Header Ads

PROFESA SARONGA: UWEKEZAJI INJINI YA MAENDELEO




PROFESA SARONGA: UWEKEZAJI INJINI YA MAENDELEO

Happiness Katabazi (UB)
ENEO   la majadilio ya biashara na uwekezaji nchini limekuwa likilalamikiwa na wananchi kila kukicha Kuwa haifanyi vizuri kwasababu ya wataalamu wa eneo Hilo kukosa maarifa na mwisho wa siku  kujikuta  taifa limeingia  mikataba na wawekezaji wa kigeni ambayo mikataba hiyo hailinufaishi taifa letu. 

 Katika makala hii  Mwandishi amefanya mahojiano na  Mkurugenzi wa Mtanganamo wa Biashara toka Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Lucas Saronga (60), ambaye ameichambua kwa kina eneo hilo kitaalamu.

Swali: Umepokeaje Hatua ya Seneti ya Chuo Kikuu Cha Bagamoyo(UB), kukutunuku wewe Lucas Saronga Kuwa   Profesa wa UB?

Jibu: Kwa kweli nimeipokea hatua hii kwa unyenyekevu na shukurani kwa vile sikuwahi kuamini ningeamka siku moja na kuitwa Profesa kwa kuzingatia umahiri wa masuala ambayo nimekuwa nikiyashughulikia kwa muda mrefu, hususan ya majadilano ya biashara na uwekezaji chini ya mfumo biashara za  Kimataifa wa WTO.

 Swali: Wewe ni Mkurugenzi wa Mtangamano wa Biashara, Wizara ya Viwanda na Biashara. Kwa Kuwa UB wameishakutangaza Kuwa wewe ni Profesa wa chuo hicho, je una Mpango wa kwenda kufundisha Katika chuo hicho?

Ndiyo niko tayari baada ya kustaafu kazi Serekalini  na  iwapo sitapewa nafasi ya kuendelea kutumikia Serikani kwa mkataba baada ya kustaafu kwa vile bado ninao uwezo wa kuendeela kulitumikia taifa langu.

Swali: Tueleze, wewe umebobea Katika eneo gani kwa mujibu wa taaluma uliyosomea?

Nimebobea zaidi kwenye masuala ya biashara na uwekezaji na kujikita zaidi kwenye majadiliano yanayoendelea  ya  Duru la Biashara la Doha (Doha Development Round) chini ya Shirika la Biashara Duniani (WTO).  Katika majadiliano haya, nilikuwa ninaongoza kundi la nchi zote changa (least developed countries-LDCs) 49 zilizo wanachama wa WTO kwa miaka 9 katika Mkataba wa Urahisishaji wa Biashara (Trade Facilitation Agreement) uliokubaliwa Bali, Indonesia mwishoni wa mwaka 2013.  Mkataba huu una maslahi mengi  kwa nchi zinazoendelea na zile changa kama Tanzania iwapo utekelezaji wake utasimamiwa vizuri kwa kuzingatia yale tuliyokubaliana, hususan kutujengea uwezo wa kuutekeleza.

Swali: Wewe ni miongoni mwa Watanzania wawili toka Wizara ya Viwanda na Biashara nchini mkiishiriki Katika Mafunzo ya jinsi ya Kujadili mikataba ya Biashara na uwekezaji iliyofanyiwa kwa siku 14 Tanzania na kushirikisha nchi 13 na Mafunzo hayo ambayo yaliratibiwa na UB na kufadhiliwa na Taasisi ya Nordic Africa, Ya Chuo Kikuu Cha Uppsalla nchini Sweeden.Una maoni gani kuhusu Mafunzo hayo ambayo Tanzania ilikuwa ni Mwenyeji? 

 Jibu: Nilikuwa ni  Mkufunzi  na nilitoa mada ya historia ya WTO , tuko wapi kwenye majadiliano, jinsi ya kusimamia maslahi ya nchi zinazoendelea na zile changa, adhari kwa nchi zetu kama hatutasimamia kidete maslahi yetu na tujikwamue vipi kutoka hapa tulipofikia kwenye majadiliano yaliyodorora hususan yale yanayohusu kilimo.  Hata hivyo, ni kweli tulikuwa na Watanzania wawili walioshiriki , mmoja akitoka Wizara ya Viwanda na Biashara na mwingine alitokea Zanzibar 

Swali: Wewe ni Ofisa Mwandamizi wa serikali , tueleze Hali ya uwekezaji Tanzania? 

Jibu: Kwa kifupi, hali ya uwekezaji Tanzania ilianza kupanda kuanzia mwaka wa  1990 chini ya Mpango wa Serikali wa kufufua uchumi (Economic Recovery Programme) baada ya Serikali kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa kupitia Mwongozo wa Uwekezaji katika Uchumi wa soko (Market-oriented Investment Code).  Hali hii ilivutia sana wawekezaji kwa vile walikuwa na uhakika wa ni nini yatakuwa matunda yake (predictability), kwa vile Serikali iliondoa ama kulegeza masharti na uthibiti wa uwekezaji.    Kabla ya hapo, ukiangalia fedha za uwekezaji wa kigeni (foreign direct investment) za dola za Kimarekani milioni 757 zilizoingia Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kuanzia 1970-1990, asilimia 90 ziliingia Kenya iliyokuwa na uchumi wa kibepari ukilinganisha na asilimia chini ya  10 tu zilizoingia Tanzania iliyokuwa inafuata uchumi wa kijamaa.  Hata hivyo, kutokana na mwitikio mdogo wa sekta ya watu binafsi kwenye Nyanja ya uwekezaji, Serikali ilanzisha sheria ya uwekezaji mwaka wa 1997 baada ya   kuanzishwa kwa sera ya uwekezaji mwaka 1996.  Kutokana na hatua  za serikali, uwekezaji ulipanda kutoka dola za Kimarekani milioni 12 mwaka 1992 hadi kufikia dola milioni 260 mwaka 2004 ambacho kilikuwa ni kipindi cha Serikali ya awamu ya tatu.  Kuna wakati ukuaji wa uwekezaji ulifikia kilele cha dola za Marekani milioni 515 mwaka 1999. 

Kuanzishwa kwa Kituo cha Uwekezaji (Tanzania Investment Centre-TIC) kuliendelea kuweka na kuimarisha  mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kukuza uwekezaji (promote), kuratibu uwekezaji, kuweka vichocheo/motisha kwa wawekezaji wa nje, kuondoa ukiritimba wa uwekezaji na Serikali kujiondoa kwenye kuingilia moja kwa moja miradi ya uwekezaji wa sekta binafsi.

Kuanzia Mwaka 2005  miradi iliyosajiliwa na kituo cha TIC mwaka wa 2005 utaona ni 550 ambayo kufikia mwaka wa 2008 ilipanda na kufikia  871 japokuwa hii nayo ilishuka tena mwaka wa 2009 kutokana na mdororo wa uchumi duniani na baadaye kuanza kupanda tena.  Tunaweza kusema fedha za uwekezaji wa kigeni ulikuwa Dola za Kimarekani millioni  403 mwaka wa 2006 na kufikia Dola zaidi ya milioni 1500 mwaka wa 2012.  Hali hii inatarajia kuendelea kupanda kutokana na upatikanaji wa gesi asilia na utafutaji wa mafuta unaoendelea, hatua mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali kwa ajili ya kukabidhiana na changamoto za uwekezaji kama vile upatikanaji wa umeme wa uhakika, ujengaji wa miundombinu, kuanzishwa kwa sheria ya ubiya wa Serikali na sekta Binafsi (Public-Private partnership), kutangaza kwa bidii fursa za vivutio vya uwekezaji tulivyonavyo kwa kupitia, TIC, TTB, TANTRADE,EPZA na kadhalika.

Swali: Unazungumziaje Sekta ya uwekezaji nchini hasa ukizingatia wewe ni mtaalamu Katika eneo Hilo?

Jibu:     Ni lazima tujue kuwa, kimsingi uwekezaji ni mzuri na ni wa muhimu kwa vile ni injini ya maendeleo ya uchumi kwa nchi ye yote.  Hakuna nchi hata moja itasema haina haja na kuvutia uwekezaji. Ndiyo maana nchi nyingi hutumia gharama nyingi wakati wa kukuza na kuvutia huu uwekezaji (promote)  ikiwa ni pamoja na kutoa vivutio vizuri zaidi kwa wawekezaji ili kushindania uwekezaji huu kati ya nchi na nchi kama vile kutoa misamaha ya kodi kwa kipindi fulani(tax holidays), misamaha ya ushuru wa forodha na kadhalika.

Pamoja na yote haya, uwekezaji unaoleta matatizo ni ule ambao haupo kwa ajili ya maendeleo endelevu (sustainable development).  Mikataba mingi ya uwekezaji inayosainiwa kati ya nchi na nchi (bilateral investment treaties –BITs) ndiyo ina kasoro zake.   Siku za karibuni kumekuwepo na wimbi la mabadiliko duniani la kuwa na muundo wa kuthibiti uwekezaji wa kimataifa (international regulatory framework).  

Nchi nyingi siyo zile tu  za Afrika zimejikuta zikitiliana sahihi mikataba ya aina hii kati yake na nchi zingine hususan kwa kutumia  modeli ya Marekani ya uwekezaji.  Mikataba hii nia yake ni kulinda na kukuuza uwekezaji hususan kwa kumlinda zaidi mwekezaji kwa kufafanuliana vipengele vipi vitumike kwenye kulinda  na kukuza uwekezaji huu.  Nchi nyingi zimejikuta katika hali ambayo hata Serikali inaweza kushtakiwa kwenye mahakama ya kimataifa na kampuni binafsi kwa vile tayari ilishajifunga na vipengele vya aina hii kwenye utatuzi wa migogoro (investor-to-state dispute systems).

Swali: Unafikiri Tanzania inafanya vizuri Katika eneo la uwekezaji na Kama haifanyi vizuri ungependa nini kifanyike ili Iweze kufanya vizuri?

Jibu:  Kwa ujumla Tanzania inafanya vizuri sana kwenye uwekezaji ukilinganisha nan chi nyingi zinazoendelea na zile changa hususan zile za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo kwa mfulilizo wa miaka mitatu iliyopita imekuwa ikiongoza kwa asilimia kama 45 kutokana na takwimu za Kamati ya Biashara na Maendeleo ya Umoja wa Mataifa- UNCTAD.

Swali: Kuna Madai Kuwa Kuwa Tanzania haifanyi vizuri kweli Sekta ya uwekezaji na Kama dai Hilo ni la kweli , unashauri nini kifanyike ili Tanzania iondokane na tatizo Hilo la kuanda kuingia mikataba na wawekezaji wa kigeni ambayo haifaidishi Taifa letu?

Jibu: Kama nilivyoeleza hapo awali, siyo tu nchi changa zinazojikuta zimeingia kwenye matatizo yaliyosababishwa na vipengele vya mikataba iliyosainiwa.  Kwa mfano, nchi nyingi zinazoendelea kama vile Afrika ya Kusini, India, Ecuador, Venezuela na Bolivia zimeanza kushtuka baada ya kukumbwa na mashtaka mengi kutoka kwa wawekezaji.  Afrika ya Kusini baada ya kutathmini BITs iliyosaini na nchi mbali mbali, iliamua haitasaini tena mikataba mipya ya aina hii; na kwamba itajitahidi kujiondoa kwenye mikataba ya zamani au kuijadili tena kwa upya.  Na hapa, ni vizuri ieleweke kuwa kwenye Mikataba mingi  (BITs)  ni vigumu kuachana nayo kwa vile mara nyingi ukishaisaini inakuwa na kipengele cha “survival clause” ambapo nchi inakuwa imejifunga na kuendelea na utekelezaji wa Mikataba hiyo kwa miaka 10-15 hata kama imeshasitisha mkataba.  Mwaka 2012, India nayo ilianza kutathmini BITs zote na ikaamua haitakubali kipengele cha “investor state dispute” pamoja  na Australia ambayo ni nchi iliyoendelea kuamua kuchukua  hatua ya namna hii mwaka wa 2011.

Swali: Unafikiri  wasomi Katika eneo Hilo la jinsi ya kujadili mikataba ya Biashara na uwekezaji nchini wana tosha? Kama hawatoshi nini kifanyike? 

Jibu: Kwa uzoefu wangu mdogo niliokuwa nao, naona kuwa wasomi hawatoshi kwenye maeneo haya ya majadiliano ya biashara na uwekezaji.  Kinachotakiwa kifanyike ni  kuanzisha masomo haya vyuo vikuu ili kutoa wahitimu  wengi (critical mass) waliobobea kwenye maeneo haya.  Ni msingi huu ninaamini nafasi niliyopewa kwenye Chuo cha Bagamoyo kitaniwezesha kuanzisha fani hii ambayo wanafunzi wataweza kutathmini na kufanya kazi ya uchambuzi, kutayarisha mada chokonozi kwenye masuala mbalimbali yanayojitokeza kwenye biashara za kimataifa na za kikanda, ikiwa ni pamoja na majadiliano ya biashara kwa kulenga zaidi uchumi wa nchi zinazoenedelea na zile changa. Hii itasaidia kutoa upeo zaidi  kwa wenye kutayarisha sera mbalimbali (policy makers), wanaofanya majadiliano ya biashara na uwekezaji (trade and investment negotiators), washauri  na wafanya utafiti kwenye maeneo husika kwa vile mara nyingi kozi hii itakuwa inawaanda kihalisia/kwa vitendo jinsi majadiliano yanavyoendeshwa (simulation).  Kutokana na mafunzo haya, wahitimu wanaweza kutathmini kwa mfano, ni nini athari za mwelekeo mpya unaojitokeza wa kufanya biashara za kikanda (new regional trade architecture)kwa nchi changa kama inavyojitokeza sasa hivi kwenye Mikataba ya Ubiya ya Biashara na Uwekezaji kati ya Marekani na Nchi za Jumuiya ya Ulaya “ the Trans-Atlantic Trade and Investment  Partnership” na majadiliano yanayoendelea kati ya Jumuiya ya nchi za Ulaya na Afrika, Karibean na Pasifiki (Regional Comprehensive Economic Partnership). Ni dhahiri kuwa, mwelekeo huu wa kikanda unaweza kuathiri biashara ya kimataifa chini ya mfumo wa WTO.

Swali: Je hapa nchini Kuna Chuo Kikuu chochote Kinachotakiwa  kozi ya jinsi ya kujadili mikataba ya Biashara na Uwekezaji?

Jibu: Ninavyokumbuka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kikishirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara kilianzisha Kozi ya namna hii kwa kufadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Denmark –DANIDA chini ya  Mradi wa kuongeza uwezo wa majadiliano ya biashara.  Wakati huo tulikuwa  watu wawili tunaotoka Geneva kuja kufundisha kwa vitendo (simulation) kwa wiki mbili jinsi ya majadiliano ya biashara yanavyoendeshwa hususan chini ya WTO.   Hata hivyo mwanzo wake ulikuwa ni mzuri sana kwa vile kozi hii ilikuwa inawatayarisha wanafunzi kihalisia zaidi kwenye maeneo husika lakini  kama sijakosea hali hii  ilibadilika na kuanza kufundisha nadharia zaidi pale ambapo ufadhili ulianza kupungua.   Aidha, msisitizo ulikuwa umejikita zaidi kwenye maeneo ya biashara na haukuhusu sana uwekezaji.  Msaada wa kifedha kutoka DANIDA uliisha baada ya mradi kufikia mwisho wake.

Swali: Ni jambo gani liliwahi kukutokea na hutalisahau Katika Maisha yako?  

Jibu: Ni wakati mnajadiliana na kuwa na msimamo wa pamoja kama vile kundi la Afrika au la nchi changa halafu inatokea nchi moja au mbili au mtu/watu  zinaamua kuuza msimamo wenu kwa nchi zilizoendelea.  Hii inaliweka kundi kwenye hali dhaifu ya kuweza kufikia lengo la suala unachojadili.

Mwandishi wa makala haya ni Ofisa Habari wa Chuo Kikuu  Cha Bagamoyo (UB)
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Septemba 9 Mwaka 2014.




 

 

 

No comments:

Powered by Blogger.