Header Ads

TANZANIA YAPONGEZWA KUHESHIMU HAKI ZA BINADAMU

Na Happiness Katabazi, Arusha

SERIKALI ya Tanzania imepongezwa kwa rekodi yake nzuri ya kuheshimu haki za binadamu na kuwalinda watetezi wa haki hizo.


Hayo yamesemwa na Ofisa wa Protection Desk of Uganda, Yona Wanjala, jana wakati akifungua mafunzo ya siku tano juu ya Usalama na Utambuzi wa Mazingira Hatarishi kwa watetezi wa haki za binadamu yanayoshirikisha watetezi wa haki hizo kutoka Ethiopia, Zimbambwe na Tanzania yanafanyika mjini Arusha.

“Hakuna ubishi kwamba Tanzania ni nchi ambayo bado ina rekodi nzuri ya kuheshimu haki za binadamu na kuwalinda watetezi wa haki za binadamu ukilinganisha na nchi nyingine kama Rwanda, Uganda, Ethiopia na Somalia kwani kila kukicha tumekuwa tukisikia watetezi wa haki za binadamu wakiuawa katika nchi hizo.

“…Kwani hadi sasa serikali ya Tanzania haina rekodi ya kutumia vyombo vyake vya dola kuwanyanyasa, kuwatesa au kuwaua watetezi wa haki za binadamu ukilinganisha na nchi nyingine… katika hili napenda kuipongeza serikali ya Tanzania,” alisema Wanjala ambaye pia ni mkufunzi katika mafunzo hayo.

Alisema, lengo ni kuwaelimisha watetezi wa haki za binadamu wa Tanzania kufahamu vema, mafunzo ya usalama na utambuzi wa mazingira hatarishi na jinsi gani wanavyoweza kujilinda kwa kuwa siku zote watetezi wa haki za binadamu wanakabiliana na hatari za kuuawa au kuteswa na serikali zao au matajiri wakubwa.

Jumla ya washiriki 14 ambao ni watetezi wa haki za binadamu toka taasisi mbalimbali za binafsi wanashiriki mafunzo hayo.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Desemba 14 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.