MAWAKILI WA TANESCO KESI YA DOWANS WAMETUSAIDIA NINI?
Na Happiness Katabazi
SEPTEMBA 6 mwaka huu, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Dk.Fauz Twaib alitupilia ombi la shauri la madai Na.8/2011 lilofunguliwa mahakamani hapo Oktoba mwaka jana na Shirika la Umeme(Tanesco) dhidi ya kampuni ya Dowans Hodlings SA(Costa Rica)Dowans Tanzania LTD,lilokuwa likiomba mahakama hiyo itoe amri ya kuzuia utekelezwaji wa hukumu ya mahakama kuu iliyotolewa Septemba 28 mwaka jana ambayo iliruhusu tuzo iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya (ICC) ya dola za Kimarekeni 65,812,630.03 kwa Dowans isajiliwe.
Katika uamuzi wake huo ambao ninayo nakala yake Jaji Dk.Twaib alisema amefikia uamuzi wa kukataa ombi hilo la mawakili wa Tanesco ambao ni Richard Rweyongeza, Lugano Mwandambo,Dk.Eve Hawa Sinare,Dk.Alex Nguluma na Majura Magafu na badala yake ikakubaliana na hoja zilizotolewa na wakili wa Dowans, Kennedy Fungamtama kwasababu mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza ombi hilo kwakuwa ni Tanesco hao ambao waliwasilisha ombi hilo la kutaka mahakama yake izuie utekelezwaji wa hukumu iliyotolewa na jaji wa mahakama Kuu Emilian Mushi Septemba 28 mwaka huu, ndiyo Tanesco hao hao pia tayari wameishawasilisha taarifa ya kusudia la kukata rufaa kupinga hukumu ya iliyotolewa na jaji Mushi katika Mahakama ya Rufani nchini. “Mahakama Kuu ilikuwa na mamlaka ya kusikiliza na kulikubali ombi la Tanesco la kuzuia Dowans isitekeleze hukumu ya Jaji Mushi kipindi kile wakati Tanesco hawajawasilisha taarifa ya kusudio la kukatia rufaa hukumu iliyotolewa na Jaji Mushi, Septemba 28 mwaka jana,katika Mahakama ya Rufani,kwa kuwa tayari Tanesco wameishawasilisha taarifa hiyo mahakama ya rufani,mahakama hii inakubaliana na hoja za wakili wa Dowans,Fungamtama kuwa mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza na kukubali ombi hilo la Tanesco’alisema Jaji Dk.Twaib. Itakumbukwa kuwa Septemba 28 mwaka 2011 jaji wa Mahahakama Kuu Emilian Mushi ambaye alikuwa akisiliza ombi la Tanesco lililokuwa likiomba Tuzo iliyotolewa na mahakama ya ICC kwa Dowans isisajiliwe hapa nchini,jaji Mushi alitupilia mbali ombi hilo la Tanesco na makundi mengine ya wakanaharakati ambao ni Kituo cha Kutetea Haki za Binadamu na akaruhusu tuzo hiyo isajiliwe hapa nchini kwasababu uamuzi wa mahakama ya ICC ulioipatia tuzo Dowans ulikidhi matakwa ya kisheria. Aidha Novemba 15 mwaka 2010 mahakama ya ICC ilipatia tuzo ya ushindi kampuni ya Dowans ya dola za kimarekani 65,812,630.03 baada ya Tanesco kukutwa na hatia ya kuivunjia mkataba Dowans kinyume na mkataba wao na ikaiamuru tanesco ilimpe dowans kiasi hicho cha fedha. Lakini Tanesco haikulidhika na uamuzi huo na kuamua kuja Mahakama kuu ya Tanzania mbele ya Jaji Mushi kuipinga hukumu hiyo ya ICC wakati ikifahamu wazi makubaliano ya Dowans na tanesco katika mkataba wao walioingia walikubaliana endapo wakigombana wataenda kusuluhishwa katika Mahakama ya ICC pekee na siyo mahakama Kuu wala Mahakama ya rufaa. Hukumu hiyo ya ICC ilizusha malumbano hapo nchini na kusababisha baadhi ya watu kutaka Dowans isilipwe kiasi hicho na wengine wakishauri serikali ieheshimu utawala wa sheria na iilipe Dowans fedha zake kwani tanesco ndiyo waliovunja mkataba na Dowans. Oktoba 2 mwaka 2011 gazeti hili lilichapisha makala yangu iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “Tanesco imevuna ilichopanda Dowans”.Ndani ya makala hiyo nilizungumzia hukumu ya iliyotolewa na Jaji Mushi na kuwasema sana Tanesco na wale wanaharakati waliokuwa wakipinga tuzo ya Dowans isisajiliwe kwasababu lengo hanawana hoja za msingi. Na leo tena narudia kusema hivi kuwa nyie mawakili mnaoitetea Tanesco kwanini lakini hamtaki kurejea zile notisi mlizofundishwa chuoni wakati mnasoma sheria na kupitia kwa makini sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai(Civil Procedure Act:RE,2002 na Sheria ya Mikataba ya mwaka 2002 na maamuzi ya kesi mbalimbali(Precedent). Naamini kama mngezisoma kwa makini na mngeheshimu maadili ya taaluma yenu na kuogopa kuumbuliwa na Mahakama ICC na Mahakama Kuu ya Tanzania kwa zaidi ya mara mbili sasa, msingekuwa mnathubutu hata siku moja kuwasilisha hayo maombi yenu yaliyotaka tuzo ya Dowans isisajiliwe na lile ombi la kutaka mahakama itoe amri ya kuzuia Dowans isitekeleze hukumu ya jaji Mushi. Aiingii akili kabisa kwa mawakili hao wa Tanesco ambao wanauzoefu wa kazi hiyo wanakubalije kila mara kwenda kusimama mbele ya mahakama nakuwasilisha maombi yao yasiyonakichwa wala miguu ambayo mwisho wa siku mahakama kuu imekuwa ikiyakataa maombi yao. Na cha kustaajabisha kama siyo cha kushangaza Tanesco hii hii ambayo kila siku imekuwa ikilia haina hela ila inapata fedha za kuwalipa mawakili hao wawatee kwenye kesi hiyo na matokeo yake wanashindwa tena kwa uzembe tu kwasababu wanawasilisha hoja dhaifu ambazo zinabaki kuwaduwaza watu kuwa inakuwaje hoja dhahifu kama hizo zinaweza kuwasilishwa na mawakili hao wenye majina makubwa kama hayo? Nimeifuatilia kesi hiyo mwanzo hadi mwisho upande wa Dowans umekuwa ukiwakilishwa na wakili mmoja tu Fungamtama lakini Tanesco wamekuwa wakiwakilishwa na lundo la mawakili ambao mwisho wa siku maombi yao yanatupiliwa mbali na mahakama.Kwanini hamjisikii aibu. Ni kweli mawakili kazi yenu ni kuisadia mahakama ikifikie hatua ya kutenda haki na pia mziwakilishe pande mbili katika kesi na mambo mengine lakini hivi inakuwaje wakili anayeheshimu taaluma yake na mwenye weledi wa taaluma ya sheria anawezaje kuwa anawasilisha hoja dhaifu kama hizi zinazowasilishwa na mawakili wa Dowans? Kwa wale waliopata fursa ya kuusoma mkataba baina ya Tanesco na Dowans wataona ndani ya mkataba huo kunakipengele cha (POA) pande hizo zilikubaliana kuwa endapo utatokea mgogoro baina yao basi mmogoro huo utasuluhishwa kwenye Mahakama ya ICC na siyo mahakama nyingine. Sasa ni kitu gani kila kukicha hawa mawakili wanaitetea Tanesco wanashindwa kukubaliana na hilo na matokeo yake wanakimbilia katika Mahakama Kuu huku wakifahamu fika mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo yasiyonakichwa wala miguu na wala haiwezi kutengua hukumu ya ICC isipokuwa tu pale kama Tanesco ingeweza kuleta ushahidi kuwa majaji wale wa ICC waliipendelea,au walihongwa na Dowans na Tanesco hilo wameshindwa kuthibitisha. Nafahamu kasumba ya baadhi ya wananchi wa taifa hili akitokea mtu au mwandishi akiandika ukweli ambao unawakera wao wanaishia kumuhukumu mwandishi huyo kaongwa na Dowans,mawazo ambayo ni ya kipuuzi. Na mwanasheria Mkuu wa Serikali jaji Fredrick Werema alishawahi kusema hatuwezi kukwepa kuilipa Dowans lakini wanaharakati uchwara na makundi mengine ambayo hata hukumu ya ICC,mkataba wa Tanesco na Dowans ulivunjwa hawakuwai kuusoma walimkebei sana lakini leo hii maana ya maneno yake yamenza kuonekana kupitia maamuzi mbalimbali ya Mahakama Kuu. Tanzania ni nchi inayoheshimu utawala wa sheria na pia inaitambua Mahakama ya ICC.Pia Tanzania ni nchi ambayo ina sera ya kuwakaribisha wawekezaji waje kuwekeza hivyo kwa mchezo huu wa kiuni unaofanywa ama na serikali kupitia njia hii ya kuwatumia mawakili kwenda kuweka mapingamizi mahakamani kuzuia Dowans isilipwe mara kuzuia hukumu ya Jaji Mushi isitekelezwe kwa njia ya kuchelewesha malipo ya Dowans,tukae tukijua mwisho wa siku utakuja kulighalimu taifa hili. Kwani tunavyozidi kuchelewa kuilipa Dowans kwa hoja hizi dhaifu zinazowasilishwa na mawakili wa Tanesco ambazo kwa mara tatu sasa mahakama za ICC,na mahakama kuu inazikataa zinasababisha deni hilo kuongezeka thamani kila kukicha na kuwachukiza wamiliki wa kampuni hizo na kuwadhalilisha kitaaluma hao mawakili wanaoitetea Tanesco mbele ya wasomi wenzao wa sheria maana kama walikuwa na uweledi mathubuti wa taaluma ya kisheria wasingethubutu kuwa wanawasilisha hoja hizo dhaifu ambazo zinakataliwa na mahakama. Na ninapenda ieleweke wazi uenda hii kesi ya Tanesco dhidi ya Dowans uenda imegeuzwa mgodi wa baadhi ya watu kujipatia fedha nyingi toka serikali kwa kisingizio kuwa wataiwasilisha fedha mahakamani Tanesco na mwisho wa siku watashinda kumbe ni uongo mtupu. Nimalizie kwa kuikumbusha serikali kuwa nchi yetu inatawaliwa kwa utawala wa sheria hivyo ni vyema ikaheshimu maamuzi ya mahakama na pia kama kweli wameamua kutumia njia hii ya kuchelewesha malipo ya dowans basi wasitumie njia hii ya kuwasilisha mapingamizi mahakamani kila kukicha kwani mbinu hiyo haifai na ndiyo kwanza inaidhalilisha serikali kupitia Tanesco kwani hata hao mawakili mapingamizi wanayoyawasilisha hayana mashiko kabisa. Na dawa ya deni ni kulipa kwani ni sisi ndiyo tulivunja mkataba na kama ndivyo hivyo lazima tukubali Dowans ilipata madhara na usumbufu wa Tanesco kumvunjia mkataba.Tulipe deni la watu ili tuendelee na mambo mengine kwani ujanja ujanja una mwisho. Na mwisho wake ndiyo huu wa Mahakama ya ICC na Mahakama Kuu ya Tanzania kuyatupilia mbali maombi ya Tanesco.Na wale wanasiasa akiwemo Samwel Sitta, Dk.Harrison Mwakyembe na wanaharakati wengine waliotufikisha leo kuhusu Dowans wamekaa kimya utafikiri hawapo wakati nao ni chanzo cha balaa lote hili. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika 0716 774494 www.katabazihappy.blogspot.com Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Septemba 9 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment