Header Ads

CHANEL TEN ,MAGIC FM TANGAZO LENU HILI LINAPOTOSHA KATIBA YA TANZANIA
CHANEL TEN,MAGIC FM TANGAZO LENU HILI LINAPOTOSHA KATIBA YA TANZANIA

N a Happiness Katabazi
BINAFSI ni mtazamaji na msikilizaji wa televisheni ya Chanel Ten na Magic Fm kwa lengo la kupata habari na kujifunza mambo mbalimbali.

Kwa siku kadhaa nimekuwa nikilitazama,kusikiliza tangazo moja linalorushwa na vituo hivyo vya utangazaji .

Tangazo hilo ambalo linaonyesha picha za sura za ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi (Albino).

Maudhui ya tangazo hilo linataka mauji ya albino yakome kwani albino ni binadamu kama sisi na na tangazo hilo likasema eti ibara ya Ibara ya 2 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatoa haki ha kuishi.

Binafsi muda wangu mwingi napenda kusoma baadhi ya Sheria ikiwemo sheria Mama ambayo ni Katiba ya nchi kwaajili ya kujifunza mambo mengi ya kisheria kuepuka kutenda makosa.

Baada ya kusikiliza tangazo hilo nimebaini tangazo hilo  limekosea  kunukuu ibara hiyo ya pili kwani ibara ya pili ya Katiba ga nchi haizungumzii kabisa haki ya kuishi.

Ibara ya pili ya Katiba ya nchi inazungumzia mambo haya ,naninanukuu kama ibara hiyo inavyosema:

2.-(1) Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la 
Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni
pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania
inapakana nayo. 

(2) Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali 
ya Jamhuri ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Rais aweza kuigawa Jamhuri ya Muungano katika 
mikoa, wilaya na maeneo mengineyo, kwa kufuata utaratibu
uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na 
Bunge:

Isipokuwa kwamba Rais atashauriana kwanza na Rais 
wa Zanzibar kabla ya kuigawa Tanzania Zanzibar katika
Mikoa, Wilaya au maeneo mengineyo".

Na kwa faida ya vituo hivyo vya utangazaji niwarahisishie kazi kuwa  haki ya kuishi inapatikana katiba ibara ya 14  ya Katiba ya nchi na siyo ibara ya pili kamamlivyoupotosha umma kupitia hilo tangazo lenu kuwa eti ya kuishi inapatikana katika ibara ya pili ya Katiba ya nchi.

Ibara ya 14 ya Katiba ya nchi inasomeka hivi,na ninanukuu: " Kila mtu anayo Haki  ya Kuishi  na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake,kwa mujibu wa sheria".

Waswahili wanamsemo mmoja usemao ' Muungwana asifiwi ushenzi'.

Naamini vituo kwa kosa hilo vitawaomba radhi watazamaji na wasikilizaji wake kwa makosa hayo ya kunukuu vibaya ibara ya Katiba ,kisheria tunaita ' wrong citation' ,  na kisha iende kulifanyia marekebisho tangazo hilo kwa kuweka ibara sahihi ya Katiba ili jamii izidi kujifunza na watu waache kuua albino.

Wito wangu kwa vyombo vya habari yaani magazeti ,redio,televisheni viwe makini katika hasa kunukuu baadhi ya vifungu vya sheria kwani vikinukuu kimakosa vikae vikijua umma ambao ni wavivu wa kutotaka kufanya utafiti wa yale yanayotangazwa na kuandikwa katika vyombo vya habari unaamini na kusadiki katika upostoshaji huo.

Nimejiuliza hivi Chanel Ten,Magic Fm haina Mwanasheria wake ambae hasa katika tangazo hilo angehusishwa kikamilifu atoe mchango wake wa kitaaluma ya sheria?

Lakini hata huyo naye aliyekubali kutia sauti yake katika tangazo lile naye kabla ya kwanza kukubali kuweka sauti yake katika tangazo lile ,alishindwa kabisa kutafuta Katiba ya nchi kuisoma ili ajiridhishe ibara ya pili anayoitangaza katika tangazo hilo kweli inasema hivyo?

Ikumbukwe kuwa makosa kama hayo yanashusha heshima ya vituo vya utangazaji na vyombo vya habari kuwa havipo  makini na kazi zake  na kusababisha baadhi ya watu wapoteze imani na taarifa zenu.

Lakini hata hiyo Idara ya Katiba ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ina maana halikulisikia au kuliona tangazo hilo ambalo limenukuu ibara isiyo sahihi?

Ikumbukwe kuwa kifungu cha 8 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 , inasema kutofahamu sheria siyo kinga kutoa adhibiwa.

Nashauri katika habari au matangazo yanayo husisha taalamu kama udaktari, sheria na fani nyingine mbali na taaluma yenu ya uandishi wa habari basi wahusisheni kwanza wanataaluma hao ili wawape utaalamu katika eneo la fani yao ili msiendelee kuwa vichekesho au kupotosha jamii.

Mungu ibariki Tanzania.

Chanzo: Facebook: Happy Katabazi
Blogg: www.katabazihappy.blogspot.com
0716 774494
Machi 25 mwaka 2015..

No comments:

Powered by Blogger.