Header Ads

VYOMBO VYA HABARI VITATUMIWA HADI LINI?

Happiness Katabazi

MAPEMA wiki iliyopita Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, alinukuliwa na gazeti moja la kila siku akikemea vikali tabia ya baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari, wafanyabiashara na wanasiasa nchini kuvitumia vyombo vya habari kuwachafua wenzao.

Bila kumung’unya maneno, alisema hivi sasa imeshajengeka tabia miongoni mwa makundi ya watu yanayokinzana kuwatumia baadhi ya wanahabari legelege kuandika habari ambazo hazina tija kwa taifa isipokuwa zina lengo la kuwachafua kisiasa au kibiashara mbele ya jamii.

Membe ambaye alitoa karipio hilo Novemba 27 mwaka huu, muda mfupi kwenye hafla ya kuapishwa kwa baraza jipya la mawaziri katika viwanja vya Ikulu, ambapo kila waziri alikuwa akizungumza matarajio yake au kile kinachomkera.

Binafsi baada ya kusoma habari hiyo iliyomnukuu Membe, niliguswa kwani alichokisema kiongozi huyo ni kweli tupu, sisi tunaoshinda kwenye vyumba vya habari kila siku, hayo yaliyosemwa na Membe tumekuwa tukiyashuhudia na kuyasikia na yalishatupa kichefuchefu na sasa yametukinai.

Hakuna ubishi kwamba miongoni mwa wanabari wana hulka ya kutofuata maadili ya fani ya uandishi wa habari na wamegeuka kuwa wachumia tumbo zaidi kuliko kuangalia maadili na masilahi ya taifa.

Naweza kuwaita watu wa aina hii ni Manyang’au. Hawa wamekuwa wakijirahisi kwa baadhi ya wanasiasa, wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiwapata fedha au ahadi fulani ili waandike habari za kuumiza watu wanaowakusudia.

Waandishi hao hudiriki hata kutoboa siri ya habari fulani za uchunguzi ambazo zinatarajia kuchapishwa au kutangazwa kwenye chombo fulani kwa lengo la kujikomba ili waonekane bora.

Mchezo huo binafsi naouna ni hatari kwa fani ya habari na usalama wa baadhi ya waandishi ambao wako mstari wa mbele kuandika habari za uchunguzi kwa lengo la kufichua maovu.

Tabia hiyo imewafanya baadhi ya waandishi wa habari mahiri na wale wanaochipukia kuandika habari za uchunguzi kuamua kupunguza kasi na wengi hufikia hatua ya kuacha kabisa kuandika habari za aina hiyo.

Kimsingi tukubaliane kuwa tasnia ya uandishi wa habari ina mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa letu, sasa inapofika baadhi ya wanahabari wenyewe kushindwa kusimamia maadili ya taaluma yao na kuwa wahujumu kwa wanahabari wenzao taifa halitoweza kuendelea kwa kiwango kinachotakiwa.

Sote tunafahamu kuwa mwanasiasa chakula chake ni vyombo vya habari, yaani wanapenda kuandikwa mazuri yao tu lakini yanapoandikwa mabaya yao huwa mbogo na kuziita habari hizo ni uzushi wenye lengo la kuwachafulia jina.

Uswahiba wa wanasiasa na waandishi wa habari katika kupanga na kuandika habari za kuwachafua watu fulani kamwe haupaswi kupewa nafasi katika jamii iliyostaarabika.

Urafiki huo huo ndiyo unaowafanya viongozi kuwa vinara wa kuingia na simu, vinasa sauti kwenye vikao vya siri vya vyama vyao na hata vikao vya serikali, kurekodi mazungumzo yao na mara baada ya kikao kumalizika yote yaliyozungumzwa humo huingia kwenye vyombo vya habari.

Vinasa sauti vilivyotumika hukabidhiwa kwa wanahabari wasikilize yote yaliyozungumzwa kwenye vikao bila kujali kuwa kilichozungumzwa mle ni siri au mkutano wa ndani.

Aina hii ya viongozi ambao hawajui nini maana ya kutunza siri ya vyama au ya serikali ndiyo inayochangia nyaraka muhimu za serikali kuanikwa juani na kila mtu kuanza kuzijadili kulingana na upeo wake na mwisho wa siku kuweza kuathiri mustakbali wa taifa.

Wanaofanya mchezo huu haramu wa kuvujisha siri wengine tuliwashuhudia wakila viapo mbele ya Rais Jakaya Kikwete na kushika Msaafu na Biblia kwamba watatunza siri na kuihifadhi Katiba ya nchi. Hivi viongozi wenye tabia hii nikisema wana laana nitakuwa nakosea?

Nchi inayoongozwa na viongozi ambao wanakiuka viapo vyao vya kutunza siri au kuwahudumia wananchi pasi upendeleo haiwezi kuendelea kwa sababu wale waliopewa madaraka tayari watakuwa na laana ya kukiuka maagizo waliyoapa kuyalinda kwa kutumia vitabu vyao vya dini.

Wanasiasa tulionao hivi sasa wamekuwa wakitumia fimbo ya fedha zao au zile wanazosaidiwa na marafiki zao kutengeneza mtandao kwenye vyombo vya habari na dola ili kutimiza mambo yao maovu.

Tasnia ya habari itaiangamiza nchi kama itaendelea na tabia hii ya kutumiwa na watu wachache wenye masilahi binafsi iwe yawe ya kibiashara au ya kisiasa.

Fukuto la Jamii, linasema Membe umenena uliposema baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari nao wamekuwa wakiingilia uhuru wa wanahabari kwa kuelekeza habari ipi ichapishwe au itangazwe na ipi isichapishwe au kutangazwa.

Kuna baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari hapa nchini wameanzisha vyombo hivyo si kwa lengo kutaka kukuza taaluma ya habari, uhuru wa habari, kutoa ajira, kufanya biashara bali wamevianzisha kwa malengo la kuwachafua wale wasiokubaliana nao.

Wameanzisha vyombo hivyo pia kwa lengo la kuficha maovu yao na maswahiba zao, hawa masilahi ya taifa kwao ni msamiata mgumu kueleweka katika vichwa vyao.

Katika taifa linalojali usalama wa wananchi wake na sheria za nchi yake, haliwezi kuvumilia uanzishwaji wa utitiri wa magazeti tena kwa msimu ambayo baadhi yao yanachapisha habari zinazomkashifu mtu kwa maslahi fulani.

Tumeshuhudia wakati wa uchaguzi mkuu hasa mwaka 2005, magazeti mengi yalianzishwa bila udhibiti ukilinganisha na harakati za uchaguzi mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.

Katika kipindi hicho magazeti mengi yalianzishwa na baadhi ya waandishi wenzetu katika magazeti hayo ama walikuwa wanajua au hawajui walijikuta wakiwa na kazi ya kuandika makala za kuwachafua baadhi ya wagombea urais na wabunge.

Hali kadhalika kwa mwaka huu, pia kuna baadhi ya wanahabari wenye utashi wa kimaamuzi kwenye vyombo vya habari wanavyovitumikia nao walijikuta wakitumika kuwachafua baadhi ya wanasiasa na vyama fulani badala ya kusimamia maadili ya taaluma yao.

Hivyo basi umefika wakati mwafaka kwa wamiliki wanaoanzisha vyombo vya habari kama hawana dhamira ya dhati ni vyema wakaachana na biashara hiyo wakaenda kuwekeza katika biashara nyingine kuliko kuanzisha kitu kwa dhamira mbaya.

Idara ya Habari (Maelezo) chini ya Wizara ya Habari, Vijana na Michezo, ilishindwa kuvichukulia hatua madhubuti baadhi ya vyombo hivyo ambavyo vimekuwa vikizua habari za kuwachafua viongoni au wananchi wasio na hatia.

Habari za aina hii kwa namna moja au nyingine zimechangia watendaji wa serikali na wa sekta binafsi kupunguza morali ya kufanyakazi hasa pale wananchi wanapoamua kuhukumu utendaji wao wa kazi wakitumia ushahidi unaotolewa na vyombo vya habari.

Watendaji hawa wamekuwa wakisikika wakilalamika Idara ya Habari (Maelezo) kwa kuyashughulikia baadhi ya magazeti yanayokiuka maadili ya uandishi wa habari huku wakiyaacha mengine yanayomilikiwa na watu wenye ushawishi ndani na nje ya serikali.

Waziri Membe, ni kiongozi wa siku nyingi serikali na kwenye chama tawala ambaye ameona uozo huo na kutoa angalizo, kilichobaki hivi sasa ni kwa wahusika kuchukua hatua.

Kwa hiyo Fukuto la Jamii, linatoa rai kwa Waziri wa Wizara ya Habari Vijana na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi na Naibu wake Dk. Fenella Mukangara kuona uozo huo, ni miongoni mwa changamoto kubwa inayoikabili ofisi yao.

Sio siri kwamba Dk. Nchimbi, ana mahusiano mazuri na wanahabari wengi, lakini tunaomba mahusiano hayo mazuri yasimpofushe macho na kushindwa kuyachukulia hatua baadhi ya magazeti yanayokiuka maadili ya taaluma zao.

Waziri huyo anapewa meno makali zaidi na sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ambayo inampa mamlaka kulifungia gazeti pale anapobaini kuwa limechapisha habari iliyokiuka maadili.

Sheria hiyo imekuwa ikilalamikiwa na wadau wengi kuwa imepitwa na wakati na inatoa fursa kwa kiongozi husika kuyafungia magazeti ama kwa kukiuka maadili au kwa sababu nyingine ikiwemo za binafsi.

Wanahabari tunapaswa kujirekebisha kwa kutokubali kutumiwa na wanasiasa au wafanyabiashara wenye masilahi binafsi ili tuweze kuheshimika mbele ya jamii inayotuzunguka.
Leo hii waandishi wa habari wametolewa thamani na jamii kutokana na kutumiwa na watu wenye malengo binafsi.

Wanahabari wakifanikiwa kujirekebisha wageukie kwenye sheria hiyo ya magazeti ya mwaka 1976 kwa kufungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu, kuiomba mahakama hiyo iibatilishe.

Kama hatutalisimamia jambo hilo, sheria hiyo itaendelea kutumiwa na waziri husika hata pale pasipokuwa na ulazima wa kulifungia gazeti sambamba na kuamua kutoyafungia magazeti yanayokiuka maadili.

Fukuto la Jamii linasema vyovyote iwavyo, mwisho wa siku mwanahabari ndiye mwenye taaluma ya habari hivyo ni vyema baadhi ya wanahabari ambao maisha yao na akili na utu wao wameamua kujibinafsisha kwa wanasiasa ambao wamekuwa na hulka za kupenda kuandikwa kwa mazuri na mabaya yafichwe wakaachana na tabia hiyo kwani wakumbuke wanasiasa ni watu wa kupita na hayo madaraka yao na taaluma za waandishi wa habari zitabaki kuwa pale pale.

Hivyo ni vyema kila mmoja wetu atimize wajibu wake kwa maslahi ya taifa letu na maadili ya taaluma inavyotutaka na si vinginevyo.

Tuna mifano hai ya machafuko yaliyotokea kwenye nchi za za Rwanda na Burundi ambako makala na habari za kichochezi zilizokuwa zikichapishwa na kutangazwa kwenye vyombo vya habari zilikuwa chanzo cha kuleta machafuko.

Fukuto la Jamii leo linampongeza Waziri Membe kwa kukemea uozo huo na linamtaka aendelee kukemea maovu mengine yanayofanywa na baadhi ya wanasiasa wenzake wenye hulka za kinyang’au ambao wanapenda kupambwa kwenye magazeti wakati hawana udhu na vigogo wengine.

Sisi wanahabari wakorofi haya anayoyasema Membe leo tuliyasema miaka minne iliyopita katika makala zetu lakini tulipuuzwa na kuonekana ni maamuma, lakini leo Mungu ni mkubwa kwani ameishaanza kuwafumbua macho hata viongozi wetu kuuona uozo huo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Desemba 12 mwaka 201o

1 comment:

Anonymous said...

Yes, I support your statement!

Twahitaji wanawake takribani mia tu wa namna yako, ili tuvuke hapa tulipo!

Mvuna's

Powered by Blogger.