Header Ads

TUJENGE KIWANDA CHA KUCHAPA VYETI

Happiness Katabazi

NASHUKURU Mungu kwa kuweza kunipa afya njema hadi siku ya Sikukuu ya Krismasi mwaka huu, nilikuwa nikitimiza umri wa miaka 32. Na pia namshukuru Mungu kwa kunipa uzima hadi nimeweza kuona Mwaka Mpya wa 2011.


Fukuto la Jamii linawapongeza wasomaji wake walioweza kumaliza sikukuu zote salama na kufanikiwa kuuona mwaka mpya na kwamba linawahidi kuwa kwa kipindi cha mwaka huu litaendelea kuwaletea makala moto moto kupitia safu hii.

Leo katika safu hii nitajadili kile kinachodaiwa kuwa ni kero na kinachowarudisha nyuma kitaaluma wanafunzi kwenye baadhi ya vyuo vikuu nchini hasa wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Ardhi na baadhi ya vyuo vingine vya serikali, kuwa ni kero na kinawarudisha nyuma kimaendeleo.

Kero hiyo ni ucheleweshaji wa kutolewa vyeti kwa wahitimu na sababu inayotolewa ni kuwa vyeti hivyo vinatengenezwa nje ya nchi na mara nyingine wahusika wa kuandaa maelezo ya vyeti hivyo hudaiwa kutotimiza wajibu wao kwa wakati.

Kilio hicho kadri siku zinavyozidi kwenda kimekuwa kikizidi kushika kasi na wahitimu wamekuwa wakikichukulia kama ni sehemu ya hujuma na inayokwamisha kupata kazi ndani na nje ya nchi

Fukuto la Jamii kwa takriban miezi miwili sasa, imekuwa ikifanya mawasiliano na baadhi ya wahitimu ambao wamekuwa wakishangazwa na watendaji wa ofisi za umma wanaoshindwa kuwajibika ipasavyo lakini wanaendelea kukalia nyadhifa mbalimbali.

Hoja kubwa wanayoijenga wahitimu hao ni kuwa mbali na kukwazwa katika ajira lakini pia wanashindwa kupata usajili wa kujiunga na vyuo vikuu vingine kwa muda mwafaka wanapotaka kuongeza maarifa zaidi.

Wanaweka wazi kuwa ofisi nyingi wanazopeleka maombi ya kazi na vyuo wanavyoomba kujiunga navyo huhitaji nakala halisi za vyeti na siyo taarifa ya matokeo ya mitihani jambo ambalo limekuwa likikwamisha kutimia kwa ndoto zao za kupata ajira mapema au kujiunga na vyuo husika.

Nimekuwa nikijuliza kuwa inawezekanaje serikali iliyosheheni watalaamu wengi ambao wametumia fedha nyingi kusomea fani za uchapaji na uandaaji wa nyaraka mbalimbali kushindwa kuchapa vyeti hivyo hapa nchini.

Kama serikali imekuwa ikiwasomesha wataalamu wa fani hiyo na nyingine, iweje sasa serikali hiyo hiyo inakubali kuidhinisha fedha nyingine za kutaka vyeti vya wahitimu wao vikatengenezwe nje ya nchi?

Inawezakana nia ya uongozi wa vyuo hivyo ni nzuri ya kufikia uamuzi huo wa kutengenezea vyeti nje ya nje kwa sababu ya kutaka kuwadhibiti wale wanaovighushi ambao binafsi nawaita Manyang'au.

Kwa muda mrefu imekuwa ikiaminika kuwa kutengeneza vyeti nje ya nchi kutadhibiti kughushiwa pamoja na kuwa na ubora mkubwa kuliko vikitengenezwa hapa nchini, jambo hilo sina uhakika nalo ila tunapaswa kuangalia sababu za kuendelea kufanya hivyo.

Nasema tunapaswa kuangalia utaratibu wa kufanya hivyo kwa sababu katika mazingira ya sasa ya maendeleo ya teknolojia vyeti hivyo vinaweza kuchapishwa hapa nchini kwa ubora mkubwa lakini pia kwa gharama nafuu.

Viongozi wa vyuo husika na serikali wanapaswa kujiuliza maswali yafuatayo kwamba; hatuoni wakati umefika kwa sisi kaka nchi kuwa na kiwanda chetu cha kutengenezea vyeti vya wahitimu wetu na vipatikane kwa wakati?

Je, uongozi wa vyuo hivyo vikuu hasa vile vya serikali, havioni ni wakati muafaka kwao kuandika michanganuo na maombi kwa serikali ya kuomba fedha za kununulia vifaa vya uchapaji, mishahara ya watendaji na kujengewa kiwanda?

Nina amini wakati mwingine serikali yetu ni sikivu hasa yanapokuja masuala kama haya kitaaluma. Kama ni serikali yeti imediriki kutoa mikopo kwa wanafunzi wasome japo haikidhi viwango vinavyohitajika, ikakubali kujenga ofisi ya Bodi ya Mikopo na hadi sasa inatoa mishahara kwa watendaji wote wa bodi hiyo, itashindwaje kujenga kiwanda.

Fukuto la Jamii, halitaielewa serikali kama itakatupilia mbali ombi la kujengwa kwa kiwanda cha uchapaji wa vyeti kwa wahitimu wake hapa nchini, endapo uongozi wa vyuo vikuu ikipeleka ombihilo kwa kufuata taratibu zote.

Nalazimika kuamini kwamba serikali haiwezi kukataa ombi hilo na kuidhinisha fedha za uanzishwa wa kiwanda hicho kwa sababu kitasaidia kuongeza ajira kwa Watanzania lakini pia kupunguza gharama za kusafirishia vyeti hivyo.

Kwani ni nyaraka ngapi za siria za serikali yetu zimekuwa zikichapwa na Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali? Mbona nyaraka hizi bado zimeendelea kuwa ni siri na hazivuji wala wala kughushiwa na Manyang'au?

Ni lazima tukubali kuwa mambo mengi tunayoyaoana hivi sasa ndani ya nchi yetu yamesababishwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa maadili pamoja na utoaji wa ajili usiozingatia umakini mkubwa.

Katika ofisi za umma na kule mitaani tumekuwa na mabingwa wa kughushi saini, vyeti, hundi, hati na vinginevyo ambao wanajulikana lakini kwa sababu ya kuporomoka kwa maadili au kulindana watu hao hatuwafikishi kwenye vyombo vya sheria.

Ninamini serikali yetu ina macho na mkono mrefu wa kuwatambua wanaofanywa uovu huo, natarajia inaweza kuwatumia watendaji wake kuwakamata na kuwachukulia hatua waharibifu wa sekta yetu ya elimu.

Katika mazingira ya kawaida watu wanaoghushi vyeti mbali na kuporomosha kiwango cha elimu lakini pia ni hatari kwani wanapoajiriwa hushindwa kutimiza matakwa husika kwa sababu wao si wabobea kwenye sekta husika.

Ila kama hao wataalamu wetu walivyokuwa vyuoni hawakuwa wakisoma vizuri na wakawa wanatazamia na kuiba mitihani kipindi cha mitihani, ni wazi kabisa hawatakuwa na mbinu ya kitaaluma ya kudhibiti vyeti hivyo vikichapwa hapa visigushiwe na matapeli wa mjini ambao hawa ni wataalamu wa kughushi saini za mtu yoyote walichoshindwa kughushi ni saini Mungu kwasababu bado hawajaona mfano wa saini ya Mungu.

Ikumbukwe kuwa moja ya kauli mbiu ya serikali ya awamu ya nne ilivyokuwa ikiingia madarakani mwaka 2005 chini ya Rais Jakaya Kikwete, ilisema itatoa ajira kwa wananchi wake, sasa inapotokea baadhi ya wahitimu wa vyuo vinavyomilikuwa na serikali hiyo hiyo vinachelewa kutoa vyeti na matokeo yake wahitimu wanakosa ajira kwa sababu ya maofisa walioomba ajira hizo wanasema ili wawape ajira ni lazima wawe na vyeti halisi.

Je tukisema uchelewaji wa kupatikana kwa vyeti hivyo vya wahitimu, kuna kwaza utekelezaji wa sera ya ajira kwa wasomi wetu tutakuwa tunakosea?

Aidha nataka nikumbushe uongozi wa vyuo vikuu vyetu kuwa kule ughaibuni mnakokimbilia kupeleka majina ya wahitimu wetu kuwatengenezea vyeti vyao, kwamba serikali za nchi hizo zilijifunga vibwebwe kuwasomesha wananchi wake hadi wakapata utaalamu huo na pia walikaa chini wakafikiri sana ndiyo maana wakaibuka na mitambo na vifaa vya kutengenezea vyeti hivyo vyenye ubora.

Sasa kila kukicha tunaambiwa nchi yetu imepiga hatua za kimaendeleo na wasomi wengi ukilinganisha na kipindi kile taifa limetoka kupata uhuru, sasa hao wasomi wanashindwa kufanya mkakati wa kuikaba koo serikali ili iweze kujenga kiwanda cha kuchapa vyeti hapa nchini?
Au wasomi wetu wanachojua hivi sasa ni kuandika tafiti mbalimbali (reseach)kwenye mashirika ya kimataifa yanashughulikia ugonjwa ukimwi, mazingira n.k. ili wajipatie fedha binafsi chap chap?

Wasomi wetu sasa wamegeuza faida ya elimu waliyonayo ni yao binafsi badala ya elimu yao iwe faida kwa taifa?

Kwani haiingii akilini kabisa kama Katiba ya Nchi, sheria za nchi mbalimbali na nyaraka nyingine za serikali zinachapwa hapa nchini halafu linapofika suala la kuchapa vyeti vya vyuo vikuu au mitihani ndiyo ikachapwe nje ya nchi.

Hata hii mantiki kwamba huenda vyeti hivyo kuchapwa nje ya nchi ni kudhibiti vyeti kughushiwa, hainiingii akilini kwani dunia ya sasa ni kijiji na hao waliopewa jukumu la kuitengeza vyeti huko nje ya nchi ni binadamu wenzetu na kama siyo waamini wanaweza kula njama na wananchi wa Tanzania na wakajikuta wanaingia kwenye 'dili' chafu ya kutengeneza vyeti feki.

Au wakati vyeti hivyo vinasafirishwa kuletwa nchini vinaweza kuporwa na majambazi pale uwanja wa ndege kama fedha zinazodaiwa kuwa ni Benki Kuu, zilivyoripotiwa kuibwa na jambazi pale uwanja wa ndege Dar es Salaam.

Lakini yote hayo hatuyaombei yatokee ila Fukuto la Jamii linatoa angalizo kwamba wakati umefika wa Taifa letu kuwa na kiwanda cha kuchapa vyeti vya wasomi wake.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Januari 2 mwaka 2011

No comments:

Powered by Blogger.