Header Ads

FREEMAN MBOWE , ' DOZEE DOZEEE'

Na Happiness Katabazi
BINAFSI ni mpenzi mkubwa na shabiki wa 'kulia'wa Bendi ya FM Academia ' Wazee wa Pamba, Wazee wa Ngwasuma'. Siwezi kuficha hisia na mapenzi yangu kwa Bendi ya FM Academia, naipenda.

 Uongozi na wanamuziki  wa bendi hii wanalijua Hilo Kwani licha ya Kuwa shabiki wa bendi hii pia tangu inaanzishwa  bendi hii ilipokuwa na maskani yake Kinondoni nilikuwa nikiandika Habari za bendi hiyo na hadi Kwenye kibao Cha Heshima kwa wanawake uliotungwa na Roger Muzungu, Ndoa ya Kisasa uliotungwa  na Mwanamuziki wa bendi hiyo  Mule Mule ' FBI ' katika albamu yao mpya  ' Chuki ya nini'  wamelitaja jina langu.

Nawapenda sana wanamuziki na wananchi wanaotokea nchi ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Kwasababu wanajua kuvaa na Kupendeza,kumiliki stage, kuimba licha nachukia tabia ya baadhi Yao ya Kupenda kujipaka 'mikorogo' inayochubua ngozi  zao.

Tuwapo Kwenye maonyesho ya bendi zenye wanamuziki Wengi wa Kongo, uwa tunasikia neno ' Dozee Dozeee' au neno ' Malembe Malembe Malembe'.

Binafsi nimekuwa Nina ukaribu na wana muziki , mafundi wa nguo,wasusi wa nywele  raia wa Kongo. Nimekuwa nikiwauliza baadhi ya maneno ya Kiswahili  kwa lugha ya Kikongo yanamaana gani na yanatamkwane na wamekuwa wakinipa mAana na maneno hayo ya Kikongo kwa lugha ya Kiswahili yanamaana Fulani na yanatamkwa HIvi.

Kichwa Cha Habari Cha makala yangu ya Leo hapo kinasomeka (Mbowe  Dozeee Dozee). 
Makamu wa Rais wa Bendi ya FM Academia, Mule Mule amenipa Tafsiri ya maneno haya mawili Kikongo  yaani Dozee Dozee  na Malembe malembe kwa lugha ya Kiswahili.

Mule Mule amesema maana yake ' pole pole , tulia'.  Na Mimi Leo nimeona nitumie neno Dozee Dozee Katika makala yangu Kwani naona ndilo linalofaa kutumika Katika makala yangu ya Leo inayomaanisha ' Chadema, pole pole'

Septemba 14 Mwaka huu, Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrsia na Maendeleo ( CHADEMA) , Freeman Mbowe baada ya kushinda tena kwa Mara ya Tatu nafasi ya uenyekiti wa Taifa wa Chama hicho, Alitangaza maazimio Sita ya Mkutano Mkuu wa CHADEMA.

Moja ya azimio Hilo ambalo lilitangazwa na Mbowe ni ' Kwanza Chama  kishirikishe  umma  kuaandaa migomo  ya kila aina  na maandamano  isiyokuwa na kikomo ya nchi nzima   na   watu washirikishwe  Katika zoezi hili ili kushinikiza Bunge Maalum la Katiba linaloendelea Dodoma lisitishwe'.

Hakuna ubishi Kuwa bado Watanzania wanaipenda Amani na nchi Yao na wapo Tayari kuilinda kwa moyo wao wote isipokuwa kuna Dalili za wazi za Watanzania wachache sana  kwa matendo na Kauli zao yanathibitisha   wameichoka amani  tunayojivunia na wapo Tayari kuona na kushangilia siku  Tanzania ikiingia  Kwenye machafuko na kusababisha Amani yetu kutoweka. Hao ni wafuasi wa Shetani na wana mapepo.

Ni kweli baadhi ya watu tunakelwa na baadhi ya mambo yanayoendeshwa na serikali yetu lakini kama kiongozi mkubwa tena wa Kiongozi wa taifa  wa Chama Cha Chadema,Mbowe kutamka maneno ya aina ile Mbele ya Jamii ya wasomi, wastaarabu waliokuwa wakifuatilia mkutano ule  ni aibu kwake binafsi kwani yamemshusha hadhi yake mbele ya watu makini , wanazingatia utawala wa sheria .

Sheria ziko wazi kabisa na zinatoa haki kwa baadhi ya kada mbalimbali kufanya migomo, maandamano. Lakini Kwa tamko la Mbowe Kuwa Chadema wanafanya maandamano, migomo bila Kibali tena bila kikomo Si tu limemshushia heshima binafsi Mbowe na Chama Chake.

Pia  tamko limethibitisha  Itikadi ya Chadema  siyo nyingine isipokuwa ni vurugu  ' Anarchism'. Ndiyo mwelekeo waliochukua  kutokana na Hotuba ya Mbowe  tofauti na Itikadi Yao waliyoiweka Kwenye Katiba ya Chama chao.

Na katika Hilo, Chadema ni sawa na CCM ambayo imeachana kivitendo  na Itikadi yake ya Ujamaa na kujitegemea  na sasa imeamua  kufuata Itikadi ambayo haipo Kwenye Katiba ya CCM ambayo Itikadi hiyo ni kukumbatia Ubepari aina ya Uliberali Mambo Leo.

Hivi kulikuwa na ulazima wowote wa Mbowe kutoa tamko la aina hiyo Mbele ya hadhara  Kama ile Kwani  maelfu ya watu wa Kada tofauti walikuwa wakimtazama na kumsikiliza?

Tuliofundishwa somo la Uongozi na Utawala na Marehemu Dk.Sengondo Mvungi Katika Chuo Kikuu Cha Bagamoyo (UB), alitutajia Moja ya sifa ya kiongozi bora ni yupi .

Dk.Mvungi alisema Moja ya kiongozi bora ni kiongozi  Kuonyesha wananchi au wafuasi wake njia iliyosahihi, mwenye maono, kuonyesha dira na mwelekeo ,anayekubali kukosolewa na anayezingatia Utawala wa Sheria.

 Mbowe  ni aina ya kiongozi ambaye wakati mwingine  , anajikuta anafanya mambo kufurahisha jukwaa tu kwani kiongozi makini huchunga matamko yake au kupima madhara ya kauli zake kwa wananchi wasio na hatia ambao wanaweza kuburuzwa  kwa kauli yake.

UKAWA  ilishasema   tangu zamani Kuwa imegoma kushiriki vikao Vya Bunge Maalum la Katiba linalooendela kufanya kazi yake kwa kasi ya ajabu mjini Dodoma na Tuliwasikia na waliowaunga  mkono waliwaunga mkono, tuliyowapuuza Ukawa tuliwapuuza na kuwafananisha na vikatuni .

Migomo ya nini tena Mbowe  si mlishagomea bunge la Katiba ? Mlishafanya mikutano nchi nzima mkitaka bunge hilo lisitishwe? Mlishasema nyie mnawakilisha wananchi walio wengi? Hivi ndo tuseme Katika  mikutano yote mliyohutubia wananchi hawakuwaelewa? 

Ikiwa hawakuwaelewa wakati ule mmetoka ndani ya Bunge   watawaelewa sasa? Kama mnafikiri  hamjaeleweka hamuoni kuwa hiyo ni ishara wananchi wamewapuuza?

Hebu jitafakarini upya ikiwa bado mna sapoti ya wananchi. Hakuna haja ya kuweweseka acheni bunge liendelee wakati wa kupiga kura ya maoni ndio tutaona na kuthibitisha ukweli wa kauli zenu kama je mawazo yenu ndo ya wananchi au la? Ikiwa wananchi wengi watasema hapana? Hapo tutafahamu kweli UKAWA  waliwakilisha Katiba  ya wananchi. Mmeishaongea na Rais Jakaya Kikwete Vya kutosha. 

Sasa tulieni subirini kura ya maoni. Kuendelea kuweweseka na kutapatapa mtafikiri mmepandisha mashetani ni ishara ya kushindwa  kama mfa maji. Maana ni kama mtu anatishia nyau mtu mzima. Nchi hii haiwezi kuendeshwa kwa mikwala Mbuzi.

Bunge Maalum la Katiba chini ya  Mwenyekiti wake Samwel Sitta ndiyo linazidi kuchapa Kazi kwa kasi ya ajabu licha ya Ukawa kila kukicha Inarusha  makombora na wajumbe wa Bunge Hilo nalo wamekuwa wakirusha makombora kwa Ukawa.

Mbowe Katika tamko lake alimshambulia Sitta wazi wazi Kuwa analiburuza Bunge Hilo na anashangaa jeuri hiyo anaupata  wapi ya kuliburuza Bunge Hilo.

Watu wenye akili timamu tunajiuliza HIvi wale wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba ni majuha na Matahira hadi Wakubali kuburuzwa na mtu  mmoja ambaye ni Sitta na wao wanakubali?

Maana hadi sasa  Hakuna lalamiko lolote limetolewa hadharani  na wajumbe wanaohudhuria  Bunge Maalum la Katiba Kuwa Sitta anawaburuza.Tumuulize Mbowe hayo ameyapata wapi?

Na hata Kama wajumbe wale wanaoshiriki Katika Bunge Maalum la Katiba ni kweli wanaburuzwa na Sitta, Mbowe na Ukawa kinawawasha kitu gani? 

Maana wao wamesusa kwenda Katika Bunge Hilo  sasa hayo maumivu na Kichefuchefu , kiungulia kinachowakera  na tabia ya Sitta ya kuliburuza bunge , vinawapataje wakati wao siyo wanaburuzwa?

Minafanamisha  hoja ya Mbowe ya kutaka maandamano na migomo ifanyike nchi nzima ili kushinikiza Bunge la Katiba lisitishwe, ni sasa na ' mume aliyemuacha Mkewe ,Mpenzi wake kwa Hila akisikitishwa Yule Mpenzi wake siku zote hatapata Mwenza   ...sasa siku Yule Mke akipata Mwenza  mpya akaanza kumtunza na kupendezesha ,mwanaume wa zamani anaibuka na Kusema ameibiwa Mke na uzushi wa kila aina.Kioja.

Sasa mfano huo ndiyo sawa sawa na Ukawa ambao walifikiri walivyosusia wao kushiriki Vikao Vya Bunge la Katiba, ndiyo wajumbe wote wa Bunge Hilo wangetusaidia, Kumbe wajumbe wengine tena Wengi wanashiriki Bunge Hilo na Matokeo yake Ukawa wamebaki wakibwata bwata mitaani   Kama Mbwa Koko eti Bunge Hilo kuendelea  na Kazi ni sawa na wizi na matumizi Mabaya ya Fedha za umma.

Hivi Tumuulize huyu Mbowe na Ukawa yake ,anafahamu maana ya neno wizi? 
Neno wizi limetafsiriwa Katika Kifungu Cha 257 Cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya Mwaka 2002.

Kifungu hicho kinasema Wizi maana yake ni  kuchukua au kuhodhi mali ya mtu mwingine inayohamishika. Mbowe sasa  atuambie Bunge Maalum La Katiba limechukua au kuhodhi Mali gani  na Mali hiyo ni ya nani ?

 Na Kama anaushahidi Bunge Hilo limeibia  licha mwenye jukumu la Kusema Fedha serikali zimeibwa au zimepotea ni Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali, Luovick Utto ambaye hata hatujamsikia akitoa ripoti yake Kuwa Bunge Maalum la Katiba limeibia Fedha za Watanzania Si Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya Mwaka 2002 Ina mruhusu Mtu yoyote kwenda kuomba Kibali mahakamani ili aweze kuendesha binafsi Kesi ya jinai. Na Mahakama pia ndiyo ina mamlaka ya kusema fulani ameiba.

Sasa mnasubiri nini kufanya hivyo Matokeo yake mnapayuka payuka mitaani?

Mama yangu Mzazi kila siku anasema mwanaume ameumbwa na koromeo na mwanaume  aliyekamilika uwa ni Mtendaji na siyo mpayukaji. Sasa inakuwaje hawa  wanaume  Kutwa kupayuka kupitia vyombo Vya Habari kuhusu Bunge la Katiba wakati wa wamelisusa?

HIvi mmeishiwa ajenda hadi kila siku mtoe matamko ya kujirudiarudia  kila siku kuhusu Bunge la Katiba? Hakuna aliyewafukuza, mlijifukuza wenyewe, kelele na kebei 
 za nini?

Chadema na vyama vingine va NCCR, CUF mmesusa kwenda Bungeni lakini kuna baadhi ya Watanzania wazalendo wao wamekataa Kususa  ,wanaendelea na Kazi na mwisho wa siku historia itaandikwa Kuwa mwanasiasa Mbowe na wenzake hawa kutaka Katiba mpya upatikane.

Kwanza Mbowe anapaswa Kuonyesha idadi ya namba na Majina ya Watanzania wanaotaka Bunge Hilo lisitishwe ili tujue ni Watanzania wangapi.

Maana kisheria wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wametokea Makundi mbalimbali ya wananchi na hivyo wamekwenda Bungeni kuwawakilisha wananchi , na wajumbe wa Bunge waliosusia Bunge Maalum la Katiba ni wachache na Wengi wanaendelea kushiriki vikao.

Sisi  Watanzania wenyewe tuliruhusu  Demokrasia  iingie nchini kwetu na siku zote maamuzi ya Wengi ndiyo maamuzi umma wote. 

Sasa wajumbe Wengi ndiyo wanashiriki Bunge Maalum la Katiba na hawa wachache wamesusa , hivyo Wengi wameshinda ndiyo maana Taasisi  zote za dola zimebariki  Bunge hilo liendelee na kweli linaendelea na Kazi zake tena kwa kasi na muda Si mrefu   Bunge Hilo litatupatia  Katiba inayopendekezwa na Bunge Hilo Maalum.

Na kwasababu hiyo basi hoja ya Ukawa iliyokuwa ikitaka Bunge Hilo lisitishwe ilifeli tangu mapema na Kama mtakumbuka  makala yangu ya Agosti 3 Mwaka huu, iliyokuwa na kichwa Cha Habari kisemacho ' UKAWA RUDINI BUNGENI' , nilieleza wazi UKAWA wanakosea na mbinu wanayoitumia hawatafanikiwa na walilolikusudia halitafanikiwa.

Kiongozi yoyote makini hawezi kutoa tamko Kama alilolitoa Mbowe ambalo ni dhahiri tamko Hilo linaamasisha wananchi washiriki Katika vitendo Vya Uvunjifu wa Sheria.

Mbowe uone Haja ya Kufuta Kauli yako kuhusu tamko Hilo Kwani Tayari limeishakuweka Kwenye rekodi chafu Katika vichwa Vya Watanzania wazalendo na wapenda Amani Kuwa wewe ni kiongozi unayoipenda vurugu.

 Mbowe tambua  Watanzania hao Hao waliokuwa  wakikushangilia  siku ulipokuwa ukitoa tamko Hilo bado wanaipenda nchi Yao na hawapo Tayari Kumuunga mkono mtu  anayetaka kuivunja Amani na mshikamano wao.

Na kinachonishangaza   ni unafki na ubaguzi unaofanywa na Jeshi la Polisi hasa inapofikia wakati wa  kuwachukulia Hatua watu wanaotoa maneno ambayo yanaamasisha  watu wawatendee vitendo Vya Uvunjifu wa Sheria na Amani.

Mbowe na Chadema wakitoa matamko ya aina hiyo Jeshi la Polisi uwa linawabembeleza na kutowachukulia Hatua za haraka. 

Lakini maneno Kama hayo aliyotamka Mbowe angeyatamka 'Mume wangu', Sheikh Ponda  au Swahiba wangu Mchungaji Chistopher Mtikila. 

TUngeshuhudia Makachero   wa Polisi wakiwa na Pisto  viunoni huku wakiwa wamevaa nguo za kirai na hawajachomekea mashati wakimwagwa mitaani , misikitini na kila kona kuwasaka haraka kuwakamata na kupelekea jarada la Kesi ofisi ya DPP  na ndani ya jarada Hilo wangeambatanisha na taarifa ya Siri ya kipelelezi  ya kumwarifi DPP siku atakapomfungulia Kesi Sheikh Ponda, amfungie dhamana kwasababu taarifa za 'kishushushu' walizozikusanya zinaonyesha mtu Huyo akipewa dhamana ataatarisha Usalama wa nchini. 

Na Mifano hiyo ni hii hapa nilishuhudia na Polisi wanalijua Hilo mAana uwa wananivutaga pembeni wananipa umbea ' Ubuyu': 

Agosti 19 Mwaka 2013 ,mchana Katibu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu nchini Sheikh Ponda Issa Ponda afunguliwa Kesi ya uchochezi  Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro na Mkurugenzi wa Mashitaka , alifunga  dhamana na hadi sasa Ponda yupo Katika gereza la Segerea kwa kukosa dhamana kwasababu DPP alimfungia dhamana .

Kwa mujibu wa kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, DPP anayo mamlaka ya Kuzuia dhamana  ya mshitakiwa yoyote hata Kama makosa yanamkabili mshitakiwa Husika yana dhamana.

Agosti 19 saa mbili asubuhi Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisuti, Mkurugenzi wa Mashitaka akamfutia Kesi ya kufanya uchochezi Na.144/ 2013 Katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Sheikh Ponda Issa Ponda chini ya Kifungu cha 91(1) Cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya Mwaka 2002.

Oktoba 18 Mwaka 2012 Ponda na wenzie 49 walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa makosa ya uchochezi , kuingia kwa jinai katika kiwanja cha Chang'ombe Markaz.Na DPP akiwasilisha hati ya kumfungia Dhamana Ponda na Mukadamu Swalehe tu ambao walisomea gerezani hadi siku ya hukumu Kesi hiyo ilipotolewa Mei 9 Mwaka 2013 ambapo washitakiwa wote waliachiliwa Huru isipokuwa Ponda peke yake ndiyo alitiwa hatiani kwa kosa Moja tu la kuingia kwa jinai katika kiwanja hicho kati makosa manne ambapo alimfungwa Kifungo Cha Mwaka mmoja nje na Mahakama ikamtaka awe raia mwema. 

Machi 21 Mwaka Jana, wafuasi  52 wa Sheikh Ponda ambao nao walikuwa wakikabiliwa na Kesi ya kufanya maandamano haramu na kukaidi amri ya Jeshi la Polisi iliyowataka wasiandane hadi Ofisi ya DPP kushinikiza DPP ampatie Ponda dhamana ,  aliyekuwa Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Sundi Fimbo  aliwahukumu   Kifungo Cha Mwaka mmoja Jela baada ya kuwakuta na hatia ya makosa hayo.

Wafuasi hao kupitia wakili wao Mohamed  Tibanyendera hawakuridhika na hukumu hiyo  ya Mahakama Kisutu , walikata rufaa Mahakama Kuu Kanda  ya Dar es Salaam.Rufaa hiyo iliyokuwa ikisikilizwa na jaji Salvatory Bongole .

Oktoba 21 mwaka 2013 Jaji Bongole   alitoa hukumu na kusema  kuwa mahakama yake imekataa kuwaachilia huru warufani hao katika kosa la pili ambalo ni la kufanya maandamano haramu kwenda ofisi ya DPP na pia mahakama yake imekataa kuwaachilia huru katika kosa la tatu la kukaidi amri ya Jeshi la Polisi iliyokuwa ikiwataka  watawanyike na kwamba  Mahakama ya Kisutu  Ilikuwa  sahihi kuwatia hatiani katika makosa hayo mawili.

Hata hivyo Jaji Bongole alisema pamoja na Mahakama yake kuwatia hatiani Katika makosa hayo mawili ambapo  kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi , mshitakiwa yoyote anayepatikana na hatia ya makosa ya aina hiyo anatakiwa ahukumiwe Kifungo Cha Miezi mitatu na kulipa faini ya sh. 50,000 , hivyo Mahakama ya Kisutu ilikosea kuwahukumu Kifungo Cha Mwaka mmoja Jela na kwamba warufani Tayari wameishakaa Jela muda mrefu na Adhabu ya Miezi mitatu imeishapatikana na akawaachiria Huru.

Hivi maneno Yale aliyotamka Ponda Mkoani Morogoro na Yale aliyotamka Mbowe HIvi karibuni si ni yote yana amasisha watu washiriki vitendo vya Uvunjifu wa Sheria na Amani?

Mbona Jeshi la Polisi haikumbembeleza Ponda Kama linavyo mbembeleza na kumlambalamba Mbowe? Jeshi la Polisi lilimkamata Ponda kihuni kule msikiti wa Temeke  kwa kumpiga ngwara na Kisha Likaja kumkamata kule Morogoro tena Ponda akiwa na jeraha bichi la risasi  alizopigiwa na watu wasiyojulikana na akasome wa Mashitaka akiwa Amelazwa Katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili?

Tuliulize Jeshi la Polisi, Mahakama, Ofisi ya DPP zina maslahi gani na baadhi ya viongozi wa Chadema? 

Hii si Mara ya kwanza    kwa baadhi ya viongozi wa Chadema kutoa matamko ambayo yana amasisha wafuasi wake washiriki vitendo vya uvunjifu wa sheria  hawaguswi na ikitokea wakiguswa na dola kwa wengine kufunguliwa Kesi mahakamani , Mahakama na Ofisi ya DPP haizipi uzito mkubwa Kama vile Mahakama iliyokuwa ikitoa Uzito wa aina yake Katika ile Kesi ya wafuasi 52 wa Ponda pale Mahakama Ya Kisutu ambayo isiendeshwa mfululizo ndani ya  siku 33 tu ikamalizika na wakahukumiwa.

Na kesi ya uchochezi iliyokuwa ikimkabili Ponda katika mahakama ya Kisutu iliyofunguliwa Okoba 18 mwaka 2012 na ikamalizika Mei 9 mwaka 2013 .Yaani ilimalizika ndani ya miezi sana tu na ilikuwa ikiwndeshwa mfululizo na mahakama na ofisi ya DPP ilikuwa ikiipa uzio wa aina yake na mwisho wa siku. ' mume wangu Ponda ' alikutwa na hatia.

Sasa inakuwaje kesi zinazowakabili wanasiasa wengine ambazo pia zina Mashitaka ya Uvunjifu wa Amani, Mahakama na ofisi ya DPP  haizipi kipaumbele Hali inayosababisha baadhi ya watuhumiwa kuendelea Kuwa na jeuri ya kuendelea Kutenda matendo ambayo ya yana amasisha watu washiriki kuvunja Sheria za nchi?

Ningali nikikumbuka bado , Desemba 24 Mwaka 2012 , Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Zainabu Mruke  alitupilia Mbali la kuomba apatiwe dhamana Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira Mkoa wa Pwani,  Hassan Othman Hassan' Hassanor' anayekabiliwa na Kesi ya kusafirisha   Pembe za ndovu zenye kwenda Hong Kong ,China zenye thamani ya Sh. Bilioni 1.1

Jaji Mruke alitoa uamuzi wa kukubaliana na ombi la Wakili wa upande wa jamhuri  la kumnyima dhamana HASSANOR kwasababu ametenda kosa jipya wakati Tayari anashitakiwa Katika Kesi nyingine Na.209/2011 ya wizi wa madini ya Shaba yenye thamani ya Sh.milioni 400 iliyokuwa Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu lakini hata Hivyo Mwaka 2013 ,HASSANOR alishinda Kesi hiyo lakini bado yupo gerezani kwasababu bado Anakabiliwa na Kesi hiyo kusafirisha Pembe za ndovu 

Taasisi husika hasa Polisi iache tabia ya kuwafumbia macho na kuwakumbatia baadhi ya watu wanaotenda makosa kwasababu inazozijua zenyewe lakini wakati huo watu wengine aina ya Ponda na Mtikila wakitoa matamko ya aina hiyo ,Jeshi la Polisi linawavalia njuga na kuwakamata na kuwafikisha mahakamani na Ofisi ya DPP Kuwasilisha hati ya Kuwafungua dhamana.

Nimalizie kwa kumuasa Boss wangu wa zamani Mbowe Kuwa akubaliane na maana ya Msemo huu   maarufu Kuwa siku zote na popote Dunia ' dola uwa alichezewi'. Na Mhimili wa Serikali una Nguvu kubwa na pindi uamuapo kumshughulikia mtu, Mtu Huyo uumia yeye na familia yake.

Mifano ipo hai na wala si ya kutafuta kwa wale waliokuwa wanajifanya wapo juu ya sheria na dola halina jeuri ya kuwashughulikia , Walibadilishiwa kibao na dola Hilo Hilo walilokuwa wakilichezea na  walishughulikiwa kikamilifu tena wengine walikuwa ni viongozi wa kubwa wa serikali Leo hii wana nidhamu ya Hali ya juu na wengine wamefilisika kabisa na wengine Kupata Maradhi ya kudumu yaliyosabishwa na ' displine' toka Kwa dola.

Mwisho ,Kama ni muungwana na unataka uendelee kuweka rekodi yako  nzuri Katika medani ya siasa nchini, ni vyema ungefuta  tamko  Lako  Kwani Watanzania walikushudia  ukitoa tamko lile na wamekuweka  Kwenye Kumbukumbu zao  Kuwa wewe ni kiongozi ambaye unaamasisha vurugu nchini.

Aidha na wataka Watanzania wote wasikubali  kutekeleza kwa vitendo agizo Hilo la Mbowe Kwani mwisho wa siku watajikuta wanakamatwa wao binafsi na kufikishwa mahakamani na siku zote kushitakiwa kwa Kesi ya jinai ni kubaya  Kwani kunaleta Usumbufu.

Wananchi Hao wa mwambie  Mbowe na wapenzi wake  ndiyo wawe wa kwanza kuingia mtaani kuandamana ili Polisi wawaone vizuri na wawape kisago vizuri. 

Maana wanaisiasa wetu hasa wa vyama va upinzani wamekuwa na tabia chafu ya kuwatia ujinga watoto wa wenzao waandamane na washiriki maandamano haramu ,mwisho wa siku watanzania hao maskini wanajikuta wakiambulia vipigo kutoka kwa polisi lakini viongozi hao wa waliwatia ujinga wananchi wa kawaida waandamane wao siku ya maandamano hawaji wanakuwa majumbani kwao.

Na hii tabia chafu ya wanasiasa, imewaghalimu sana baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu kama Chuo Kikuu Dodoma, UDSM , madaktari kwani ilidaiwa kuna chama kimoja ndicho kilikuwa kikiwatumia wanafunzi wa vyuo na madaktari kuzusha migomo kila kukicha ili nchi isitawalike na kweli wanafunzi hao walizidisha migomo matokeo yake wakasimamishwa masomo na wengine 50 kufunguliwa Kesi katikaa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa  kushiriki maandamano haramu.

Wanafunzi wale ambao wakati mwingine walikuwa wakikosa hata nauli ya Kuja kuudhulia Kesi ya mahakamani,Hakuna mwanasiasa yoyote Aliyekuwa akifika mahakamani pale hata kuwapa hela ya Kunywa chai.

Ndiyo Watanzania muwafahamu aina ya wanasiasa hasa wale wanasiasa ambao wanaamasisha wananchi wao watende matendo ya kuvuruga Amani na muwapuuze, hawa Tayari wanamahela Yao na wana majumbani Yao nje ya nchi hata Tanzania Leo hii ikiingia Kwenye machafuko ya wenyewe kwa wenyewe wanauwezo wa kukimbia nchi na kwenda kuishi nje ya nchi.

Sisi Malofa na tusioweza kukimbia tutafia hapa hapa.Tusiwape nafasi viongozi wapuuzi wa aina hiyo ambao uenda Kabla ya Kupanda majukwaani kutoa matamko uenda wanatumia kwanza 'ulevi Fulani ambao uharibu akili zao kwa muda. Freeman Mbowe  'Dozee Dozee'.

Mungu ibariki Tanzania
0716 774494
Facebook: Happy Katabazi
Blog: www.katabazihappy.blogspot.com
Chanzo: Gazeti la Rai, Septemba 18 Mwaka 2014

No comments:

Powered by Blogger.