ALIYEKUWA MKURUGENZI WILAYA YA ILALA ASHINDA KESI
ALIYEKUWA MKURUGENZI ILALA ASHINDA KESI
Na Happiness Katabazi
HATIMAYE Mahakama ya Wilaya ya Ilala Dar es Salaam, imemuachia huru aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilala, John Lubuva na wenzake wanne waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 1.7.
Mbali na Lubuva washtakiwa wengine ni Mhandisi Mkuu wa Idara ya Maji, Idd Kisisa, Mkuu wa Idara ya Sheria na Ulinzi, Anderson Msumba na Mwanasheria Andrew Kanonyele.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi, Juma Hassan alisema kuwa upande wa mashtaka ambao ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), umeshindwa kutoa vielelezo vinavyoonyesha ni kwa jinsi gani ubomoaji wa nyumba zilizopo Tabata Dampo ulikuwa ni kinyume cha sheria.
Alidai kuwa Lubuva na wenzake walikuwa na kibali kinachoruhusu bomoabomoa ya eneo hilo kwani walitekeleza agizo la Mahakama ya Ardhi iliyotaka wakazi hao wahame katika eneo hilo kwani walikuwa wanaishi kinyume na sheria.
“Pamoja na upande wa mashtaka kuleta malalamiko ya watu walionewa lakini hakuna mlalamikaji hata mmoja aliyekuja kuthibitisha kuhusu madai ya uvunjwaji wa nyumba zao kama wameonewa,” alisema Hakimu Juma.
Alisema kuwa pamoja na kwamba wakazi 88 wa eneo hilo walilipwa fidia ya Sh milioni 20 kila mmoja licha ya kuwa kila nyumba ilikuwa na thamani yake, fedha hizo zililipwa kimakosa kwani hawakuwa na hati inayoonesha umiliki halali wa eneo hilo.
Mkurugenzi Lubuva na wenzake walikuwa wanakabilikwa na shtaka la kubomoabomoa nyumba za wakazi wa eneo la Tabata Dampo kinyume na sheria pamoja na kutumia vibaya madaraka yao, kula njama na kuisababishia hasara Serikali.
Washtakiwa kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani Julai, 2011, wakidaiwa kuwa Februari 28, 2008, walikula njama na kutenda kosa la kuvunja nyumba za makazi ya watu katika kiwanja namba 52 kilichopo Barabara ya Mandela, eneo la Tabata, Dar es Salaam.
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne , Julai 2 Mwaka 2014.
No comments:
Post a Comment