Header Ads

KIGOGO ANUSURIKA KISUTU

• Ofisi ya DPP yadaiwa kumuokoa dakika za majeruhi

Na Happiness Katabazi

MMOJA wa mawaziri aliyepata kuingia katika mkumbo wa watu wanaofikishwa mahakamani wakikabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za serikali amenusurika, Tanzania Daima imegundua.

Habari za uhakika ambazo Tanzania Daima ilizipata jana zinaeleza kuwa, mwanasiasa huyo ambaye kwa sasa ni mbunge wa jimbo moja lililo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, alinusurika kupelekwa mahakamani jana kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kutosha.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, waziri huyo wa zamani aliyepata kuhusishwa na mkataba wenye utata wa uchimbaji wa madini alikuwa afikishwe mahakamani kwa kosa la kutumia vibaya madaraka yake wakati akiwa waziri.

Chanzo cha habari cha kuaminika kilichozungumza na Tanzania Daima kinaeleza kwamba, hatua ya Ofisi ya Mwendesha Mashitaka nchini (DPP) kumnusuru mwanasiasa huyo, imewashtua baadhi ya maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ambao kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa wamekuwa wakilichunguza sakata linalomhusu mwanasiasa huyo.

Mtoa habari wetu aliieleza Tanzania Daima kwamba, kabla ya kuwasilishwa kwa DPP kwa ajili ya uchunguzi zaidi, maofisa wa TAKUKURU walikuwa wamejiridhisha kuhusu kukamilika kwa shauri hilo na kumuacha DPP akichunguza uzito wa ushahidi uliowasilishwa.

“Leo ilikuwa apandishwe kizimbani kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka yake na kulisababishia taifa hasara kubwa lakini katika hali ya kushangaza Ofisi ya DPP imegoma kupeleka mahakamani kesi hii,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa ili kuelezea taarifa hizi, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Elieza Feleshi, alikanusha kuingia katika undani wa suala hilo zaidi tu ya kueleza kwamba hawezi kamwe kufanya kazi kwa shinikizo au kwa kusikiliza taarifa za kuzusha.

Feleshi, alisema kila kitu anachokifanya kinatokana na uchunguzi uliofanyika na taasisi mbalimbali zinazohusika na uchunguzi na yeye hupatiwa mafaili ya wahusika ili kujiridhisha kama kuna ushahidi wa kutosha kuwafikisha mahakamani.

‘Eehe bwana wee, mambo hayo unayoyasikia umeongea na vyombo vya uchunguzi na vikakupa taarifa? Maana siku hizi kila mtu anasema lake, mimi sifanyi kazi kwa namna wanavyotaka watu pasipo kufuata sheria,” alisema Feleshi.

Alisema yeye anafanya kazi kulingana na taaluma yake, ndiyo maana kila faili analoletewa ni lazima alifanyie uchambuzi wa kina ili kuepusha kumuonea mtu au kulitumbukiza taifa katika matatizo ambayo yanaweza kuepukika, iwapo ataachiwa afanye kazi yake kulingana na taaluma aliyonayo.

Alisema kila kukicha kumekuwa na taarifa zisizo sahihi kuhusu watu kufikishwa mahakamani katika kesi mbalimbali, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linaifanya Ofisi ya DPP iwe katika wakati mgumu wa kujibu maswali ya watu mbalimbali.

“Watanzania wasiwe na wasiwasi kwani kila kitu tunachokifanya, kitaonekana kwa jamii, ni jambo la kuvuta subira na kuona nani atafikishwa mahakamani na kwa kosa gani kuliko kueneza uvumi usio na tija kwa taifa,” alisema Feleshi.

Alisema wiki iliyopita alishaeleza wazi kuwa DPP atawafikisha mahakamani watuhumiwa wote ambao ushahidi wao utakamilika ili mahakama iweze kuthibitisha wana hatia au la.

“Sioni sababu ya kila siku kuulizwa maswali yale yale kuhusu kesi nitakazozifikisha mahakamani, kama mtu ana kiu ya kuona watu watakaofikishwa mahakamani, basi avute subira,” alisema Feleshi.

Tukio hili lilikuja ikiwa ni siku moja tu tangu Waziri wa Fedha wa zamani, Basil Mramba na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona, kupandishwa kizimbazi juzi wakikabiliwa na mashitaka 13 ya kutumia vibaya madaraka yao, kwa kusaini mikataba na kulisababishia taifa hasara ya sh bilioni 11.7.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi Novemba 27 mwaka 2008

No comments:

Powered by Blogger.