Header Ads

GRATIAN MKOBA NI KIBWETERE WA WALIMU WALIOGOMA?


Na Happiness Katabazi 

KIFUNGU cha 8 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 ya mwaka 2012,kinasomeka hivi; ‘kutofahamu sheria siyo kinga ya kutokuadhibiwa’. 

Nimelazimika kutumia nukuu ya kifungu hicho kwasababu hivi karibuni baadhi ya walimu wa shule za serikali hapa nchini kupitia chama chao CWT waliendesha mgomo ambapo kupitia Rais wa chama hicho,Gration Mkoba ndiye aliyeuitisha na mara kwa mara kiongozi huyo alikuwa akinukuliwa na vyombo vya habari akijigamba kuwa mgomo huo ambao hauna kikomo upo halali kisheria na baadhi ya walimu ambao naweza kusema akili zao zimeshikiliwa na Mkoba walianza kugoma tangu Julai 30 mwaka huu. Lakini Julai 26 mwaka huu, Katibu Mkuu Kiongozi, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Ufundi na Mwanasheria Mkuu wa serikali kupitia mawakili wa serikali Obadia Kamea na Pius Mboya dhidi ya CWT waliokuwa wakitetewa na wakili wa kujitegemea Gabriel Mnyele. Walalamikaji hao walifungua maombi madogo Mahakama Kuu Divesheni ya Kazi yaliyopewa Na.96/2012 chini ya hati ya dharula chini ya kanuni ya 25(1) ya Kanuni za Mahakama ya Kazi ya mwaka 2007,wakiomba mahakama itoe amri ya zuio la muda la kuzuia kufanyika kwa mgomo wa walimu kwasababu mgomo huo ni batili na haujakithi matakwa ya Kanuni ya 43(1) ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 na kifungu cha 80(1) vya sheria hiyo. Hivyo Wakili Kamea alidai endapo mgomo huo ukifanyika utailetea wakati mgumu serikali ,kuvuruga mitaala ya elimu na muda wa vipindi vya masomo,wanafunzi na wazazi watapata madhara ambayo hayatalipika endapo mgomo huo ukifanyika na wakaiomba mahakama imwamuru Mkoba aende kwenye vyombo vya habari kuutangazia umma mgomo ule ni batili na kwamba mgomo huo uliadhishwa kwa dhamira mbaya. Wakati wakili Mnyele alipokuwa akiwasilisha hoja zake mbele ya Jaji Sophia Wambura alidai kuwa CWT iliendesha zoezi lake la kupiga kuunga mkono ongezeko la mishahara kwa asilimia 100, posho za kufundishia kwa walimu wa Sayansi asilimia 55 na walimu wa Sanaa kwa asilimia 50 na posho ya mazingira magumu ya asilimia 30 kwa kufuata sheria hivyo mgomo ule hauna mawaa. Ilipofika Agosti 2 mwaka huu saa tisa alasiri minilikuwa miongoni mwaandishi wa habari waliofuatilishia shauri hilotangu linafunguliwa hadi linatolewa uamuzi siku hiyo, Jaji Wambura katika uamuzi wake ambayo nakala yake ninayo alisema anakubaliana hoja ya wakili wa serikali, Kamea kuwa mgomo huo ni batili kwa mujibu wa Kanuni ya 43(1) ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ambapo aliinukuu kanuni hiyo kama ifuatavyo; “Kama kuna mgogoro wa kimaslahi umeshindikana kusuluhishwa na msuruhishi,msuruhishi atajaribu kuzipatia pande zinazolumbana kanuni za kuitisha mgomo,kanuni hizo zitatangazwa kwa utaratibu,utaratibu wakuendesha mgomo huo,kutolewa noti yakuonyesha mgomo utaanza lini,eneo,muda,mazingira ya mgomo huo na utangazwe kwa wafanyakazi hao kabla mgomo kuanza,usalama wa wafanyakazi katika kipindi cha mgomo’ Jaji Wambura akasema wakati CWT ikijiandaa kuingia kwenye mgomo huo,pia ilikuwa haijakamilisha masharti ya kifungu cha 80(1) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini,kwasabababu amebaini kuwa wakati inaendesha zoezi la upigaji kula za kuunga mgomo ,iliwapotosha wanachama wake kuwa zoezi hilo liliitishwa rasmi na limekidhi matakwa ya kisheria, upigaji kula ule ni batili kwani walimu walikuwa hawajahalifiwa vizuri madhara yatakayojikoze kwenye mgomo ule,zoezi halikufuata taratibu za kisheria,hati ya nia ya kusudia la kugoma la CWT ambalo walimpelekea Katibu Mkuu Kiongozi Julai 27 saa tisa Alasiri wakati taratibu za upigaji kula hazijafanyika pia nayo iliuwa ni batili,kushindwa kwa CWT kutekeleza matakwa ya Kanuni ya 42 na 43 ya Shera ya Ajira na Mahusiano Kazini. “Mahakama hii inasema taratibu zote zilizofanywa na CWT kuitisha mgomo zilifanywa kwa dhamila mbaya kwasababu ni CWT ndiyo ilikata kuendelea na majadiliano kuhusu madai yao na mwajiri wake,tangu mwanzo CWT ilikuwa na majadiliano na serikali kuhusu maslahi yao lakini CWT akaamua kuyakacha mazungumzo hayo na kwenda njia anayoijua yeye,Julai 27 mimi nilitoa amri katika shauri hili la kuzitaka pande zote kubaki kama zilivyo hadi maombi haya yatakapokuja kusikilizwa baada ya siku hiyo pande mbili kutoka mahakamani hapo CWT saa tisa jioni ilienda kutoa notisi ya kuitisha mgomo na kwasababu hiyo mahakama hii inasisitiza CWT ilikuwa na dhamira mbaya ya kuitisha mgomo huu na ninaamuru walimu wote warejee kazini na wawalipe wanafunzi fidia”alisema Jaji Wambura. Kwanza napenda nitoe pongezi kwa Jaji Wambura kwa kuweza kutoa uamuzi huo mzuri kisheria na ambao umeudhiirishia umma kuwa walimu waliogoma ambao rais wao ni Mkoba ni mambumbumbu wa sheria ambao akili zao zimeifadhiwa ndani ya mkoba anaotembea nao Rais wa CWT,Gration Mkoba. Walimu mliogoma napenda mrejee tukio hili la mauji ya aina yake yaliyohusisha zaidi ya wafuasi wa dini "Movement for the Restoration of the Ten Commandments" 1,000 walioyokuwa wakiongozwa na kiongozi wao wa kidini Joseph Kibwetere, ambapo Machi 17 mwaka 2000 wafuasi zaidi ya 500 wa kanisa hilo waliingia kwenye jengo dogo lisilo na madirisha huko Kangngu small church in Kangngu,Magharibi mwa Uganda. Wafuasi hao waliimba sana nyimbo za kumtukuza mungu kabla jengo hilo dogo kuanza kuteketea kwa moto ambapo moto huo uliwashwa kutokea ndani ya jengo hilo kwa madai kuwa mwisho wa dunia ulikuwa umefika na kwamba wakifa wanaenda kuonana na mungu.Machi 19 mwaka 2002,serikali ya Uganda ndiyo ikaja kugundua watu hao wamefariki duniani ndani ya jengo hilo.Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na serikali ya Uganda baadaye zilidai mwaka 1998 Kibwetere ambaye naye alifariki katika mauji hayo na ndugu zake waliweza kuugundua mkono wake, aliwai kulazwa hospitalini akisumbuliwa na maradhi ya akili bila hao wafuasi wake kutofahamu kuwa kiongozi wao huyo aliwahi kuugua maradhi ya akili wakaendelea kumuamini na kumtii. Kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyotokea kwa wafuasi waliokuwa wakimtii Kibwetere ambaye aliwaaminisha mwaka 2000 ni mwisho wa duania na amewasiliana na mungu, basi walimu wa shule za serikali hapa nchini ambao wanayafuata maagizo ya Mkoba yanayowataka wagome wakati maagizo hayo ni batili kisheria na mwisho wa siku mahakama inakuja kusema mgomo ni batili, wajiulize je hawaoni ipo siku Mkoba anaweza kuwafanya kama Kibwetere alivyowafanyia wafuasi wake na wao wakakubali ? Kokote duniani mwalimu anaonekana ni mtu anayefahamu mambo na anayependa kujisomea wakati wote ili anapoingia darasani kufundisha akiulizwa maswali na wanafunzi wake aweze kuwapatia majibu. Lakini hapa Tanzania hivi sasa walimu wetu wengi hasa wa shule za serikali kwa mara ya pili sasa wameingia kwenye migomo batili ambayo inatenguliwa na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.Mgomo wa kwanza ni ule uliofanyika mwaka 2008, ambapo serikali ilifungua kesi Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ambapo Jaji wa Mahakama ya Rufaa hivi sasa William Mandia,aliutangaza mgomo ule wa walimu ni batili na akawataka warejee kazini na wakarejea na mgomo wa pili ni huu uliobatilishwa na Jaji Wambura Alhamisi ya wiki iliyopita. Hivi walimu waliowafundisheni nyie hadi leo na nyie mmekuwa walimu nao kipindi wanawafundisha wangegoma kuwafundisha leo hii mngekuwa walimu? Baadhi ya wanafunzi katika mgomo wa wiki iliyopita wamedai kulikuwa na walimu waliokuwa wakiwafundisha wanafunzi kuandamana kuunga mkono madai ya walimu hao.Hili jambo limenisikitisha sana na ndiyo maana napendekeza uchunguzi ufanyike ilikuwabaini walimu waliokuwa wakiwafundisha wanafunzi kufanya ufedhuli huo kwani leo walimu wameweza kuwafundisha ufedhuli huo wanafunzi kesho wanawaweza kuwafundisha wanafunzi wawe wanawadhau watawala na hata wazazi wao. Na kwasababu hiyo sisi watu tunaofikiri sawa sawa tumeanza kuhoji umakini, ufahamu na usomi wa walimu hao wanaojiingiza kichwa kichwa kwenye migomo hiyo bila kwanza kujiridhisha kama migomo hiyo imekithi matakwa ya kisheria kama wana akili timamu au akili zao wameshikiwa na Mkoba kwani haingii akilini, Mkoba akiitisha mgomo haramu baadhi ya walimu bila kujifikiria wanakubaliana naye na kugoma kutokwenda kazini wakati kila mwalimu anafahamu adha na machungu ya kufukuzwa kazi,kushitakiwa mahakamani,kushushwa cheo au kuamishiwa vijijini pindi unapobainika umeshiriki mgomo huo na mwajiri wako? Nilitegemea walimu wale waliogoma hasa wa Shule za Dar es Salaam,kabla ya kukubali kuingia kwenye mgomo wa juzi wangeukumbuka ule mkutano wao walioufanya pale ukumbi wa Dimond Jubilee , Oktoba 14 mwaka 2008 ambapo siku hiyo walimu walioudhuria pale walikuwa wameazimia kuanza mgomo lakini ilipofika mchana wa siku hiyo Mkoba alisema yeye haungi mkono kuanza kwa mgomo huo hali iliyosababisha kuzuka kwa tafrani kubwa baina ya walimu hao na Mkoba ambao walimu hao waligeuza chupa za maji ya kunywa,soda na viti kurusha meza kuu ambapo alikuwa ameketi Mkoba na viongozi wenzake wakimtuhumu kuwa amewasaliti hali iliyosababisha Makachero wa polisi kutumia mbinu zao za kijeshi kumwokoa Mkoba ambaye alikuwa amevalia vazi la suti na kumpitisha mlango wa dhalura na kisha kumpandisha kwenye gari la polisi na kumuondoa kwenye eneo hilo ili asidhulike na walimu hao kwa hasira wakatoka nje ya ukumbi na kuanza kulilirushia mawe gari la polisi hali iliyosababisha polisi hao kuanza kurusha risasi hewani kuwatawanya walimu hao ambao walitawanyika kwa kuogopa risasi na kesho yake baadhi ya walimu waligoma. Halafu leo hii Mkoba kanukuliwa na gazeti hili akijigamba kuwa aogopi kujeruhiwa kama alivyojeruhiwa Dk.Steven Ulimboka.Kwa kweli nilisikia hasira baada ya kuisoma habari hiyo kwani ni huyu huyu Mkoba siku ile ya Oktoba 14 mwaka 2008, pale Dimond Jubilee,mimi binafsi nilikuwepo katika mkutano ule na nilimshuhudia Mkoba alivyokuwa amehamaki na kutweta na kujikuta akitumbukia kwenye mtalo wa nyuma ya ukumbi huo wakati akipandishwa gari la polisi baada ya kuponyeshwa kipigo cha walimu hao ambao wengi wao walikuwa ni wanawake. Sasa Mkoba anataka kuhadaa umma kuwa yeye ni shujaa na siyo mwoga. Kwakuwa nilimshuhudia Mkoba siku ile akiloana jasho,woga na kukumbwa na taaruki kwa bahati nzuri polisi ndio waliomwokoa, nasema hana ushujaa,ujasiri na anaogopa kufa na kudhulika hivyo siyo mwanaharakati wala mpiganaji wa kweli kama walivyo wanaharakati wa nchi za wenzeti kama Somalia, Syria,Afghanistan,Libya . Mkoba anajaribu kutaka kuhadaa walimu na umma kuwa ni mwanaharakati na yupo tayari kufa kwaajili ya madai ya walimu kumbe si kweli kwani kama ni kweli angekataa kuokolewa na polisi siku ile ya Oktoba 14 mwaka 2008 na angekubali kupokea kipigo cha walimu wengi wa kike ambao walikuwa wanataka kumtia adabu. Nawaomba wale baadhi ya walimu ambao ni bendera fuata upepo msitekeleze maagizo yanayovunja sheria za nchi yanayotolewa na Mkoba kwani mwisho wa siku mtakaopata madhara ni nyie walimu na familia zenu ,na Mkoba wala hapati madhara zaidi jina lake linazidi kujiandika katika historia ya viongozi wa CWT wanaoitisha migomo inayobatilishwa na mahakama,cheo chake cha urais na posho zinazotokana na cheo chake zinaendelea kuwepo,kwenye meza ya majadiliano na mwajiri wenu anaenda yeye na huko atakunywa na chai na mikate yenye Blue Band na Soseji na nyie walimu mazuzu amtoambulia chochote mtaendelea kufanyabiashara zenu za kuwalazimisha wanafunzi wanunue bagia, ubuyu na ice cream zenu za Ukwaju madarasani. Na jinsi ninavyoifahamu serikali yetu makini ni wazi kabisa hivi sasa imeishatuma wachunguze mashuleni ni mwalimu gani alikuwa Chakubimbi ,kimbelembele wa kuamasisha mgomo na kuwafundisha wanafunzi waingie barabarani kuandamana na kwakuwa sisi Watanzania tunanyimana matonge ya ugali lakini habari tunapeana, watajulikana na watachukuliwa hatua za kiutumishi kimya kimya na msije kulia na mtu na wakati hatua zikianza kuchukuliwa dhidi yenu Mkoba yeye bado atendelea kuwa rais wenu na wala hatapata madhara makubwa kama ya nyie walimu mambumbumbu msiokuwa tofauti na Misukule. Ifike mahali walimu wa shule za serikali ambazo serikali ina shule nyingi zaidi, mjiulize ni kwanini walimu wa shule binafsi ambao hawalipwi pesheni pindi wanapostaafu baadhi ya walimu wa shule binafsi licha wanalipwa vizuri hawana ajira za uhakika,huduma ya matibabu hawagomi? Ila nyie walimu wa shule za serikali ajira zenu ni za uhakika, mnaruhusiwa kupata mikopo, wengine ni walimu wa ngazi ya cheti(voda Fasta),mnapata pesheni mnapostaafu, pesheni mnapostaafu lakini mnagoma? Sikatai kuwa ndani ya sekta ya walimu wa serikali kuna matatizo yake kwani kuna malalamiko ya baadhi ya walimu ambao walikuwa wakifundisha kisha wakaamua kwenda kujiendeleza vyuoni na wanavyorudi na vyetu kwa mwajiri wao,mwajiri wao amekuwa akichelewa kuwapandisha madaraja na kuwabadilishia mishahara yao,uhaba wa nyumba za walimu,mishahara midogo ambayo haitoshelezi kwani gharama za maisha zimepanda hali inayosababisha wafanyakazi kuwavunja moyo lakini matatizo hayo yasiwe kigezo cha walimu wasifuate sheria wakati wanapodai madai yao. Siasa ifuate sheria siyo sheria ifuate siasa.Na hapo ndipo Vyama vya wafanyakazi vinapokosea katika kudai madai yao kwani wanataka sheria ifuate siasa badala ya siasa ifuate sheria kitendo ambacho hakikubaliki katika dola letu ambalo linaongozwa kwa utawala wa sheria. Baada ya Jaji Wambura kutoa uamuzi huo ,baadhi ya wasomi wa sheria na wananchi wa kawaida walikuwa wakinipigia simu wakiubeza uamuzi huo kwasababu jana yake Rais Jakaya Kikwete alilihutubia taifa na akasema serikali yake haiwezi kuyalipa madai ya walimu kwani hayalipiki.Wasomi hao walikwenda mbali na kuongeza kuwa jaji huyo alikuwa ameandika uamuzi huo kwa maelekezo ya serikali kwasababu jana yake kabla hajatoa uamuzi huyo Rais Kikwete alishazungumzia mgomo huo. Kwa kweli nilisikitishwa na kauli hizi kwani zilikuwa zikitolewa na wasomi wa sheria ambao awali nilikuwa na waheshimu sana na siku sita kuwahoji ni kwanini wamefikia hatua ya kutoa shutuma hizo wakati hata nakala ya uamuzi huo hawajaipata na kuisoma, hawakuwepo mahakamani wakati shauri hilo linasikilizwa na kuamriwa na niliwataka wanipe ushahidi wa jaji huyo aliandikiwa uamuzi huo na Rais Kikwete,walishindwa kufanya hivyo na kusema Tanzania hivi sasa ina majaji wana ojikomba kwa serikali. Wakati baadhi ya wanasheria hao wakitoa tuhuma hizo kwangu wakili wa CWT ,Mnyele aliwaeleza waandishi wa habari kuwa yeye kama wakili amekubaliana na uamauzi wa Jaji Wambura.Na kwa wale wanaofahamu sheria wasomi wa sheria wanaelewa kuwa amri za muda zinazotolewa na mahakama hazikatiwi rufaa hivyo hata uamuzi huo wa Jaji Wambura,CWT haiwezi kuukatia rufaa katika mahakama yoyote ile hadi kesi ya msingi itakapotolewa hukumu. Kadri siku zinavyozidi kwenda Tanzania imekuwa na wananchi tena wengine wasomi na sisi baadhi ya waandishi wa habari kuropoka au kuandika habari tusizokuwa na ushahidi nazo na kwa bahati mbaya wananchi wengine wanaziamini taarifa zinazochapishwa katika vyombo vya habari hata kama sisi wanahabari tunajua habari hiyo ina mapungufu ya kitaaluma. Nimalizie kwa kuwaasa wananchi wenzangu kila mtu katika eneo lake la kazi afanyekazi kwa bidii kwani nchi yetu bado inaitaji kuletewa maendeleo na sisi wenyewe na ndiyo uchumi wetu utaimarika na kamwe uchumi wa taifa hili hautaweza kukukua kwa kila kukicha kuzuka kwa migomo ya kipumbavu ya wanafunzi wa vyuo na wafanyakazi. Tulishuhudia jinsi ya migomo ya vyuo vya elimu ya juu ilivyokuwa imeshika kasi lakini hatimaye serikali iliamka usingizini na kuanza kuwasaka wanafunzi wanaoshiriki kwenye mikusanyiko haramu na kuwafikisha mahakamani na hatimaye tunaweza kusema hivi sasa hali ni shwari katika vyuo vikuu vingi hapa nchini.Mwaka huu zaidi ya wanafunzi 50 wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, walifunguliwa kesi pale Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kosa la kufanya mkusanyiko haramu na hadi sasa kesi hiyo inaendelea kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema na baadhi ya waadhiri wa UDSM wanasema hatua hiyo ndiyo imesababisha mitihani ya kufunga mwaka wa masomo uliomalizika Julai mwaka huu kufanyika kwa amani bila ghasia. Aidha Januari,Machi na Julai mwaka huu tulishuhudia mgomo wa Madaktari hapa nchini hali iliyosababisha wananchi wenzetu wasiona hatia kupoteza maisha kwa kukosa huduma kwa kile kilichodaiwa na madaktari wanaitaka serikali iwaongezee mishahara,posho na iweke mashine za citscan amasivyo hawatarejea kazini. Lakini mwisho wa siku Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikwenda kufungua ombi dogo Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi dhidi ya Chama cha Madaktari akiomba mahakama isema mgomo ule ni batili na mahakama ilitamka mgomo ni batili na ilimtaka Mwenyekiti wa chama cha Madaktari Dk.Namala Mkopi kwenda kuutangazia umma kuwa mgomo huo ni batili lakini hakufanya hivyo hadi Julai 10 mwaka huu, Dk.Mkopi alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Faisal Kahamba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa makosa mawili ya kudharau amri ya mahakama iliyomtaka akatangaze mgomo ule ulikuwa ni batili na kosa la pili ni kuwashawishi wanachama wake wagome,kesi hiyo imekuja jana kwaajili ya kutajwa. Na hatimaye madaktari wameamua kufyata mkia na kurejea kazi kimya kimya ,wengine wamesimamishwa kazi licha madaktari hawa walikuwa wakijiapiza kuwa hawatarejea makazini hadi madai yao yatekelezwe na Citscan zinunuliwe,lakini wamerejea kazini bila kuboroshewa hayo maslahi wala mazingira ya kazi na cha ajabu hawa madaktari waliokuwa wakijifanya wanamsimamo thabiti wamebaki wakitushangaza ni kwanini wameamua kurejea kazini wakati pia walieleza hawatalejea kazini hadi mwenzao Dk.Steven Ulimboka apone. Pia tujikumbushe katika miaka ya nyuma hapa nchi kulikukwa na kikundi cha baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu waliochoma mabucha yaliyokuwa yakiuza nyama ya Nguruwe pale Manzese, wananchama wa chama cha CUF walikuwa wakipambana na Jeshi la Polisi enzi hizo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Gewe wakati Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspekta Jenerali Omar Mahita,wafuasi wa chama cha NCCR-Mageuzi kilichokuwa kikiongozwa na Agustine Mrema. Serikali kupitia vyomvo vyake vya dola iliweza kupambana na makundi hayo ya waandamanaji waliokuwa wakikiuka sheria za nchi na hatimaye ikafanikiwa kuwasambaratisha na ndiyo maana leo hii chama cha CUF,NCCR,TLP na wale waislamu waliokuwa wakivunja mabucha ya nyama ya nguruwe na kuendesha mazoezi ya kareti misikitini hawafanyi tena vitendo hivyo kwani miongoni mwao walipata vilema katika mapambano hayo akiwemo marehemu Sheikhe Magezi. Nimelazimika kwa kusema hapa Tanzania hakuna waandamanaji wa kweli wala wanaharakati.Kuna waandamanaji ‘kunguru’ yaani waoga.Waandamanaji au wagomaji gani kutwa wapo kwenye bar wanakunywa pombe na nyama choma na vimada pembeni wakiburudika kwenye kumbi za starehe na wanawakimbia polisi wanaokuja kutawanya maandamano yao? Waandamanaji,wagomaji na wanaharakati wa kweli wapo nchi za wenzetu huko kama Misri,Libya, Afghanistan,Syria na Somalia ambapo waandamanaji wa huko siyo wanafki,wachumia tumbo tofauti na wanaharakati wapuuzi wa Tanzania ambao miongoni mwao wanadiriki kutoa matamko yao mbalimbali mbele ya waandishi wa habari huku wakinuka Konyagi. Hivyo kimsingi tukubaliane hapa Tanzania hakuna wagomaji na wanaharakati wa kweli kuna wauza sura na masharobalo na wanaotaka kujijenga kisiasa ili mwisho wa siku wawanie nafasi za kisiasa. Na mfano mzuri wala si wa kutafuta ni enzi zile Rais wa CWT alikuwa Magreth Sitta.Sitta alijipambanua kama mtetezi wa maslahi ya walimu na enzi hizo Joseph Mungai ndiyo alikuwa waziri wa Elimu, kila kukicha mwana mama huyu alikuwa akitoa matamko ya kukosoa utendaji wa wizara ile iliyokuwa ikiongozwa na Mungai. Lakini mwaka 2005 Sitta naye aliingia kwenye ulingo wa siasa na kugombea ubunge wa viti maalum na kufanikiwa kupata na Rais Jakaya Kikwete alivyoapishwa Desemba 21 mwaka 2005 na alipounda baraza lake la mawaziri alimteua mama huyo kuwa Waziri wa Elimu, alivyompatia wadhifa huo hadi leo hii sijamsikia tena mama huyo akiendeleza harakati zake za wazi wazi kama zamani za kumtetea mwalimu wa nchi hii. Natoa rai kwa serikali kuanza uchunguzi makini wa vyeti vya taaluma vya walimu wote walioshiriki mgomo ule batili kwani siamini mwalimu aliyesoma kwa kutumia akili zake pasipo kugelezea mitihani au kununua vyetu angekubali kushiriki mgomo wa kipuuzi kama ule. Hivyo nimalizie kwa kuunga mkono kauli iliyotolewa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Fredrick Werema kuwa kazi ya kichwa sio kufuga nywele,ni kufikiri hivyo wafanyakazi wenzangu ambao mnaingizwa kichwa kichwa kwenye migomo hiyo batili mnatakiwa mjiulize na mtafakari kwanza kabla ya kuunga mkono mgomo kwani mwisho wa siku walimu mmejidhalilisha kuwa mmeunga mkono mgomo ambapo mlikuwa hamfahamu kama taratibu za kuitisha zilifuatwa.Niitimishe kwa kuuliza swali je Mkoba ni Kibwetere wa walimu waliogoma? Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika 0716 774494 Chanzo:www.katabazihappy.blogspot.com, Agosti 8 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.