Header Ads

NI MTIKISIKO

*Mawaziri wawili wa Mkapa wapandishwa kizimbani kwa ufisadi
*Ni Basil Mramba aliyekuwa Waziri wa Fedha na Yona wa Madini na Nishati
*Wahusishwa kuisababishia serikali hasara ya shilingi bilioni 11.7
*Washindwa kutimiza masharti ya dhamana, wapelekwa gereza la Keko

Na Happiness Katabazi

WALIOKUWA mawaziri wawili waandamizi katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Basil Pesambili Mramba na Daniel Yona, jana walipanda mahakamani kujibu mashitaka ya ufisadi ya kutumia madaraka ya umma vibaya na kuisababishia serikali hasara kubwa ya fedha wakati wakiwa madarakani.
Kufikishwa mahakamani kwa mawaziri hao wawili ambako fununu zake zimekuwa zikisikika kwa muda mrefu sasa kulisababisha hali ya watu kutoamini kile walichokuwa wakikisikia kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Katika hali ya kushtusha, taarifa za kufikishwa mahakamani kwa vigogo hao wawili zilisambaa haraka katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na katika mikoa mbalimbali ya Tanzania mapema jana asubuhi.
Kwa siku nzima ya jana, chumba cha habari cha Tanzania Daima kilikuwa kikipokea simu kutoka kwa watu mbalimbali nchini, wakiwamo viongozi wa kisiasa, kidini, wastaafu na watu wa kawaida waliokuwa wakiuliza iwapo ni kweli vigogo hao wawili walikuwa wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za ufisadi.
Tukio hilo ambalo limedhihirisha ahadi iliyopata kutolewa kwa zaidi ya mara moja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Edward Hoseah, limesababisha hii kuwa ni mara ya tatu kwa mwanasiasa aliyepata kuwa waziri kufikishwa mahakamani akihusishwa na maamuzi aliyofanya akiwa madarakani.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, tukio kama hilo liliwahi kumfika aliyekuwa Waziri wa Sheria miaka ya mwanzo ya 1960, Abdallah Fundikira na kisha wakati wa serikali ya Mkapa, enzi ya aliyepata kuwa Waziri wa Ujenzi, Nalaila Kiula, alipofikishwa mahakamani kwa sababu kama hizo. Hata hivyo katika kesi hizo zote, wanasiasa hao walishinda.
Nje na ndani ya eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jana, umati mkubwa wa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, ulifurika kufuatilia suala hilo lililokuwa likiwagusa viongozi muhimu na mashuhuri enzi za serikali ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa.
Taarifa za kufikishwa mahakamani kwa mawaziri hao zilianza kusambaa katika kona mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam majira ya saa tatu na kusababisha watu wengi kuacha shughuli zao na kuelekea mahakamani hapo kushuhudia tukio hilo.
Wanasiasa hao, Basil Mramba aliyekuwa Waziri wa Fedha na sasa ni Mbunge wa Rombo na Daniel Yona aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini na mbunge wa zamani wa Same Mashariki, walifikishwa mahakamani hapo majira ya saa 3:26 asubuhi.
Wote wawili, Mramba na Yona walifika mahakamani hapo wakiwa ndani ya gari moja aina Toyota Land Cruiser, la rangi ya kijani lililokuwa na namba za usajili T 319 ATD ambalo taarifa za baadaye zilieleza kuwa ni mali ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Gari hilo baada ya kuegeshwa nyuma ya viunga vya mahakama lilibaki likiwa limefungwa milango yote kwa takriban saa mbili huku likiwa chini ya ulinzi mkali wa makachero wa polisi na wale wa Takukuru.
Kwa muda huo wa saa mbili, Mramba na Yona hawakushuka ndani ya gari hilo hadi ilipotimu saa 5:10 asubuhi, ndipo waliposhushwa na kupandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka yanayowakabili.
Mwanasheria Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface, akisaidiana na wakili wa Takukuru, Joseph Holle, mbele ya Hakimu Henzron Mwankenja, walidai kwamba, kesi hiyo namba 1,200 ya mwaka huu ina jumla ya mashitaka 13.
Alidai kwamba katika shitaka la kwanza, pili, tatu na nne linawakabili washitakiwa wote wawili, wakati lile la tano, sita, saba, nane, tisa, 10 na 11 linamkabili Mramba pekee, huku shitaka la 12 likiwakabili washitakiwa wote wawili na la 13 likiwa la Mramba peke yake.
Kutokana na hilo katika mashitaka hayo, Mramba anakabiliwa na mashitaka 13 wakati Yona akikabiliwa na jumla ya mashitaka matano.
Boniface alidai kwamba, washitakiwa kwa makusudi au kwa kushindwa kuchukua tahadhari kwa mujibu wa taratibu za kazi wakiwa mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu, waliruhusu kutolewa kibali cha serikali kilichoisaidia Kampuni ya M/S Alex Stewart (Assayers) Government Bussiness Corporation kutolipa kodi, tofauti na mapendekezo ya Mamlaka ya Mapato (TRA), uamuzi ambao uliisababishia serikali hasara ya sh 11,752,350,148.00.
Wakili Boniface alidai kwamba Mramba na Yona kati ya mwaka 2002-2005, Mramba akiwa Waziri wa Fedha na Yona akiwa Waziri wa Nishati na Madini, walitumia madaraka yao vibaya kwa kuingia mkataba wa miaka miwili na Kampuni ya M/S Alex Sterwart (Assayers) Government Bussiness Corporation kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Mwaka 2002.
Alidai kuwa, mkataba huo ulianza Juni 14 mwaka 2005 hadi Juni 23 mwaka 2007.
Boniface alidai kwamba, kati ya Machi na Mei 28 mwaka 2005 watuhumiwa hao walitumia vibaya ofisi za umma kwa kumualika Dk. Enrique Segure wa M/S Alex Stewart (Assayers) Government Bussiness Corporation kuja nchini na kumtaarifu kuwa wizara walizokuwa wakizisimamia zimeidhinisha kuipatia mkataba wa miaka miwili kampuni hiyo ya uhakiki wa madini kabla ya timu ya serikali kuruhusu kuingiwa kwa mkataba na kampuni hiyo.
Aliendelea kudai kwamba, Oktoba 10 mwaka 2003 Mramba ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Fedha, alitumia madaraka yake vibaya na kudharau maelekezo ya Mamlaka ya Mapato (TRA) ya kutaka kampuni hiyo isipewe msamaha wa kodi.
Boniface, wakili aliyejizolea umaarufu mkubwa tangu kesi za wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) zianze kuunguruma mahakamani hapo, alidai kwamba, kati ya 2003 -2005 Mramba aliibeba kampuni hiyo kwa kutoa notisi ya serikali ya kuisamehe kodi kampuni hiyo. Hati hizo ni 423/2003,424/2003,497/2004 na 498/2004,377/2005 na 378/2005 na kuisababishia serikali hasara ya sh 11,752,350,148.00.
Washitakiwa wote walikana mashitaka na Hakimu Mwankenja alisema dhamana yao ipo wazi.
Alisema ili mshitakiwa apate dhamana ni lazima kila mmoja wao atoe fedha taslimu sh bilioni 3.9 na wadhamini wawili wa kuaminika ambao wanapaswa kusalimisha hati zao za kusafiria mahakamani.
Aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 2 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
Muda wote ambao kesi hiyo ilikuwa ikiendelea katika mahakama ya wazi, korti namba moja, umati ulikuwa umefurika katika eneo zima la Mahakama ya Kisutu kiasi cha kusababisha hewa katika eneo hilo kuwa nzito.
Watuhumiwa hao ambao walikuwa wakilindwa na maofisa usalama maalumu wa Jeshi la Magareza waliokuwa na silaha nzito, wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Majura Magafu, Ngaro, Salum Mapande na Joseph Tadayo.
Awali kabla ya hakimu kutoa masharti ya dhamana, wakili wa utetezi Joseph Tadayo, aliomba mahakama izingatie masharti nafuu ya dhamana kwa wateja wake kwa sababu tuhuma zinazowakabili zilianza kupelelezwa miaka mitatu nyuma na kwamba wakati huo watuhumiwa walikuwa nje na walikuwa wakitoa ushirikiano kwa wapelelezi, hoja ambayo haikupewa uzito za hakimu huyo.
Hata hivyo, washitakiwa wote walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kupelekwa mahabusu katika gereza la Keko majira ya saa 8:02 mchana.
Walipelekwa gerezani kwa kutumia gari lililowaleta mahakamani hapo asubuhi.
Hata hivyo, hali ilibadilika ghafla na kuwa ya wasiwasi wakati watuhumiwa hao wakitolewa mahabusu kupelekwa kupanda gari tayari kwa safari ya Keko ambako umati wa watu waliokuwa mahakamani hapo wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi walianza kulizonga gari walilopanda watuhumiwa huku wakiwarushia maneno makali.
Baadhi walisikika wakisema ‘wezi hao, mafisadi hao, wanakula fedha zetu hadi tuna kosa dawa mahospitalini.’
Hali hiyo iliwafanya makachero waliokuwa wakiwalinda kupata wakati mgumu kuwazua wananchi kulifikia gari lililokuwa na watuhumiwa hao pamoja na kuwatawanya ili waweza kupata njia ya kuondoka mahakamani hapo.
Msafara wa watuhumiwa hao kuelekea mahabusu uliondoka mahakamani kwa mwendo wa kasi ukisindikizwa na magari kadhaa ya Jeshi la Magereza.
Dalili za watuhumiwa hao kwenda mahabusu zilianza kuonekana majira ya saa saba baada ya jamaa za watuhumiwa hao kuonekana wakihaha kwenda maduka ya jirani kununua kandambili na maji kwa ajili ya kuwapeleka watuhumiwa hao mahabusu.
Wakati huo huo, mtuhumiwa mwingine wa kesi ya wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje katika (BoT), Farijala Hussein, amepata dhamana.
Aidha, kesi nyingine inayomkabili mshitakiwa huyo na kada wa CCM, Rajabu Maranda, ambayo ilipangwa jana kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali imeahirishwa hadi Januari 15 mwakani.
Hadi kufikia jana, jumla ya watuhumiwa 19 wamepata dhamana kati ya watuhumiwa 20. Anayeendelea kusota rumande ni Mkuu wa Kitengo cha Madeni BoT, Iman Mwakosya.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Novemba 26 mwaka 2008

No comments:

Powered by Blogger.