Header Ads

MPENDAZOE AMGWAYA DK.MAHANGA

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman ameliondoa Mahakama ya Rufani nchini,ombi la kusudio la kukata rufaa iliyowasilishwa Mahakama hapo, na Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Fredy Mpendazoe.


Mei 7 mwaka huu, Mpendazoe aliwasilisha mahakamani hapo taarifa ya kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam katika kesi yake ya uchaguzi wa jimbo la Segerea na Julai 12 mwaka huu,wakili wa Mpendazoe, Peter Kibatara aliwasilisha ombi la kutaka kuiondoa taarifa hiyo ya kusudio la kukata rufaa.

Katika kesi hiyo namba 98 ya mwaka 2010, Mpendazoe alikuwa akipinga matokeo yaliyomtangaza Dk.Makongoro Mahanga (CCM) kuwa mbunge wa jimbo hilo la Segerea.
Jaji wa Mahakama Kuu Profesa Ibrahim Juma alitoa hukumu ya kumtangaza Dk.Mahanga kuwa ndiye mbunge halali wa jimbo hilo na kwamba matokeo yaliyompa ushindi hayakukiuka taratibu za sheria na akawa ameitupilia mbali kesi hiyo iliyokuwa imefunguliwa na Mpendazoe.

Hata hivyo Jaji Mkuu Othman alimuru taarifa hiyo iondolewe mahakamani hapo chini ya Kanuni ya 89 (1) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani za mwaka 2009.
Jaji Mkuu Othman alitoa amri hiyo Agosti 2, 2012, baada Mpendazoe kuamua kuondoe nia yake hiyo ya kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Katika kesi ya msingi aliyoifungua Novemba10, 2010, Mpendazoe alikuwa akipinga ushindi wa Dk. Mahanga akidai kuwa haukuwa huru na wa haki kwa kuwa taratibu na kanuni za Sheria ya Uchaguzi zilikiukwa, katika hatua ya kuhesabu, kujumlisha na kutanga matokeo.

Hivyo aliiomba mahakama itengue matokeo hayo na kuamuru uchaguzi mdogo uitishwe katika jimbo hilo ama imtangaze yeye kuwa mshindi.
Wadaiwa katika katika kesi hiyo walikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala ambaye ndiye Msimamizi wa Uchaguzi wa majimbo yaliyoko katika manispaa hiyo likiwemo Segerea na Dk. Mahanga.

Dk. Mahanga alikuwa akitetewa na mawakili wakili, Jerome Msemwa, na Aliko Mwamanenge, AG na RO walikuwa wakitetewa na Mawakili Waandamizi wa Serikali David Kakwaya na Seth Mkemwa.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Septemba 11 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.