Header Ads

HONGERA DK.FELESHI,MKASIMONGWA KUTEULIWA KUWA MAJAJI


HONGERA JAJI DK. FELESHI, MKASIMONGWA KUTEULWA KUWA MAJAJI

Na Happiness Katabazi
RAIS Jakaya Kikwete Jana  alimteua aliyekuwa  Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),Dk.Eliezer Mbuki Feleshi "Msukuma' (47) na wasomi wengine washeria nchini akiwemo Aliyekuwa Katibu wa Jaji Mkuu, Edson Mkasimongwa " Raia wa Msumbiji' '  Kuwa  Majaji wa Mahakama Kuu  ya Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo Vya Habari iliyonysha  Majaji hao wataapishwa Na rais Kikwete Agosti 15 Mwaka huu, Ikulu Dar Es Salaam.

Awali ya yote napenda kutoa pongezi kwa Rais  Kikwete Kwa kuteua jumla ya Majaji 20 jana, idadi ambayo ni kubwa na ni Kama imetekeleza ahadi zake ambazo amekuwa akizitoa  kupitia hotuba zake  mbalimbali Katika siku ya Sheria nchini ambayo ufanyika mwanzoni mwa wiki ya kwanza ya Februali kila Mwaka ambapo binafsi nimekuwa nikiudhuria na amekuwa akihaidi  Kuwa   Katika Utawala wake ataakikisha  anateua   idadi kubwa ya Majaji ili idadi ya Majaji nchini iongezeke na idadi hiyo iende kumaliza mlundikano wa Kesi mahakamani na  Hilo amelitimiza  kwa Mara ya Tatu sasa.

Kwa faida ya wananchi wasiyomfahamu Jaji mteule Mkasimongwa. Mkasimongwa ameishawahi Kuwa Hakimu Mkazi  Katika Mahakama mbalimbali hapa nchini na Kabla ya Kuwa Hakimu aliwahi Kuwa karabiner wa Mahakama na Akaamua kujiendeleza na fani ya Sheria na hatimaye akawa Hakimu na mwisho wa siku Jana akatandika   historia mpya kwa  Rais   Kikwete Kumteua  Kuwa Jaji wa Mahakama Kuu nchini.

Kwa wale tuliokuwa  tunafuatilia na kuudhuria   Kesi ya matumizi mabaya ya madaraka iliyokuwa inamkabili Aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba  Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar Es Salaam, ilikuwa ikisikilzwa na jopo la Mahakimu wakazi watatu Mkasimongwa, Lameck Mlacha na Jaji mteule Benedict Mwingwa. Siku ya kutoa hukumu Jopo Hilo lilitofautiana kimaamuzi. 

Ambapo Mkasimongwa alitofautiana na wenzake ' yeye kwa upande wake alitoa hukumu ya kumwachiria Huru Liyumba " Decent Judgement' lakini  Mlacha na Jaji Mteule Mwingwa walitoa hukumu ya Kumtia hatiani Liyumba Kifungo Cha Miaka miwili gerezani ambapo hukumu ya Mahakama iliyohesabiwa ni hukumu iliyotolewa na Mahakimu wale Wawili na hukumu ya Mkasimongwa ikitunzwa Kwenye rekodi ya Mahakama.

Mkasimongwa Kabla ya Kuwa Katibu wa Jaji Mkuu, alikuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani. Pia Mkasimongwa ndiyo kiongozi wa jopo la Mahakimu wanaosikiliza Kesi ya wizi wa sh Bilioni Sita (EPA), inayowakabili ndugu Wawili Johnson Lukaza na Mwesigwa Lukaza Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ipo Katika Hatua ya usikilizwaji.

Hivyo Mkasimongwa Kuwa Jaji inawafundisha makarani  wa Mahakama Kuwa ,wakiamua kujiendeleza kielimu Kama Alivyofanya Mkasimongwa ambaye  ni mzaliwa wa Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara , ipo siku nao wanaweza kutoka Katika Kazi ya ukarani Kuwa Hakimu na jaji pia.

Hongera sana rafiki yangu Mkasimongwa ambaye yeye amekuwa akinitania Mimi na Mzee wangu Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Laurian Karegeya Kuwa sisi ni raia  wa Rwanda kwasababu sisi ni Wanyambo tunaotokea wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera na kwamba twende nchini Afrika Kusini , tukamzike ndugu yetu Patrick Kalegeya ambaye alikuwa ni Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa wa Rwanda ambaye aliuwawa nchini Afrika Kusini.

Na mimi ( Katabazi) na Jaji Kalegeya  tumekuwa tukimtania sana tu Mkasimongwa Kuwa yeye ni Raia wa Msumbiji na tunashangaa sana huyu Jaji Mkuu Mohamed Chande Othaman kukubali Kuwa na Katibu wake ambaye  ni raia wa Msumbiji yaani Mkasimongwa na kwamba tu najiandaa kwenda Idara ya Uhamiaji kwenda kutoa taarifa Kuwa Jaji Mkuu Othaman anamuhifadhi raia Huyo  wa Msumbiji na kwamba Ndio mAana wakazi wa Mtwara wanachoma Mahakama kule mkoani Mtwara Hawachukulii Hatua kwasababu raia mwenzio wa Msumbiji ni Katibu wa Jaji Mkuu. Hongera Mkasimongwa.

DK.ELIEZER  MBUKI FELESHI ' MSUKUMA'

Dk.Feleshi ni DPP wa kwanza  kushika wadhifa wa Ukurugenzi wa Mashitaka akiwa na umri Mdogo kuliko watangulizi wake na Ndie DPP aliyevunja rekodi ya kukaa Katika Kiti hicho kwa  muda mrefu ukilinganisha na watangulizi wake tangu Tanzania ilipota Uhuru wake. 

Hakuna Shaka wala ubishi kwamba Mimi Happiness Katabazi ndiye nilikuwa Mwandishi pekee nchini ambaye nilianza na kumaliza kufanyakazi kwa karibu sana na DPP-Feleshi na Timu yake ya waendesha Mashitaka ambayo Mimi niliipachika  jina la " Siafu wa DPP'

Dk.Feleshi Ana shahada ya Uzamivu   ya Criminology and Penalogy ya Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam.

Kwa Wenzangu na mie tunaofuatilia masuala ya kisheria hapa nchini, huwezi kuzungumzia Kesi Abdalah Zombe na wenzake,Basil Mramba, Kesi za EPA, Kesi za utakatishaji Fedha, Uvuvi haramu, matumizi Mabaya  ya madaraka, ugaidi, maandamano haramu, uchochezi, DECI, Kesi ya Vigogo wa Suma JKT, dawa za kulevya,Pembe za ndovu bila ya kumtaja au kumkumbuka Dk.Feleshi na vijana wake yaani Mawakili wa serikali Kwani ndiyo walikuwa akizifungua Kesi hizo na kuziendesha mahakamani.

Binafsi Nitamkumbuka Feleshi ambaye ni kaka yangu na rafiki yangu na amekuwa Mshauri wangu mkubwa hasa Katika Maisha yangu binafsi, Kazi  na Katika harakati zangu za kujiendeleza kielimu Katika fani ya Sheria Kwani nikutanapo naye uwa napenda kumwambia Kuwa  ipo siku nitakuja kuandika historia ya Kuwa DPP mwanamke nchini tunacheka sana na yeye pia amekuwa akipenda kuniita Binti wa Kinyambo,Binti wa Katabazi na kunitania  Kuwa Mimi ni raia wa Rwanda na Mimi na mwambia  yeye ni Msukuma na Wasukuma wanafuga Nyoka.

Katika Utawala wa Feleshi , aliruhusu maofisa wake  (Mawakili wa serikali) kutoa ushirikiano  wa hali na mali kwa sisi waandishi wa Habari za mahakamani na kweli tulipewa.

Feleshi ambaye kwa sasa ni Jaji Mteuli, siyo tu alikuwa ni Chanzo Cha Habari Kwa sisi waandishi wa Habari za mahakamani, Bali Feleshi wakati mwingine alijigeuza Kuwa mwalimu kwa sisi waandishi wa Habari ambao tulikuwa tutafika ofisini kwake kumuuliza kuhusu taarifa mbalimbali zinazohusu Kesi mbalimbali  ambazo tulikuwa Tunataka tuziandike bila kufahamu Kuwa tukiandika Habari hizo Mwisho wa siku tunavuruga Kesi na kuupa wakati mgumu upande wa jamhuri Katika Kesi hiyo.

Dk.Feleshi alikuwa akitusikiliza na kueleza faida na Hasara za kuandika taarifa hizo wakati vyombo Vya dola zinazifanyia  Kazi, na tulikuwa tuna mwelewa na kweli baadhi ya  waandishi wa Habari za  mahakamani tuliokubali kusikiliza nasaa za Dk. Dk.Feleshi za kututaka twende tukasome Sheria na tuwe wazalendo  na tuwe na subira na kufanya utafiti kwanza Kabla ya kuanika Habari,  Matunda ya ushauri wa Feleshi ambaye ni Mbobevu  wa masuala ya uendeshaji wa kesi za jinai nchini,  tumeanza kuyaona.

Kwani waandishi wakongwe wa Habari za mahakamani (Katabazi), Bernad James(Citzen), wanafunzi wa sheria wa Chuo Kikuo Kikuu cha Bagamoyo(UB) na Faustine Kapama(Daily News) (OUT), tupo Katika vyuo hivyo tu naendelea kusoma shahada ya Sheria na siku hizi wala hatupati Shida ya kujua lugha za kisheria na tunazungumza lugha Moja na Wanasheria.Nakushuru sana Dk.Feleshi.

Hakika mchango wako Dk.Feleshi kwa sisi wanahabari wa Habari za mahakamani tutahukumbuka na ushauri tutauzingatia, na kwakuwa hivi sasa umeama toka Kwenye Mhimili wa serikali kwenda Kwenye Mhimili mpya wa Mahakama, tutakutana huko na tutaendeleza harakati zetu za kukuza utawala na uwelewa wa Sheria.

Dk.Feleshi kutoka uwakili wa serikali ambao Wakili wa serikali awapo  mahakamani uwa anaiomba  Mahakama, na sasa Feleshi amekuwa Jaji anakuwa sasa ni mtu  wa kutoa Haki na kutafsiri Sheria "Precedent" na kukubali au kukata Maombi ya yanayowasilishwa Mbele yake na pande mbili Katika Kesi husika.Nitacheka sana siku nikimuona Dk.Feleshi akiwa amekaa  Katika Kiti ha Enzi Kama Jaji  anasikiliza Kesi na sitojali " Contempt of Court".

Ikumbukwe siku Chache   baada ya Dk.Feleshi kuteuliwa Kuwa DPP, ndipo Tanzania ili achana na utaratibu wa maofisa wa Polisi Kuwa waendesha mashitaka.Polisi wa lirudishiwa jukumu Lao la upelelezi na Mawakili wa serikali chini ya Ofisi ya DPP ndiyo ikachukua jukumu la Kuwa linaendesha Kesi za jinai mahakamani.

Poleni Ofisi ya DPP,Kwani mlimzoea Boss wenu Feleshi lakini ndiyo hivyo Rais  Kikwete kampa jukumu jipya la Ujaji.Ombi langu Kwa DPP ajaye aendeleze mazuri yaliyoachwa na Feleshi na Mabaya asiyafuate na aje na mikakati yake Mipya ambayo ataona yataongeza   tija Katika ofisi hiyo.

Nawatakia kila la kheri Majaji wataeule wote akiwemo Feleshi, Mkasimojwa, Mwingwa ,mungu awatangulie Katika nafasi hiyo mpya , Muende mkatende Haki kwa mujibu wa Sheria. 

 Agosti 14 Mwaka 2014: Chanzo: www.katabazihappy.blogspot.com: Facebook: Happy Katabazi.

TUJIKUMBUSHE MAKALA HII ILIYOCHAPISHWA NA GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI ,APRIL 15 MWAKA 2007

DPP KIJANA ANAYEINGIA OFISINI NA MSAAFU WA SHERIA 
Na Happiness Katabazi

ELIEZER MBUKI FELESHI

.Ndiye DPP mpya Tanzania, ana miaka 39
.Apania kumfuta tongotongo Rais Kikwete
.Aliungurumisha kesi ya MV Bukoba
.Adai ilijaa mambo ya ajabu, ataka kutungia kitabu
.Uhaba wa wanasheria wampasua kichwa

HIVI karibuni Rais Jakaya Kikwete, alimteua mwanasheria mwandamizi wa serikali, Eliezer Mbuki Feleshi (39), kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP). Uteuzi wa Feleshi ambaye alijizoelea sifa nyingi wakati wa kesi ya MV Bukoba aliposhiriki kama mwendesha mashitaka msaidizi na mchango mkubwa alioutoa katika tume ya kuchunguza mauaji ya wafanyabishara wanne wakazi wa Mahenge, ambayo iliwatia hatiani polisi, umekuwa ukielezwa na baadhi ya watu kama muarobaini wa ofisi hiyo. Katika makala hii MWANDISHI WETU HAPPINESS KATABAZI, anamuhoji jinsi alivyoupokea uteuzi huo, na pia alivyojiandaa kukabiliana na changamoto za ofisi hiyo.

Swali: Kuteuliwa kwako na Rais Jakaya Kikwete, kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) katika umri mdogo ulionao, kumedhihirisha jinsi rais alivyo na imani na utendaji kazi wako, umeupokeaje uteuzi huo?
Jibu: Nimeupokea kwa heshima kubwa. Natambua kuwa rais ananiamini na ndio maana akafikia uamuzi wa kunitwisha mzigo huu mzito katika umri mdogo nilionao.
Lakini uteuzi wangu nina hakika umezingatia sifa zilizowekwa kikatiba za mtu anayestahili kuteuliwa kushika wadhifa huu, binafsi ninafarijika kwamba, Mheshimiwa Rais aliisoma katiba kabla ya kuniteua, na aliporidhika, ndipo akaniteua.
Ni fahari kwangu, familia yangu, vijana wenzangu na taifa kwa ujumla, kuwa na vijana wanaoweza kuaminiwa na kukabidhiwa majukumu makubwa kama hili la kuongoza ofisi nyeti na kubwa.
Kazi iliyopo ni kuhakikisha kuwa simuangushi rais wangu na Watanzania kwa ujumla, nimepania kuwaonyesha kuwa vijana tunaweza kazi.

Swali: Umejipanga vipi kuthibitisha kuwa unaweza?

Jibu: Jambo la msingi ambalo nitalizingatia siku zote, nitakapokuwa katika ofisi hii, ni kutekeleza majukumu yangu kwa kuzingatia taratibu na misingi ya sheria ambayo ndio muhimili mkuu wa ofisi hii.

Misahafu ya sheria haidanganyi hata siku moja, na mimi ni muumini wake mkubwa, siku zote nimekuwa muumini wa sheria na ninaziishi, na kwa imani yangu hiyo ambayo imenipa mafanikio tangu nikiwa ngazi za chini, naamini nitafanya kitu kitakachomtoa tongotongo rais wangu.

Mimi na wenzangu tumeshajipanga, na bado tunaendelea kujipanga, sina cha kueleza zaidi katika hili…, unajua ofisi kama hizi ndugu yangu mambo mengine yanabaki ya kiofisi, lakini ninachotaka kuwaambia Watanzania ni kwamba, nitaiendesha ofisi hii kwa kufuata taratibu na sheria za nchi.

Bahati nzuri ni kwamba, kuna maofisa wengi tu hapa waliobobea katika fani ya sheria ambao utendaji wao, ninaamini kabisa kuwa hauna shaka hata kidogo, na tangu awali nilikuwa nikifanya nao kazi pamoja, na kwa ushirikiano wa dhati.
Majukumu tuliyokuwa tukitekeleza pamoja hapo awali, si kwamba yatabadilika baada ya mimi kuingia ofisini hapa, hapana, kimsingi ni yale yale, lakini ninachotaka tufanye kwa sasa ni kuhakikisha tunasonga mbele kukabiliana na changamoto zilizopo kwa kuwa nyakati zinabadilika kwa kasi sana.
Na ieleweke kuwa ofisi ya DPP ni ya kikatiba, si ya mtu binafsi, wala haitawaliwi kwa msingi wa umri, bali inaongozwa na mtu anayeonekana kuwa na sifa ya kupewa wadhifa huo. Watangulizi wangu waliteuliwa kushika wadhifa huo si kwa kuwa na umri mkubwa, bali kwa kuwa walikuwa na sifa za kuongoza ofisi hii.

Swali: Kuna malalamiko mengi ya kucheleweshwa kwa upelelezi wa kesi, hasa za mauaji, hili umelipangia mkakati gani?

Jibu: Kesi ni ushahidi, na ushahidi unapatikana kwa kuukusanya. Jamii inao wajibu wa kushirikiana na taasisi zinazofanya upelelezi ili kuharakisha kazi ya kukusanya ushahidi. Kwa nyakati fulani wananchi wamekuwa waoga kutoa ushahidi au wakati mwingine kuutoa kwa wasiwasi.
Kuna wakati wapelelezi wamezorota kufanya kazi zao na kuna wakati wamejitahidi, ila wanakwamishwa na nyenzo.
Kwa sababu hiyo, sipingi kuwa kuna malalamiko kama hayo kutoka kwa jamii, yapo, na ili kukabiliana na hali hiyo, nitaanza kwa kulifanyia kazi tatizo la vitendea kazi, pili ofisi yangu itafanya jitihada za makusudi za kuwaomba wananchi kushirikiana na waendesha mashitaka katika kukusanya ushahidi.
Kikubwa ni kuwaelimisha wananchi kuwa, wanayo sehemu yao ya kutoa taarifa dhidi ya wapelelezi wasio waadilifu, hasa kama wapelelezi wanawazungusha kupokea ushahidi wanaowapelekea, ninaamini nitafanikiwa kuondoa malalamiko hayo.

Swali: Idara yako ina wataalamu mahiri wa kutosha kuweza kukabiliana na changamoto zinazoikabili sasa?

Jibu: Wataalamu wazuri wapo, ila ukweli ni kwamba, hawatoshi. Hili ni tatizo. Mmmm, ni tatizo hili... Nchi ni kubwa na inayo mahitaji mengi. Na idara hii ni eneo lenye changamoto nyingi na kubwa. Hivyo kuna kila sababu ya kuwatambua kwa karibu wataalamu wachache waliopo na kuwathamini, na hili ni kwa idara zote zilizo chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Swali: Kuna mpango wa kutenganishwa kwa wapelelezi wa kesi za jinai na waendeshaji wa kesi za jinai, utekelezaji wake utaanza hili?

Jibu: Inatakiwa ieleweke kuwa, hapatakuwa na wakati wa mpelelezi na mwendesha mashitaka kufanya kazi bila ushirikiano wa karibu, kutokana na kutegemeana kwa kazi zao.

Kinachokusudiwa kufanyika ni kuiwezesha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka kuwa na waendesha mashitaka wa kutosha ili wao kama waendesha mashitaka, wafanye kazi ya kuendesha mashitaka na wapelelezi waimarishe kazi ya kupeleleza na kuwasaidia waendesha mashitaka kupata ushahidi.
Hivyo askari polisi wanaoendesha kesi leo kwa kupewa kazi hiyo na DPP, watapata fursa nzuri ya kufanya kazi za kupeleleza kesi za watuhumiwa mbalimbali. 
Uimarishaji wa mkakati huu ulishaanza, na mwaka ujao wa fedha tunatumaini, baadhi ya maeneo ya nchi yetu, wataanza kushuhudia kesi zikiendeshwa na maofisa kutoka ofisi ya DPP, kuanzia ngazi ya wilaya.

Swali: Hili la kutengenisha majukumu haya likifanyika, ofisi yako itakuwa na mamlaka gani ya kuhakikisha kesi zinaendeshwa katika muda unaotakiwa?

Jibu: Upelelezi ni taaluma iliyo na mafunzo, mbinu na miiko yake, na haitegemei zoezi la kutenganisha kazi ya upelelezi na uendeshaji mashitaka. Hivyo tangu awali wapelelezi wanatakiwa kupeleleza kesi kwa umahiri na haraka. 
Lakini ni matarajio yangu kuwa Ofisi ya DPP itakapoanza kuendesha kesi nchi nzima au katika maeneo machache, polisi waliokuwa awali wanahusika kwenye zoezi la kuendesha mashitaka, watapata fursa nzuri ya kuongeza nguvu kwenye eneo la upelelezi.

Swali: Unazungumziaje madai kuwa baadhi ya mawakili wa serikali hawana ujuzi wa kutosha, na kwamba mishahara midogo inawafanya baadhi yao, wajihusishe na vitendo vya rushwa?

Jibu: Ujuzi haununuliwi, unatokana na mafunzo na utendaji wa mtu mwenye bidii ya kujifunza, kuna mawakili wengi wanafanya kazi vizuri ingawa wana mishahara midogo.
Mshahara mdogo si kigezo cha kula rushwa. La msingi ni kuangalia jinsi ya kumwezesha wakili awe na mshahara mzuri, utakaomwezesha kupangilia mambo yake kwa uhakika, aweze kununulia vitabu vya kujisomea na nyenzo nyingine za kazi, jambo ambalo viongozi wetu wanapaswa kuliangalia kwa jicho makini.

Swali: Una maoni gani kuhusu watu wanaopinga mamlaka makubwa aliyonayo DPP?

Jibu: Katiba iko wazi, na sioni sababu ya kuliongelea hili. Huenda kinachoweza kuangaliwa ni kama kuna ukiukwaji au matumizi mabaya ya madaraka ya DPP. Unajua DPP kama taasisi, hawezi kuwa na tatizo, ila tatizo linaweza kuwa kwa mtu anayeweza kutumia madaraka hayo vibaya, kitu ambacho kitahitaji ushahidi.

Swali: Unaridhika na mfumo wa uendeshaji mashitaka hapa nchini?

Jibu: Siyo mmbaya, naweza kusema unaridhisha, lakini pia ni lazima nikiri kuwa kuna mapungufu yanayosababishwa na uhaba wa vitendea kazi.
Kama nilivyoeleza awali, wataalamu hawatoshi na kuna tatizo la mashahidi kutokupatikana kuja kutoa ushahidi, na hasa katika maeneo yaliyo na mila na desturi za kufanya mapatano ya kutozana fidia.

Swali: Ni tukio gani unalolikumbuka, liwe zuri ama baya katika maisha yako?

Jibu; Ninayo mambo mengi, lakini kubwa ni kesi ya MV Bukoba ambayo nilikuwa mwendesha mashitaka, nikimsaidia Wakili Mkuu wa Serikali W.C. Magoma.
Kesi hii ilikuwa ya mauaji, mamia ya watu walipoteza maisha yao, mashahidi wengi walipokuja mahakamani na kutoa ushahidi, ilinibidi kuwa makini sana, kulikuwa na mambo ya ajabu sana katika kesi hiyo, ni vigumu kuelezea, labda kama kuna siku nitaandika kitabu, nitaeleza kwa unaga ubaga.
Mahakama ilikuwa ikigubikwa na simanzi kila siku kesi hii ilipokuwa ikisikilizwa, kama binadamu, hata mwendesha mashitaka kuna wakati unakuwa na majonzi kama hao waliofiwa na ndugu na jamaa zao, lakini kazi kwanza, nilikuwa natakiwa kusimamia ukweli.

Swali: Tueleze historia ya maisha yako kwa mapana zaidi.

Jibu: Nimezaliwa Julai mosi, mwaka 1967, katika Kijiji cha Malya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, nikiwa mtoto wa mwisho kati ya watoto tisa wa familia yetu ya mzee Mussa Mbuki Feleshi na mama yangu Ruth N’gweshemi.
Baba yangu alikuwa mchungaji wa Kanisa la African Inland Church na mama alikuwa mama wa nyumbani.

Baba yangu alifariki mwaka 1973 kwa ajali ya gari na mama yeye alifariki mwaka 1991, wakati huo nikiwa mwanafunzi wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Nimesoma Shule ya Sekondari Shinyanga, baadaye nilijiunga na Shule ya Sekondari Galanos mkoani Tanga ambako nilisoma kidato cha tano na sita.

Baada ya kumaliza kidato sita nilijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT Ruvu).
Nilijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1991, nikichukua shahada ya kwanza ya sheria na kuhitimu mwaka 1994. mwaka 2003 nilirudi tena Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusoma shahada ya uzamili ya sheria (Masters in Law), nilihitimu mwaka 2005.
Kabla ya kuteuliwa kuwa DDP, nilikuwa Mwanasheria wa Serikali na kituo changu cha kazi kilikuwa mkoani Mwanza. 

 PhD in Law Criminology and Penology. Nina mke mmoja, Suzana Majija, ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Nyamagana mkoani Mwanza na tuna watoto wanne. 

0716 774494
www.katabazihappy.blogspot.com
facebook: Happy Katabazi

Chanzo;Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, April 15,2007

No comments:

Powered by Blogger.