Header Ads

KESI YA DK.MKOPO,BADWEL ZAPIGWA KALENDA

Na Happiness Katabazi UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kudharau amri ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na kuwashawishi madaktari wagome inayomkabili Rais wa Chama cha Madaktari nchini(MALT), Dk.Namala Mkopi ulieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam.alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Wakili wa serikali Mwanaisha Komba mbele ya Hakimu Mkazi Faisal Kahamba aliikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kwaajili ya kutajwa lakini wanaomba kesi hiyo iairishwe kwa sababu upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Hakimu Kahamba alikubaliana na ombi hilo na akaiarisha kesi hiyo hadi Septemba 3 mwaka huu. Julai 10 mwaka huu, ilidaiwa na wakili wa serikali Tumaini Kweka kuwa kati ya Juni 26 na 28 mwaka huu,Dk.Mkopi akiwa ni Rais wa chama cha Madaktari alidharau amri halali ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ya Juni 26 mwaka huu, ambayo ilimtaka mshitakiwa huyo kwenda kwenye vyombo vya habari kuwatangazia wanachama wa chama hicho wasitishe mgomo kwani mgomo ule waliokuwa wakitaka kuufanya ni batili kama ambayo mahakama hiyo ya Divisheni ya Kazi Juni 22 mwaka huu, ilitoa amri kama hiyo ya kuubatilisha mgomo huo, lakini mshitakiwa huyo hakufanya hivyo. Wakili Kweka alilitaja kosa la pili kuwa ni kuwashawishi madaktari wagome kinyume na kifungu 390 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, kuwa Juni 27 mwaka huu, mshitakiwa huyo akiwa rais wa chama hicho aliwashawishi madaktari wasitekeleze amri hiyo ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ya Juni 22 mwaka huu. Wakati huo huo ,kesi ya kuomba na kupokea rushwa ya shilingi milioni moja toka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Jonathan Liana inayomkabili Mbunge wa Jimbo la Bahi(CCM), Omary Ahmed Badwel (43) ambayo ilikuja jana mbele ya Hakimu Mkazi Kahamba kwaajili ya kuanza kusikilizwa iliarishwa kwasababu mshitakiwa huyo hakuwepo mahakamani kwasababu amekwenda kuudhulia msiba wa dada yake hivyo hakimu huyo aliarisha kesi hiyo hadi Septemba 3 mwaka huu. Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Agosti 7 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.