huo ni mkubwa, siwezi kukumbuka.

Wakili: Ni nani alikuwa na maamuzi ya mwisho ya hili lifanyike au hili lisifanyike?

Shahidi: Gavana.

Wakili: Nani alikuwa na maamuzi ya mwisho ya kuidhinisha mabadiliko ya mradi na fedha?

Shahidi: Ni bodi ya wakurugenzi ambayo mwenyekiti wake ni gavana.

Wakili: Je, mkurugenzi wa idara zozote pale BoT anaweza kutoa maamuzi bila gavana na bodi kujua?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Kuna kipindi chochote wakati mradi huu unaendelea Liyumba aliwahi kuandika maombi ambayo hayaendani na matakwa ya menejimeti?

Shahidi: Sikumbuki.

Wakili: Kuna kipindi chochote wakati wewe ukiwa Naibu Gavana, wewe binafsi na gavana mliwahi kupeleka maombi kwenye bodi yakakataliwa?

Shahidi: Hatujawahi kupeleka.

Wakili: Kwa hiyo Liyumba alikuwa anapata maelekezo ya ujenzi kutoka kwa Meneja Mradi Deogratius Kweka?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili: Kuna siku Mkurugenzi wa Fedha wa benki hiyo aliwahi kulalamikia matumizi mabaya ya fedha katika huo mradi?

Shahidi: Sikumbuki (watu wakaangua vicheko).

Wakili: Nyie kama BoT, huu mradi umeleta madhara kwenu?

Shahidi: Haujaleta madhara kabisa.

Wakili: Hadi hapa tulipofikia kuna hasara yoyote imepatikana kutokana na ujenzi wa mradi huo?

Shahidi: Siwezi kusema wala kuthibitisha hasara eti imetokea katika mradi huo kwa sababu hadi hivi sasa ninapotoa ushahidi ripoti ya mwisho ya matumizi ya fedha za ujenzi wa mradi huo ‘Finacial Account’ haijakamilika. (watu wakaangua vicheko).

Mahojiano kati ya Hakimu Mkazi na shahidi huyo yalikuwa kama ifuatavyo:

Hakimu: Shahidi kumbuka mshitakiwa (Liyumba) ameshitakiwa kwa kesi ya kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221, sasa mahakama hii tunatafuta uthibitisho wa kiasi hicho kutoka pande zote mbili za kesi hii?

Shahidi: Sipendi kudanganya ila ukweli ni kwamba hatuwezi kuthibitisha hasara kwa sababu Financial Account haijakamilika.

Hakimu: Ulisema mradi huu haukupitia kwenye menejimenti, ulipitia moja kwa moja kwenye bodi ya wakurugenzi, ieleze mahakama ulifikajefikaje kwenye bodi na ni Liyumba yeye kama yeye ndiye aliupeleka?

Shahidi: Kama nilivyokwishaeleza, gavana ana nguvu za kisheria. Jambo linaweza kutoka idara fulani akalipitisha bila ya kuwepo kwa wajumbe wengine wa bodi au menejimenti na kisheria anaruhusiwa.

Baada ya shahidi kumaliza kutoa ushahidi wake, Wakili wa Serikali, Juma Mzarau, aliiomba mahakama hiyo iahirishe kesi hiyo hadi Februari 4-5 mwaka huu, kwani wanatarajia kupunguza idadi ya mashahidi kutoka mashahidi 15.

Aliieleza mahakama kwamba kuna shahidi wanayemtegemea kutoka nchini Singapore na waliihakikishia mahakama kuwa katika siku hizo wataleta mashahidi watu wa mwisho.

Hata hivyo wakili wa utetezi, Magafu alidai upande wa mashitaka haupo makini na kazi yao na kuongeza kuwa kama watakubaliana na kesi hiyo ikiahirishwa hadi tarehe hiyo, basi uhakikishe unawaleta mashahidi hao bila kukosa, la sivyo siku hiyo wafunge kesi yao.

Aidha, Kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi, Edson Mkasimongwa, alikubaliana na ombi hilo na kwa mujibu wa ratiba ilipangwa itaanza kusikilizwa mfululizo kuanzia jana hadi Februari 5, mwaka huu.

Aidha, aliamuru upande wa utetezi upewe nakala ya mwenendo mzima wa kesi ili waweze kujiandaa kwa ajili ya kujibu hoja kama mshitakiwa ana kesi ya kujibu au la.

Liyumba alifikishwa mahakamani hapo Januari 26, mwaka jana akikabiliwa na makosa mawili ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Hadi sasa Liyumba yupo rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 27 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.