Header Ads

HAKIMU KESI YA KIBANDA ACHARUKA

Na Happiness Katabazi MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,imetoa amri ya mwisho kwa upande wa Jamhuri katika kesi ya kuandika na kuchapisha makala ya uchochezi inayomkabili Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima,Absalom Kibanda na wenzake inayoutaka upande wa jamhuri kuwapatia nakala ya maelezo ya awali ya mlalamikaji katika kesi hiyo ili washitakiwa waweze kujiandaa na utetezi. Amri hiyo ilitolewa jana Hakimu Mkazi Waliarwande Lema muda mfupi baada ya wakili jopo la mawakili wa utetezi linaloongozwa na Mabere Marando anayesaidiwa na Isaya Matamba, Juvenalis Ngowi na Hohn Mhozya na Frank Mwilongo kuieleza mahakama hiyo kuwa licha ya Juni 26 mwaka huu kutoa amri iliyoutaka upande wa jamhuri kuwapatia maelezo ya mlalamikaji washitakiwa na kwamba leo kesi hiyo ilikuwa inakuja kwaajili ya mashahidi wa upande wa jamhuri kuanza kutoa ushahidi wao,bado upande wa jamhuri ulikuwa haujawapatia maelezo hayo. “Leo natoa amri ya mwisho kwa upande wa jamhuri uakikishe unawapatia maelezo hayo washitakiwa na ninaiarisha kesi hii hadi Septemba 10 mwaka huu, kesi hii itakapokuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa”alisema Hakimu Lema. Awali wakili wa serikali Ester Kyala aliambia mahakama kuwa wakili wa serikali Elizabeth Kaganda ambaye ndiye alikuwa akiendesha kesi hiyo yupo mkoani Arusha kikazi na kwamba yeye jana ndiyo alikuwa amekuja kuiendesha kesi hiyo hivyo akaiadi mahakama kuitekeleza amri hiyo na kukiri kuwa ni kweli hadi kufikia jana upande wa jamhuri ulikuwa haujawapatia maelezo hayo ya mlalamikaji washitakiwa. Mbali na Kibanda washitakiwa wengine ni Samson Mwigamba ambaye ni mwandishi wa makala wa gazeti la Tanzania Daima na Kaimu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd, Theophil Makunga ambapo Desemba mwaka jana ilidaiwa mahakamani hapo na wakili Kaganda kuwa K mshtakiwa wa kwanza na wapili(Mwigamba na Kibanda) wanakabiliwa na kosa la kwanza la kuandika makala ya uchochezi iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “Waraka maalum kwa askari wote’. Alidai kuwa Mwigamba ambaye aliwahi kuwa Mhasibu wa Chama Cha Demokrasi Chadema na Kibanda ambaye ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la Tanzania Daima, kwa pamoja waliandika na waliruhusu makala hiyo ichapishwe kwenye gazeti hilo ambayo iliandikwa na gazeti la Tanzania Daima la Toleo Na. 2552 la Novemba 30 mwaka 2011 na makala hiyo ambayo ni ya uchochezi ikaja kuchapishwa na mshiutakiwa wa tatu (Makunga) kupitia kiwanda cha upachaji ambacho kipo chini ya uongozi wake. “Sisi upande wa jamhuri tunadai kuwa makala hiyo ni ya uchochezi na ilikuwa ikiwashawishi askari wa Jeshi la Wananchi,Polisi,Magereza na KMKM wasiitii amri za makamanda wao jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi na hata Desemba 6 na Desemba 20 mwaka jana, washitakiwa hao walipofika katika Wakili Kaganda alidai kosa la kwanza kosa la kwanza ni la uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1)(c) na 31(1)(a) cha Sheria ya Magazeti Sura ya 229 ya mwaka 2002 ambalo lina mkabili mshtakiwa wa kwanza na wa pili yaani Mwigamba na Kibanda. Ambapo wakili Kaganda alidai kuwa mnamo Novemba 30 mwaka 2011 jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao wawili kwa makusudi na kwa nia kuvunja sheria za mamlaka ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitenda kosa hilo la uchochezi kwa kuruhusu makala hiyo ichapishwe kwenye gazeti la Tanzania Daima la Novemba 30 mwaka 2011 iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “ Waraka Maalum kwa askari wote’ ambapo ilikuwa ikiwachochea askari hao wasitii mamlaka za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Agosti 8 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.