Header Ads

MTIKILA AMWANGUSHA KIKWETE KORTINI

Na Happiness Katabazi HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam ,imemfutia kesi ya uchochezi ya kuchapisha na kumiliki waraka wa uchochezi dhidi ya Rais Jakaya Kikwete iliyokuwa ikimkabili Mwenyekiti wa Chama cha Democratic(DP), Mchungaji Christopher Mtikila badaa ya upande wa jamhuri kushindwa kuleta ushahidi wa kuthibitisha kesi hiyo. Hukumu hiyo ya kesi hiyo ya jinai Na.132/2010 ilitolewa jana mchana na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo,Elvin Mugeta ambapo alianza kwa kuikumbusha mahakama hiyo kuwa mshitakiwa huyo alikuwa akikabiliwa na makosa mawili.Kosa la kwanza ni kusambaza waraka wa uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1),(c) cha Sheria ya Magazeti ya mwaka 2002 na kosa la pili ni la kumiliki waraka huo wa uchochezi kinyume na kifungu cha 32(2) cha sheria hiyo. Hakimu Mugeta aliyasoma maelezo ya makosa hayo kuwa ilidaiwa na wakili wa serikali mwaka 2010 mahakamani hapo kuwa Novemba 1 mwaka 2009 na April 17 mwaka 2010 jijini Dar es Salaam, akiwa na nia ya kutenda kosa la uchochezi ,Mtikila alisambaza kwa umma waraka huo uliokuwa na kichwa cha habari kisemacho (Kikwete Kuangamiza Kabisa Ukristo!(Wakristo wasipoungana upesi kuweka Mkristo Ikulu),huku akijua kufanya hivyo ni uchochezi. Na maelezo ya kosa la pili ni kwamba katika ya Aprili 16 mwaka 2010 huko Mikocheni alikutwa akimiliki waraka huo wa uchochezi. Akianza kusoma hukumu yake Hakimu Mugeta ambaye alisema kwanza Mtikila katika utetezi wake alikiri kuaanda waraka huo na alikiri pia alikuwa akiumiliki waraka huo na kwamba waraka huo ulitolewa mahakamani hapo kama kielezo cha tatu na jumla ya mashahidi wanne waliletwa na upande wa Jamhuri kuthibitisha kesi hiyo wakati Mtikila akuleta shahidi,alijitetea yeye mwenyewe kwa madai hakuona haja ya kuwaleta mashahidi kwasababu endapo angefanya hivyo angekuwa anamaliza fedha za mahakama na kupoteza muda wa mahakama bure. Hakimu Mugeta alisema kufuatia mashitaka yanayomkabili mshitakiwa kabla ya kutoa hukumu yake alijiuliza maswali yafuatayo kuwa je ni kweli waraka huo ni wa uchochezi?Je waraka huo ulileta madhara katika jamii?Je waraka huo wa mshitakiwa ulikuwa ukitaka kumpindua rais Kikwete kinyume na sheria za nchini kwani ofisi ya Rais imeanzishwa kwa sheria husika? “Mimi nimeusoma waraka huo unaodaiwa na upande wa Jamhuri kuwa ni uchochezi na nimebaini kuwa waraka huo si wa uchochezi kwani Mtikila licha ni mwanasiasa pia ni kiongozi wa kidini na waraka ule ulikuwa umejaa maneno ya kidini ambayo ndani yake Mtikila alikuwa akiwataka wakristo wenzake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 watumie haki yao ya msingi ya kumpigia kura mgombea ambaye ni mkristo … na kumng’oa madarakani rais Kikwete kwa njia ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu siyo kosa la jinai: “Kitendo ambacho mahakama hii kwa kauli moja imeona upande wa Jamhuri imeshindwa kuleta ushahidi unaonyesha Mtikila alikuwa anataka wakristo wamuondoe rais Kikwete Ikulu kwa njia haramu na pia kusambazwa kwa waraka huo na mshitakiwa kulileta madhara na kwamba wameshindwa kuleta ushahidi unaonyesha waumini wa dini ya kikristo walishawishika na waraka huo na wakajaribu kumuondoa Rais Kikwete madarakani kwa njia haramu”alisema Hakimu Mugeta. Alisema mshitakiwa angeweza kukutwa na hatia kama ingethibitika kuwa alikuwa akitumia karata ya dini kuligawa taifa na kuongeza kuwa mahakama hiyo imejiridhisha kuwa waraka huo haukuibia chuki mbaya baina ya waumini wa dini ya kiislamu na Kikristo na kwasababu hiyo mahakama hii imemuona Mtikila hajatenda kosa la uchochezi kwasababu hakuna madhara mabaya yaliyojitokeza katika taifa kupitia waraka huo na kwasababu hiyo mahakama hii inamwachiria huru mshitakiwa. Baada ya Hakimu Mugeta kumwachiria huyu Mtikila, Mtikila alisimama kizimbani akipaza sauti akisema “Haleluya,Haleyula…kesi hii ni ya mungu na hakuna binadamu yoyote anayeweza kushindana na mungu na kuwataka Watanzania wakasome Bibilia ,Waraka wa pili wa Timotheo Sura :4:2 ambao unasema ‘fanyakazi yako wewe Mhubiri wa Injili onya,karipia na kemea dhambi’ . Mtikila akasema yeye alichokifanya katika waraka ule ni kukemea dhambi na kutangaza neno la mungu lakini cha kusganga serikali ikamfungulia kesi hiyo ambayo ni jumla ya kesi ya jinai ya 43 amefunguliwa na serikali tangua aanze harakati zake za ukombi wa wanchi hii na kwamba kati ya kesi hiyo serikali ilimfunga kesi mmoja tu ambayo ilikuwa ni yakutoa maneno ya uchochezi ambapo alisema CCM, ndiyo ilimuua aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho,Horace Korimba ambapo alipokuwa Hakimu wa mahakama ya Wilaya ya Kinondoni Stella Mwandu alimfunga mwaka mmoja jela Kabla ya Hukumu kusomewa Mtikila alizungumza na waandishi wa habari nje ya viwanja vya mahakama ambapo alijigamba kuwa ni lazima atashinda kesi hiyo kwani alichokifanya kutangaza injili na kesi hiyo ni ya mungu na haogopi kufungwa. Baada ya Mtikila kushinda kesi hiyo hali ilikuwa ni tofauti karibu na mahabasu ya mahakama hiyo ambapo alikuja mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa mfanyabiashara anaitwa Gotem Ndunguru akiwaamrisha askari polisi wamkamate Mtikila kwa madai kuwa ana taarifa ya Kumkamata iliyotolewa na kituo cha polisi Kimara yenye namba RB/10482/12 ambapo alidai Mtikila alimtishia kumuua kwa maneno. Hata hivyo askari polisi na Ndunguru walishindwa kumkamata Mtikila kwasababu Mtikila alianza kumfokea askari polisi mmoja ambaye hatukuweza kufanikiwa kulipata jina lake ambaye alikuwa na cheo cha Koplo akimwambia kwa ukali kuwa hana hadi ya kumkamata yeye ana hadhi ya kukamatawa na polisi mwenye cheo cha Mrakibu wa Polisi na kwamba Nduguru ni mwizi mkubwa. “We askari huyo Ndunguru kakuonga uje unifanyie fujo hapa kwa taarifa yako mimi najua sheria ,wewe huna mamlaka ya kunikamata na huwezi kunikamata kiuni hivi…hata huyo bosi wako IGP-Said Mwema kabla ya kunikamata ananipigia simu kwa adabu na mimi mwenyewe ndiyo naenda polisi…sasa nawaambia hivi hauna hadhi ya kunikamata.”alifoka Mtikila na kusababisha askari huyo kunyewa na kuitwa na maaskari wenzake ambao walimtaka amwache Mtikila aende zake na maaskari hao wakimtaka Ndunguru anyamaze asiwafundishe kazi na baadae Ngunguru aliondoka mahakamani hapo kimya kimya na kuelekea nyumbani kwake. Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Septemba 26 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.