SERIKALI ISOME ZABURI YA 17
Na Happiness Katabazi
AGOSTI 9 mwaka huu, Hakimu Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Ilvin Mugeta alitoa hukumu ya kesi ya kihistoria Na.1/2007 ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Grace Martin kutokana na ushahidi wa upande wa serikali kushindwa kuwatia hatiani.
Hukumu hiyo inaweza kutafsiriwa kama ni kubwagwa kwa serikali ya Rais Jakaya Kikwete, kutokana na hatua ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa Mei 7 mwaka huu, kukubali kupanda kizimbani na kumtetea Mahalu dhidi ya serikali, tukio ambalo ni la kwanza katika historia ya nchi hii. Hakimu Mugeta ambaye alikuwa akionyesha umakini wa hali ya juu wakati akiisoma hukumu hiyo alisema Mahalu na Grace waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka sita.Washitakiwa hao walikuwa wanatetewa na mawakili Mabere Marando, Alex Mgongolwa, Beatus Malima na Cuthert Tenga na upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na Ben Lincoln na Vicent Haule toka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Ponsia Lukosi toka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP). Aliyaja makosa hayo kuwa ni kula njama, kutumia nyaraka za manunuzi ya jengo la ubalozi ili kumdanganya mwajiri wao serikali, wizi wa Euro milioni 2,065,827 na kuisababishia serikali hasara. ““Lakini mahakama hii imejiuliza kama serikali ilikubali kulinunulia jengo hilo,ikatoa fedha kwaajili ya ununuzi, ikampatia Mahalu nguvu ya kisheria ya kuendelea na mchakato wa manunuzi, mkataba wa kwanza ulikuwa ni rasmi na mkataba wa pili ulikuwa ni wa kibiashara. ..Na mkataba huo ndiyo ulitumiwa na ubalozi wa Tanzania kumuhamishia fedha wakala wa uuzaji wa jengo na wala muuzaji wa jengo lile akakubali kuikabidhi Tanzani lile jengo na hajalalamika kuwa fedha hazikumfikia…mahakama hii inasema washtakiwa hawana hatia katika kosa hilo la kutumia nyaraka kumdangaya mwajiri wao kwasababu ushahidi wa upande wa jamhuri unajichanganya,”alisema. Aidha alisema kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa jamhuri kuwa taratibu za manunuzi ya jengo hilo mjini Rome haukufuatwa ni sawa na serikali kusindika risasi kwenye bastola kisha kujielekezea yenyewe kifuani. “Mahakama imebaki ikijiuliza ni kwanini Grace alishitakiwa katika kesi hiyo na kwa sababu hiyo nahitimisha kwa kusema serikali imeshindwa kuthibitisha kesi yake na hivyo ninawaachia huru washtakiwa wote,”alisema na kusababisha washitakiwa kuangua vilio Baada ya hakimu Mugeta kumaliza kusoma hukumu hiyo iliyowaliza washitakiwa na ndugu zao, Mahalu alikataa kuhojiwa na waandishi wa habari na badala yake aliwataka waandishi wa habari waende wakaisomea Zaburi ya 17 katika Biblia ya Agano la Kale ambayo inasomeka hivi: “ Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu, Utege sikio lako kwa maombi yangu, Yasiyotoka katika midomo ya hila. Hukumu yangu na itoke kwako, Macho yako na yatazame mambo ya adili. Umenijaribu moyo wangu, umenijilia usiku, Umenihakikisha usione neno; Nimenuia kinywa changu kisikose, Mintarafu matendo ya wanadamu; Kwa neno la midomo yako Nimejiepusha na njia za wenye jeuri. Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikuondoshwa. “.. Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, Utege sikio lako ulisikie neno langu. Dhihirisha fadhili zako za ajabu Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia; Kwa mkono wako wa kuume Uwaokoe nao wanaowaondokea. Unilinde kama mboni ya jicho, Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako; mbali ya mashambulio ya waovu ,mbali na adui zangu hatari wanaonizunguka. Hao hawana huruma yoyote moyoni wanajua maneno ya kujigamba .Wananifuatia na kunizunguka ,wananivizia waniangushe chini.Wako tayari kunilalua kama Simba kama Simba aviziapo mawindo.Inuka e mwenyezi mungu uwakabili na kuwaporomosha kwa upanga ,uiokeo nafsi yangu kutoka kwa waovu.Kwa mkono wako uniokoe na watu, Watu ambao ridhiki yao ni dunia hii tu.Uwanjaze adhabu uliyowawekea ,wapate ya kuwatosha na watoto wao .Waachie hata na wajukuu wao.Lakini mmi nitauona uso wako kwani ni mwadilifu,niamkapo nitajaa furaha kwa kukuona”. Awali ya yote naomba nieleweke kwamba kuna baadhi ya kesi serikali imeweza kufanya vizuri na kuibuka mshindi na nimekuwa nikiandika makala kuipongeza kwa ushindi huo na pindi serikali inaposhindwa kufuruka katika kesi kubwa kadhaa niliandika makala ya kukosoa na leo katika kesi ya Mahalu naandika makala hii kukosoa kwa kushindwa kuthibitisha kesi yake. Binafsi mimi ni miongoni mwa mwandishi wachache sana ambao tulianza kuiripoti kesi hii tangu ilipofunguliwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Januari 22 mwaka 2007 hadi Agosti 10 mwaka huu ilipomalizika kwa kutolewa hukumu. Lakini nadiriki kusema mimi ni mwandishi pekee hapa nchini niliyeifahamu kesi kiundani zaidi ya kesi ilivyokuwa mahakamani na nje ya mahakama na ndiyo maana kuna wakati ilifikia mahali kukopishana kauli na baadhi ya wakili wa mmoja wa serikali ambaye nilimweleza wazi wazi kuwa wanamaliza muda wa serikali bure na fedha za walipa kodi kwa kesi hiyo hiyo isiyokuwa na kichwa wala miguu na hatimaye Hakimu Mugeta amekuta kuitimisha kwa kutupilia mbali kesi hiyo iliyofunguliwa kwa mbele na kuendeshwa na TAKUKURU.. Kupata kwangu fursa ya kuifahamu kesi hii nje na ndani ya mahakama napenda niseme wazi kuwa kumenifundisha mambo kadhaa ya msingi: Mambo hayo ni kwamba kumbe ndani ya serikali kuna baadhi ya watumishi ambao ama kwa kutaka umaarufu au waonekane ni wachapakazi wanaamua kuwazulia wenzao uongo na mwisho wa siku uongo huo unasababisha wafikishwe mahakamani na mwisho serikali inajikuta ikibwagwa kwasababu hakuna ushahidi wa kuwatia hatiani washitakiwa. Pili,Rais Jakaya Kikwete wakati mwingine anasingiziwa na kugeuzwa Mwanasesere kwani katika kesi ya Mahalu kuna baadhi ya watu wakiwemo watumishi wa umma na baadhi ya wananchi bila kumung’unya maneno walikuwa wakisema Kikwete anamchukia Mahalu kwasababu eti wakati alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimatai na Mahalu alikuwa Balozi wetu nchini Italia, alikuwa akimdharau Kikwete hivyo ndiyo maana kikwete alivyokuwa rais alianza kwa kumlipizia kisasi Mahalu kwa kuagiza kwa njia ya siri vyombo vyake vimfikishe mahakamani. Tatu;kuna watumishi wa umma ambao hawana hofu ya mungu,vibaraka wa wakuu wao wa kazi,wapo kwaajili ya kuwaumiza baadhi ya wananchi wengine wasiyo na hatia kwa kisingizio kwamba wao ndiyo wasomi wa sheria na wapelelelezi wa makosa ya rushwa na wanatumia madaraka yao vibaya kwaajili ya wakati mwingine kuwaumiza watu wanaodhani wanamagomvi nao binafsi hali hii isipothibitiwa inaweza kujenga chuki ndani ya jamii yetu. Nne;baadhi ya watumishi hao wamekuwa wakivitumia vyombo vya habari kuakikisha vinatangaza uzushi huo ili mwisho umma unaamini watu hao wanaotuhumiwa kuwa ni mafisadi na hatimaye serikali kupitia vyombo vyake vinatoa uamuzi watu hao washitakiwe.Na katika sakata hili lilopelekea kuzaliwa kesi ya Mahalu ifunguliwe kuna baadhi ya waandishi wa chache maarufu hapa nchini walitumika ama kwa kutokujua au walijua kuwa walikuwa wakitumika vibaya kuibua sakata hilo kwa kwa maslahi ya watu wachache waliokuwa na lengo la kumuangamiza Mahalu na Grace.Waandishi hao wanajifahamu na hivi sasa hawana budi kutubu mbele ya mungu wao. Haikuitaji mtu awe na taaluma ya sheria kubaini kuwa ile kesi ya Mahalu ili ni miongoni mwa kesi za kipuuzi ,majungu na iliyokuwa na lengo la kuwakomoa na kuwahalibia maisha washitakiwa hao na mwisho wa siku imekuja kuiwekea rekodi serikali yetu ya kushindwa kufurukuta katika baadhi ya kesi kubwa mahakamani. Wasomi wa sheria tunafahamu fika jukumu la kuthibitisha kesi ya jinai ni la upande wa Jamhuri.TAKUKU ambayo ndiyo ilikuwa ikiiendesha kesi hii kwa mbwembwe ,ilishindwa kuyathibitisha mashitaka yote. Na cha kushangaza wakati kesi ikiendelea mawakili wa serikali wakaibua hoja ambayo haipo katika hati ya mashitaka kuwa washitakiwa walinunua jengo kwa mikataba miwili na walikuwa wakijaliribu kutaka kuishawishi mahakama ione kununua jengo lile kwa mikataba miwili ni kosa na lakini kwakuwa Hakimu Mugeta kwale tunaomfahamu ni hakimu kijana ambaye uadilifu wake haujawai kutiliwa mashaka na ni mtu mwenye msimamo usiyoyumba katika kile anachokiamini ,katika hukumu yake alisema wazi wazi kuwa hakuna kifungu chochote cha sheria kinachokataza mikataba miwili na kwamba hoja ya mikataba miwili simiongoni mwa makosa yanayowakabili washitakiwa ,aliitupilia mbali hoja hiyo na kwamba haiwezi kumshawishi kuwatia hatiani washitakiwa. Na ikumbukwe kuwa kesi hii ni kesi kubwa ya kwanza kufunguliwa ikiwa ni mwaka mmoja baakatika serikali ya Kikwete na ilifunguliwa muda mfupi baada ya Dk.Edward Hosea kuteuliwa na rais kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU na fedha za serikali zilitumika kutuma timu wachunguzi wa PCCB kwenda Italia kufanya uchunguzi,kulipigia gharama za kupokea ushahidi wa mmoja wa Marco Papi ambaye ni raia wa Italia kwanjia ya Video Conference, lakini matunda ya uchunguzi huo uliotumia kodi zetu ndiyo yale matunda yaliyooza tuliyoyavuna Agosti 9 mwaka huu, ambapo Hakimu Mugeta alimwachiria huru washitakiwa. Kwa sisi tunaofahamu kesi ya Mahalu ndani na nje ya mahakama tulikuwa tukishuhudia makundi mawili yakiwa yanapambana kimya kimya.Kundi moja lilikuwa linajitahidi washitakiwa hao wafungwe madai kuwa kesi hiyo inamkono wa rais wakati kundi jingine ambalo lilikuwa likipambana kisheria kuakikisha hawafungwi kwasababu walikuwa wakidai kuwa wanafahamu Mahalu na Grace ni wahadilifu na walibambikiwa kesi. Tujiulize kama kweli Rais Kikwete alikuwa ana mkono wake katika kesi hiyo ni kwanini walishinda kesi hiyo?Maana sote tufahamu nguvu alizokuwa nazo rais za kisheria na kimabavu na zinazoonekana na zisizoonekana kama kweli alikuwa na mkono wake katika kesi hiyo si angetumia vyombo vyake kwa njia anazozijua na angeakikisha Mahalu anafungwa?Na hakuna mtu yoyote ambaye angeweza kuleta ushahidi kuwa rais alihusika kufanya unyama huo na washitakiwa wangewekwanda gerezani. Kesi hii haikufunguliwa na rais kwasababu sisi wasomi wa sheria tunafahamu rais haina mamkala ya kufungua kesi ya jinai mahakamani ,kwa mujibu wa kifungu cha 90 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, kinasema Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP),ndiye mwenye mamlaka ya kufungua na kuendesha kesi za jinai mahakamani kwaniaba ya serikali. Hivyo uvuvi uliokuwa ukienezwa chinichini wa kwamba Rais Kikwete ndiye yupo nyuma ya kesi hiyo ni uongo mkubwa na walioanzisha uongo huo naamini walikuwa na lengo baya la kumpaka matope rais wetu na kumchonganisha na wananchi wake na uenda uongo huo ulikuwa ukitumiwa na wale wapika majungu waliosababisha kesi hiyo ifunguliwe ili waweze kumtisha Hakimu Mugeta atoe maamuzi yasiyoyahaki kwa kisingizio kesi hiyo inamkono wa rais lakini kwakuwa bado katika Mahakama zetu tuna mahakimu na majaji waadilifu akiwemo Hakimu Mugeta ambaye kwa wale tunaomfahamu Mugeta kupitia maamuzi yake kadhaa ni kwamba kama unashitakiwa mbele yake na utapata haki yako kama kwa mujibu wa sheria. Na hivyo ndivyo anavyosifika Mugeta ndani ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kwenye mhimili wa mahakama hapa nchini kwamba ni hakimu kijana ambaye na ayumbishwi na mtu wakati akitekeleza majukumu yake.Na hilo lilithibitika siku alipotoa hukumu hiyo kwani baadhi ya wananchi waliokuwa wametoka ndani ya chumba kilichokuwa kikisomewa hukumu walikuwa wakisema hakimu huyo ni jasiri kwani kesi hiyo ilikuwa na maneno mengi sana. Kama nilivyosema kesi hii imenifundisha mambo mengi sana likiwemo la kumbe hapa duniani kuna watu wana roho za ukatili wapo kwaajili ya kuwazulia wenzao uongo na kuwaaribia maisha lakini kwakuwa Mungu ni mwingi wa rehema mwisho wa siku Mungu ujiinua na kuwakumbatia watu wake walionewa na kudhalikishwa na makatili na hivyo ndivyo ilivyotokea katika kesi ya Mahalu wale wote walimuomdhulia balaa lile na kusababishia serikali iingie gharama za kuendesha kesi hii leo hii sijui wanajisikiaje katika nafsi zao. Nitoe rai kwa kuwataka wale wote walioshiriki kumfanyia madhira Mahalu, Grace waende wakaisome Zaburi 17 na wailewe na kisha kila mmoja hatubu kwa mungu wake dhambi hiyo kwani siku zote adhabu ya Mungu ni kali sana. Lakini mwisho niwakumbushe wale baadhi ya watumishi wa serikali ambao wapo serikalini kwaajili ya kutumia madaraka yao kuwaumiza wenzao na kuwazulia wenzao uongo ,wafahamu cheo ni dhamana na mwisho wa umri wa utumishi umma ni miaka 60.Baada ya hapo mnarudi uraiani mnakuja kukutana na wale mliopikia majungu wakafukuzwa kazi mnatafana au uenda yule uliyemfukuzisha kazi kabla ya umri wa kustaafu haujafika mungu akaja kumbariki akawa na maishai mazuri kuliko wewe uliostaafu kwa mujibu wa sheria,sura yako utaiweka wapi? Tumieni madaraka yenu vizuri enyi wote mliobahatika kupewa madaraka,msiumize wenzenu kwa ahadi za kupewa vyeo zaidi na wakubwa zenu kwani mkifanya hivyo mtakuwa mkikiuka maadili ya taaluma zenu na Mungu anawaona na siku atakapoanza kuwaadhibu msije kulia na mtu.Kumbukeni Mbinguni hakuna atakayekwenda na madaraka wala mali vyote tutaviacha hapa hapa. Pia wale mliowasababishia Mahalu na Grace mkawavurugia maisha yao ya utumishi wa umma na kuwaletea njaa na dhiki katika familia zao katika kipindi chote,mimi nafahamu ndugu na jamaa washitakiwa hao walikuwa wakifunga na kusali kwa mungu ,naamini maombi yale na machozi ya washitakiwa hayo hayatakwenda bure,mungu ameanza kuyajibu kama Mahalu alivyosema baada ya hukumu kutolewa kuwa ‘Mungu amemjibu maombi yake’.Siku zote tumheshimu na kumuogopa mtu anayemtumaini mungu katika jambo lake kwani mungu ni mtu wa haki. Naitimisha kwa kutoa raia kwa Rais Kikwete asifanye papara kuakikisha wale wote waliohusika kupika majungu na kumdanganya kuwa wanaushahidi mzito katika kesi hii licha kuna baadhi ya watendaji wa serikali ambao walishawahi kuishauri kwa siri serikali iifute kesi hii mapema kwani walibaini si kesi wala silolote na mwisho wa siku ni serikali ndiyo itadhalilika ,wachukuliwe hatua hatua au kubadilisha nyadhifa zao. Maana hakuna ubishi kwamba kwasisi tuofuatilia kesi mbalimbali kila siku ikiwemo kesi hii,Kikwete alikuwa akitajwa kichinichini kuwa ana mkono katika kesi hii sasa ili kuonyesha urais wako hauna ubia,na wewe ni rais wa wananchi wote na haukuchaguliwa na wanachi kwenda Ikulu kuwaumiza wananchi ni wakati sasa wakuwashughulikia au kuwaondoa madarakani wale wote walioshiriki kulizua sakata hili hadi siku ile ulipotembelea kwa mara ya kwanza Wizara ya Habari na Utamaduni ,ukalipongeza gazeti la Thise Day kwa kazi yake kubwa ya kuandika habari ya kuhusu ufisadi wa ununuzi wa jengo la Italia ambalo lilisababisha baadaye Mahalu kufikishwa mahakamani na ameshinda kesi hiyo na ukasahau tamko lako ulilolitoa Bungeni mwaka 2004 amba katika kikao cha Bajeti ambapo ulinukuliwa katika Hansard za bunge ukisema taratibu za ununuzi wa jengo hilo ulifuatwa na kwamba serikali ilituma fedha za manunuzi katika akaunti mbili za nchini Italia. Na tungali tukikumbuka hotuba yako wakati ukitangaza baraza lako jipya la mawaziri hivi karibu ambalo ulilifanyia marekebisho na kuingiza mawaziri wapya na mawaziri wengine kuwaacha, ulisema ‘kuna mawaziri wengine wamewajibika kwasababu ya makosa yaliyotendwa na wasaidizi wao na kwamba hao waliosababisha mawaziri hao wakawajibika nao haatabaki salama kwasababu kuna watu wapo serikali kazi yao ni kuwapikia majungu wenzao” Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika 0716 774494 www.katabazihappy.blogspot.com Chanzo:Gazeti la Tanzania la Daima la Jumapili,Agosti 12 mwaka 2012.
1 comment:
Nimeipenda makala yako. Hongera kutujuza.
Post a Comment