Header Ads

HEKO IDARA YA USALAMA WA TAIFA

Na Happiness Katabazi

KATIKA mchakato wa mageuzi ambayo yamefanyika kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, mfumo wa sheria na siasa za nchi, taasisi za dola zimejikuta zikiwa nyuma wakati vuguvugu la mageuzi likienda mbele.


Moja ya tasisisi zilizokumbwa na fukuto hilo ni Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), ambayo hapo awali, yaani chini ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Kwanza na ya Pili, ilikuwa ni taasisi ambayo haikutambulika kisheria kutokana na muundo wake kuwa wa siri na wa gizani mno.

Matokeo ya utendaji wa idara hiyo uliiletea sifa ya kuogopwa sana na kuonekana ni chombo cha majungu, chuki na wauaji wa wananchi wenye misimamo tofauti na watawala wa serikali hizo mbili zilizopita zilizoongozwa na hayati Rais Julius Kambarage Nyerere na Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.

Maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa wakiwa katika umbile la kiraia ni wanajeshi na; idara hiyo ni chombo nyeti katika uhai wa dola letu.

Ni kweli kiasili, chombo hiki hufanya kazi kwa taratibu za idara zote za usalama wa taifa na kamwe mwanasiasa hawezi kukitumia; hata hivyo mwanasiasa anaweza kumtumia ofisa wa idara hiyo kwa siri kitendo ambacho ni cha ukiukwaji wa maadili.

Nchi inapoingia kwenye matatizo, migogoro ya kisiasa, lawama kubwa huelekezwa kwa taasisi hii kwani ndiyo inayotambua, kubashiri na kutoa ushauri wa nchi inavyoweza kukabiliana na hatari zozote zile za kiusalama na kiulinzi.

Hapa Tanzania, mageuzi ya mwaka 1992 yaliyoanzisha mfumo wa vyama vingi na mabadiliko mengine ya kisheria na Katiba, yalisababisha kuundwa kisheria kwa Idara ya Usalama wa Taifa.

Kutambulika rasmi kisheria hapa nchini kulianza mwaka 1996, baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha Sheria ya Idara ya Usalama wa Taifa Na.5 ya mwaka 1996 na kutambulika rasmi kwa jina la Tanzania Intelligence and Security Services (TISS), ambapo kwa sasa idara hiyo inaongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Rashid Othman.

Cheo hicho cha Mkurugenzi Mkuu ni sawa na Mkuu wa Jeshi la Ulinzi na Kujenga Taifa (CDF), David Mwamunyange, na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema.
Kwa mujibu wa sehemu ya nne ya sheria hiyo inayounda (TISS), kazi na mamlaka iliyonayo ni kukusanya habari, kuchunguza na kutathmini habari zote zinazohatarisha usalama wa taifa na hatimaye kuishauri serikali hatua muafaka za kuchukua kwa maslahi ya taifa.

Ni wazi kwamba idara hii imechangia kwa kiasi kukubwa kudhibiti na kuzuia matendo mengi ya kihalifu ambayo yametendeka au yanayotarajia kutendeka kwa kutoa taarifa mapema kwa Jeshi la Polisi na taasisi nyingine husika ambazo mwisho wa siku ndizo zimeshiriki na kufanikisha kushindwa kwa matukio ya kihalifu.

Hivyo hatuna budi kuipongeza TISS kwa kazi nzuri wanayoifanya; haiwezi kuonekana moja kwa moja na wananchi kwa sababu moja ya miiko ya kazi zinazofanywa na idara hii ni siri.

Na idara hii imenyang’anywa mamlaka ya kukamata wahalifu kwani enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere idara hii ilikuwa na mamlaka hayo chini ya ‘Detention Order’ yaani sheria ya kumuweka mtu kizuizini.

Kwa muktadha wa majukumu hayo, idara hiyo ilitakiwa ijiunde upya kutoka kwenye giza na usiri ili ifanye kazi kama chombo cha dola chenye majukumu ya kulinda amani, usalama na demokrasia. Kwa vyovyote vile idara hiyo haiwezi kufuta mfumo wa utaratibu wake wa kufanya kazi zake kwa siri kwa kuwa hiyo ndiyo namna pekee inayowezesha kupata taarifa na habari za kiusalama.

Lakini pia katika dola ya kidemokrasia lazima chombo hiki kivae umbile la uwazi katika utendaji kazi wake ili wananchi wakijue, wajue majukumu yake na waweze kushirikiana nacho pale inapobidi.

Kwa vyovyote vile usalama wa taifa unalindwa na kusalitiwa na wananchi ambao ndiyo wenye nchi; hivyo ni bora wakajua masuala mbalimbali yanayowazunguka.

Idara hiyo isipojijengea haiba ya kupendwa na wananchi, na hasa wazalendo, mwisho wa siku itajikuta inashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kwa urahisi zaidi.

Hivi sasa lawama nyingi zinahusu kuibwa au kuporwa kwa rasilimali za nchi kunakodaiwa kufanywa na matapeli kwa kushirikiana na baadhi ya wawekezaji. Idara hii inaelekezewa lawama hizo, kuhujumiwa kwa uchumi wa nchi, kuuzwa kwa mashirika ya umma kwa bei chee na sasa mikataba mibovu mbalimbali ambayo dola imeingia na wawekezaji lazima ielekezwe kwenye idara hii. Kwa vyovyote vile kashfa ya ufisadi wa BoT, EPA na ombwe la viongozi bora lazima shutuma zielekezwe kwenye idara hii.

Kumbe basi wajibu wake si kama ilivyosadikiwa hapo zamani; yaani kuwa kazi kubwa ya maofisa wa idara hii ni kubeba mikoba ya viongozi, kuwatayarishia malazi salama viongozi pindi wanaposafiri, kuwakuwadia mabibi viongozi, kuhesabu vizibo kwenye mabaa, majungu, chuki dhidi ya wananchi na viongozi wao.

Kwa hiyo tunapojikuta leo tuna mgogoro wa kisiasa katika vyama vya siasa vya ushindani vikiwa vimehujumiwa visifanye kazi, makundi yanayohasimiana kuibuka ndani ya CCM, ufisadi wa kupindukia mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika, ni mambo yanayowaelemea maofisa wetu wa idara yetu ya usalama.

Kwa vyovyote vile mbeba lawama wa mwisho ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Yeye ndiye anamteua Mkurugenzi Mkuu wa idara hiyo. Idara hiyo nyeti isipofanya kazi vizuri rais atayumba, ataboronga na dola kwa ujumla itaonekana ni ya hovyo ndani na nje ya nchi.

Wananchi wanailalamikia dola kwamba inawanyanyasa na kuminya haki zao bila fidia ya kutosha. Hii inatoa tahadhari kwamba malalamiko hayo yanatokana na utendaji usioridhisha wa idara hiyo.

Natoa wito kwa viongozi wa idara hii kuamka na kushika nafasi kikamilifu kwenye kazi hiyo nyeti ya usalama kwa maslahi ya taifa letu bila kuyumbishwa na wanasiasa manyang’au na wachumia tumbo.

Hatujasikia idara hii kukosa uwezo au vitendea kazi; kwa hiyo haya mambo madogo madogo yanayotishia usalama wa nchi, hayawezi kutolewa visingizio kwamba haijawezeshwa.

Hivi sasa nchi yetu imekuwa na uhuru mkubwa zaidi wa kutoa maoni ambapo wananchi wamekuwa wakijadili kashfa mbalimbali hadharani kila zinapoibuka pasi mtu kukamatwa, kuwekwa mbaroni na kuteswa; tunaamini Idara ya Usalama wa Taifa inafanya kazi yake kwa maadili yanayostahili. Kwa hili tunaipa heko.

Nchi nyingine maofisa wa idara kama hii hawajaenda shule vizuri na wala hawajui maadili ya kazi zao.

Watanzania wengi wangeishia kuumia na kuteswa kwenye majumba ya siri yenye giza, nge na kila aina ya mateso.

Tunasema haya kwa sababu tunajua yanayoendelea kufanywa na idara kama hii katika nchi nyingi za Afrika.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Januari 24 mwaka 2010

5 comments:

Anonymous said...

Happy,
Hongera tena kwa kazi nzuri.Makala hii pamoja na nyingi ulizokwisha kuziandika, ni uthibitisho tosha kwamba wewe ni mzalendo wa kweli na unalitakia mema taifa lako. Hakika unafanya likupasalo, ni heri wahusika wakikusikia na wakatenda sawasawa na yatakiwayo. Keep it up

Anonymous said...

nashukuru,kwa kuandika kuhusu hii idara,pamoja ni kitengo cha siri lakni utendaji wake hakidhi mahitaji ya nchi.zaidi inatumika kama jukumu na a tool kwa viongoz wa chama tawala na mambo mengi ya siri ambayo siwezi sema.
kwa ufupi,TISS inahitaji kubadilika na kuleta ORDER ndani ya nchi,kutoinglia au lufavour chama chochote cha siasa.
hichi ni chombo muhimu sana,angalia hata katika serikali za nchi zinazoendela.
kuna haja ya kufanya kazi zaid TISS.
Ni hivo tu.

Anonymous said...

http://katabazihappy.blogspot.com/2008/02/idara-ya-usalama-wa-taifa-ni-sehemu-ya.html

Anonymous said...

Usalama wa taifa unaegemea matakwa ya watu binafsi

Info@tiss.go.tz said...

Vizuri sana umeelezea tunashukuru kwa kuekeza maekezo mazuri

Powered by Blogger.