Header Ads

EPA YAIVURUGA KORTI YA KISUTU

EPA yaivuruga Korti ya Kisutu

Na Happiness Katabazi

KESI za wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambazo zinaendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, zimewavuruga baadhi ya mahakimu na watendaji wa mahakama hiyo.

Vyanzo vya habari vya kuaminika kutoka ndani ya mahakama hiyo, vimeliambia gazeti hili kwamba, baadhi ya watendaji wa mahakama hiyo, wameanza kutuhumiana waziwazi kwamba miongoni mwao wanapokea rushwa kwa ndugu wa watuhumiwa hao.

Kuzagaa kwa tuhuma hizo kulisababisha jana watendaji wa mahakama hiyo kuitisha kikao cha makarani wote kujadili hali hiyo.

Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho ambazo Tanzania Daima ilizipata, zilisema kuwa, makarani hao walionywa kwamba endapo yoyote atabainika kujihusisha na mchezo huo, hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

“Nakwambia hivi, nchi hii imeoza kwa rushwa na haiwezi kuisha licha kwamba tunaipiga vita, kwani baadhi ya watendaji hapa Kisutu wamegeuza kesi za EPA kama mtaji na kuna wengine wanatoka jioni ili waweze kupata kitu chochote kutoka kwa ndugu wa watuhumiwa wa kesi hizo.

“Na leo tumeitwa kuonywa kwamba imebainika miongoni mwetu wanafanya mchezo huu mchafu, binafsi nakerwa na hali na siyo siri tangu kesi za EPA baadhi ya watendaji hapa mahakamani, wanatuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa ndugu wa watuhumiwa wa EPA,” alisema karani mmoja aliyezungumza na Tanzania Daima kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini.

Ofisa mwingine wa mahakama aliyezungumza na gazeti hili alisema, tayari kumeanza kuibuka kwa maneno kwamba, hata baadhi ya watuhumiwa waliotoka kwa dhamana katika kesi hizo za EPA wametolewa hata pasipo kukamilisha masharti yote ya dhamana kama yalivyoainishwa na mahakimu wanaosikiliza kesi zao.

“Pia kuna minong’ono kwamba kuna baadhi ya watuhumiwa wamepewa dhamana licha hati zao kuwa na kasoro, huku watuhumiwa wengine wenye kesi hizo wakiendelea kusota rumande baada ya hati zao kuwa na kasoro kama za wengine waliopata dhamana,” kilisema chanzo kingine cha habari kutoka hapo hapo Kisutu.

Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima jana unaonyesha kwamba, baada ya kumalizika kwa kikao hicho majira ya saa 3:00 asubuhi hiyo jana, mahakimu nao waliitwa kwenye kikao kingine ambacho hata hivyo kilichojadiliwa hakikuweza kubainika mara moja.

Taarifa zilizopatikana baadaye jana zilikuwa zikieleza kwamba, mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho, mahakimu hao walikwenda Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuonana na Jaji Mfawidhi Semstokres Kaijage ili waweze kumueleza yanayotokea katika mahakama hiyo hususani juu ya watuhumiwa wa kesi ya EPA.

Hata hivyo habari ambazo Tanzania Daima imezipata, zinasema kuwa, mahakimu hao, walishindwa kuonana na Jaji Kaijage kwa sababu alikuwa kwenye vikao vingine na badala yake walizungumza na Msajili wa Mahakama (Wilaya) na saa 5:00 walirejea Kisutu.

Wakati hayo yote ya kitendeka waendesha mashitaka, mawakili wa kujitegemea, watuhumiwa, wadhamini wa watuhumiwa mbalimbali walikuwa wakirandaranda mahakamani hapo bila kujua kinachoendelea, hali iliyosababisha baadhi ya watu hao kuanza kulalamikia hali hiyo.

Ilipofika majira ya saa 8:12, Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Ferdinand Wambari, akiwa ameongozana na maofisa wengine waandamizi wa Mahakama Kuu waliwasili Kisutu na kufanya kikao na mahakimu wote na kusabisha Hakimu Eva Nkya ambaye alikuwa mahakamani kusikiliza kesi ya Jeetu Patel na wenzake kuomba udhuru wa dakika 15 ili kuhudhuria kikao hicho.

Ilipofika majira ya saa 9:14, kikao hicho kilimalizika na mahakimu waliokuwa wakiendesha kesi za EPA, walirudi mahakamani kuendelea na kesi hizo.

Juhudi za waandishi wa habari, waliokwenda katika Ofisi ya Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Euphemia Mingi ili waweze kupata ukweli wa tuhuma hizo walikwama na badala yake wakaelekezwa kupitisha maswali yao kupitia kwa Katibu Muhtasi.

Akizungumza na waandishi wa habari kupiria kwa katibu muhtasi wake, Hakimu Mingi alisema hata yeye alisikia kuhusu kuwapo kwa mgogoro huo wa kiutendaji ambao hata hivyo hakuwa tayari kuueleza zaidi ya kuwataka waende kwa Msajili wa Mahakama ya Rufaa Wambali kwani ndiye msemaji wa mahakama nchini.

Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili jana, Wambali alithibitisha kufika katika Mahakama ya Kisutu na kufanya kikao na mahakimu wote.

Aliyataja mambo waliyoyadili kuwa ni pamoja na hali ya usalama wa mahakama hiyo kwa watendaji wake na akawataka mahakimu kuendesha kesi nyingine sambamba na zile za EPA.

Aidha Wambali alisema mahakimu hao walilalamikia tatizo la kuchelewa kurudi makwao kutokana na kuelemewa na kesi jambo ambalo ni la hatari.

“Kweli nimefika Kisutu na kufanya kikao na mahakimu, nimezungumza nao mambo niliyoyataja,” alisema Wambari.

Hata hivyo hakuweza kukubali wala kukataa kwamba alipata taarifa za kuwapo kwa rushwa kwa baadhi ya watendaji tangu kuanza kwa kesi hiyo.

Hadi kufikia jana jumla ya watuhumiwa wanane wa EPA walikuwa wamepewa dhamana.

Kwa jana peke yake waliopata dhamana ni Mwanasheria wa Benki Kuu Sophia Joseph, Mwesiga Lukaza, Johnson Lukaza na Kenten Chocken.

Hata hivyo mfanyabiashara maarufu, Jeetu Patel na wenzake wawili, walipata dhamana katika kesi mbili, lakini wakashindwa kupata dhamana katika kesi ya nne kwa sababu hati zao za kusafiria na barua ya mdhamini, zilikuwa zikitofautiana.

Hali hiyo ilimfanya Hakimu Mingi kuamuru upande wa mawakili wa utetezi kurudi kwenda kukamilisha dosari zilizojitokeza na kisha warudi Jumatatu ili watuhumiwa waweze kupata dhamana.

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Eliezer Feleshi amesema kwamba, tayari ofisi yake imepokea majalada yote yanayohusiana na EPA na yanaendelea kufanyiwa kazi.

Katika taarifa yake iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari ilisema majalada ambayo yanahitaji uchunguzi zaidi, yanaendelea kufanyiwa kazi kama alivyoelekeza vyombo vya uchunguzi.

Ni kwa misingi hiyo ninaomba wananchi kuwa na subira na kuiacha ofisi yangu kufanya kazi yake kwa kwa mujibu wa sheria,” alisema Feleshi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Novemba 15 mwaka 2008

No comments:

Powered by Blogger.