Header Ads

AUGUSTINE RAMADHANI:KESI YA MGOMBEA BINAFSI SITAISAHAU


Na Happiness Katabazi


“KESHOKUTWA, nitakuwa nikikumbuka siku yangu ya kuzaliwa na nitakuwa ninatimiza umri wa miaka 65, siku hiyo pia itakuwa ya kihistoria kwangu kwani ndiyo nitakuwa nastaafu kazi ya utumishi wa umma kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Nchi.”


Hii ni nukuu ya maneno ya Jaji Mkuu, Agustino Ramadhan, alipoanza kuzungumza na jahazi Jumapili kuhusu maisha yake na kazi


Anasema kuwa katika kipindi chote cha utawala wake amefanya kazi kwa ushirikino mkubwa na watendaji wa serikali pamoja na wale wa mahakama.


Anabinisha kuwa anajivunia kuwa katika uongozi wake aliheshimu sheria na Katiba na hata watendaji wenzake kwa kiasi kikubwa walijitahidi kufuata mambo hayo Yafuatayo ni mahojiano ya Jaji Ramadhani na Jahazi Jumapili.
Swali:
Ulijisikiaje wakati ukiteuliwa kuwa jaji mkuu mwaka 2007 na changamoto zipi ulizozikuta?
Jibu:
Nilifarijika kuteuliwa kushika wadhifa huo wa kuongoza mhimili wa mahakama kwa sababu ni nadra kupata nafasi kuu kama hii.


Changamoto kubwa niliyoikuta ni uhaba wa watendaji, ambapo majaji wa Mahakama Kuu na Rufaa kwa wakati huo walikuwa 11 na hivi sasa tuko 16.


Katika Mahakama Kuu, Rais Kikwete, aliteua majaji 30 kuanzia mwaka 2008 hadi sasa ambapo ni wastani wa majaji 10 kila mwaka.


Mahakimu wa mahakama za mwanzo wapatao 100 wameajiriwa kuongoza mahakama hizo jambo ambalo kwa kiasi fulani limeharakisha usikilizaji wa kesi.


Hivi sasa Mahakama Kuu ina Kanda 13 na kanda hizo zina majaji wawili wawili isipokuwa Kanda ya Tabora, Mwanza majaji wanne, Arusha watatu.


Changamoto nyingine ni uhaba wa vitendea kazi na teknolojia za kizamani za kurekodi mashauri lakini nashukuru Desemba 6 mwaka huu, tulizindua mfumo wa kidigitali wa kurekodia mwenendo wa kesi pamoja na tovuti ya mahakama.


Teknolojia hiyo ya kidijitali imeishafungwa inatumika kwenye Mahakama ya Rufaa, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na vitengo vyake vya Kazi, Ardhi na Biashara.
Swali: Ushirikiano wa mahakama na mhimili mingine ulikuwaje Jibu: Kimsingi wakati nikiingia mambo yalikuwa si mazuri, watendaji wa mahakama tulikuwa tukilalamikiwa na wabunge, wakuu wa mikoa na viongozi wengine wa serikali.


Jibu: Tatizo hilo nililitatua kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali na Rais Jakaya Kikwete pamoja na aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta kwenye shehere zetu mbalimbali.
Nami pia nilikuwa nikihudhuria sherehe za kiserikali pamoja na vikao vya Bunge hasa vile vya bajeti.


Kupitia ushirikiano huo mpya tuliweza kuhabarishana changamoto zinazotukabili na namna ya kuzitatua kulingana na uwezo tuliokuwa nao.


Swali: Kwa nini mahakama huchelewesha usikilizaji wa kesi?


Jibu: Kuna aina mbili za ucheweshwaji wa kesi, mosi mahakama pili ni Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ofisi ya Mwanasheria, polisi na mawakili wa kujitegemea.
Wakati mwingine hakimu au jaji anakuwa yuko tayari kusikiliza kesi lakini upande wa mashtaka unadai haujakamilisha upelelezi au unashindwa kuleta mashahidi kwa wakati.
Sababu nyingine ni baadhi ya mawakili wa kujitegemea wanakuwa hawajajiandaa kuendesha kesi husika sasa kwa sababu hizo ndiyo maana kesi zinashindwa kumalizika mapema.
Wananchi wengi hawatambui mchakato wa uendeshaji wa kesi ndiyo maana mwisho wa siku huishia kuitupia lawama mahakama kuwa inachelewesha kesi.


Lakini pia mhimili wa mahakama umeweza kusimamia sheria na Katiba. Pia mfumo wenyewe na baadhi ya sheria kwani tumeweza kubadilisha kanuni za uendeshaji wa kesi za Mahakama ya Rufani.


Kanuni za awali zilizotungwa mwaka 1979 zikafutwa na kanuni hizo mpya zilizopitishwa mwaka 2009 zimeanza kutumika Februari mwaka huu.
Swali: Wazee wa baraza wa mahakama wamekuwa wakilalamika kutolipwa posho kwa nini hali hiyo inajitokeza?


Jibu: Ni kweli kulikuwa na malalamiko hayo na wazee wa baraza walikuwa wanapata posho ya sh 1,500. Ila kuanzia Julai mwaka huu posho yao imeongezeka wanapata posho ya sh 5,000.
Wakati mwingine wazee hao walikuwa wanakopwa na mahakama wanakwenda kusikiliza kesi, hili lilikuwa linasababishwa na ufinyu wa bajeti ya mahakama.


Swali: una maana gani unaposema uongozi wako mahakama ilizingatia sheria na Katiba?


Jibu: Aah! Namaanisha kwamba mahakama imeangalia Katiba kwa mtizamo mpya unaopaswa uwe, ibara za Katiba zinazohusu majaji na ajira zao.
Huko nyuma majaji wa mahakama kuu walikuwa wanastaafu kwa mujibu wa sheria wakiwa na umri wa miaka 60 na wale wa mahakama ya rufaa miaka 65, halafu wanapewa mafao yao na kisha wanaweza kurejeshwa kufanya kazi hiyo kwa mkataba.
Hivi sasa hivi Rais wa nchi anaweza kuongeza umri wa kustaafu wa jaji anayekaribia kustaafu, Mfano Jaji wa Mahakama Kuu ana miaka 59;
Rais anaruhusiwa kumuongezea hata miaka mitatu mbele ya utumishi kabla ya umri wa miaka 60 kustaafu na akishastaafu katika umri huo alioongezewa na rais ndiyo anatapewa mafao yake yote.
Swali: Serikali imefanya jambo gani kwa mahakama mbalo utalikumbuka?
Jibu: Kubwa zaidi ni kukubali ombi letu la kutaka tuwe na mfuko wa mahakama ambao tunaamini utatusaidia kutatua matatizo yetu yanayokwamishwa na uhaba wa fedha.
Kilio chetu kikubwa kilikuwa ni kuiomba serikali ituwekee angalau asilimia mbili ya bajeti ya seriakli katika mfuko huo, sasa hivi mahakama inapewa asilimia 0.4 ya bajeti ya serikali.
Kiwango hiki ni kidogo sana kwani hata mikoa ya Lindi na Mtwara bajeti yake ni kubwa kuliko bajeti ya mahakama ambayo ina ofisi katika kata, wilaya na mkoa.


Pia naishukuru serikali kwa kutujengea mahakama za mwanzo mbili za kisasa zilizopo Kerege na Lugoba mkoani Pwani ambazo zimezinduliwa mapema wiki hii na ujenzi wake umegharimu zaidi ya sh milioni 600.
Swali: Kipi unajivunia katika utawala wako?


Jibu: Ni kuanzisha mchakato wa mahakama kupata mfuko wake na ninaamini hadi kufikia Julai mwakani mwakani mfuko huo utapatikana.

Jibu: Ikumbukwe kwamba licha ya kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, mimi ni Jaji wa Mahakama ya Haki za Binadamu na za watu ya Afrika yenye makao makuu yake jijini Arusha.
Katika mahakama hiyo tuko majaji 11. Ila majaji wa mahakama hiyo hatufanyi kazi muda wote, tunakutana mara nne kwa mwaka na kwa siku 10.
Kwa hiyo nafasi hiyo ya ujaji wa mahakama hiyo ya Afrika nayo itaniwezesha kuniingizia kipato. Pia nitakuwa nikilipwa pesheni za kustaafu na serikali yetu.
Nakusudia kuwa mhadhiri wa sheria (Visiting Lecturer), katika baadhi ya vyuo vikuu na ninakusudia kuandika vitabu.


Swali: Ni kesi gani ulishiriki kuisikiliza na kuitolea maamuzi ambayo hutoisahau?
Jibu: Ni kesi ya Kikatiba ambayo mwanasheria mkuu wa serikali alikata rufaa katika Mahakama ya Rufaa, dhidi ya Mchungaji Christopher Mtikila, kwamba mahakama inaweza kutamka kwamba ibara ya Katiba inaweza kuvunja ibara nyingine ya Katiba?


Nitaikumbuka kesi hiyo kwa sababu ni mara ya kwanza kwa mahakama ya rufani nchini kuketi majaji saba kusikiliza rufaa moja , pia ni mara ya kwanza kwa mahakama ya rufaa kuwaita marafiki wa mahakama-Mkuu wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Paramaganda Kabudi.


Alikuwapo pia aliyekuwa mhadhiri mwandamizi wa sheria wa UDSM, marehemu Profesa Jwani Mwaikusa na Mkurugenzi wa Mashtaka wa Zanzibar (DPP), Masoud Othman Masoud.
Sababu hasa inayonifanya niikumbuke kesi hiyo ambayo mimi nilikuwa kiongozi wa jopo hilo la majaji ni muda niliotumia kufanya utafiti na hatimaye tukafikia uamuzi wa kutoa hukumu; kesi ile ambayo wananchi wengi hupenda kuita kesi ya mgombea binafsi.
Ila mimi siiti kesi ya mgombea binafsi bali naiita kesi ya Kikatiba.


Swali: Wosia gani unautoa kwa majaji na mahakimu?


Jibu: Ninawaasa waendelee kuzingatia sheria na Katiba ya nchi katika utendaji wao wa kila siku kwani wakumbuke wao ndiyo kimbilio la wananchi wenye kudhulumiwa au kuminywa haki zao.
Ni vema wakaendelea kuilinda heshima ya mahakama kwa kutoa haki bila upendeleo wowote.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Desemba 26 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.