Header Ads

LIYUMBA AGONGA MWAMBA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imesema hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mei 24 mwaka huu dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu (BoT), Amatus Liyumba, ya kwenda jela miaka miwili ni sahihi na imekidhi matakwa ya sheria.

Hayo yalisemwa jana na Jaji wa Mahakama Kuu, Emilian Mushi, wakati akitoa hukumu ya rufaa namba 56 ya mwaka 2010 iliyokatwa na mrufani Liyumba dhidi ya Jamhuri.
Liyumba alikuwa akiomba mahakama hiyo ya juu kutengua hukumu ya Mahakama ya Kisutu kwa hoja kuwa ilijielekeza vibaya kisheria katika kutoa hukumu yake.

Jaji Mushi alisema upande wa mrufani ambao ulikuwa ukiwakilishwa na mawakili wa kujitegemea, Jaji Mstaafu Hillary Mkate, Majura Magafu, Onesmo Kyauke na Hudson Ndusyepo, kupitia hoja zao 12 za kupinga hukumu ya Mahakama Kisutu, umeshindwa kuishawishi mahakama kuu ifikie uamuzi wa kutengua hukumu ya mahakama ya chini.

“Baada ya kupitia kwa kina hoja 12 zilizowasilishwa mahakamani na hoja za upande wa Jamhuri mahakama hii inakubaliana na hoja za Jamhuri kwamba iliweza kuthibitisha kesi yao hivyo inatupilia mbali rufaa hii iliyokatwa na mwomba rufaa (Liyumba),” alisema Jaji Mushi.

Jaji Mushi alisema kutokana na uhalisia wa kesi hiyo mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilikuwa sahihi kufikia uamuzi wa kuona jamii isingeridhika endapo ingempatia adhabu ya kulipa faini tu bila kwenda jela kutumikia kifungo.

“Nimejiridhisha kwamba hukumu iliyotolewa na Mahakama ya chini dhidi ya Liyumba ilikidhi matakwa ya kisheria na wala haikupitiliza matakwa ya kisheria katika mazingira ya kesi …na nimeshindwa kubaini misingi ya kisheria niweze kutengua hukumu ya mahakama ya chini na kwa sababu hiyo zile saa 12 za kupinga hukumu hii zilizotolewa na Liyumba mahakama hii inazitupilia mbali na kama hajaridhishwa na hukumu hii anaruhusiwa kukata rufaa.

“Mshtakiwa anayetiwa hatiani kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya umma kwa mujibu wa kifungu cha 35 cha Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 atafungwa jela miaka miwili au kulipa faini au kutumikia adhabu zote mbili kwa pamoja…lakini kwa uhalisia wa kesi hii nakubaliana na mahakama ya Kisutu kwamba mshtakiwa alistahili kwenda jela kwa sababu jamii na taifa liko kwenye mapambano dhidi ya rushwa,” alisema Jaji Mushi.

Liyumba kupitia kwa mawakili wake alikuwa amepinga hoja ya mahakama ya Kisutu ambayo ilisema wameamua kumfunga jela kwa sababu nchi iko kwenye mapambano ya rushwa na kwamba kiwango cha rushwa kiko juu.

Akitoa ufafanuzi wake juu ya hilo, Jaji Mushi alisema anaamini mahakimu wa mahakama hiyo ya chini peni zao ziliteleza kuandika hilo na kusisitiza kwamba hawakuwa wakimaanisha hivyo.
“Ukweli ni kwamba mshtakiwa alikuwa akikabiliwa na shtaka moja la matumizi mabaya ya ofisi ya umma kinyume na kifungu cha 96(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 na siyo shtaka la rushwa,” alisema Jaji Mushi.

Aidha, alisema anakubaliana na hukumu hiyo kwamba hakukuwa na uharaka wa Liyumba na aliyekuwa Gavana wa BoT, marehemu Daudi Balali kufanya mabadiliko ya ongezeko la mradi wa ujenzi wa majengo ya Minara Pacha kabla ya kupata idhini ya Bodi ya Wakurugenzi kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria ya BoT inayoruhusu uwepo kwa bodi hiyo.

Kisha aliongeza, “Kitendo cha Balali na Liyumba kuruhusu mabadiliko ya ujenzi halafu baada ya mabadiliko kutekelezwa ndiyo wanaleta taarifa kwa bodi ili iwape idhini ni udhalilisha kwa bodi hiyo.”

Liyumba ambaye hadi sasa ameshatumikia robo ya kifungo chake, alikata rufaa Mahakama Kuu mwezi Juni mwaka huu akipinga hukumu ya Mahakama ya Kisutu akitaka mahakama hiyo ya juu imwachilie huru.

Mei 24 mwaka huu, jopo la mahakimu wakazi watatu lililokuwa likiongozwa na Edson Mkasimongwa aliyekuwa akisaidiwa na Benedict Mwingwa na Lameck Mlacha lilitofautiana katika kutoa hukumu hiyo.

Mkasimongwa aliandika hukumu peke yake ambayo ilifikia uamuzi wa kumwachilia huru mshtakiwa kwa hoja kuwa upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha kesi yake.

Hukumu hiyo ilibaki kwenye rekodi za mahakama, huku hukumu iliyoandikwa na mahakimu wawili Mwingwa na Mlacha ikibaki kuwa ndiyo hukumu rasmi ya Mahakama ya Kisutu. Hukumu hiyo ndiyo iliyomtia hatiani Liyumba kabla ya kukata rufaa hiyo iliyogonga mwamba.

April 9 mwaka huu jopo la mahakimu hao wakazi lilimfutia shtaka moja la kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 lakini lilimuona ana kesi ya kujibu katika shtaka moja la matumizi mabaya ya ofisi ya umma.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Desemba 22 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.