Header Ads

BALALI ATAJWA TENA KESI YA EPA

Na Happiness Katabazi MSHTAKIWA wanne katika kesi ya wizi wa zaidi ya sh.bilioni 3.9 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania, Imani Mwakosya (54) jana ameileleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salama, kuwa aliyekuwa gavana wa wakati huo marehemu Daudi Balali ndiye aliyeidhinisha kiasi hicho cha fedha kilipwe kwa kampuni ya Mibare Farm kwakuwa ilionekana ni deni halali. Mwakosya anayetetewa na wakili wa kujitegemea Majura Magafu alitoa maelezo hayo mbele ya jopo la majaji Samuel Kalua,Beatrice Mutungu na Hakimu Mfawidhi Ilvin Mugeta wakati akitoa utetezi wake Mshtakiwa huyo ambaye alikuwa kifanya kazi idara ya Madeni BoT,alidai kuwa nyaraka mbalimbali vilizowasilishwa BoT na kampuni hiyo wakati ikiombwa kulipwa fedha hizo,zilionekana ni halali baada ya kupitiwa na maofisa mbalimbali wa benki hiyo. Mwakosya alizitaja baadhi ya nyaraka hizo kuwa ni pamoja na hati ya makabidhiano ya kuamisha deni hilo baina ya Kampuni ya Mibare Farm na Kampuni ya Lackshim Textile Mills Ltd ya India. Alidai kuwa deni hilo pia lilionekana katika mtandao wa BoT huku taarifa zake zikionekana kulingana na vielelezo zilivyowasilishwa na kampuni ya Mibare Farm wakati wakidai deni hilo. "Napenda mahakama ielewe kuwa malipo yalifanyika kihalali kwasababu vithivitisho vyote vilivyotakiwa kuthibitisha deni vililetwa BoT na vilitiwa na vikaonekana halali na ndipo gavana alipitisha malipo hayo"alidai Mwakosya. Alidai kuwa katika mchakato wa ulipwaji wa deni hilo yeye aliwahi kuandika dokezo la kulipwa kwa deni hilo kwenda kwa gavana. Alidai kuwa kampuni ya Kampuni ya Lackshmi Textile Mills Ltd ya India ilikuwa inaidai serikali ya Tanzania Yeni milioni 307,595,400 pamoja na fedha za india rupia milioni 29,220,686.92 ambazo ni sawa na sh.bilioni 3,868,805,737.13 Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Kada wa CCM Rajabu Maranda,Farijala Hussein ambao tayari wameishafungwa jela jumla ya miaka nane katika kesi mbili tofauti za EPA, Ajay Somani, Ester Komu na Sophia Lalika. Katika kesi hiyo washitakiwa hao wanadaiwa kula njama,kugushi na kuiba zaidi ya Shbilioni 3 .8 kutoka BoT, baada kudanganya kuwa imepewa deni na Kampuni ya Lackshim Textile Mills Ltd ya India na kujipatia inginzo hilo. Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Julai 31 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.