Header Ads

'MAWAKILI KESI YA EPA WANAKIUKA SHERIA '

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa mashitaka katika kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) inayomkabili Farijala Hussein na Shaban Maranda, umeelezwa kushangazwa na upande wa utetezi kung’ang’ania kukata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, kuwaona washitakiwa hao wana kesi ya kujibu.


Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface aliyekuwa anasaidiana na Wakili Mwandamizi, Fredrick Manyanda, alidai kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria.

“Msomi Magafu (Wakili wa utetezi) anafahamu sheria inakataza maamuzi yoyote kukatiwa rufaa hadi mahakama inapotoa hukumu, hivyo kinachofanywa na upande wa utetezi ni kukiuka sheria kwa makusudi na lengo hasa wanataka kuchelewesha kesi,” alidai Boniface.

Hata hivyo, madai hayo yalipingwa na wakili wa utetezi, Majura Magafu kwa maelezo kuwa msimamo wa kukata rufaa unabaki pale pale na kwamba nakala ya rufaa hiyo ipo kwenye maandalizi ya mwisho kwa ajili ya kuiwasilisha Mahakama Kuu.

Hakimu Mkazi, Cypriana William, alisema ombi la Magafu litaendelea kubaki kama lilivyo kuahirisha kesi hadi Agosti 28 mwaka huu, itakapotajwa.

Wakati huohuo, mshitakiwa wa pili katika kesi ya EPA, Amit Nandi, amewasilisha maombi mahakamani hapo akiiomba mahakama impatie hati yake ya kusafiria, ili aweze kumsindikiza mkewe nchini India kwa matibabu.

Ombi hilo liliwasilishwa katika kesi tatu tofauti tofauti zinazomkabili mshitakiwa huyo na wenzake na wakili wake, Gabriel Mnyere, ambapo jana kesi hiyo ilikuja kwa kutajwa.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali, Michael Lwena na Arafa Msafiri, waliiambia mahakama kuwa mshitakiwa huyo ni raia wa kigeni, hivyo akipewa ruhusa hiyo anaweza kutoroka na endapo atatoroka serikali itakuwa na wakati mgumu wa kumsaka. Uamuzi wa ombi hilo utatolewa Agosti 3.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Julai 30 ,2009

No comments:

Powered by Blogger.