RAIS MWINYI APANDA KIZIMBANI KUTOA USHAHIDI KATIKA KESI YA KUIBIWA SH.MIL 37
Na Happiness Katabazi
RAIS mstaafu wa awamu ya pili, Ally Hassan Mwinyi amefuata
nyayo za Rais wa awamu ya tatu,Benjamin Mkapa kwa kufika katika Mahakama ya
Hakimu MKazi Kisutu Dar es Salaam, na kupanda kizimbani na kutoa ushahidi
katika kesi za jinai zilizofunguliwa mahakamani hapo na Mkurugenzi wa Mashitaka
nchini(DPP), Dk.Eliezer Feleshi dhidi ya washitakiwa wa kesi hizo za jinai.
Rais Mwinyi jana alitua katika mahakama hiyo huku
akiongozwa na maofisa Usalama wa Taifa(TISS)
kuja kutoa ushahidi katika kesi ya jinai Na. 201/2012 iliyofunguliwa na
upande wa Jamhuri dhidi ya wakala wa Mwinyi Abdallah Nassoro Mzombe(39),mbele ya Hakimu Mkazi Genivitus
Dudu ambapo mshitakiwa huyo ambaye ni
Mfanyabiashara na mkazi wa Kinondoni
Mkwajuni anashitakiwa kwa makosa ya kumuibia Rais Mwinyi Sh. 37,440,000 zikiwa ni
kodi ya pango katika nyumba mbili
zinazomilikiwa na rais huyo mstaafu.
Kabla ya Mwinyi kuanza kwa kesi hiyo jana, rais huyo
mstaafu alipelekwa kna kuifadhiwa kwa muda kwenye chumba namba moja cha
mahakama hiyo kwaajili wakili wa serikali Charles Anindo kumuandaa kiongozi huyo kutoa
ushahidi huo na wakati huo huo maafisa
wanne wa usalama wa taifa walikuwa wakifanya dolia kali ndani na nje ya chumba
hicho alichokuwa ameifadhiwa kiongozi huyo.
Ilipofika saa 5:05 asubuhi, askari mmoja wa jeshi la
Magereza alimtoa mshitakiwa Zombe katika mahabusu ya mahakama hiyo na kisha
kumpandisha kizimbani kwaajili ya kesi yake kuanza kusikilizwa.
Baada ya mshtakiwa huyo kupandishwa kizimbani na askari
huyo wa Jeshi la Magereza, waandishi wa habari za mahakamani tuliokuwepo
mahakamani hapo nao walijiandaa kuingia katika chumba cha kuendeshea kesi hiyo
ili waweze kusikiliza kesi hiyo, lakini waandishi hao walipowakaribia
maofisa usalama hao ,wanausalama hao waliwazuia kuingia ndani ya chumba cha kusikilizia kesi hiyo na wanausalama hao wakawahoji wanahabari hao
kuwa wao ni wakinanani?
Miongoni mwa maofisa usalama hao ,mmoja wao aliwauliza
waandishi wa habari kuwa wanakwenda wapi?
Waandishi wa habari: Tunataka kuingia kwenye hicho chumba
kusikiliza kesi hiyo ya mshitakiwa anayedaiwa kumibia rais Mwinyi.
Afisa usalama: Nyie ni wakina nani?
Jibu : Waandishi wa habari za mahakamani.
Afisa usalama: mmeambiwa kuna mahakama humu?
Jibu: Ndiyo hiyo ni mahakama.
Baada ya waandishi wa habari kumjibu hiyo,
afisa huyo wa usalama alinyoosha mkono na kuzuia waandishi kuingia kwenye mahakama hiyo. “Msiingie humu
ndani haiwahusu”. Baada ya kuambiwa hivyo na mwanausala huyo
ilitubidi tukaa nje hadi saa 6:21 mchana
na muda huo ndiyo kesi hiyo ilipamalizika kusikilizwa na tukamuona rais Mwinyi akitoka ndani ya chumba hicho na
kuongozwa na maafisa usalama hao kwenda nje ya mahakama hiyo na kisha kupanda gari
aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili T 914 BJT na kisha kuondoka katika
viwanja vya mahakama hiyo.
Licha ya jitihada hizo za wanausalama kuzuia waandishi wa
habari za mahakama kuingia ndani ya chumba cha mahakama kusikiliza ushahidi
uliokuwa ukitolewa na rais Mwinyi, lakini waandishi hao nao walitumia mbinu zao
na wakafanikiwa kupata hati ya mashitaka ya kesi hiyo ambayo ilifunguliwa
mahakamani hapo Agosti 21 mwaka huu, na
waandishi wa habari za mahakamani kwa kipindi chote hicho hawakuwa wakifahamu
kuna kesi ya aina hiyo ilikuwa imefunguliwa mahakamani hapo.
Kwa mujibu wa hati hiyo ya mashitaka ambayo waandishi wa
habari za mahakama walifanikiwa kuipata mahakamani hapo jana ,upande wa Jamhuri
unadai Mzombe anadaiwa kufanya makosa
hayo kinyume na kifungu cha 258 na 273 (b) (e) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu
ya Sura ya 16 ya mwaka 2002.
Siku hiyo ya Agosti 21 mwaka huu, ilidaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, mwaka 2011 na Julai 2012
huko Mikocheni , Mzombe akiwa Wakala wa rais huyo mstaafu,
alimwibia Sh 17,640,000 ambazo ni pato la kodi ya nyumba yake
iliyopo eneo la Mikocheni wilaya ya Kinondoni.
Iliendelea kudai kuwa kiasi hicho cha fedha ambacho Mzombe
alimwibia rais Mwinyi kilikuwa ni kodi ya pango la nyumba namba 481,
iliyopo kwenye ploti A ,huko Mikocheni ya mwaka 2011/2012 na 2012/2013.
Aidha Mbali anadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, mwaka
2011 na Julai 10, mwaka huu huko Msasani Village wilaya ya Kinondoni,
mshtakiwa huyo alimwibia tena rais huyo mstaafu Sh 19,800,000
ambayo ilikuwa ni kodi ya nyumba namba 55 iliyopo kwenye Kitalu C .
Iliongezwa kudaiwa kuwa kiasi hicho cha fedha kilikuwa ni
kodi ya pango la nyumba hiyo la mwaka 2011/2012 na 2012/2013, hata hivyo
mshitakiwa huyo alikana mashitaka yote
na yupo rumande hadi oktoba 22 mwaka,itakapokuja kuendelea kusikilizwa.
Itakumbukwa kuwa Mei 7 mwaka Rais Mkapa
alifika mbele ya Hakimu Mfawidhi wa
mahakama ya Kisutu, Elvin Mugeta m
katika kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania
nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Grace Martin kutoa ushahidi katika kesi
hiyo ambapo alikuwa alikuwa ni shahidi wa Mahalu ambapo Agosti 9 mwaka huu, Hakimu Mugeta
alitoa hukumu ya kesi hiyo ya kihistoria na kuwaachiria huru washitakiwa wote
kwa madai kuwa upande wa jamhuri wameleta ushahidi dhahifu ambao umeshindwa
kuishawishi mahakama imtie hatiani Mahalu na Grace.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Oktoba 10 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment