Header Ads

KAKOBE AKWAA KISIKI MAHAKAMANI

Na Happiness Katabazi HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali pingamizi lililowekwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBC) Zakaria Kakobe dhidi ya wachungaji wa tatu wa kanisa hilo waliomfungulia kesi ya ubadhirifu wa fedha za kanisa hilo. Kesi hiyo namba 79/2011 ilifunguliwa Mei 26 mwaka 2011 na wachungaji watatu wa kanisa hilo, Mchungaji Deuzidelius Patrick, Angelo Mutasingwa na Benedict Kaduma. Wachungaji hao wanamtuhumu Askofu Kakobe kuwa amekuwa akifanya ubadhirifu wa fedha wa kanisa hilo Sh.bilioni 14 14 na anakiuka matakwa ya Katiba ya kanisa hilo. Kakobe kupitia kwa wakili wake Miriamu Majamba aliwawekea pingamizi la awali walalamikaji hao akidai kuwa hawana haki ya kisheria kumfungulia kesi hiyo Kakobe kwasababu si wachungaji wa kanisa hilo kwasababu Bodi ya Wadhamini wa Kanisa hilo ilishawafunguza uchungaji tangu mwaka 2010. Hata hivyo mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili , Kakobe kupitia kwa wakili wake, Majamba na walalamikaji kupitia kwa wakili wao Barnaba Luguwa zilizowasilisha kwa njia ya maandishi, ilitupilia mbali pingamizi la Kakobe na kulikubali ombi la walalamikaji . Katika uamuzi wake dhidi ya pingamizi hilo la awali, alioutoa Julai 16 na Jaji Agustine Shangwa alisema kuwa hati ya madai ya walalamikaji haioneshi sababu za madai na kwamba hawana haki ya kisheria kumfungulia mashtaka Askofu Kakobe . Jaji Shangwa alisema kuwa anakubaliana na wakili wa walalamikaji, Luguwa, kuwa hati ya madai ya walalamikaji hao inabainisha cause of action kwa maana ambayo kinadharia ina madai ambayo walalamikaji watapaswa kuyathibitisha. Aliyataja baadhi ya mambo ambayo walalamikaji hao watapaswa kuyathibitisha na kwamba kama yakithibitika Kakobe atawajiba kwayo kuwa ni pamoja na mabilioni ya fedha za kanisa hilo ambayo wanamtuhumu Kakobe kuyatafuta. Mengine ni mahubiri ya uwongo kwa waumini wa kanisa hilo kuwa kwa kufunga pamoja naye watakingwa dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi au kwamba wanaweza hata kuponywa kwa jina la Yesu anayemwabudu. Katika hilo Jaji Shangwa alisema kuwa walalamikaji watapaswa kuthibitisha kwamba mahubiri hayo ya uwongo ni makosa wanapaswa kulipwa fidia au kuadhibiwa. Madai mengine ni kuwa Askofu Kakobe amekuwa akiwafungisha ndoa waumini wake bila kuwapa vyeti vya ndoa na kwamba kwa kufanya hivyo ni kosa ambalo watapaswa kulipwa fidia au mlalamikiwa kuadhibiwa. BAADA YA KUSOMA UAMUZI Baada ya kutoa uamuzi huo Jaji Shangwa alipanga shauri hilo kuendelea Agosti 6, 2012, kwa ajili ya hatua ya usuluhishi huku akiwataka walalamikaji katika kesi hiyo kuwatafuta maaskofu wengine kutoka madhebu tofauti tofauti ili kutoa ushauri wa masuala ya kidini na kiimani ambayo mimi siyajui . Hata hivyo alisema hiyo ni hiyari yao wakiona ni vema kufanya usuluhishi na kuongeza kuwa kama hatakuwa tayari naye atalipeleka jalada hilo kwa Jaji Mfawidhi ili wapangiwe jaji wa kuanza kuisikiliza rasmi kesi yao. Jaji Shangwa alisema kuwa kesi hiyo ni kubwa na kwamba ndio maana alishauri mapema wahusika katika kesi hiyo wapatane kwanza wenyewe kwa kuwa ni hatari kwa upande ambao utashindwa. Mkithibitisha kuwa hatoi vyeti wakati anapofungisha ndoa hili litakuwa ni kosa kubwa kisheria na uthibitisho wa kwanza utoke kwenu wenyewe.”, alisem Jaji Shangwa. Katika hati ya madai yao, walalamikaji hao wanamtuhumu Kakobe kuwa amekuwa akikusanya pesa nyingi kutoka kwa waumini wake kwa madai ya kufanyia shughuli na miradi mbalimbali ya kanisa na kuzitumia kinyume cha malengo. Mbali na kuzitumia fedha hizo isivyo kama vile kugharimia kampeni za kisiasa kinyume cha katiba ya kanisa hilo, pia wanadai kuwa Kakobe amekuwa hatoi taarifa ya mapato ya pesa anazozikusanya wala matumizi yake. Kuhusu ukiukwaji wa Katiba ya kanisa hilo, walalamikaji hao wanadai kuwa katiba inataka kuitishwa kwa mkutano mkuu kila baada ya miaka mitano ambao ndio chombo cha juu cha maamuzi lakini Kakobe hajawahi kuitisha mkutano huo tangu mwaka 1989. Pia wanadai kuwa katiba hiyo inaelekeza kuwa kanisa liwe na Katibu Mkuu na Mweka Hazina ambao ndio watakaolinda mali za kanisa lakini Kakobe ndio amekuwa akifanya maamuzi na shughuli zote yeye mwenyewe. Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Julai 19 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.