Header Ads

MRAMBA,YONA WALIVYOMALIZIA WIKIENDI MAHABUSU YA KEKO

*Kesi yao yafananishwa na ya Fundikira, Kiula

Na Happiness Katabazi

NATUMAINI wasomaji wa safu hii mpya mnaelewa yaliyojiri katika kesi mbili mpya za kihistoria, kuhusu matumizi mabaya ya madaraka, ambazo zimelitikisa taifa.
Kesi hizo zinawahusu mawaziri wa zamani wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Basil Mramba (Fedha) na Daniel Yona (Nishati na Madini), ambao wanatuhumiwa kwa kosa la kutumia vibaya madaraka yao na kulisababishia taifa hasara ya zaidi ya sh bilioni 11.
Kesi hizo zimefunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaaam.
Jumanne ya Novemba 24 mwaka huu, upande wa serikali katika kesi moja ya wizi wa sh bilioni 2.2, mali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ulishindwa kuwasomea maelezo ya awali watuhumiwa wawili wa kesi hiyo kutokana na wakili wa watuhumiwa kutokuwepo mahakamani.
Watuhumiwa katika kesi hiyo namba 1163 ya mwaka huu ni Mweka Hazina wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kigoma Rajab Maranda na Farijara Hussein, ambao wote kwa pamoja wanakabiliwa na kosa la kula njama kutenda kosa, kughushi, wizi na kujipatia ingizo kwenye akaunti lenye thamani ya sh bilioni mbili.
Wakili wa Serikali Stanslaus Boniface, mbele ya Hakimu Anyimilile Mwaseba aliiambia mahakama kuwa wakili wa upande wa utetezi, Mark Anthony, hakuwa amefika mahakamani, hivyo wasingeweza kusoma maelezo hayo.
Hata hivyo mshitakiwa wa kwanza Maranda aliiambia mahakama kwamba wakili wao alishindwa kufika mahakamani kwa sababu alikwenda kuhudhuria kesi nyingine katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara.
Hoja ambayo ilikubaliwa na Hakimu Mwaseba, ambaye aliahirisha kesi hiyo hadi kesho ambapo itakuja kwa ajili ya kusomwa maelezo ya awali.
Hadi sasa, jumla ya watuhumiwa 19 kati ya 20 wamepata dhamana. Mtuhumiwa anayeendelea kusota rumande ni Mkuu wa Kitengo cha Madeni ya Nje BoT, Iman Mwakosya.
Jumanne ya Novemba 25 mwaka huu, Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mtuhumiwa mwingine katika kesi ya wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (BoT), Farijala Hussein, alipata dhamana.
Aidha, kesi nyingine inayomkabili mshitakiwa huyo na kada wa CCM, Rajabu Maranda, ambayo ilipangwa siku hiyo kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali iliahirishwa hadi Januari 15 mwakani.
Siku hiyo ya Jumanne iliyopita, pia waliokuwa mawaziri wawili waandamizi katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Basil Mramba na Daniel Yona, walipandishwa mahakamani hapo kujibu mashitaka ya ufisadi ya kutumia madaraka ya umma vibaya na kuisababishia serikali hasara kubwa ya fedha wakati wakiwa madarakani.
Kufikishwa mahakamani kwa mawaziri hao wawili ambako fununu zake zimekuwa zikisikika kwa muda mrefu sasa, kulisababisha baadhi ya watu kutoamini kile walichokuwa wakikisikia kutoka maeneo mbalimbali nchini hususan vyombo vya habari.
Taarifa za kufikishwa mahakamani kwa vigogo hao wawili, zilisambaa haraka katika maeneo mengi katika Jiji la Dar es Salaam na katika mikoa mbalimbali nchini.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, tukio kama hilo liliwahi kumfika aliyekuwa Waziri wa Sheria miaka ya mwanzo ya 1960, Abdallah Fundikira na kisha wakati wa serikali ya Mkapa, enzi ya aliyepata kuwa Waziri wa Ujenzi, Nalaila Kiula, alipofikishwa mahakamani kwa sababu kama hizo.
Hata hivyo katika kesi hizo zote, wanasiasa hao walishinda.
Wanasiasa hao, Basil Mramba aliyekuwa Waziri wa Fedha na sasa ni Mbunge wa Rombo (CCM) na Daniel Yona aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini na mbunge wa zamani wa Same Mashariki, walifikishwa mahakamani hapo majira ya saa 3:26 asubuhi.
Wote wawili, Mramba na Yona walifika mahakamani hapo wakiwa ndani ya gari moja aina Toyota Land Cruiser, lenye rangi ya kijani, lililokuwa na namba za usajili T 319 ATD, ambalo taarifa za baadaye zilieleza kuwa ni mali ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Gari hilo baada ya kuegeshwa nyuma ya viunga vya mahakama hiyo, lilibaki likiwa limefungwa milango yote kwa takriban saa mbili, huku likiwa chini ya ulinzi mkali wa makachero wa polisi na wale wa Takukuru.
Kwa muda huo wa saa mbili, Mramba na Yona hawakushuka ndani ya gari hilo hadi ilipotimu saa 5:10 asubuhi, ndipo waliposhushwa na kupandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka yanayowakabili.
Mwanasheria Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface, akisaidiana na wakili wa Takukuru, Joseph Holle, mbele ya Hakimu Henzron Mwankenja, walidai kwamba, kesi hiyo namba 1200 ya mwaka huu ina jumla ya mashitaka 13.
Alidai kwamba katika shitaka la kwanza, pili, tatu na nne linawakabili washitakiwa wote wawili, wakati lile la tano, sita, saba, nane, tisa, 10 na 11, linamkabili Mramba pekee, huku shitaka la 12 likiwakabili washitakiwa wote wawili na la 13 likiwa la Mramba peke yake.
Kutokana na hilo katika mashitaka hayo, Mramba anakabiliwa na mashitaka 13 wakati Yona akikabiliwa na mashitaka matano.
Boniface alidai kwamba, washitakiwa kwa makusudi au kwa kushindwa kuchukua tahadhari kwa mujibu wa taratibu za kazi, wakiwa mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu, waliruhusu kutolewa kibali cha serikali kilichoisaidia Kampuni ya M/S Alex Stewart (Assayers) Government Bussiness Corporation kutolipa kodi, tofauti na mapendekezo ya Mamlaka ya Mapato (TRA), uamuzi ambao uliisababishia serikali hasara ya sh 11,752,350,148.00.
Wakili Boniface alidai kwamba Mramba na Yona kati ya mwaka 2002-2005, Mramba akiwa Waziri wa Fedha na Yona akiwa Waziri wa Nishati na Madini, walitumia madaraka yao vibaya kwa kuingia mkataba wa miaka miwili na Kampuni ya M/S Alex Sterwart (Assayers) Government Bussiness Corporation kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Mwaka 2002.
Alidai kuwa, mkataba huo ulianza Juni 14 mwaka 2005 hadi Juni 23 mwaka 2007.
Boniface alidai kwamba, kati ya Machi na Mei 28 mwaka 2005, watuhumiwa hao walitumia vibaya ofisi za umma kwa kumualika Dk. Enrique Segure wa M/S Alex Stewart (Assayers) Government Bussiness Corporation kuja nchini na kumtaarifu kuwa wizara walizokuwa wakizisimamia zimeidhinisha kuipatia mkataba wa miaka miwili kampuni hiyo ya uhakiki wa madini kabla ya timu ya serikali kuruhusu kuingiwa kwa mkataba na kampuni hiyo.
Aliendelea kudai kwamba, Oktoba 10 mwaka 2003 Mramba ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Fedha, alitumia madaraka yake vibaya na kudharau maelekezo ya Mamlaka ya Mapato (TRA) ya kutaka kampuni hiyo isipewe msamaha wa kodi.
Boniface, wakili aliyejizolea umaarufu mkubwa tangu kesi za wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) zianze kunguruma mahakamani hapo, alidai kwamba, kati ya 2003 -2005 Mramba aliibeba kampuni hiyo kwa kutoa notisi ya serikali ya kuisamehe kodi kampuni hiyo.
Hati hizo ni 423/2003, 424/2003, 497/2004 498/2004, 377/2005 na 378/2005 na kuisababishia serikali hasara ya sh 11,752,350,148.00.
Washitakiwa wote walikana mashitaka na Hakimu Mwankenja alisema dhamana yao ipo wazi.
Awali kabla ya hakimu kutoa masharti ya dhamana, wakili wa utetezi Joseph Tadayo, aliomba mahakama izingatie masharti nafuu ya dhamana kwa wateja wake kwa sababu tuhuma zinazowakabili zilianza kupelelezwa miaka mitatu nyuma na kwamba wakati huo watuhumiwa walikuwa nje na walikuwa wakitoa ushirikiano kwa wapelelezi, hoja ambayo haikupewa uzito na hakimu huyo.
Hata hivyo, washitakiwa wote walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kupelekwa mahabusu katika gereza la Keko.
Hata hivyo, hali ilibadilika ghafla na kuwa ya wasiwasi wakati watuhumiwa hao wakitolewa mahabusu kupelekwa kupanda gari tayari kwa safari ya Keko ambako umati wa watu waliokuwa mahakamani hapo wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi walianza kulizonga gari walilopanda watuhumiwa huku wakiwarushia maneno makali.
Msafara wa watuhumiwa hao kuelekea mahabusu uliondoka mahakamani kwa mwendo wa kasi, ukisindikizwa na magari kadhaa ya Jeshi la Magereza.
Dalili za watuhumiwa hao kwenda mahabusu zilianza kuonekana majira ya saa saba baada ya ndugu wa watuhumiwa hao, kuonekana wakihaha kwenda maduka ya jirani kununua kandambili na maji kwa ajili ya kuwapeleka watuhumiwa hao mahabusu.
Aidha, Jumatano ya Novemba 26 mwaka huu, mawakili wa Yona na Mramba waliwasilisha ombi katika Mahakama ya Kisutu, wakidai wapatie mwenendo wa shauri la kesi ya wateja wao ili waweze kulipitia na kuwasilisha ombi la kupinga masharti ya dhamana katika Mahakama Kuu Tanzania.
Saa sita na nusu alasiri ya siku hiyo Wakili wa kujitegemea Michael Ngaro kwa niaba ya mawakili wenzake wanaowatetea Mramba na Yona waliwasilisha maombi ya kupinga masharti ya dhamana Mahakama Kuu.
Alhamisi ya wiki hii, saa nane mchana, mwandishi wa makala hii alizungumza na Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Saul Kinemela, ofisini kwake ambapo alisema maombi hayo yaliwasilishwa chini ya hati ya kiapo cha dharura na yamepewa namba 54 ya mwaka huu na yatasikilizwa na Jaji Njengafibili Mwaikugile siku ya Ijumaa saa tatu asubuhi.
Kinemeleza alisema pia Mwakosya naye aliwasilisha maombi ya kutaka kulegezewa masharti ya dhamana ambapo anaiomba mahakama, imruhusu aweze kutoa hati ya mali isiyohamishika badala ya fedha taslimu ili aweze kupata dhamana, kwani hivi sasa bado anaendelea kusota rumande kwa kushindwa kutimiza sharti la kutoa fedha taslimu sh milioni 104.
Alisema ombi hilo limepewa namba 53 ya mwaka huu na limepangwa kusikilizwa siku hiyo ya Ijumaa, mbele ya Jaji Razia Shekhe.
Ijumaa ya Novemba 28 mwaka huu, yaliyojiri Kisutu, ni watuhumiwa mbalimbali wa kesi za EPA walionekana kwa wingi katika Mahakama ya Kisutu ambapo walikuja kwa ajili ya kutimiza sharti linalowataka kuripoti mahakamani hapo kila mwisho wa mwezi.
Siku hiyo hiyo katika ukumbi namba moja wa Mahakama Kuu, Jaji Mwaikugile ambaye aliingia mahakamani saa 4:10 na kuanza kusikiliza hoja za upande wa mawakili wa utetezi uliokuwa ukiongozwa na Joseph Tadayo na Michael Ngaro, wakati upande wa serikali ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Fredrick Manyanda, hadi saa 5:12 na aliahirisha usikilizaji huo na kusema atarudi saa saba mchana kwa ajili ya kuja kutoa uamuzi.
Wananchi mbalimbali waliokuwa na kiu ya kusikiliza uamuzi huo walianza kuketi katika ukumbi huo saa sita mchana na jaji aliingia tena mahakamani hapo saa 8:26 hadi saa 8:40 alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili alitoa amri ya kurekebishwa mara moja kwa sharti lililokuwa likiwataka Mramba na Yona kutoa fedha taslimu sh bilioni 2.9 ili wapate dhamana, badala yake alisema kisheria mtuhumiwa anatakiwa apate dhamana kwa kutoa kiasi cha fedha au kuwasilisha hati ya mali yenye thamani sawa na kiwango hicho.
Jaji Mwaikugile alisema masharti mengine kama kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, kusalimisha hati ya kusafiria na kutotoka nje ya Dar es Salaam, yatabaki kama yalivyo, lakini endapo watuhumiwa wanataka kutoka nje ya Jiji la Dar es Salaam, watakapaswa kuomba ruhusa mahakamani.
“Masharti mengine yatabaki kama yalivyo ila lile sharti la kuwataka waombaji kutoa fedha taslimu sh bilioni 2.9 ndipo wapate dhamana sikubaliani nalo na kwa sababu hiyo nabadilisha sharti hilo; hivyo watuhumiwa watapata dhamana endapo watatoa kiasi hicho cha fedha au kuwasilisha hati ya mali yenye thamani sawa na sh bilioni 2.9,” alisema Jaji Mwaikugile.
Hata hivyo jaji huyo pia aliamuru wadhamini wa watuhumiwa hao wahakikiwe na msajili namba mbili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Lameck Mlacha, agizo ambalo lilianza kutekelezwa kwa mawakili wa pande zote mbili kwenda ofisi ya msajili huyo, saa 9:03 alasiri.
Ilipofika saa 10:23, Msajili Mlacha aliwaambia waandishi wa habari kuwa muda wote aliokuwa na mawakili hao kwa ajili ya kuwahakiki, lakini muda wa kazi wa ofisi za umma ulikuwa umemalizika bila kazi hiyo kukamilika.
Kutokana na hali hiyo, aliwaagiza watuhumiwa hao warudi rumande hadi Jumatatu (kesho), ambapo watapelekwa katika Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya hatua za mwisho za uhakiki wa hati za mali zilizowasilishwa na wadhamini wao.
Baada ya kumaliza kuzungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, watuhumiwa hao walitolewa mahabusu na kupakizwa kwenye basi la Magereza lenye namba za usajili STK 4310 na kurudishwa katika mahabusu ya Keko na kuacha baadhi ya ndugu na jamaa waliokuja kufuatilia shauri hilo, kububujikwa machozi huku wengine wakijiinamia kwa huzuni.
Jumanne, Hakimu Henzron Mwankenja ambaye ndiye anayesikiliza kesi ya msingi ya Mramba na Yona, alitamka kwa kinywa chake kwamba ili watuhumiwa wapate dhamana, lazima kila mmoja atoe fedha taslimu sh bilioni 3.9 wakati katika rekodi za mwenendo wa shauri hilo alizoziandika yeye mwenyewe kwa mkono wake, zinaonyesha aliandika sharti la dhamana ni sh bilioni 2.9 kwa kila mmoja.
Sharti hilo la sh bilioni 3.9, limeripotiwa na vyombo vya habari na umma uliojitokeza siku hiyo kufuatilia shauri hilo, ulisikia lakini mawakili wa washitakiwa walipoomba mwenendo wa shauri hilo ili walipeleke Mahakama Kuu Jumatano hii kwa ajili ya kupinga dhamana, ndipo walipogundua kosa hilo.
Wakati huo huo, Jaji Razia Shekhe ambaye naye juzi alikuwa akisikiliza ombi la Mwakosya anayetetewa na wakili wa kujitegemea Makaki Masatu, ambaye alikuwa anapinga sharti la kutakiwa kutoa fedha taslimu sh milioni 104 na risiti ya benki, kwa madai kuwa hakimu alitoa sharti hilo moja bila kutoa sharti mbadala kama kifungu cha 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, inavyoelekeza, amerekebishiwa.
Jaji Shekhe alikubaliana na ombi la Mwakosya na kurekebisha kiwango hicho cha fedha alichotakiwa kutoa na badala yake mshitakiwa huyo sasa atatakiwa kutoa sh milioni 26 au kuwasilisha hati ya mali yenye thamani ya kiwango hicho.
Hata hivyo Mwakosya amerudishwa rumande kwa sababu ya kutokamilisha taratibu za dhamana yake.
Kwa mujibu wa hati ya madai ya Mwakosya aliyoiwasilisha mahakamani hapo Novemba 20 mwaka huu, aliiomba mahakama hiyo imruhusu atoe hati ya mali isiyohamishika badala ya fedha taslimu ili aweze kupata dhamana.
Hakimu Henzron Mwankenja, Novemba 11 mwaka huu, alitoa sharti la dhamana la kutoa fedha taslimu sh milioni 104 kwa washitakiwa wanne wa kesi ya jinai namba 1162, Mweka Hazina wa CCM Mkoa wa Kigoma, Rajabu Maranda, Iman Mwakosya, Kaimu Mkurugenzi wa Madeni ya Nje (BoT), Ester Komu na Mwanasheria wa benki hiyo, Bosco Kimela, sharti ambalo lilitimizwa kwa nyakati tofauti na washitakiwa hao isipokuwa Mwakosya.
Hata hivyo wakili wa Mwakosya, Masatu, aliwasilisha ombi mbele ya hakimu huyo akieleza kuwa mahakama ilipitiwa katika kutoa sharti hilo na kuomba mahakama itekeleze masharti yote yaliyoainishwa kwenye kifungu cha 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Sheria hiyo inatamka bayana kwamba mtuhumiwa anayetuhumiwa kuiba zaidi ya sh milioni 10, atatakiwa kulipa nusu ya fedha anazotuhumiwa kuiba, kutoa hati ya mali yenye thamani ya nusu ya kiwango hicho.
Akitoa uamuzi wake, Mwankenja alisema anakubaliana na hoja za wakili huyo na inamuwia vigumu kwenda kubadilisha sharti hilo kwa sababu tayari watuhumiwa wenzake katika kesi hiyo, walishatekeleza sharti hilo.
Mramba na Yona wanakabiliwa na mashitaka 13 ya kutumia madaraka ya umma vibaya na kuisababishia serikali hasara kubwa ya sh bilioni 11.7

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili,Novemba 30 mwaka 2008


No comments:

Powered by Blogger.