Header Ads

KWANINI WATU WANAHAMA VYAMA?

Na Happiness Katabazi

KILA penye nguvu hasi, pana nguvu chanya, kwa hiyo kila penye mrisho pana mrejesho.

Ukiweka nadharia hiyo ya kisayansi katika suala la watu kuhama kwenye vyama vyao vya siasa, ni dhahiri kwamba kama kuna watu watahama CCM kwenda vyama vya upinzani, basi ni lazima kutakuwepo na watu kuhama vyama vya upinzani kwenda CCM.

Leo nazitaja sababu ambazo nimezigawa kwenye makundi matatu ambayo binafsi naamini yamekuwa yakisababisha watu kuhama CCM kwenda kujiunga na vyama vingine.

Kundi la kwanza ni waliohama CCM , waliona kule hapatoshi, hapafai au hapawawezeshi kufanya mambo au mabadiliko waliyotaka kwa masilahi ya nchi yao.

Kundi la pili ni kwa sababu watu hao walishindwa kutekeleza misingi, malengo na nidhamu ndani ya CCM, kwa hiyo chama hicho tawala kikawatema na wao wakaona kwa sababu wametemwa, wakaamua kujiunga na upinzani.

Kundi la tatu, ni walioona kuwa walipokuwa CCM hawakuwa na fursa au matumaini ya kujiendeleza kimasilahi au kupanda juu kisiasa.
Sasa makundi hayo matatu yapo kwenye vyama vya upinzani kuelekea CCM.

Kwenye vyama vya upinzani kuna jambo la ziada kwamba kwenda CCM ni fursa mpya ya wao kupanda juu au kujineemesha kimasilahi, kwa kuwa ukiondoka upinzani na kwenda CCM, utaridhisha wale walio chama tawala kwamba wameweza kubomoa upinzani.

Ikumbukwe mtu akitoka CCM kwenda kujiunga na upinzani, sifa ni wapinzani wameweza kuibomoa CCM. Ebu tujiulize pande hizi mbili kifikra ziko sawa?

Si sawa kwa sababu mwanasiasa ni mtumishi na utumishi huo utatukuka tu kama utatumikia masilahi ya umma. Hivyo kundi lile la pili na la tatu, ambayo nimeyataja hapo juu, yasingekuwepo tungekuwa na kundi la kwanza, basi.

Lakini ukweli ulio wazi, hivi sasa watu wanahama vyama kwa sababu ya dhiki zao walizoamua kuzifungulia feni, ukosefu wa nidhamu, ubinafsi, ulafi wa madaraka, yaani mtu anataka miaka yote awe kiongozi, siku akikosa uongozi anahama chama.

Lakini sasa kiupembuzi, tuliangalie jambo la watu kuhama vyama kwa njia nyingine. Mtu au kikundi kinaweza kuhama na kujiunga na chama kingine ili kukiteka au kukiharibu chama wanachohamia au kukiimarisha.

Katika kuliangalia hili, tuiangalie Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inamruhusu mtu kuchagua chama anachokitaka kujiunga nacho na hakuna atakayelazimishwa kujiunga na chama asichokitaka.

Kwa hiyo, waliohama kwenye vyama vya upinzani, tunaweza kuwaweka kwenye makundi hayo matatu niliyokwisha kuyataja hapo juu kwenye makala hii.
Na ili kuthibitisha hayo makundi, rejea sababu mbalimbali walizotoa wanachama waliohama vyama vyao.

Ni mara chache mno kusikia mtu aliyehama chama na kusema sababu yake ya msingi ni kutekeleza haki yake ya kibinadamu ya kuchagua chama anachokitaka.

Dk. Masumbuko Lamwai, ambaye hivi sasa amefungiwa kufanya kazi ya uwakili na Mahakama Kuu ya Tanzania, Mei mwaka huu, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kukiuka maadili ya uwakili, enzi hizo alipokihama Chama cha NCCR –Mageuzi kwenda CCM, alisema alirubuniwa na aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho wakati huo, ambaye ni Mwenyekiti wa TLP sasa, Augustine Mrema, na atazunguka nchi nzima kubomoa mageuzi kama alivyoshiriki kuyajenga.
Na zawadi aliyopewa Dk. Lamwai muda mfupi tu baada ya kurejea kwa kishindo CCM ni ubunge wa kuteuliwa.

Aliyekuwa Mweka hazina wa NCCR-Mageuzi enzi hizo James Nyakyoma, alipohamia CCM alisema anarudi nyumbani, akimaanisha CCM, kwa kuwa kule kwa wana mageuzi kuna baridi kali. Na wengine wengi walitoa kauli tofauti.

Nitakuwa sijakosea kama nikisema kauli hiyo iliyotolewa na Dk. Masumbuko Lamwai, si ya kiungwana, kwa kuwa kauli yake hiyo inaonyesha alivyokuwa ameahidiwa ubunge na kutaka kubomoa mageuzi yaliyojengwa kwa nguvu na akili nyingi za Watanzania, ambao waliweka maisha yao rehani.

Jamii inayotuzunguka inakuwa na kasumba ya kulaumu mno, si kwa medani ya kisiasa pekee, tena bila kuangalia hali halisi ya utendaji wa kisiasa.

Kwa maana gani? Watu wanapenda kuamini kwamba kila mwanasiasa awaye chama tawala au vyama vya upinzani analipwa na serikali.

Wanapomuona mwanachama au kiongozi wa CCM wanajua analipwa, jambo ambalo si kweli. Wanamuona kiongozi wa upinzani wanajua analipwa na serikali kupitia chama chake.

Hizi ni fikra potofu ambazo hazina ukweli wowote, kwa sababu viongozi wengi wa vyama vya siasa hawalipwi mishahara na wachache tu waliopo CCM na vyama vya upinzani vinavyolipwa ruzuku ndio wanaweza kulipwa hata posho.

Ukitaka katibu wa CCM awe na maisha ya uhakika, inabidi ateuliwe kuwa mbunge ili apate mshahara na posho. Je, makatibu wa vyama vya upinzani nao mbona hawajateuliwa kuwa wabunge ili nao wawe na maisha ya uhakika?

Wananchi wengi wana fikra nyingine potofu, wanafikiri mazingira ya utendaji wa kazi za siasa ni sawa kwa vyama vyote, wanasahau kwamba kuna vyama vinavyopata ruzuku na visivyopata ruzuku.

Wanasahau kwamba ukubwa wa ruzuku unategemeana na kura na nafasi ambazo chama kinapata kwenye uchaguzi. Kwa hiyo uwezo wa chama kutumia ruzuku kuendesha shughuli za siasa utakuwa mkubwa au mdogo kutokana na ruzuku. Na chama kisicho na ruzuku hakitakuwa na uwezo wowote ule.

Wananchi wanasahau pia kuwa chama tawala kina maanisha kuwa na uwezo wa kujichotea fedha katika serikali kwa visingizio mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuanzisha makampuni ya kifisadi ambayo hupewa mikopo isiyo na dhamana na serikali na kisha kuzifilisi kampuni hizo kwa visingizio mbalimbali baada ya kufaulu kuchota mabilioni ya fedha za wananchi.

Pia wananchi wanasahau ukweli kwamba wafanyabiashara wakubwa wengi hudhamini na kufadhili chama tawala ili wapewe misamaha ya kodi, wapewe hati na serikali inayowatambulisha kwamba wana rekodi nzuri ya kulipa kodi na mizigo yao hata ikiwa ni ya magendo haitakaguliwa na wapewe tenda nono za serikali.

Kutokana na hayo yote, ni rahisi kwa chama tawala kokote duniani kurubuni na hata kununua viongozi kutoka vyama vya upinzani kwa kuwa fedha na vyeo inavyo.

Kwa ujumla viongozi wengi walio kwenye vyama vya upinzani hawana kazi, biashara zozote na pia hakuna jinsi ambavyo wanaweza kujipatia riziki yao kutokana na kazi yao ya kisiasa.

Hili ni jeshi la kujitolea, wananchi wanatizamia hawa wajitolee kwa kiwango gani na mpaka lini? Na je, wakati wa kujitolea, wao na familia zao wanaishi vipi?

Tusipofikiria hilo, siasa za upinzani Afrika lazima zianzie msituni, hiyo ndiyo njia pekee ya kuharakisha mchakato wa mageuzi ya wale walio msituni kuja kuwang’oa walio madarakani kabla ya wapinzani kudhoofu kwa njaa.

Mwandishi wa makala hii anapatika kwa simu 0755 312 859;barua pepe ;katabazihappy@yahoo.com ; na kwenye tovuti ya www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima Jumatano, Septemba 12, 2007

2 comments:

Anonymous said...

Nam! Hii ni makala makini. Imetanahabaisha mambo ambayo watu wengi tumekuwa hatuyaelewi kwa undani zaidi.

Heko Happy.... endendelea kujikita katika maeneo kama haya hususani pale unapo ona au kuhisi kuwa watanzania bado wana utando wa giza ktk ufahamu.

Maisha mema kwa wasomaji wote!

Anonymous said...

Happy makala yako imedai itatoa uchambuzi wa kisayansi lakini imeishia kutoa mawazo yako uliyonayo kichwani!

Hakuna mifano ya kanuni za siasa/nadharia za kisiasa ulmwenguni kuhusu mabadiliko au hata kanuni za sayansi kuhusu deflection and reflections as means of switching parties?!

''Kisayansi'' manake nini? na baada ya maana hiyo tueleze umefikia vipi conclusions zako?

Nasikitika hujaweza kutaja hayo.

Ningetegemea ungemtaja mwanasiasa SHAIBU AKWILOMBE alierejea CCM hivi karibuni na sababu zake ili kujua namna mwanasiasa mkongwe wa CHADEMA ana maoni gani, manake Naibu Katibu Mkuu wa chama kuhama si jambo dogo ni pigo,

Ungemzungumzia KABURU,TAMBWE HIZZA nk...

Umeishia kuendelea kupiga mbiu ya gazeti lenu la CHADEMA kuwa Lamwai hivi Lamwai vile lakini wapi,

mada yako ingefaa uipe nyama zaidi.

Hata hivyo nafurahi kuwa ni miongoni mwa wanawake mliojitokeza kwa makini kuandika mambo muhimu ya taifa, jitahidi usome vitabu zaidi ili uelimike.

CCM OYEE!!

Powered by Blogger.