Header Ads

SHEIKH PONDA KORTINI KWA UCHOCHEZI,WIZI

*DPP AFUNGA DHAMANA YA SHEIKH PONDA
Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu(T), Sheikh Issa Ponda na wafuasi wake 49 jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam chini ya ulinzi mkali wa wanausalama kwa kosa la uchochezi na wizi wa malighafi zenye thamani ya Shilingi milioni 59.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP),Dk.Eliezer Feleshi aliwasilishwa mahakamani hapo hati ya kuzuia Ponda asipewe dhamana chini ya kifungu cha 84(4) cha Sheria ya Mwenendo wa  Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, ambapo kifungi hicho kinampa mamlaka DPP kufunga dhamana kwa mshtakiwa anayekabiliwa na makosa yanayodhaminika na  mahakama inakuwa imefungwa mikono hivyo mahakama inakuwa haina mamlaka ya kuipinga hati hiyo ya DPP hadi pale siku DPP atakapojisikia kuiondoa mahakamani hati hiyo.

Washitakiwa hao 50 ambao wanawake ni 12 na wanaume ni 40 wakati mshitakiwa wa nne ni mwanamke aitwaye Zaida Yusuf mwenye umri wa miaka 100, na wanatetewa na wakili wa kujitegemea Nassor Mansoor ambao wakati wanaingizwa na kuondoka kwenye viwanja vya mahakama hiyo ndani ya magari ya polisi na jeshi la Magereza  walikuwa wakisikika wakipaza sauti wakisema ‘Allah akbar, Allah akbar’.

Askari wa Jeshi la Polisi wakiwa wamevalia kombati huku wakiwa wamebeba silaha nzito na makachero wengine wakiwa wamevalia nguo za kiraia walianza kutanda ndani na nje ya viwanja hivyo tangu asubuhi na walifikisha mahakamani hapo washitakiwa hao kwa awamu mbili tofauti.

Awamu ya kwanza ilikuwa ni ya msafara wa magari matatu  aina ya Defenda lenye namba za usajili PF 2118 na Z 442 BZ lilokuwa limebeba askari wa doria na Karandinga   aina ya Layland lenye namba za usajili STH 2508  ambalo gari hilo lilikuwa limewabeba washitakiwa wake kwa waume 49 ambao walikuwa wamevalia baibu,na baadhi ya wanaume walikuwa wamevalia kanzu na vilemba kichwani maarufu kama ‘haghal’ wengine zikiwa zimechanika na wengine wakionekana kushindwa kutembea kwasababu ya majeraha waliyokuwa nayo miguuni na wengine walionekana kushindwa kukaa kwa muda mrefu kwenye viti vya mahakama hiyo na hivyo kukaa chini ya sakafu ambao uliwasili mahakamani hapo saa 5:16 asubuhi na kupelekwa moja kwa moja kuketi katika ukumbi namba moja wa mahakama hiyo.

Kisha msafara wa pili ambao ulikuwa na magari manne yenye namba za usajili PT 0886 gari lilobeba maji ya kuwasha  ambalo ambapo katika msafara huu ndiyo uliwasili mahakamani hapo na mshitakiwa wa kwanza Ponda  saa 6:23 mchana chini ya ulinzi mkali wa makachero zaidi 20 na kisha kumpitisha mlango wa nyuma ya mahakama hiyo na kumuingiza haraka ndani ya ukumbi namba moja wa mahakama kwenda kuunganishwa na washitakiwa wenzie ambao waliketi ndani ya chumba hicho mapema tayari kwaajili kuanza kusomewa mashitaka yao.

Hakimu Mkazi Stewart Sanga alivyoingia ndani ukumbi huo wa mahakama na kuketi katika keti chake kabla ya mawakili kuanza kuzungumza chochote alianza kwa kusema kesi hiyo mpya namba 245/2012 kuwa yeye siye hakimu aliyepangwa kusikiliza kesi hiyo,uongozi wa mahakama hiyo umempanga Hakimu Mkazi Victoria Nongwa kusikiliza kesi hiyo na kwamba hakimu Nongwa yupo kwenye semina hivyo ana udhuru na alivyomaliza kusema maneno hayo alimtaka  Wakili Mwandamizi wa Serikali Tumaini Kweka na Zeberi Mkakatu kuanza kuwasomea mashitaka washitakiwa hao.

Wakili Kweka  alianza kueleza kuwa Sheikh  Ponda peke yake anakabiliwa na makosa matano isipokuwa washitakiwa wenzake 49 ambao wanakabiliwa na makosa manne ambayo makosa yote yanadhaminika kwa mujibu wa sheria.

Alidai shitaka la kwanza ni la kula njama kinyume na kifungu 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2012,kwamba Oktoba 12 mwaka huu, huko eneo la Chang’ombe Markasi washitakiwa wote walikula  kwa nia ya kutenda kosa hilo.

Wakili Kweka alidai shitaka la pili ni kwaajili ya washitakiwa wote  ambalo ni la kuingia kwa nguvu  kwa nia ya kutenda kosa  kinyume na kiufungu cha 85 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu  na kwamba  Oktoba 12 mwaka huu,  huko Chang’ombe  Markasi , kwa jinai  wasipokuwa na sababu  za msingi  washitakiwa hao waliingia  kwenye kiwanja kinachomilikiwa kampuni ya AgriTanzania  Ltd  kwania ya kujimilikisha  kiwanja hicho isivyo halali.

Kabla ya washitakiwa hakubali au kataa shitala hilo Ponda aliripoka na kusema yeye anakanusha shitaka hilo na kwamba washitakiwa wenzake nao wanalikanusha shitaka hilo,jambo ambalo lilikataliwa na Hakimu Sanga ambaye alimrisha kila mshitakiwa ajibu shitaka hilo kwa kinywa chake ambapo kila mshitakiwa kwa kinywa chake alikanusha shitaka hilo kinyume na alivyokuwa anataka Ponda iwe kwa yeye kukanusha shitaka hilo kwa niaba ya wenzake.

Wakili Kweka alilitaja shitaka la tatu kuwa ni  kujimilikisha  kiwanja kwa jinai kinyume na kifungu cha 86 na 35 cha sheria hiyo  na kwamba kati ya Oktoba 12-16 mwaka huu huko Chang’ambe  Markasi  pasipo na uhalali wowote washitakiwa wote  katika hali  iliyokuwa ikipelekea  uvunjifu wa amani  walijimilikisha  kwa nguvu ardhi  ya  kampuni ya Agritanza Ltd.

Shitaka la nne, wakili Kweka alidai ni la wizi  ambalo ni kinyume na kifungu cha 258  cha sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, na kuwa kati ya Oktoba 12-16 mwaka huu,  washitakiwa hao waliiba vifaa na malighafi,matofali 1500,nondo,Tani 36 za Kokoto vitu vyote hivyo vikiwa na thamani ya Sh 59,650,000 mali ya kampuni ya Agritanza Ltd.

Aidha shitaka la tano Kweka alidai ni la uchochezi ambalo linamkabili Sheikh Ponda peke yake  ambalo ni kinyume na kifungu cha 390 na 35 cha sheria hiyo  kwamba kati ya Oktoba 12-16 mwaka huu katika eneo hilo la Chang’ombe Markasi  kwa maelezo kuwa yeye ni Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu(T) aliwashawishi  wafuasi wake ambao ni washitakiwa hao  kutenda makosa hayo  na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

“Mheshimiwa hakimu pamoja na kuwasomea mashitaka hayo ambayo yanadhamana kwa mujibu wa sheria, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk.Elizer Feleshi kwa mkono wake amenituma kuwasilisha kwaniaba yake mahakamani hapo hati ya kufunga dhamana kwa mshitakiwa wa kwanza (Ponda) peke yake chini ya kifungu cha  148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2012’alidai wakili Kweka.

Kwa upande wake wakili wa shitakiwa hao Mansoor alidai anashangazwa na DPP-Dk.Feleshi kuwawasilisha hati hiyo ya kumfungia Ponda dhamana wakati dhamana ni haki ya Kikatiba na kwamba hati hiyo ya DPP imetaja sababu mbili ambazo ni mosi kwaajili ya usalama na sababu ya pili ni maslahi ya jamhuri.Nakuongeza kuwa sababu hizo hazijafafanuliwa kwa mabana na kudai kuwa washitakiwa wameishakaa kwa muda mrefu rumande na kwamba mshitakiwa wanne ni mwanamke mwenye umri wa 100 hivyo anaomba wapatiwe dhamana.

Akijibu hoja hizo wakili wa serikali Kweka alidai anashangazwa na hoja za wakili washitakiwa za kuikosoa hati hiyo iliyowasilishwa na DPP kwasababu kifungu cha 184(4) cha Sheria Makosa ya Jinai, kinasomeka wazi kuwa hati hiyo ya DPP  hata mahakama haiwezi kuipinga na kwamba inapowasilishwa mahakamani hati hiyo mahakama inakuwa imefungwa mikono  na kwamba mwenye mamlaka ya kuiondoa makamani hapo ni DPP mwenyewe siku atapoona inafahaa kuiondoa na sivinginevyo.

Hata hivyo hakimu Sanga alisema hivi baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili; “Kama nilivyokwisha sema tangu awali naingia kuanza kusikiliza kesi hii kuwa mimi siyo hakimu niliyepangwa kusikiliza kesi hii ,aliyepangwa kusikiliza kesi hii ni Hakimu Victoria Nongwa ambaye yupo kwenye semina  kwahiyo endapo pande zote mbili katika kesi hii mnataka kuwasilisha hoja zenu msubirini Hakimu Nongwa akimaliza semina yake mje muwasilishe hoja hizo mbele yake”alisema Hakimu Sanga.

Hata hivyo wakili washitakiwa Mansoor alionekana kutoridhishwa na jibu hilo aliinuka na kumuomba hakimu Sanga aiarishe kesi hiyo hadi leo ili washitakiwa 49 waletwe leo kwaajili ya kupatiwa dhamana kwasababu makosa yao yanadhamana lakini hakimu Sanga alisema haitawezekana kwasababu Hakimu Nongwa bado yupo kwenye semina na leo hatakuwepo mahakamani hapo na hivyo akaamuru washitakiwa hao warejeshwe rumande hadi Novemba mosi,kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya kutajwa.

Baada ya  kesi hiyo kumaliza wanausalama walikuwa wamejazana kwa mtindo tofauti ndani ya ukumbi huo wa mahakama waliwataka waandishi wa habari na watu wengine watoke nje na ndani wabaki washitakiwa peke yake na wanausalama na kisha wakatolea mlango wa nyuma washitakiwa hao na kisha kwenye kuwapakiza kwenye mabasi ya Jeshi la Magereza, Karandika na Defenda tayari kwaajili ya kuanza safari ya kupeleka gerezani  ambapo magari ya askari wa usalama Barabarani walilazimika kuifunga barabara iliyopakana na mahakama hiyo kwa muda kwaajili ya kuruhusu msafara wa zaidi ya magari saba yaliyokuwa yamebeba washitakiwa hao,wanausalama kuelekea gerezani.

Baadhi ya watu waliofika mahakamani hapo kusikiliza kesi hiyo ,walizungumza na gazeti hili walisema wamefurahishwa na hatua ya serikali ya kuwafikisha washitakiwa hao mahakamani kwani Tanzania ni nchi inayoongozwa kwa Sheria na Katiba ya nchi na siyo sheria za dini ya Kiisilamu.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Oktoba 19 mwaka 2012.

1 comment:

Anonymous said...

When I originally commented I clicked the "Notify me when new comments are added" checkbox and now each time a comment is added I get three e-mails with the same comment.
Is there any way you can remove people from that service?
Thanks!

Check out my web page: home cellulite treatment

Powered by Blogger.