Header Ads

• Hatima ya Mwakosya wa BoT nayo kujulikana

Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, leo inatarajia kusikiliza maombi ya kupinga masharti ya dhamana yaliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam hivi karibuni katika kesi mbili mpya za matumizi mabaya ya madaraka ambazo zimelitikisa taifa.

Waombaji ni waliokuwa mawaziri waandamizi wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Basil Mramba (Fedha) na Daniel Yona (Nishati na Madini), ambao wanakabiliwa na makosa ya matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia hasara serikali ya sh bilioni 11.7.

Mwombaji mwingine ni Mkuu wa Kitengo cha Madeni Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Iman Mwakosya, ambaye ni mshitakiwa wa pili katika kesi ya jinai namba 1162 ya mwaka huu, iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya wizi wa sh milioni 207, mali ya BoT.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Saul Kinemela, alisema maombi hayo yamewasilishwa chini ya hati ya dharura.

Alisema kuwa ombi la Mwakosya, limepewa namba 53, la mwaka huu na litasikilizwa na Jaji Raziah Sheikh.

Ombi hilo limewasilishwa mahakamani hapo Novemba 21 mwaka huu na wakili wake, Makaki Masaju.

Kinemela alisema ombi la Mramba na Yona, lililowasilishwa mahakamani hapo juzi na wakili wa kujitegemea, Michael Ngaro, limepewa namba 54 na leo linakuja kwa ajili ya kutajwa, mbele ya Jaji Njengafibili Mwaikugile.

“Ni kweli maombi ya Mwakosya, Mramba na Yona ya kupinga masharti ya dhamana, yaliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu hivi karibuni, yamewasilishwa katika mahakama hii na tayari majaji wameishapangiwa kuyasikiliza (kesho), leo,” alisema Kinemela.

Kwa mujibu wa hati za madai ya maombi ya waombaji hao ambayo Tanzania Daima inazo, Mramba na Yona wanaomba Mahakama Kuu, ilegeze masharti ya dhamana ya kutoa fedha taslimu sh bilioni 3.9 kwa kila mmoja na sharti la kuzuiwa kutoka nje ya Dar es Salaam, kwa madai kuwa yatawaathiri washitakiwa hao hususan mshitakiwa wa kwanza, Basil Mramba, kwani ni Mbunge wa Rombo (CCM).

Hati hiyo ilidai kwamba katiba ya nchi, inatamka kuwa kila Mtanzania ana haki ya kutembea sehemu yoyote nchini na kwamba sharti hilo, litamuathiri zaidi Mramba ambaye ni Mbunge wa Rombo, hivyo kama sharti hilo litaendelea kuwapo, litamzuia kuwatumikia wananchi wake na pia atashindwa kuhudhuria vikao mbalimbali vya Bunge.

Aidha, wanaomba Mahakama Kuu iwaruhusu watuhumiwa hao kuwasilisha hati moja ya mali iyohamishika, yenye thamani ya sh bilioni 5.8, ambayo ni nusu ya kiasi wanachotuhumiwa kuiba ili itumike kwa ajili ya kuwadhamini waombaji wote wawili.

Hati hiyo iliendelea kupinga sharti la kutoa fedha taslimu sh bilioni 3.9 ili kupata dhamana kwa mtuhumiwa ni gumu, kwani kiasi hicho ni kikubwa na la kikatili dhidi ya waombaji.

Kwa upande wa hati ya maombi ya Mwakosya, mwombaji anapinga sharti la kutakiwa atoe fedha taslimu sh milioni 104 na risiti ya benki, kwa madai kuwa hakimu alitoa sharti hilo moja bila kutoa sharti mbadala kama sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 1985, inavyoelekeza.

Alidai kuwa sheria hiyo, inatamka mtuhumiwa atoe nusu ya fedha anazotuhumiwa kuiba au kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya nusu ya kiasi walichotuhumiwa kuiba, na kuongeza kwamba yeye anakabiliwa na kesi mbili katika Mahakama ya Kisutu na kesi moja iliyopo mbele ya Hakimu Waliarwande Lema, alitoa sharti la kutoa fedha taslimu au hati ya mali isiyohamishika ambapo yeye na washitakiwa wenzake, walitoa hati ya mali isiyohamishika, yenye thamani ya sh milioni 800 na walipata dhamana.

Mwakosya alidai kwamba anaomba Mahakama Kuu, imruhusu aweze kutoa hati ya mali isiyohamishika badala ya fedha taslimu ili aweze kupata dhamana, kwani hivi sasa bado anaendelea kusota rumande kwa kushindwa kutimiza sharti la kutoa fedha taslimu sh milioni 104.

Hakimu Henzron Mwankenja, Novemba 11 mwaka huu, alitoa sharti la dhamana la kutoa fedha taslimu sh milioni 104 kwa washitakiwa wanne wa kesi ya jinai namba 1162, Mweka Hazina wa CCM Mkoa wa Kigoma, Shaban Maranda, Iman Mwakosya, Kaimu Mkurugenzi wa Madeni ya Nje (BoT), Ester Komu na Mwanasheria wa benki hiyo, Bosco Kimela, sharti ambalo lilitimizwa kwa nyakati tofauti na washitakiwa hao isipokuwa Mwakosya.

Hata hivyo wakili wa Mwakosya, Masatu, aliwasilisha ombi mbele ya hakimu huyo akieleza kuwa mahakama ilipitiwa katika kutoa sharti hilo na kuomba mahakama itekeleze masharti yote yaliyoainishwa kwenye kifungu cha 148 (5) (g) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Sheria hiyo inatamka kwamba mtuhumiwa atatakiwa kulipa nusu ya fedha anazotuhumiwa kuiba au kutoa hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya nusu ya kiwango hicho.

Akitoa uamuzi wake, Mwankenja alisema anakubaliana na hoja za wakili huyo na inamuwia vigumu kwenda kubadilisha sharti hilo kwa sababu tayari watuhumiwa wenzake katika kesi hiyo, walishatekeleza sharti hilo.

Juzi Mramba na Yona, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mwankenja, ambapo pia alisema ili watuhumiwa hao wapate dhamana lazima kila mmoja wao atoe fedha taslimu sh bilioni 3.9, sharti ambalo walishindwa kulitimiza na kwenda rumande.

Mramba na Yona, wanatuhumiwa kwa mashitaka 13 ya kutumia madaraka ya umma vibaya na kuisababishia serikali hasara kubwa ya fedha wakati wakiwa madarakani.

Alidai kwamba shitaka la kwanza, pili, tatu na nne linawakabili washitakiwa wote wawili, wakati lile la tano, sita, saba, nane, tisa, 10 na 11 linamkabili Mramba pekee, huku shitaka la 12 likiwakabili washitakiwa wote wawili na la 13 likiwa la Mramba peke yake.

Ilidaiwa kuwa washitakiwa kwa makusudi au kwa kushindwa kuchukua tahadhari kwa mujibu wa taratibu za kazi, wakiwa mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu, iliyoongozwa na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, waliruhusu kutolewa kibali cha serikali kilichoisaidia Kampuni ya M/S Alex Stewart (Assayers) Government Bussiness Corporation kutolipa kodi, tofauti na mapendekezo ya Mamlaka ya Mapato (TRA), uamuzi ambao uliisababishia serikali hasara ya sh 11,752,350,148.00.

Ilidaiwa kuwa Mramba na Yona, kati ya mwaka 2002-2005, Mramba akiwa Waziri wa Fedha na Yona akiwa Waziri wa Nishati na Madini, walitumia madaraka yao vibaya kwa kuingia mkataba wa miaka miwili na Kampuni ya M/S Alex Sterwart (Assayers), Government Bussiness Corporation kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Mwaka 2002.

Alidai kuwa, mkataba huo ulianza Juni 14 mwaka 2005 hadi Juni 23 mwaka 2007.

Kwa mujibu wa hati yao ya mashitaka, kati ya Machi na Mei 28 mwaka 2005, watuhumiwa hao walitumia vibaya ofisi za umma kwa kumualika Dk. Enrique Segure wa M/S Alex Stewart (Assayers) Government Bussiness Corporation, kuja nchini na kumtaarifu kuwa wizara walizokuwa wakizisimamia zimeidhinisha kuipatia mkataba wa miaka miwili kampuni hiyo ya uhakiki wa madini kabla ya timu ya serikali kuruhusu kuingiwa kwa mkataba na kampuni hiyo.

Inadaiwa kuwa Oktoba 10 mwaka 2003, Mramba alitumia madaraka yake vibaya na kudharau maelekezo ya Mamlaka ya Mapato (TRA) ya kutaka kampuni hiyo isipewe msamaha wa kodi.

Mramba anadaiwa kuwa kati ya 2003 - 2005 aliibeba kampuni hiyo kwa kutoa notisi ya serikali ya kuisamehe kodi.

Hati hizo ni 423/2003, 424/2003, 497/2004, 498/2004, 377/2005 na 378/2005 na kuisababishia serikali hasara ya sh 11,752,350,148.00.

Washitakiwa wote walikana mashitaka na Hakimu Mwankenja alisema dhamana yao ipo wazi kwa sharti kwamba kila mmoja atoe fedha taslimu sh bilioni 3.9, na wadhamini wawili wa kuaminika ambao wanapaswa kusalimisha hati zao za kusafiria mahakamani.

Kesi hiyo ya kihistoria itatajwa tena Desemba 2, mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa,Novemba 28 mwaka 2008


No comments:

Powered by Blogger.