Header Ads

CHENGE ATIWA HATIANI

*HUKUMU YAKE YAIBUA MASWALI

Na Happiness Katabazi

MBUNGE wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, jana alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kutozwa faini ya jumla ya sh 700,000 huku hukumu hiyo iliyotokana na makosa matatu yaliyokuwa yakimkabili ikizua maswali kwa watu wa kada mbalimbali wakiwemo wanasheria na baadhi ya watu wengine waliowahi kushtakiwa kwa makosa kama hayo.

Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni ilimtia hatiani Chenge kwa makosa matatu yaliyokuwa yakimkabili yakiwemo ya kuendesha gari kizembe na kusababisha vifo vya watu wawili: Victoria John na Beatrice Costatino.


Chenge alisababisha vifo hivyo baada ya gari alilokuwa akiliendesha kuigonga pikipiki ya miguu mitatu (Bajaj) ambayo marehemu walikuwa wamepanda.


Shtaka la tatu ni la kuendesha gari wakati bima ya gari hiyo ikiwa imekwisha muda wake. Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikana mashtaka yote.


Hukumu hiyo ambayo ilikuwa ikisubiriwa kwa shauku na wananchi wengi, ilisomwa jana saa nne asubuhi na Hakimu Mfawidhi Kwey Lusema ambaye alisema amefikia uamuzi wa kumtia hatiani mshtakiwa huyo kwa sababu upande wa Jamhuri uliweza kuthibitisha kesi yake bila kuacha mashaka yoyote.


Upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na wakili wa kujitegemea Richard Rweyongeza ambaye aliteuliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuendesha kesi hiyo akisaidiwa na wakili David Mwafwimbo.


Hakimu Lusema alisema endapo mshtakiwa huyo ataamua kutumikia adhabu ya kulipa faini, basi atapaswa kulipa faini hiyo kama ifuatavyo: 'Katika shtaka la kwanza na pili atalazimika kulipa jumla ya faini ya sh 500,000 na katika shtaka la tatu ambalo ni la kuendesha gari wakati bima yake imemalizika muda wake atalipa faini ya sh 100,000 pamoja na sh 100,000 kama faini ya uharibifu wa mali, hivyo kufanya jumla ya fidia anayotakiwa kuilipa kuwa ni sh 700,000.'
Chenge alinusurika kwenda jela baada ya kulipa sh 700,000 iliyotakiwa kama fidia kwa kuonekana na hatia kwa makosa yote hayo matatu; kiasi ambacho ni visenti tu kwake.


Kwa malipo hayo ya fidia, Hakimu Lusema alisema mshtakiwa huyo kuanzia jana yuko huru na anaweza kuendelea na shughuli zake kama kawaida.


Hata hivyo, Deus Mallya mmoja wa watu waliowahi kushtakiwa kwa makosa yanayofanana na ya Chenge, alielezea kushangazwa kwake na hukumu hiyo huku akidai kuwa mbunge huyo amependelewa kupewa fursa ya kulipa fidia.


Deus Mallya aliwahi kuhukumiwa kuendesha gari kwa uzembe na bila leseni na kusababisha kifo cha aliyekuwa mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe na kudai kwamba alihukumiwa moja kwa moja kwenda jela miaka mitatu bila kupewa fursa ya kutoa faini kama alivyopewa Chenge.


'Nchi hii ina sheria za matabaka! Wengine hawastahili kugusa mlango wa gereza na wengine ni wa kufungwa hata kwa maneno ya wanasiasa. Makosa yetu yanafanana, tena mwenzangu amekutwa na makosa matatu zaidi, mimi nilishtakiwa kwa makosa mawili lakini lilithibitika moja tu, la kuendesha gari kizembe na kusababisha kifo, kosa ambalo limo katika orodha ya makosa matatu ya Chenge. Inatia aibu, hukumu ya Chenge ni hukumu ya kishikaji,' alisema Mallya.


Aidha, baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa majina yao walihoji uhalali wa mtu kutozwa faini wakati alisababisha kifo.


Mapema mwaka jana Chenge alifikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na mashtaka hayo lakini wakati kesi ikiendelea mshtakiwa alikuwa nje kwa sababu aliweza kutimiza masharti ya dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Desemba 30 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.