Header Ads

MATUKIO MAKUBWA KUTOKA MAHAKAMANI MWAKA 2010

Na Happiness Katabazi

LEO ndio Ijumaa ya mwisho ya mwaka 2010. Kesho panapo majaliwa tunaukaribisha mwaka mpya wa 2011.

Ungana nami mwandishi wa habari za mahakamani ili uweze kupata mtiririko wa matukio makubwa yaliyotokea mahakamani kuanzia Januari hadi Desemba mwaka huu.

Desemba 29
Chenge atiwa hatiani

ALIYEKUWA Waziri wa Miundombinu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge alihukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya sh 700,000 baada ya kutiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa makosa matatu ya kuendesha gari kwa uzembe, kusababisha vifo vya watu wawili na kuendesha gari lililokuwa na bima iliyokwisha muda wake. Chenge alifanikiwa kukwepa kwenda jela baada ya kulipa faini na sasa yupo huru.

Desemba 28
Jaji Mkuu Agustino Ramadhani astaafu
JAJI Mkuu Agustino Ramadhani alistaafu rasmi kazi hiyo kwa mujibu wa sheria baada ya kushika wadhifa huo kwa miaka mitatu na nusu.Na siku hiyo ndiyo alikuwa akitimiza umri wa miaka 65.

Desemba 27
Jaji Mkuu Chande aapishwa
JAJI Mkuu mteule,Mohamed Othman Chande aliapishwa rasmi katika viwanja vya Ikulu na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo.

Desemba 26
Kikwete amteua Chande kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania
RAIS Jakaya Kikwete alimteua Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mohamed Othman Chande kuwa Jaji Mkuu mpya wa Tanzania.

Desemba 21
Mahakama yalidhia hukumu ya Liyumba

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilisema hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mei 24 mwaka huu, dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu (BoT), Amatus Liyumba ya kwenda jela miaka miwili ni sahihi na imekidhi matakwa ya sheria.

Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji wa Mahakama Kuu, Emilian Mushi, wakati akitoa hukumu ya rufaa namba 56 ya mwaka 2010 iliyokatwa na mrufani Liyumba dhidi ya Jamhuri.

Desemba 16
Jaji Mkuu Mstaafu akataliwa
kesi ya Samaki wa Magufuli

UPANDE wa Jamhuri katika rufaa iliyokatwa na raia 36 wanaokabiliwa na kesi ya uvuvi haramu katika Mahakama ya Rufani nchini kwa kutumia meli ya meli ya Tawaliq 1 inayowakanili raia 36 wa kigeni ilimwomba aliyekuwa Jaji Mkuu Augustino Ramadhani kujitoea kwenye kesi hiyo kwasababu aliwahi kuizungumzia kesi hiyo nje ya mahakama kwa kutumia magazeti.

Desemba 6
Mahakama Tanzania yazindua tovuti yake
MAKAMU wa Rais, Dk.Mohamed Gharib Bilal alizindua uanzishwaji wa mfumo wa kurekodi mashauri kwa kompyuta na tovuti ya mahakama www.judiciary.go.tz., na kusema kuwa utaboresha mazingira na hadhi ya mahakama nchini.

Oktoba 4
Mahalu aibwaga serikali
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam,ilitamka kuwa kifungu cha 36(4)(e) sua ya 200 ya Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2002, ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Kesi hiyo ya Kikatiba ilifunguliwa mahakamani hapo na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali .

Hukumu hiyo ilitolewa na jopo la majaji watatu waliokuwa wakiongozwa na Jaji Kiongozi, Fakhi Jundu, Agustine Mwarija na Prejest Rugazia ambapo kwa kauli moja walisema wanakubaliana na hoja za mawakili wa mlalamikaji (Mahalu),dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali akitetewa na mawakili wa kujitegema, Alex Mgongolwa kwamba kifungu hicho kinakwenda kinyume na Katiba ya nchi na kinaleta ubaguzi.

Julai 2
Kesi kubwa ya ufisadi yafutwa

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ilimwaachia huru Ofisa Ugavi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Elias Mziray, na maofisa wenzake wanne waliokuwa wakikabiliwa na makosa matatu ya kula njama ya wizi wa sh milioni 119.
Mahakama hiyo, ilifikia uwamuzi huo baada ya kuwaona washtakiwa wote kwa pamoja hawana kesi ya kujibu.

Mbali na Mziray, washtakiwa wengine ni Ofisa Manunuzi, David Kakoti, Gene Moshi na Mhasibu Joseph Rweyemamu ambao wote ni watumishi wa wizara hiyo, Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Mkazi Stewart Sanga

Julai 9
Waziri Maua aamuliwa kulipa sh mil. 100
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilimwamuru Naibu Waziri wa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, Dk. Maua Daftari, kumlipa mfanyabiashara Fatma Salim, sh milioni 100.7 baada ya kubaini alivunja mkataba na mdaiwa huyo.

Hukumu hiyo, ilikuwa ni mara ya pili ikiwa chini ya Jaji Fedrica Mgaya, ambapo mwaka juzi hukumu hiyo, ilisomwa na jaji Laurian Kalegeya ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.

Juni 11
Korti Kuu yatengua masharti ya dhamana

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitengua masharti ya dhamana yaliyotolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Agnes Mchome, kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Benki Kuu(BoT), Simon Jengo na wenzake wawili ambao wanakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma baada ya kubaini hakimu huyo hakufuata sheria husika kutoa masharti hayo ya dhamana. Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Emilian Mushi.

Juni 21
Mafisadi wa Lukuvi mahakamani
OFISA Ardhi wa Manispaa ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Magesa Magesa (33), alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka moja la kughushi dondoo ya barua ya kumilikishwa ardhi inayoonyesha imetolewa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Noel Mkomola Mahyenga.

Juni 23
Rufaa ya Kasusura yagonga mwamba

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitupilia mbali rufaa iliyokatwa na aliyekuwa dereva wa Kampuni ya ulinzi ya Knight Support, Justine Kasusura, kwa maelezo kwamba sababu sita alizozitumia kukata rufaa zimeshindwa kuthibitisha na kwamba hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyomtia hatiani kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha na wizi dola milioni mbili za Marekani mali ya Citibank ilikuwa na dosari za kisheria. Hukumu ya Rufaa hiyo ilitolewa jana na Jaji mstaafu Thomas Mihayo.

Juni 8
Utumbo wa samaki wa Magufuli uteketezwe- Mahakama

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliamuru utambuzi wa utumbo wa samaki waliokamatwa wakivuliwa na wavuvi haramu 36 ambao ni raia wa kigeni katika meli ya Tawaliq katika eneo la Bahari ya Hindi, uharibiwe kutokana na kutoa harufu mbaya.

Juni 17
Majaji Saba wamgwaya mgombea binafsi

MAHAKAMA ya Rufaa Tanzania, ilitengua hukumu ya kuruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi katika uchaguzi, iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kusema suala hilo litaamuliwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akisoma hukumu hiyo kwa zaidi ya saa moja, Jaji Ramadhani alisema suala la mgombea binafsi limekaa kisiasa sana, sio kisheria kama ilivyoaminika.

Mei 28
Liyumba akata rufaa korti kuu

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba(62) aliyehukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwenda jela miaka miwili alikata rufaa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam akipinga hukumu hiyo.

Mei 24
Liyumba afungwa miaka miwili jela

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ilimuhukumu kwenda jela miaka miwili, aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba baada ya kumtia hatiani kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi za umma.

Mei 13
Liyumba hana hatia -Wakili
MAWAKILI wa upande wa utetezi katika kesi ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatusi Liyumba waliiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imuone mteja wao hana hatia kwasababu hakuwa na mamlaka ya kuamua jambo lolote ile katika mradi wa ujenzi wa mradi wa majengo pacha.

Mei 8
Mkurugenzi BoT afutiwa kesi
MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam,ilimuachia huru aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Benki Kuu(BoT), Bosco Kimela aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 104 ambaye amesota rumande kwa miezi nane sasa kwaajili ya kesi hiyo.

Mei 7
Vigogo BoT waachiwa, wakamatwa

MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, iliwafutia mashtaka ya uhujumu uchumi yaliyokuwa yakiwakabili wakurugenzi wanne wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), lakini wakurugenzi hao walijikuta wakikamatwa tena baada ya kutuhumiwa mashtaka matatu ya matumizi mabaya ya ofisi za umma.

Washtakiwa hao ni Mkurungezi wa BoT, Simon Jengo, Naibu Mkurugenzi wa Fedha za Nje, Kisima Mkango, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kitengo cha Sheria, Bosco Kimela na Mkurugenzi wa Huduma za Benki, Ally Bakari.

Mei 10
Waziri Daftari ashinda kesi
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilimfutia kesi ya madai ya kashfa iliyokuwa ikimkabili Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,Dk.Maua Daftari kwasababu hati ya madai ina dosari za kisheria.

Juni 17
Majaji Saba wamgwaya mgombea binafsi


HATIMAYE Mahakama ya Rufaa Tanzania, ilitengua hukumu ya kuruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi katika uchaguzi, iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kusema suala hilo litaamuliwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aprili 23
Liyumba atumia hoja za Yesu kujitetea

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba (62), aliyekuwa akikabiliwa na shtaka moja la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma, alidai serikali haijui itendalo dhidi ya kesi iyomfungulia.

Liyumba aliiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, izingatie ukweli wakati wa kutoa hukumu dhidi yake Mei 24 badala ya kuwasikiliza watu wasiojua watendalo.Maneno hayo mawili ‘hawajui watendalo’ yanafanana na yale aliyotumia Yesu Kristo, anayeaminika kuwa ni Mwokozi wa waumini wa Kikristo wakati akieleza kitendo cha Wayahudi waliokuwa wakimsulubisha (Luka 23:34).

Aprili 5
Maranda aanza kujitetea kesi ya EPA

MWEKA Hazina wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma, Rajabu Maranda, aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa alichokizingatia katika mchakato wa kudai deni lake la Sh bilioni 1.8 katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu ya Tanzania ni kupata fedha na si kutazama nyaraka.

Aprili 13
Wazee EAC waiteka Mahakama Kuu Dar

WAZEE wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) walizusha tafrani katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, muda mfupi baada ya Jaji Njengafibili Mwaikugile kutoa maelekezo ya kuwataka waende wakatafakari upya na kumletea taarifa sahihi zitakazomwezesha kufikia uamuzi wa kutoa haki katika shauri lao.

Aprili 9
Liyumba apangua shtaka kuu

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ilimfutia shitaka moja kati ya mashitaka mawili yaliyokuwa yakimkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, kwa maelezo kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kupeleka ushahidi wa kuthibitisha shitaka mojawapo.

Uamuzi huo ulitolewa na kiongozi wa Jopo la Mahakimu Wakazi, Edson Mkasimongwa, aliyekuwa akisaidiana na Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa.

April 9
Mgombea binafsi bado alitesa taifa

MAHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Palamagamba Kabudi na Profesa Jwani Mwaikusa, wakishirikiana na Mkurugenzi wa Mashitaka wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (DDP), Othman Masoud.Walikuwa wanaishauri Mahakama ya Rufaa kabla haijatoa hukumu ya rufaa iliyofunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka jana kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyoruhusu mgombea binafsi, katika kesi ya msingi iliyofunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila.

Aprili 9
Babu Seya, mwanaye waomba
hukumu yao ipitiwe upya

MWANAMUZIKI mahiri wa muziki wa dansi nchini Nguza Vikings “Babu Seya na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha” walirusha karata yao ya mwisho katika Mahakama ya Rufaa Tanzania wakiomba mahakama hiyo ipitie upya hukumu iliyotolewa mahakama hiyo ambayo ilisisitiza kwamba warufani hao waendelee kutumikia kifungo cha maisha jela na kuwaachilia huru watoto wake wawili baada ya kuwaona hawana hatia.

Aprili 8
Majaji waitoa serikali jasho Kortini Dar

RUFAA ya kesi ya Mgombea binafsi ilianza kusikilizwa rasmi na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, aliyedai kuwa hakuna mahakama yoyote nchini ambayo inaweza kusikiliza kesi ya kutaka kuwepo kwa mgombea binafsi.Masaju alitoa madai hayo wakati akiwasilisha hoja zake za kupinga hukumu ya Mahakama Kuu.

Machi 30
Mkurugenzi wa Easy Finance Kortini

MMOJA wa Wakurugenzi wa Kampuni ya kutoa mikopo nchini ya Easy Finance, Aloycious Gonzaga (43) na mkewe, Magreth Gonzaga (38), walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka manne ya kula njama na kuwasilisha hati ya kiwanja ya kughushi na kisha kujipatia isivyo halali sh milioni 50.

Machi 29
Serikali yamng’ang’ania Liyumba

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya matumizi mabaya ya Ofisi ya Umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba uliiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imuone mshitakiwa ana kesi ya kujibu.

Machi 22
Mawakili wataka Liyumba aachiwe

UPANDE wa utetezi katika kesi ya matumizi mabaya ya Ofisi ya Umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumushi na Utawala wa BoT ,Amatus Liyumba, uliiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imuone mshitakiwa hana kesi ya kujibu na imuachirie huru kwasababu upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha kesi yao(prima facie case).

Februali 11
Babu Seya,Papii wakwama tena

MWANAMUZIKI mahiri wa muziki wa dansi nchini, Nguza Viking (Babu Seya) na mwanaye Papii Kocha walishindwa kujinasua kwenye hukumu ya kifungo cha maisha jela.

Mahakama ya Rufaa Tanzania jana ilikazia hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, lakini iliwaachia huru watoto wawili wa Babu Seya ambao ni Nguza Mbangu (Mashine) na Francis Nguza (Chichi).

Januari 15
Mahakama Kuu yatengua uamuzi wa kesi ya Jeetu Patel
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitengua uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wa kusimamisha usikilizaji wa kesi ya wizi wa sh bilioni 7.9 katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu, inayomkabili Mfanyabiashara maarufu Jayantkumar Chandubhai Patel maarufu ‘Jeetu Patel na wenzake wawili.

Januari 14
Washtakiwa wizi NBC Ubungo huru

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imewaachiria huru Ramadhani Dodo na wenzake nane waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya wizi wa sh milioni 168 kwa kutumia silaha mali ya Benki ya Taifa ya Biashara(NBC)Tawi la Ubungo maarufu kama ‘kesi ya mtandao’baada ya kuwaona hawana hati.

Januari 11
Mtikila atupwa rumande

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, ilimtupa rumande Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila baada ya kumfutia dhamana kwa kukiuka masharti. Amri ya kumfutia dhamana na kutupwa rumande ilitolewa baata ya Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema, kusikiliza utetezi wa Mtikila aliyechelewa kuhudhuria kesi ya uchochezi iliyomkabili.

Nawatakieni wasomaji wote wa gazeti hili na wale wadau wote wa mhimili wa mahakama ya Tanzania, maandalizi mema ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2011.

0716- 774494
www.katabazihappy.blogspot.com

No comments:

Powered by Blogger.