Header Ads

KESI YA MRAMBA YAPIGWA KALENDA

Na Happiness Katabazi

KESI ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake, jana ilishindwa kuendelea kutokana na mahakimu wanaosikiliza kesi hiyo kutokuwapo mahakamani.


Hakimu Mkazi, Saul Kinemela, ambaye ni mjumbe wa jopo la mahakimu wakazi wanaosikiliza kesi hiyo, alisema jana kuwa kesi hiyo haitaweza kuendelea kutokana na Mwenyekiti wa jopo hilo, John Utamwa, kuwa safarini katika ziara ya Jaji Mkuu, Agustino Ramadhan na mjumbe mwingine wa jopo hilo, Fatma Masengi, kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.

Kinemela alisema kutokana na Masengi kuteuliwa kuwa jaji, nafasi yake itajazwa na Hakimu Mkazi, Sam Rumanyika.

Alisema kwa sababu hizo, anaahirisha kesi hiyo hadi Julai 31 itakapokuja kwa ajili ya washitakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Aidha, Wakili wa Mramba, Hurbet Nyange na Peter Swai, waliomba mahakama impatie ruhusa mteja wao, ili aweze kwenda jimboni kwake, jambo ambalo lilikubaliwa na kuruhusiwa kutoka nje ya Dar es Salaam kuanzia Julai 22-30 mwaka huu.

Mbali na Mramba, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja, ambao wote kwa pamoja wanakabiliwa na shitaka hilo la matumizi mabaya ya ofisi za umma ambapo walidharau ushauri wa Mamlaka ya Mapato (TRA) uliokuwa ukiwataka wasitoe msamahama wa kodi kwa Kampuni ya M/S Alex Stewart.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Julai 21,2009

No comments:

Powered by Blogger.