Header Ads

MAHALU,MKAPA WAMBWAGA JK


*HAKIMU ASEMA KIKWETE ALITOA NGUVU YA KISHERIA 

Na Happiness Katabazi 
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imemwachilia huru aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na aliyekuwa Meneja Utawala na fedha Grace Martin waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya wizi wa Euro milioni mbili kutokana na ushahidi wa jamhuri kushindwa kuwatia hatiani. 

Hukumu hiyo inaweza kutafsiriwa kama ni kubwagwa kwa serikali ya Rais Jakaya Kikwete, kutokana na hatua ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa kukubali kupanda kizimbani na kumtetea Mahalu dhidi ya serikali, tukio ambalo ni la kwanza katika historia ya nchi hii. Hukumu hiyo ya kihistoria ya kesi ya uhujumu uchumi Na.1/2007 ilitolewa jana kuanzia saa 6:03 hadi 7:39 mchana na Hakimu Mwandamizi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Ilvin Mugeta huku akisikilizwa na umati wa ndugu jamaa,marafiki wa washitakiwa hao. 

Washtakiwa hao waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka sita walikuwa wanatetewa na mawakili Mabere Marando, Alex Mgongolwa, Beatus Malima na Cuthert Tenga na upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na Ben Lincoln na Vicent Haule toka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Ponsia Lukosi toka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP). 

 Aliyaja makosa hayo kuwa ni kula njama, kutumia nyaraka za manunuzi ya jengo la ubalozi ili kumdanganya mwajiri wao serikali, wizi wa Euro milioni 2,065,827 na kuisababishia serikali hasara. Hakimu Mugeta alisema kuwa hata hivyo hati hiyo ya mashitaka haikuonyesha maelezo ya makosa hayo yanayowakabili washitakiwa. Alisema uamuzi huo ni kwa mujibu wa kielelezo cha tatu ambacho ni barua Na. FAC/0.40/58/62 ya Septemba 11 mwaka ya mwaka 2001 ambayo ni ya uamuzi wa serikali ya Tanzania wa jengo la ubalozi wake nchini Italia ambacho kilitolewa mahakamani hapo na Mahalu wakati akijitetea. Hakimu Mugeta alisema baada ya kupitia ushahidi na vielelezo vyote vya pande mbili, mahakama imeona manunuzi ya jengo yalifanyika kwa njia ya mikataba miwili ambayo ilisainiwa kwa siku moja na kwa bei tofauti. Alisema mkataba wa kwanza ni ule uliosainiwa na wakili wa Serikali ya Italia (Marco Papi) ambaye alikuwa ni shahidi wa pili wa Jamhuri ambao unaonyesha jengo lile lilinunuliwa kwa Euro 1,032,913 na mkataba wa pili ambao ni kielelezo cha sita ambao uliingiwa na wakala wa uuzwaji wa jengo na Balazo Mahalu na haukushuhudiwa na wakili wa serikali ya Italia. Alisema kuwa mkataba unaonyesha jengo lilinuliwa kwa thamani ya Euro 3,098,741. Hakimu Mugeta alisema kielezo cha nne ambacho ni taarifa ya benki kinaonyesha manunuzi ya jengo hilo yalifanyika Septemba 24 mwaka 2002 katika akaunti mbili tofauti . “Kielezo cha pili kinaonyesha malipo ya ununuzi ni Euro 2,065,827 ambayo yaliingizwa kwenye akanti Na.106705 ya Monaco na malipo mengine ni Euro 1,032,913 ambayo fedha hiyo iliingizwa kwenye akaunti Na.2182/51 ya Bromitrdnor ya zote za mjini Rome,” alisema. Kwamba baada ya mikataba yote kusainiwa na fedha kupokelewa Oktoba mosi 2002,wakala aliitoa risiti ya kuthibitishia kupokea Euro 3,098,741.58 na Septemba 23 mwaka huo, ubalozi wa Tanzania iliidhinisha vocha ya malipo ambayo ni kilielezo namba tatu ya Euro milioni 3,098.741. Alifafanua kuwa siku hiyo hiyo ubalozi wa Tanzania ulimuelekeza mfanyakazi wa benki nchini Italia, ahamishe kiasi hicho cha fedha kutoka kwenye akaunti ya ubalozi wa Tanzania kwenda kwenye akaunti hizo mbili tofauti ambazo ni za wakala wa uuzaji wa jengo hilo. Hakimu huyo alisema kwa mujibu wa vielelezo hivyo hapo juu mahakama imeridhika ndivyo vilivyotumika kununulia jengo la ubalozi na kwamba washtakiwa hao walifunguliwa kesi hiyo kwa kielelezo cha 3, 6 na 8. Kilelezo cha 3 ambacho ndicho kinaunda kosa la pili wakati kielelezo cha sita kinajenga kosa la nne na utofauti wa bei ya manunuzi ni kielelezo cha 1 na sita ambacho ni Euro 2,065,827.60 ambacho kinaunda kosa la tano na sita. Kuhusu ushahidi wa jamhuri, alisema kuwa Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu,Martin Lumbanga katika ushahidi wake alidai hakumbuki kama aliidhinisha jengo lile linunuliwe kwa njia ya mikataba miwili wakati shahidi wa pili (Papi) alidai yeye alisaini mkataba mmoja wa manunuzi ulionyesha jengo lilinuliwa kwa Euro 1,032,913.80. “Shahidi wa tatu Stewart Migwano ambaye ndiye alikuwa mhasibu wa ubalozi Utalia, alieleza kuwa ni ndiye aliyeandaa na zile vocha za malipo na kuzisaini ambazo mawakili wa serikali wanadai washitakiwa hao walizitumia kumdanganya mwajiri wao,” alisema. Hakimu aliongeza kuwa shahidi wa nne, Simon Maige alitoa kielelezo cha tano ambazo ni cheki ambazo zinaonyesha jinsi fedha za manunuzi ya jengo hilo zilivyohamishwa kutoka Tanzania kwenda ubalozi wake mjini Rome,Italia. Alisema kuwa shahidi wa tano ambaye ni mchunguzi toka (Takukuru), Isidori Kyando, alidai kubaini jengo hilo lilinuliwa kwa mikataba miwili na shahidi wa sita Edwin Mikongoti ambaye alikuwa ni Mkurugenzi wa Utawala wa wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa alidai yeye alikuwa akitunza rekodi za majengo yote ya ubalozi na kwamba hakushirikishwa katika ununuzi wa jengo hilo. “Shahidi wa saba Abubakar Rajabu alidai taratibu za manunuzi hazikufuatwa,” alisema. Mugeta alisema kuwa mashahidi watatu walitoa ushahidi kwa upande wa utetezi na wa pili alikuwa Rais mstaafu Benjamin Mkapa ambaye alieleza mahakama yeye na serikali yake walilidhia jengo linunuliwe kwa njia ya mikataba miwili na kwamba alitoa baraka zote kwa washtakiwa wanunue jengo hilo. “Kwa maelezo hayo hapo juu kabla ya kutoa hukumu yangu nimejiuliza maswali manne ambayo ni kama kweli washitakiwa walitenda kosa la kula njama na kuiba, kama walitumia nyaraka za manunuzi ya jengo kumdanganya mwajiri wao, kama waliibia seriakali Euro 2,065,827.60, kama wwaliisababishia serikali hasara ya Euro 2,065,827.60? alisema Mugeta. Akilichambua swali la kwanza, alisema ushahidi wa upande wa jamhuri umeshindwa kuweka wazi makubaliano na mipango ya siri waliyodai imefanywa na washitakiwa kuiba fedha hizo kwamba katika kesi hiyo endapo kosa la wizi likithibitika, kosa la kula njama linakufa kifo cha asili. “Hoja hii ya kwanza inanipeleka kulijadili kosa la tano ambalo ilidaiwa Oktoba mosi mwaka 2002 katika ubalozi wa Tanzania nchini Italia, washitakiwa hao waliibia serikali Euro hizo na kwamba kosa hili la tano nilijiuliza kwenye hoja yangu ya tatu kwamba washitakiwa waliiba kiasi hicho cha fedha? “Ushahidi wa upande wa jamhuri katika kosa hili si wa moja kwa moja unaonyesha washitakiwa walitenda kosa la wizi na kwa mujibu wa ushahidi wa jamhuri ulilotelewa mahakamani una shauri kuwa washitakiwa hao wanaweza kuwa walitenda kosa hilo, hivyo ushahidi huo ni mazingira si thabiti,” alisema. Alisema Mahalu alidai kuwa kule Italia muuzaji wa jengo anaruhusiwa kuuza jengo lake kwa mikataba miwili na upande wa jamhuri katika kesi hii haukupinga hilo na mawakili wa serikali wakadai sheria za ununuzi wa jengo hazikufuatwa wakati shahidi 6 na 7 walieleza pindi serikali inataka kununua jengo na kabla. Alisema Katibu Mkuu Kiongozi wa serikali anatuma timu ya wataalamu kulikagua na kisha ndiyo wanatuma fedha na kisha wizara ya Sheria na Katiba inahusishwa na katika ununuzi wa jengo hilo hayo yote yalifanyika, mahakama inakataa madai ya serikali ya kununua jengo kwa mikataba miwili kwa sababu hakuna kifungu chochote cha sheria hapa nchini kinachosema kununua jengo kwa njia ya mikataba miwili ni kosa la jinai. Alisema upande wa jamhuri ulikuwa unataka kuonyesha kuwa washitakiwa waliingia mikataba hiyo miwili bila ruhusa ya serikali wakati Mahalu katika ushahidi wake alitoa kielelezo ambacho ni nguvu ya kisheria aliyopewa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo ambaye kwa sasa ni Rais Jakaya Kikwete. “Lakini mahakama hii imejiuliza kama serikali ilikubali kulinunulia jengo hilo,ikatoa fedha kwaajili ya ununuzi, ikampatia Mahalu nguvu ya kisheria ya kuendelea na mchakato wa manunuzi, mkataba wa kwanza ulikuwa ni rasmi na mkataba wa pili ulikuwa ni wa kibiashara. ..Na mkataba huo ndiyo ulitumiwa na ubalozi wa Tanzania kumuhamishia fedha wakala wa uuzaji wa jengo na wala muuzaji wa jengo lile akakubali kuikabidhi Tanzani lile jengo na hajalalamika kuwa fedha hazikumfikia…mahakama hii inasema washtakiwa hawana hatia katika kosa hilo la kutumia nyaraka kumdangaya mwajiri wao kwasababu ushahidi wa upande wa jamhuri unajichanganya,”alisema. Aidha alisema kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa jamhuri kuwa taratibu za manunuzi ya jengo hilo mjini Rome haukufuatwa ni sawa na serikali kusindika risasi kwenye bastola kisha kujielekezea yenyewe kifuani. “Kwa sababu mashahidi wa jamhuri walieleza mahakama kuwa serikali ilituma timu ya wataalumu wa majengo iliyongozwa na Kimweri kwenda kulikagua jengo na ikaridhika na jengo lile na ikaishauri serikali ilinunue kabla halijanunuliwa na wizara kupitia menejimenti ilishakaa vikao na kuafiki jengo linunuliwe na waziri wa mambo ya nje ndiye aliyempa Mahalu nguvu ya kisheria kununua jengo hilo na serikali ilikuwa na taarifa, mahakama hii inasema washitakiwa hawakukiuka taratibu zozote za manunuzi. “Kwa kuwa kununua jengo kwa njia ya mikataba miwili hakuundi kosa la jinai na kwa sababu hiyo hakuna ushahidi ambao unathibitisha hoja yangu ya pili, nilichokigundua ni kwamba baada ya Euro 2,065,827,59 kuhamishwa kwenye akaunti zilizopo Monaco, hakuna ushahidi kuwa washitakiwa hao walizihamisha na kuiziingiza kwenye akaunti zao. Pia jamhuri imeshindwa kuleta ushahidi kuonyesha umiliki wa akaunti zile mbili na kwamba hakukuwepo na ubishi kuwa akaunti zile kuwa hazikuwa Monaco na jamhuri haikuwahi kumhoji wakala wa uuzaji wa jengo kama hakulipwa kiasi hicho cha fedha,”alisema Hakimu Mugeta. Kuhusu hoja ya pili la nyakara hizo kuonesha jengo kununuliwa kwa Euro 3,098,741.40 na washitakiwa kumdanganya wajiri wao, hakimu huyo alisema amegundua nyaraka hizo hazina udanganyifu wowote. Kwamba kwa kuwa Jamhuri imeshindwa kuthibitisha kuwa nyaraka hizo zilikuwa za udanganyifu, kosa la kwanza la kula njama na wizi limeshindwa kuthibitishwa. “Mahakama imebaki ikijiuliza ni kwanini Grace alishitakiwa katika kesi hiyo na kwa sababu hiyo nahitimisha kwa kusema serikali imeshindwa kuthibitisha kesi yake na hivyo ninawaachia huru washtakiwa wote,”alisema na kusababisha washitakiwa kuangua vilio. Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu hukumu hiyo, Mahalu aliwataka waandishi waende wakasome Zaburi ya 17 katika Biblia huku akionekana kulengwa kwa machozi ya furaha. Mkewe Winfrida Mahalu ambaye aliogopa kuoingia ndani ya chumba ilikosomewa hukumu hiyo, alitolewa ndani ya gari na ndugu zake huku akiangua kilio baada ya hukumu hiyo na huku mshtakiwa wa pili Grace naye akiangua mahakamani hapo. Kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Januari 22 mwaka 2007. Ili kuithibisha kesi yao, upande wa Jamhuri ilileta jumla ya mashahidi saba wakati upande wa utetezi ulileta mashahidi watatu akiwemo Rais mstaafu Benjamion Mkapa. Mei 8 mwaka huu, upande wa utetezi ulifunga ushahidi wake baada ya Grace kumaliza kujitetea. Mei 7 mwaka huu,Mahalu ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu kipya cha Bagamoyo cha jijini Dar es Salaam alimaliza kujitetea na siku hiyo ndiyo Rais Mkapa aliandika historia mpya nchini kwa upande wa marais ambapo alifika mahakamani hapo na kutoa ushahidi wake katika kesi hiyo. Julai 16 mwaka 2009, Jaji Sivangilwa Mwangesi ambaye ndiye alikuwa akiisilikiza kesi hiyo tangu ilipofunguliwa mwaka 2007 alitoa uamuzi wake ambapo aliwaona washitakiwa hao wana kesi ya kujibu. Machi 25 mwaka jana. Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Agosti 10 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.