Header Ads

TOVUTI YA MAHAKAMA KUPUNGUZA KERO

Na Happiness Katabazi

DESEMBA 6 mwaka huu, Mahakama ya Tanzania iliandika historia mpya ya kimaendeleo kwa uzinduzi wa mfumo wa shughuli za mahakama na mradi wa kutoa elimu ya nadharia itumiayo mfumo wa kompyuta kurekodi na kutengeneza tovuti ya mahakama za Tanzanzia.


Makamamu wa Rais wa Seriakali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Mohamed Gharib Bilal ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo,kupitia hotuba yake yake alisema kuwa uanzishwaji wa mfumo wa kurekodi mashauri kwa kompyuta na tovuti ya Mahakama, utaboresha mazingira na hadhi ya mhimili wa mahakama nchini.

Katika uzinduzi huo uliohudhuriwa na viongozi wakuu akiwemo Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, Jaji Mkuu, Agustino Ramadhani, Ofisa Mtendaji Mkuu wa (ICF) Omar Issa, majaji wa mahakama ya rufaa na mahakama kuu, Dk.Bilal aliizindua tovuti ya mahakama itakayotambulika kwa kwa jina la ‘www.judiciary.go.tz’.

“Kabla ya mfumo huu kuuzindua,ile haki iliyoainishwa katika Katiba ya nchi, yaani haki za binadamu zilikuwa hazipatikani kwa wakati kutokana na mahakama zetu kurekodi mwenendo wa kesi na huduma nyingine kwa kutumia mkono…

“Lakini sasa napenda niipongeze mahakama kwani imepiga hatua kwa kuanzisha mfumo huu ambao umefadhiliwa na Shirika la ICF nawapeni hongera sana mahakama kwa sababu hii ni hatua bora zaidi,” alisisitiza Dk. Bilal.

Na kwa upande wake Jaji Mkuu Agustino Ramadhani, alisema hadi sasa Mahakama Kuu na vitengo vyake ambavyo ni Biashara, Ardhi na Kazi, vimewekewa vifaa vya kisasa vya kurekodi na kufanya huduma ya kuandika kwa mikono kuwa historia na kuongeza kuwa Mahakama ya Rufaa nayo imeboresha huduma zake na kuwa ya kisasa huku zaidi.

Kwa uzinduzi huo, Fukuto la Jamii ambalo lilikuwa ni miongoni mwa watu walioudhulia hafla fupi ya uzinduzi huo uliofanyika katika kordo ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, na pia ni mdau mkubwa wa mahakama kwasababu ni mwandishi wa habari za mahakamani nchini, linapongeza hatua hiyo ya kimaendeleo iliyopigwa na mhimili wa mahakama.

Kwani Fukuto la Jamii,linaamini kufungwa kwa teknolojia hiyo katika mahakama ni wazi kutapunguza kwa kiasi kikubwa urasimu wa upatikanaji bahari za wazi za mahakama ikiwemo maamuzi yanayotolewa na majaji mbalimbali.

Na pia itaondoa adha kwa wananchi wenye kesi kwenye mahakama hizo kujua kesi zao zimepangwa kwa jaji nani na tarehe ngapi na siku ya tarehe hiyo kesi yake inakuja kwaajili gani, Je kutajwa,kusikilizwa,kuwasilisha ombi,kutolewa maamuzi au kutolewa hukumu.

Kwani wananchi wengi wenye kesi katika mahakama hizo wengine wanaishi mikoa ya mbali hivyo wamekuwa wakitumia gharama nyingi kufika mahakama kuu,mahakama ya rufaa kwaajili ya kufuatilia kesi zao zimepangwa kwa jaji nani na itatajwa au kuanza kusikilizwa tarehe ngani?

Na Fukuto la Jamii, ambayo siku zote za jumaa ufanya shughuli zake mahakama mara kwa mara imekuwa ikiwashuhudia wananchi hao wakitokea mikoa mbalimbali wakishinda kwenye ofisi za makarani wa kesi za jinai na madai katika mahakama ya rufaa na mahakama kuu Kanda ya Dar es Salaam,wakitaka kujua hatima za kesi zao na wengine wamekuwa wakilalamika kesi zao zimekuwa zikichelewa kupangwa hivyo wamekuwa wakitumia nauli mara kwa mara lakini kupitia tovuti hiyo sasa wananchi wenzetu ambao watakuwa na uwezo wa kutumia teknolojia hiyo wataondokana na msalaba wa kutumia nauli kuja mkoa mmoja hadi mwingi kwaajili ya kujua maendeleo ya kesi zao.

Hakuna ubishi kwamba mahakama nchini imekuwa ikilalamikiwa kuwa imekuwa ikichelewa kutoa maamuzi katika kesi mbalimbali kwasababu imekuwa ikifanyakazi kwa kutumia teknolojia ya zamani ya majaji na mahakimu kurekodi mwenendo wa mashauri kwa kutumia karamu na peni wakati mahakama za wenzetu majaji na mahakimu wao wamekuwa wakitumia teknolojia ya kisasa kurekodi mwenendo wa kesi zinazofunguliwa katika mahakama zao.

Na siyo tu imekuwa ikilalamikiwa tu katika hilo, pia imekuwa ikilalamikiwa na washtakiwa waliohukumiwa na mahakama kuu ambao wanataka kukata rufaa katika mahakama ya rufaa kwa kuchelewesha kuwapatia nakala ya kuhumu warufani hili waweze kutumia nakala hiyo kukataa rufaa katika mahakama ya rufaa, kwa kisingizio kwamba mahakama haina haina fungu la kuchapa haraka nakala za hukumu na kwamba teknolojia waliyokuwa wakiitumia si ya kisasa, hali iliyosababisha wananchi waliohukumuwa kuendelea kusota rumande muda mrefu bila kukata rufaa kwasababu uongozi wa mahakama kuu unawaeleza teknolojia ya kuchapa mwenendo wa hukumu siyo ya kisasa.Hiki kisingizio kuanzia mahakama ulipozindua mfumo huo wa kisasa, kife mara moja.

Na siyo kundi hilo tu limekuwa likilalamika, pia sisi waandishi wa habari za mahakama wakati mwingine tumekuwa tukipata wakati mgumu kupata nakala ya hati ya kesi ya madai hata kama kesi hiyo imefunguliwa asubuhi kwa kigezo kwamba, nakala ipo moja na nakala hiyo inapelekwa kwa Jaji Mfawidhi Kanda ya Dar es Salaam, Semistocles Kaijage ili aiidhinishe kesi hiyo mpya sambamba na kuipangia jaji wa kuisikiliza.

Naamini kupitia mfumo huo mpya wa teknolojia, hicho kisingizio ambacho mara nyingi kimekuwa kikitolewa na baadhi ya makarani wa masijala ya kesi za madai pale Mahakama Kuu,kitakwisha.

Aidha naamini teknolojia hiyo mpya itawasaidia wadau wa mahakama na sheria wakiwemo mawakili wa serikali na binafsi, wanafunzi wanaosoma sheria na wale wananchi wanaopenda kufuatilia maamuzi na hukumu mbalimbali kupata na kuzisoma kwa urahisi hukumu mbalimbali zinazotolewa na majaji wetu ambazo katika uzinduzi huo tuliambiwa kuwa zitakuwa zikiwekwa ndani ya tovuti ya mahakama ili wananchi waweze kuzisoma.

Na katika hilo, Fukuto la Jamii linaupongeza uongozi mzima wa mahakama nchini chini ya Jaji Mkuu Ramadhani ambaye pia ni Brigedia mstaafu wa JWTZ, Msajili wa Mahakama ya Rufaani Francis Mutungi, Mkuu wa Teknohama wa Mahakama ya Tanzania, Jaji Robert Makaramba,majaji wa mahakama ya rufaa na mahakama kuu na watendaji wote wa mhimili huo kwa kushirikiana kikamilifu kimawazo na vitendo na kuakikisha wanafikia lengo la kufungwa kwa teknolojia hiyo ya kurekodi mashauri katika mahakama zetu.Tunawapongeza sana.

Aidha safu hii inampongeza Ofisa Mtendaji Mkuu wa (ICF) Omar Issa na shirika lake hilo kwa msaada wake wa kufunga mfumo huo na kutoa mafunzo kwa watumishi wa mhimili huo ya jinsi ya kutumia mfumo na hadi kufanikisha leo hii mahakama yetu kwenda sambamba na sayansi ya teknolojia kwa kufunga mfumo katika Mahakama ya Rufaa , Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, Aridhi na Biashara ambazo tayari zimefungwa mtandao huo, ni wazi kumerejesha heshima ya mahakama zetu hapa nchini.

Nimalizie kwa kuwaasa watumishi waliokwenye nafasi ya kutumia mfumo huo mahakamani kuwa waangalifu na kutumia vizuri kwani hata kama mfumo huo umefungwa kutokana na fedha za wahisani tukumbuke kuwa , utabaki kuwa ni mali ya watanzania wote.Nimesema hivyo kwasababu kuna mifano hai ya baadhi ya watumishi wanaopewa dhamana ya kutumia mali za umma hawazingalii mali hizo kwa umakini na matokeo yake wanazifuja na baada ya muda mfupi tunashuhudia uharibu wa hali ya juu.Msitufikishe huko.

Mwisho, safu hii inawatakieni wasomaji wake kheri na fanaka katika kusherehekea Siku Kuu ya Kristmasi ambao uazimishwa duniani kote Desemba 25, kila mwaka. Pia Fukuto la Jamii ninawaalika wasomaji wa safu hii kusherekea na kufurahi pamoja na mwandishi wa safu hii siku hiyo ya Kristmasi, kwani siku hiyo mwandishi wa safu hii(Happiness Katabazi) nitakuwa naazimisha siku yangu ya kuzaliwa na nitakuwa nikitimiza miaka 32.Namshukuru Mungu kwa kunipa afya njema.

Mungu ibariki Tanzania,Mungu ibariki Afrika
0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Desemba 19 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.