Header Ads

MAHAKAMA YAMLIZA MRAMBA

*Ataikosa ndoa, harusi ya bintiye leo
*Ndugu wajawa simanzi mahakamani
*Masharti ya dhamana yao yalegezwa

Na Happiness Katabazi

LICHA ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutoa amri ya kurekebisha masharti ya dhamana kwa waliokuwa mawaziri waandamizi wa Serikali ya Awamu ya Tatu ambao ni Basil Mramba ( Fedha) na Daniel Yona (Nishati na Madini), Mramba atashindwa kushuhudia harusi ya binti yake inayofanyika leo baada ya kulazimika kurudi tena Keko.
Mramba na Yona wanaoshtakiwa katika kesi ya jinai namba 1,200 ya mwaka huu ya matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7, walirudi rumande baada ya muda wa kazi kwa ofisi za umma kumalizika.
Kwa sababu hiyo basi, watuhumiwa hao wawili sasa watalazimika kwenda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu keshokutwa Jumatatu kwa ajili ya kukamilisha taratibu za dhamana.
Kurejea mahabusu kwa Mramba kunamfanya ashindwe kuhudhuria ndoa na harusi ya binti yake ambaye leo hii anatarajia kufunga ndoa na mtoto wa aliyekuwa Rais wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo nchini (TCCIA), Aristablus Elvis Musiba.
Ndoa hiyo ya bintiye Mramba inatarajia kufungwa katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph na hafla yake kufanyika katika Hoteli ya Movenpick.
Habari ambazo Tanzania Daima imezipata, zinasema kuwa maandalizi yote ya harusi hiyo yamekamilika, lakini huenda harusi hiyo isihudhuriwe na ndugu wengi kutokana na Mramba kushindwa kutoka rumande.

Muda wote jana wakati Jaji wa Mahakama Kuu, Njegafibili Mwaikugile alipokuwa akipitia rufaa ya Mramba na Yona, ndugu na jamaa wa watuhumiwa hao walionekana wakisali kwa sauti za chini muda wote.
Mbali ya Mramba na Yona, muombaji mwingine wa kupunguziwa masharti ya dhamana alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Madeni Benki ya Tanzania (BoT), Iman Mwakosya, ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi ya jinai namba 1162 ya mwaka huu, iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya wizi wa sh milioni 207, mali ya BoT.

Akitoa uamuzi wake jana saa 8:26 hadi 8:40 baada ya kusikiliza hoja za wakili wa kujitegemea Michael Ngaro na Joseph Tadayo wanaowatetea Mramba na Yona, pamoja na wakili mwandamizi wa serikali Fredrick Manyanda, Jaji Njengafibili Mwaikugile alitoa amri ya kurekebishwa mara moja kwa sharti lililokuwa likiwataka Mramba na Yona kutoa fedha taslimu sh bilioni 2.9 ili wapate dhamana badala yake alisema kisheria mtuhumiwa anatakiwa apate dhamana kwa kutoa kiasi au kuwasilisha hati ya mali yenye thamani sawa na kiwango hicho.
Jaji Mwaikugile alisema masharti mengine kama kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, kusalimisha hati ya kusafiria na kutotoka nje ya Dar es Salaam, yatabaki kama yalivyo, lakini endapo watuhumiwa wanataka kutoka nje ya Jiji la Dar es Salaam, watapaswa kuomba ruhusu mahakamani.
“Masharti mengine yatabaki kama yalivyo ila lile sharti la kuwataka waombaji kutoa fedha taslimu sh bilioni 2.9 ndiyo wapate dhamana sikubaliani nalo na kwa sababu hiyo nabadilisha sharti hilo; hivyo watuhumiwa watapata dhamana endapo watatoa kiasi hicho cha fedha au kuwasilisha hati ya mali yenye thamani sawa na sh bilioni 2.9,” alisema Jaji Mwaikugile.
Hata hivyo Jaji huyo pia aliamuru wadhamini wa watuhumiwa hao wahakikiwe na msajili namba mbili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Lameck Mlacha, agizo ambalo lilianza kutekelezwa kwa mawakili wa pande zote mbili kwenda ofisi ya msajili huyo, saa 9:03 alasiri.
Ilipofika saa 10:23, Msajili Mlacha aliwaambia waandishi wa habari kuwa muda wote aliokuwa na mawakili hao kwa ajili ya kuwahakiki, lakini muda wa kazi wa ofisi za umma ulikuwa umemalizika bila kazi hiyo kukamilika.
Kutokana na hali hiyo, aliwaagiza watuhumiwa hao warudi rumande hadi Jumatatu ijayo ambapo watapelekwa katika Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya hatua za mwisho za uhakiki wa hati za mali zilizowasilishwa na wadhamini wao.
“Ndugu waandishi tulikuwa na mawakili wa pande zote mbili kwa ajili ya kuhakiki wadhamini na hati zao, lakini kwa bahati mbaya muda wa kazi katika ofisi za umma umekwisha, hatuwezi kuendelea kufanyakazi hii na kwa sababu hiyo, washitakiwa warudi rumande hadi Jumatatu watakapopelekwa Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya kazi hiyo ya uhakiki,” alisema Lameck.
Baada ya kumaliza kuzungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, watuhumiwa hao walitolewa mahabusu na kupakizwa kwenye basi la magereza lenye namba za usajili STK 4310 na kurudishwa katika Mahabusu ya Keko, na kuacha baadhi ya ndugu na jamaa walikuja kufuatilia shauri hilo kububujikwa na machozi huku wengine wakijiinamia kwa huzuni.
Kwa mujibu wa hati ya waombaji hao ambayo Tanzania Daima inazo, Mramba na Yona walikuwa wanaiomba Mahakama Kuu ilegeze masharti ya dhamana ya kutoa sh bilioni 3.9 kwa kila mmoja na sharti la kuzuiwa kutoka nje ya Dar es Salaam kwa madai kuwa yatawaathiri washitakiwa hao hususani Basil Mramba kwani ni Mbunge wa Rombo.
Hivyo kama sharti hili lingeendelea kuwapo, lingemzuia kuwatumikia wananchi wake na pia atashindwa kuhudhuria vikao vya Bunge, mjini Dodoma.
Jumanne wiki hii Hakimu Henzron Mwankenja ambaye ndiye anayesikiliza kesi ya msingi ya Mramba na Yona, alitamka kwa kinywa chake kwamba ili watuhumiwa wapate dhamana, lazima kila mmoja atoe fedha taslimu sh bilioni 3.9 wakati katika rekodi za mwenendo wa shauri hilo alizoiandika yeye mwenyewe, zinaonyesha aliandika sharti la dhamana ni sh bilioni 2.9 kwa kila mmoja.
Sharti hilo la sh bilioni 3.9 limeripotiwa na vyombo vya habari na umma uliojitokeza siku hiyo kufuatilia shauri hilo ulisikia lakini mawakili wa washtakiwa walipoomba mwenendo wa shauri hilo ili walipeleke Mahakama Kuu Jumatano hii kwa ajili ya kupinga dhamana, ndipo walipogundua kosa hilo.
Wakati huo huo Jaji Razia Shekhe ambaye naye jana alikuwa akisikiliza ombi la Mwakosya anayetetewa na wakili wa kujitegemea Makaki Masatu, ambaye alikuwa anapinga sharti la kutakiwa kutoa fedha taslimu sh milioni 104 na risiti ya benki, kwa madai kuwa hakimu alitoa sharti hilo moja bila kutoa sharti mbadala kama kifungu cha 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, inavyoelekeza, amerekebishiwa.
Jaji Shekhe alikubaliana na ombi Mwakosya na kurekebisha kiwango hicho cha fedha alichotakiwa kutoa na badala yake mshitakiwa huyo sasa atatakiwa kutoa sh milioni 26 au kuwasilisha hati ya mali yenye thamani ya kiwango hicho.
Hata hivyo Mwakosya amerudishwa rumande kwa sababu ya kutokamilisha taratibu za dhamana yake.
Kwa mujibu wa hati ya madai ya Mwakosya aliyoiwasilisha mahakamani hapo Novemba 20 mwaka huu, aliiomba mahakama hiyo imruhusu atoe hati ya mali isiyohamishika badala ya fedha taslimu ili aweze kupata dhamana.
Hakimu Henzron Mwankenja, Novemba 11 mwaka huu, alitoa sharti la dhamana la kutoa fedha taslimu sh milioni 104 kwa washtakiwa wanne wa kesi ya jinai namba 1162, Mweka Hazina wa CCM Mkoa wa Kigoma, Rajabu Maranda, Iman Mwakosya, Kaimu Mkurugenzi wa Madeni ya Nje (BoT), Ester Komu na Mwanasheria wa benki hiyo, Bosco Kimela sharti ambalo lilitimizwa kwa nyakati tofauti na washtakiwa hao isipokuwa Mwakosya.
Hata hivyo wakili wa Mwakosya, Masatu , aliwasilisha ombi mbele ya hakimu huyo akieleza kuwa mahakama ilipitiwa katika kutoa sharti hilo na kuomba mahakama itekeleze masharti yote yaliyoainishwa kwenye kifungu cha 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Sheria hiyo inatamka bayana kwamba mtuhumiwa anayetuhumiwa kuiba zaidi ya sh milini 10, atatakiwa kulipa nusu ya fedha anazotuhumiwa kuiba kutoa hati ya mali yenye thamani ya nusu ya kiwango hicho.
Akitoa uamuzi wake, Mwankenja alisema anakubaliana na hoja za wakili huyo na inamuwia vigumu kwenda kubadilisha sharti hilo kwa sababu tayari watuhumiwa wenzake katika kesi hiyo,walishatekeleza sharti hilo.
Mramba na Yona wanakabiliwa na mashtaka 13 ya kutumia madaraka ya umma vibaya na kuisababishia serikali hasara kubwa ya sh bilioni 11.7
Ilidaiwa kuwa washtakiwa kwa makusudi au kushindwa kuchukua tahadhari kwa mujibu wa taratibu za kazi wakiwa mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu, iliyokuwa inaongozwa na Rais Benjamin Mkapa, waliruhusu kutolewa kibali cha serikali kilichoisaidia kampuni ya M/S Alex Stewart (Assayers) Gorvement Bussiness Corporation kutolipa kodi tofauti na mapendekezo ya Mamlaka ya Mapato (TRA); uamuzi ulioisababishia hasara serikali ya sh 11,752,350,148.00.
Ilidaiwa kuwa Mramba na Yona, kati ya mwaka 2002 na Mei 2005, Mramba akiwa Waziri wa Fedha na Yona, Waziri wa Nishati na Madini, waliiruhusu kampuni ya M/S Alex Sterwart(Assayers) Government Bussiness Corporation kutolipa kodi hivyo kutumia madaraka yao vibaya kwa kusaini mkataba wa miaka miwili na kampuni hiyo toka Juni 14 mwaka 2005 hadi Juni23 mwaka 2007, kinyume na sheria ya Manunuzi ya Serikali ya mwaka 2002.
Kwa mujibu wa hati yao ya mashtaka, kati ya Machi na Mei 28 mwaka 2005 watuhumiwa hao walitumia vibaya ofisi za umma na kumualika Dk. Enrique Segure wa M/S Alex Stewart (Assayers) Government Bussiness Corporation na kuidhinisha kuipatia mkataba wa miaka miwili kampuni hiyo ya uzalishaji madini kabla ya timu ya serikali kuruhusu kuingiwa kwa mkataba na kampuni hiyo.
Ilidaiwa kuwa Oktoba 10 mwaka 2003, Mramba alitumia madaraka vibaya na kudharau maelekezo ya Mamlaka ya Mapato (TRA) kwamba kampuni hiyo isipewe msamaha wa kodi.
Washtakiwa wote walikana shtaka na kesi yao itatajwa tena Desemba 2 mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Novemba 29 mwaka 2008

No comments:

Powered by Blogger.