Header Ads

KASHFA YA NORTH MARA,VIONGOZI WAWAJIBIKE

Na Happiness Katabazi

HIVI karibuni wananchi waishio katika Wilaya ya Tarime wameulalamikia mgodi wa dhahabu wa North Mara, kwamba unatiririsha maji ya kemikali ambayo wamedai maji hayo yamedhuru afya za baadhi yao wanaoishi maeneo jirani na mgodi huo.


Kilio hicho cha wakazi hao kimeendelea kusambaa karibu pande zote za nchi, kwani baadhi ya viongozi wanaharakati na wasomi wamejitokeza kuishinikiza serikali kuingilia kati na kuyapatia ufumbuzi wa haraka madai ya wakazi hao.

Si hao pekee, bali hata Watanzania wazalendo waliokerwa na unyama huo wameendelea kulalamikia hali hiyo kwa nguvu zote na kuitaka seriakali kuingilia kati kunusuru janga hilo.

Binafsi nasema yanayofanywa na North Mara dhidi ya wananchi wenzetu wa Tarime, ni matokeo ya sera mbovu ya madini kwasababu mgodi hauna tofauti na migodi mingine hapa nchini.

Kwa hiyo, Watanzania wenzangu wasiitazame North Mara kama kisiwa, yale yanayotokea katika mgodi huo yapo katika migodi mingine nchini. Utaratibu wa kusafisha dhahabu unaofanywa na mgodi huo ni utaratibu unaofanywa pia na migodi mingine.

Kwa hiyo, tujiulize tuna sera ya uchimbaji wa madini inayowalinda wananchi wa taifa hili kutokana na athari za mifumo ya usafishaji wa madini? Je, tunasheria inayowalinmda wananchi dhidi ya utaratibu wa usafishaji wa madini isiyokidhi viwango vya dunia vya usalama wa afya za raia?

Tunachokiona North Mara ni kwamba wawekezaji wameamua kukiuka viwango vya dunia vya usalama wa afya za wananchi, ili kukwepa gharama za teknolojia za kisasa.

Matokeo yake wananchi wenzetu wanakunywa maji, wanaoga na mifugo pia mifugo yao inatumia maji hayo yenye kemikali yenye madhara kwa binadamu na hayo yote yanafanyika chini ya ulinzi wa polisi wa nchi hii, serikali ya nchi hii na sheria hizo zinawalinda wawekezaji.

Kumbe sheria za madini si tu zinawaruhusu wawekezaji kuchukua madini yetu kwa wingi sisi tubaki mikono mitupu, ila pia zinawaruhusu kutumia teknolojia duni inayoumiza au kujeruhi au kuathiri vibaya afya za binadamu na mifugo na viumbe hai vilivyopo.

Kashfa ya North Mara ni kubwa ambayo mapana yake yangemlazimisha Waziri wa Nishati na Madini ajiuzulu. Kwa kuwa awali serikali ilipinga kuwa hakuna athari zozote kwa binadamu, na kwamba hakuna yeyote wala mifugo iliyoathirika na maji hayo yanayotiririshwa na mgodi huo.

Na huo ndiyo umekuwa msimamo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake. Hii ina maana kwamba CCM na seriakali yake katika Mkoa wa Mara imetupiwa mfupa ilikuficha ukweli.

Na kwa sababu wamekuwa wakificha ukweli huo ndiyo maana hata Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Balozi Khamis Kagasheki, alivyotumwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwenda mgodini hapo serikali Mkoa wa Mara ilimgeuza mwanaserere waziri huyo na kumficha ukweli.

Sasa tujiulize hao walioficha ukweli walikuwa na malengo gani? Je, ni watetezi wa wananchi au watetezi wa kampuni hayo ya migodi? Kwa nini wananchi walalamike kuathirika? Kiongozi akatae kama si rushwa ni nini?

Kwa hiyo watu wa Mara waendelee kusimama kidete kutetea haki zao kwa kuanzisha kesi kubwa ya madai ya fidia ya Mazingira ,mifugo,,mazao na afya zao.
Pili, watu wa Mara wawafichue viongozi ambao wamelishwa rushwa na makampuni ya migodi.

Mungu ibariki Tanzania,Mungu ibariki Afrika

0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Julai 23, 2009

No comments:

Powered by Blogger.