Header Ads

RAIS KIKWETE FUTA MACHOZI YA MAHAKAMA

Happiness Katabazi

“NAKUMBUKA Rais Jakaya Kikwete Mei, 2008 ulipokutana na majaji wote Bagamoyo, ulikubali kuutengea mhimili wa Mahakama mfuko wake lakini hadi leo hilo halijafanyika, tunajua kuwa nia yako bado ipo pale pale.

Lakini nakumbuka jeshini niliambiwa mjue kamanda wako, nami nathubutu kusema kuwa ninamjua kamanda wangu, hana kauli mbili, alisemalo ni sahihi atalitenda tu ni suala la muda.”
Maneno haya yalitamkwa na Jaji Mkuu Agustino Ramadhani, Februari 4 mwaka huu, katika sherehe ya Siku ya Sheria nchini ambayo huadhimishwa hapa nchini na mahakama zote, kuashiria mwanzo wa mwaka wa mahakama.

Kaulimbiu ya mwaka huu ilikuwa “Mahakama ikiwa mdau muhimu wa maendeleo katika taifa na umuhimu wa kuboresha mazingira yake ya kazi ili iweze kutoa huduma bora zaidi.”

Jaji Mkuu anasema kama kuna tatizo basi itungwe sheria au kama ipo sheria basi ifanyiwe marekebisho. Lakini hii miaka miwili na nusu ya kuwa Jaji Mkuu ameng’amua kuwa mafanikio yote ni lazima yakubiliwe na watendaji husika wa chombo hicho.

‘Wahenga wanasema penye udhia, penyeza rupia,’ hiyo ni rushwa, lakini nimetambua ili ufanikiwe lazima uelewane na watendaji ambao ndio mashine muhimu ya kutekeleza mipango yote iliyokusudiwa.

Anasema mahakama kuwa na mfuko wake ndio njia ya uhakika ya kung’oa mzizi wa fitina wa sababu zinazochelewesha utoaji wa haki kwa wakati na kuongeza kuwa suala muhimu linatakiwa kutekelezwa kwa haraka ni ujazwaji wa huo mfuko.

Anaeleza kuwa kifungu cha 16 cha Sheria ya Vyama vya Siasa, yaani The Political Parties Act, Mlango wa 258 wa sheria za Tanzania,kinasema: The Government shall...disburse up to not more than two per centum of annual recurrent budget. Na kwamba kwa mwaka huu wa fedha mahakama imepata asilimia 056 tu ya bajeti ya serikali . Lakini vyama vya siasa vimewekewa kisheria kiwango cha juu cha asilimia mbili.

“Mahakama ni mhimili ambao vyama vya siasa vyenyewe vinautegemea sana, fomu za uteuzi wa kugombea urais, ubunge na udiwani lazima zipitie mahakamani, baada ya uchaguzi mkuu kunakuwepo na kesi za kupinga matokeo.

“Nina hakika alichotuambia Bagamoyo Mei mwaka 2008, kuhusu mfumo wa Mahakama, atatupa bajeti hii, tena tunaomba ututilie walau asimilia mbili tu ya bajeti ya serikali, kwa hesabu za mwaka huu wa fedha itatakiwa kiasi cha sh bilioni 133.7 kiasi ambacho bado ni kidogo kuliko walichopewa Mkoa wa Mwanza cha sh 135,019,803,000,” anasema.

Jaji Ramadhani anaendelea kueleza kuwa hicho ndio kilio chake cha mwisho kwa rais na kwamba siku hiyo ya sheria ilikuwa siku yake ya mwisho kwani Desemba mwaka huu anang’atuka na kuongeza kuwa hilo ni hitaji la kikatiba na lazima alitii kwani Rais Amani Karume ametoa somo muhimu pamoja na kutakiwa na chama cha upinzani aendelee.

Aidha, anasema Katiba ya nchi inaiagiza Mahakama itoe haki kwa haraka lakini pia inawaruhusu kuchelewa kutoa haki kama zipo sababu za msingi.

Moja ya sababu ni ufinyu wa bajeti,kwa mwaka wa fedha wa 2009-2010 mahakama imepewa sh 37,854,397,000 (recurrent), kwa wilaya 123 za Tanzania Bara, mhimili huo upo mikoa yote 21 lakini bajeti inayopewa mikoa ni kubwa ukilinganisha na ile inayopewa mahakama na kutolea mfano kwa kipindi cha mwaka huu wa fedha na kwa current budgets, amechukua mikoa mitatu ambayo ni midogo kieneo, Mkoa wa Mtwara umepewa sh 51,691,383,000, Mkoa wa Mwanza sh 135,019,803,000 na Mkoa wa Mara umepewa sh 74,617,161,000.

“Bajeti ya Mtwara imezidi ile ya Mahakama kwa takriban sh bilioni 13, Mwanza ni kubwa zaidi ya mara tatu wakati bajeti ya Mara ni kubwa mara dufu.

“Narejea tena kusema Rais Kikwete mahakama tupo katika kila wilaya lakini tunayo bajeti ndogo kuliko mikoa yote hata ule mdogo kabisa,” anasema kwa masikitiko.

Hata hivyo anasema Mahakama inachukua hatua kadhaa kujaribu kukabiliana na upungufu huo, kwa mfano kwa upande wa Mahakama Kuu kuna mrundikano mkubwa wa kesi za jinai ambazo zinaleta kero kubwa na kufanya mahabusu katika magereza kadhaa kugoma kula.

Mradi wa Kurekebisha Sekta ya Sheria umekubali ombi lao na kuipatia Mahakama sh 831,640,000 ili kukabiliana na mrundikano wa kesi unaoendelea kukua siku hadi siku na kuzusha malalamiko yasiyoisha.

Jaji Ramadhani ambaye ni Brigedia Jenerali mstaafu, anaeleza kuwa Desemba 30 mwaka jana, alikutana na majaji wafawidhi wote 13, Naibu Mwanasheria Mkuu, Inspekta Jenerali wa Polisi, Mkurugenzi wa Mashitaka na mwakilishi wa Kamishna Mkuu wa Magereza kupanga mkakati wa kuzishughulikia kesi za jinai na namna ya kuzishughulikia hizo fedha katika hiyo miezi mitano iliyobaki kabla ya mwaka wa fedha kumalizika.

Katika kikao hicho anasema lilizuka suala la msingi, mahakama ndiyo waliopewa hizo fedha lakini wadau wengine muhimu hawakuambulia kitu, alikubali kugawana kiasi hicho ili wote wafanye kiwezekanacho badala ya kuzirejesha hizo fedha.

Kuhusu upande wa kesi za madai zinazohusiana na uchumi, anasema amekwishazungumza na Chama cha wenye mabenki nchini, zipo jumla ya kesi 261 katika kundi hilo zinazosubiri kumalizwa kusikilizwa zenye thamani ya trilioni za fedha za Kitanzania na za kigeni, chama cha wenye mabenki wamekubali kimsingi kuchangia fedha ili waweke mbinu za kuzimaliza hizo kesi haraka iwezekanavyo.

“Nimetumia unconventional ways, au kama wasemavyo kule nilipokuwa nikifanyakazi zamani, nimetumia madaraka kutafuta njia za kujikwamua, mashauri haya yanaathiri mno uchumi na maendeleo, trilioni za shilingi zimegandishwa kusubiri maamuzi ya hizi kesi, katu hatuwezi kuwa na maendeleo bila kutatua kesi hizi,” anasema Jaji Mkuu huku akionyesha kukerwa na hali hiyo.

Akiitaja sababu nyingine ni ile ya vitendea kazi hasusan zana za kitekinolojia za kisasa ambavyo vina gharama kubwa na kulipia mafunzo yake. Hata hivyo Aprili ,2008 mahakama iliingia mkataba na Investment Climate Facility for Africa ambayo Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ni Mwenyekiti Mwenza wa mfuko huo na Omari Issa ni Afisa Mtendaji Mkuu kwenye makao makuu yao hapa jijini.

Anasema ICF imeipatia Mahakama dola za Marekani 2,000,000 na kupitia fedha hizo majaji wote wa Mahakama ya Rufaa, majaji wa Mahakama Kuu wote waliopo Dar es Salaam pamoja na makatibu wamepatiwa mafunzo ya hali ya juu ya kompyuta huko ESAMI, Arusha.

Anaendelea kueleza kuwa si hivyo tu bali zimenunuliwa kompyuta za mezani 164, laptop 126, printer heavy duty 4, photocopy kubwa 6, scanner 9, server kubwa 10 na vifaa vingine na kuongeza kuwa mwaka huu wanatarajia kutiliana saini mapatano mengine ya kiasi hicho.

Jaji Ramadhani anasema wakati mwingine sheria zenyewe zinawafanya wasuesue, kwa mfano uanzishwaji wa Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kunawafanya majaji watano kushughulikia kesi zote za ardhi za nchi nzima.

Ardhi ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi yoyote duniani, kuanzia Desemba mosi mwaka jana, alitoa agizo kuwa majaji wote wa Mahakama Kuu kote nchini ni majaji wa Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi.

Anasema agizo hilo lilipokewa vyema hata na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, John Chiligati, kwani sheria imefanyiwa marekebisho kuhusu hilo. Lakini bado watakuja na mapendekezo ya kufuta hata mabaraza ya ardhi ya wilaya (District Land Tribunals) watumie mfumo wa kawaida wa mahakama.

Aliongeza kuwa kuna uhaba wa majaji, kuwa anamshukuru Rais Kikwete kwa kuteua majaji wa Mahakama Kuu wengi zaidi, katika kipindi kifupi cha miaka minne ya uongozi wake ameweza kuteua majaji 41 na anajua kuwa hivi karibuni atampatia majaji wengine kumi na atateua majaji saba wa rufaa.

Katika kipindi cha miaka minne wapo waliostaafu au kumaliza mikataba yao, jumla ya majaji wa Mahakama Kuu 14 na 11 rais aliwateua kuwa majaji wa rufaa kujazia pengo la majaji 25 waliopungua Mahakama Kuu.

Hivyo majaji 41 walioteuliwa wameziba mapengo hayo 25 na ni majaji 16 tu ndiyo wamekuwa wa ziada na kukuza idadi ya majaji, kwa upande wa mahakama ya rufaa, majaji watatu wamestaafu na mmoja amefariki, Rais Kikwete alipoingia madarakani Mahakama ya Rufaa ilikuwa na majaji 8 sasa wapo 16, ongezeko la mara mbili, hilo ni jambo la kumpongeza rais.

Aidha, anaeleza katika kukabiliana na tatizo hilo la uchache wa majaji, majaji wa rufaa kumi waliamua kukatisha likizo yao ya mwaka na wakarudi kazini ambapo Januari 11 mwaka huu, walianza kusikiliza jumla ya rufaa na maombi 83, katika hizo walimaliza kabisa mashauri 61, mashauri manane yanasubiri kutolewa maamuzi na mashauri 13 yameahirishwa kwa sababu mbalimbali.

Kwa maelezo hayo ya kina yaliyotolewa na Jaji Mkuu, binafsi napongeza hatua zote za kimaendeleo zilizochukuliwa na uongozi wa Mahakama pia nawahamasisha wananchi wa kada zote wakiwemo wanasiasa tuungane na uongozi wa Mahakama kwa hatua yake ya kuanzisha mfuko wa Mahakama, kwa kumkaba koo Rais Kikwete na serikali yake kwa ujumla ili kuhakikisha anatimiza ahadi yake ya kuuchangia fedha mfuko huo.

Ieleweke kwamba wananchi wote ni wadau wa Mahakama kwa namna moja au nyingine hivyo tutambue huo msongamano wa viporo vya kesi mahakamani unasababisha wananchi wenzetu wanaokabiliwa na kesi za jinai ambao wameshindwa kutimiza masharti ya dhamana, au dhamana zao zimefungwa, au kesi zinazowakabili hazina dhamana kwa mujibu wa sheria ni wazi wataendelea kusota rumande.

Na siyo hivyo tu, pia tukae tukijua mahakama zinaposhindwa kutoa uamuzi wa kesi hizo ni wazi wanaokabiliwa na kesi hizo wawe washitakiwa au walalamikaji kwa nafasi zao watashindwa kushiriki shughuli za uzalishaji mali kwa ajili ya kesi hizo.

Hivyo rai yangu kwa Rais Kikwete, kama wewe mwenyewe kwa kinywa chako bila shinikizo la mtu yeyote ulilidhia uanzishe mfuko wa mahakama, basi uwe mwepesi kuagiza serikali yako ichangie fedha mfuko huo, uamuzi wa kuwateua majaji wengi bila kuuwezesha mhimili wa Mahakama ili uwe na bajeti imara kwani mwisho wa siku uamuzi huo usipotekelezwa utazidisha kilio.

Wakati umefika kwa serikali yetu kuongeza fedha kwenye sekta nyingine zinazoshirikiana na mahakama ambazo zinapata fedha kidogo kwani hakuna ubishi, serikali yetu imeelekeza fedha nyingi kwenye shughuli za kisiasa.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Februali 14 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.