Header Ads

KESI YA MAHALU:SHAIDI AMGEUKA KIKWETE

Na Happiness Katabazi

BALOZI Abubakar Rajab Ibrahim, shahidi wa serikali katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia Prose Costa Mahalu na mwezake, jana aliambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kwamba aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati huo, Jakaya Kikwete, ambaye kwa sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano, hakutoa taarifa sahihi bungeni.

Shahidi huyo aliyekuwa ni (balozi kazi maalum) Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alifikia uamuzi wa kuiambia mahakama kuwa waziri huyo hakusema ukweli bungeni katika mkutano wa 16, kikao cha 39 cha Agosti 3, 2004, wakati Bunge likijadili bajeti ya wizara hiyo ya mwaka wa fedha 2004/2005, baada ya kutakiwa na wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa, kusoma kwa sauti Hansard ya Bunge ya wakati huo.

Kwa mujibu wa hansard hiyo, naibu waziri alijibu maswali kwa niaba ya waziri na inasomeka hivi.

“Mheshimiwa Naibu Spika mwaka 2001/2002, wizara ilinunua jengo la ofisi ya ubalozi - counsel - katika ubalozi wa Rome katika jitihada za kuondokana na tatizo la kupanga majumba ya watu huko nje, na pia kupunguza gharama za kuendelea kulipa pango la nyumba kila mwaka.

“Ununuzi wa jengo hili ulifuata taratibu zote za ununuzi wa majengo ya Serikali kwa kuzishirikisha Wizara za Ujenzi, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, na Wizara ya Fedha. Jengo lilifanyiwa tathmini na wataalamu wetu hao na kukubaliana na ununuzi kwa euro 3,098,741.40.

“Machi 6, 2002 fedha za awamu ya kwanza katika ubalozi wa Rome zilipelekwa sh 120,000,000, mwishoni mwa Agosti 26, 2002 tena zilipelekwa sh 1,000,000,000, jumla ya fedha zilizopelekwa zikafikia sh 2,900,000,000. Baada ya hapo ubalozi wetu Rome ulitekeleza taratibu zote za ununuzi wa jengo husika na kumlipa mwenye nyumba kiasi hicho cha fedha,” ilisomeka nakala hiyo ya kumbukumbu za Bunge.

“Mimi ndiyo niliyekuwa kiongozi wa timu ya watu watatu tuliokwenda Rome kuchunguza malalamiko, kwamba jengo hilo la ubalozi limenunuliwa kwa gharama kubwa na nilikuta jengo hilo ni bovu na linavuja, halifai kwa makazi ya ofisi. Hivyo nasisitiza waziri alilidanganya Bunge,” alidai shahidi huyo.

Awali akitoa ushahidi wake, Balozi Ibrahim, kapteni mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), alisema baada ya uchunguzi walibaini jengo hilo ni dogo, halifai kwa matumizi ya ofisi na lilikuwa mbali na mjini…lilinunuliwa kwa gharama kubwa kuliko balozi zote. Alipiga picha ambazo aliziwasilisha mahakamani kama kielelezo lakini zilikataliwa.

Mahojiano kati ya wakili na shahidi huyo yalikuwa kama ifuatavyo:

Wakili: Unafahamu lolote kuhusu nyaraka za uhamishaji wa fedha katika ununuzi wa jengo la ubalozi Rome?

Shahidi: Ndiyo

Wakili: Unasema hukuhusika kwenye manunuzi ya jengo hili ila ulikuja kusikia manung’uniko kwenye jamii.

Shahidi: Ndiyo

Wakili: Ulitaka usikie kama nani?

Shahidi: Kama mtumishi wa serikali.

Wakili: Unafikiri nani alipaswa kukuhusisha kwenye suala hilo?

Shahidi: Balozi alipaswa anihusishe.

Wakili: Soma hii barua ya Novemba 12, 2001.

Shahidi: Barua hii ni ya Wizara ya Mambo ya Nje na aliandikiwa Balozi Mahalu na ilitiwa saini na S.G. Mlai kwa niaba ya katibu mkuu wa wizara.

Wakili: Una habari kwamba Mkaguzi Mkuu wa Majengo ya Serikali Kimweri alikwenda Rome, Julai 11-21, 2001 kuchunguza jengo hilo na barua yake ambayo anashukuru ushirikiano alioupata kutoka kwa Balozi Mahalu na maofisa wa ubalozi wetu huko, je, hii si saini yake?

Shahidi: Kweli hii ni saini ya Kimweri.

Wakili: Katika uchunguzi wako, hamjawahi kugundua kwamba serikali ilifikia uamuzi wa kununua jengo hilo kutokana na ushauri wa kitaalamu ulitolewa na ripoti ya Kimweri?

Shahidi: Sijawahi kuiona ripoti hiyo.

Wakili: Soma barua hii ya wizara ya Septemba 11, 2001 kwenda kwa balozi wetu nchini Italia wakati huo Profesa Mahalu.

Shahidi: Inasomeka hivi rejea ukaguzi uliofanywa na Mkaguzi wa Majengo ya Serikali Kimweri, ilisema iliona majengo matatu na kupendekeza jengo hilo la Rome linunuliwe kwa sababu linafaa hata kwa matumizi ya baadaye.

Wakili: Kwenye uchunguzi wako kwa nini hukubaini majengo mawili hayakupendekezwa na ripoti ya Kimweri yasinunuliwe, uchunguzi wako haukujua hilo?

Shahidi: Mimi si injinia wa majengo.

Wakili: Katika uchunguzi wenu, mlibaini uratibu wa ununuzi wa jengo ulifuatwa?

Shahidi: Haukufutwa

Wakili: Kivipi?

Shahidi: Balozi hakufanya vikao na maofisa wake.

Wakili: Katika uchunguzi wenu, hamjabaini kama wizara ya fedha ilikuwa na taarifa?

Shahidi: Wizara ya Fedha haikuwa na taarifa

Wakili: Umeamua kuidanganya mahakama? Soma hii nakala ya kumbukumbu za bunge?

Shahidi: Taratibu zote zilifutwa katika ununuzi wa jengo hilo na Wizara ya Ujenzi, Ardhi zilishirikishwa.

Baada ya kusoma nakala hiyo hakutaka kukubaliana nayo na kusema kwamba waziri alidanganya bunge na kwamba timu yake ilikuwa sahihi.

Wakili: Kwa kujiamini unasema waziri alilidanga bunge, hivi majibu yanayotolewa na waziri bungeni si yanatokana na kazi zilizofanywa na wasaidizi ukiwemo wewe?

Shahidi: Ndiyo

Wakili: Unasema alidanganya bunge kwa sababu umestaafu utumishi wa umma?

Shahidi: (Kimya).

Wakili: Unasema jengo hilo limenunuliwa kwa euro milioni moja, mbona hapa mahakamani mshitakiwa anashitakiwa kwa wizi wa euro milioni 3?

Shahidi: Ndiyo nakwambia ni euro milioni moja.

Wakili: Wewe si mhandishi kitaaluma na wala hujaja na ripoti ya timu yako kwa nini unapinga jengo hilo halina thamani hiyo na je, unapingana na ushauri uliotolewa na wataalamu?

Shahidi: Sikuona umuhimu wa kuja na ripoti ya timu yangu.

Wakili: Umesema unafahamu vizuri suala hili la Rome, hivi uchunguzi wenu uliweza kubaini kwamba fedha za ununuzi wa jengo zilitolewa taslimu au kwa njia ya benki?

Shahidi: (Kimya).

Wakili: Kuna ushaidi wa kujitosheleza kwamba serikali inunua jengo kwa kuingiza fedha kwenye akaunti ya muuzaji, utanikatalia?

Shahidi: Sijui

Wakili: Nikisema timu yako ya uchunguzi ilifanya kazi kwa umahiri wa hali ya juu?

Shahidi: Tulifanya uchungizi wa kawaida

Wakili: Ni sahihi nikisema timu yako ilikusanya ushahidi wote muhimu wa kesi hii?

Shahidi: Hapana

Wakili: Timu yenu iliandika ripoti ya huo uchunguzi wenu?

Shahidi: Ndiyo

Wakili: Unayoyaongea hapa leo ndiyo yapo kwenye hiyo ripoti na iko wapi hiyo ripoti?

Shahidi: Sikuona umuhimi wa kuja nayo leo.

Wakili: Jengo la Rome lilikuwa ni la kampuni au la mtu binafsi?

Shahidi: Sijui

Wakili: Unajui nini wakati wewe uliongoza timu ya kwenda kuchunguza?

Shahidi: (Kimya).

Wakili: Tukisema katika shauri hili lina majungu ndani yake utakata?

Shahidi: (Kimya).

Kesi hiyo alianza saa 4:00 asubuhi na kumalizika saa 7.14 mchana. Jopo la mawakili watatu wa upande wa utetezi wakiongozwa na Alex Mgongolwa, Mabere Marando na Cuthbert Tenga walimbana kwa maswali shahidi huyo aliyekuwa akitoa majibu yasiyoeleweka na kusababisha mara kadhaa Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufaa, Sivangilwa Mwangesi, kumwamuru shahidi ajibu maswali anayoulizwa na mawakili hao na si vinginevyo.

Mwangesi ambaye alikuwa akilazimika kumuamuru shaidi huyo kujibu maswali anayoulizwa na wakili Mgongolwa, aliahirisha kesi hiyo hadi Deseaba 12. Upande wa serikali unaowakilishwa na wakili Ponsian Lukosi utamleta shahidi mwingine.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Novemba 8 mwaka 2008

No comments:

Powered by Blogger.