Header Ads

MAOFISA ELIMU KORTINI KWA WIZI


Na Happiness Katabazi

MAKAIMU Afisa elimu wa Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam wakikabiliwa na makosa ya matumizi mabaya ya madaraka ya kuibia serikali jumla ya shilingi milioni11.8.

Mawakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Alen Kasamala na Sophia Gula mbele ya Hakimu Mkazi Agnes Mchome waliwataja washitakiwa hao kuwa Clara Nyongeja, Elizabeth Thomas,Mercy Nyalusi,Simon Pilla na Joseph Kaika.

Wakili Kasamala alidai kosa la kwanza la matumizi mabaya ya madaraka ni kinyume cha kifungu cha 31 cha Sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 ambapo linawakabili washitakiwa wote  katika ya Februali  mwaka 2010, Dar es Salaam mshitakiwa wa kwanza akiwa   ni mwajiriwa  wa Wizara ya Fedha  kama mtaalamu wa Kompyuta,mshitakiwa wa pili,tatu na tano wakiwa ni waajiriwa makaimu afisa elimu wa manispaa ya Ilala,mhasibu wakati akitekeleza majukumu yake kwa makusudi walitumia madaraka yao vibaya  kwa kushindwa kusimamia na kukagua  nyaraka za malimbikizo ya mishahara za walimu wa  23 wa Manispaa ya Ilala ambazo nyaraka hizo ziliwasilishwa na walimu hao kwa washitakiwa hao yenye thamani ya shilingi 11,825,000 na kisha kumlipa malimbikizo hayo  Simon Pilla ambaye ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya MSingi ya Juhudi na Ukonga.

Kasamala alidai shitaka la pili ni la matumizi mabaya ya madaraka ambalo linamkabili Simon Pilla kuwa Machi mosi mwaka 2010 katika Shule ya Juhudi  akiwa ni mwajiriwa  wa manispaa ya Ilala alitumia madaraka yake vibaya kwa kumlazimisha George Masinde  ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi UKonga  kuwamchia yeye malimbikizo ya mishahara anayodai  ambayo ni sh 3,900,000.

Aidha katika shitaka la nne linamkabili tena Pilla kuwa Machi 2 mwaka 2010 katika shule ya msingi Juhudi akiwa ni mwalimu mkuu wa shule hiyo  alimlazimisha Bahati Said  mwalimu wa shule ya ya msingi Ukonga  kuwamchia  yeye hayo malimbikizo hayo anayoyadai sh. 3,895,000 kwaajili ya kujinufaisha yeye na fedha hizo.

Wakili huyo alidai shitaka la nne ni la matumizi mabaya ya madaraka  ambalo linamkabili tena Pilla  ambapo Machi 2 mwaka 2010 katika shule ya Juhudi  akiwa ni mwalimu mkuu wa shule hiyo  alimlazimisha Ester Mdachi  ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi Ukonga kuwamchia yeye malimbiko ya mishahara anayodai ili yaweze kumnufaisha yeye mshitakiwa ambayo ni shilingi 4,030,000.

Na kwamba shitaka la tano ni la matumuzi mabaya ya madataka ambapo Machi 3 mwaka 2010 alimlamizisha Mwaija Chowo kuwachia yeye malimbikizo ya mishahara anayodai ambayo ni sh 3,000,000 ili yaweze kumnufaisha mshitakiwa huyo.

Wakili huyo wa serikali alidai shitaka la sita ni la wizi ambapo Pilla ,Machi 3 mwaka 2010  akiwa ni mwalimu Mkuu wa shule ya Juhudi na mwajiriwa  wa manispaa ya wilaya ya Ilala alimwibia mwajiri wake jumla ya shilingi 11,825,000.

Wakili Kasamala alidai kosa la saba ambalo ni mbadala wa kosa la sita ambalo alipokea fedha za rushwa Machi 3 mwaka 2010 akiwa ni mwalimu Mkuu wa Shule ya Juhudi ,shilingi 3,000,00 kutoka kwa Mwaija Chowo mwalimuwa shule ya msingi Ukonga ili asichukuliwe hatua za kinidhamu   kwakuwa Mwaija alikuwa akikabiliwa na kosa la kushindwa kumpatia malimbikizo ya mshahara na kuongeza upelelezi wa kesi hiyo umekamilika .

Washitakiwa walikana mashitaka na hakimu Mchome alisema ili washitakiwa wapate dhamana ni lazima kila mmoja asaini bondi ya shingi milioni  tano na hakimu huyo akatoa hati ya kuitwa maakamani kwa mshitakiwa wa pili na watatu (Thomas na Nyalusi) ambao hawakuwepo mahakamani hapo na akaiarisha kesi hiyo hadi Oktoba 24 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa na washitakiwa wote walitimiza masharti ya dhamana.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Oktoba 12 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.