Header Ads

WAZUNGU WEZI ATM WAMKATAA MKALIMANI

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa mashitaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ulishindwa kuwasomea mashitaka raia wawili wa Bulgaria ambao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kwa tuhuma za wizi wa sh milioni 70 mali ya Benki ya Barclays.


Mwendesha Mashitaka Mfawidhi, Edger Luoga, mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema, aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Nedkolazarous’ Standaev (35) na Stela Peteva Nedelcheva (23).

Luoga alipokuwa akijiandaa kuanza kuwasomea mashitaka huku mkalimani aliyetafutwa na serikali kwa ajili ya kutafsiri lugha ya Kiingereza kwenda lugha ya Bulgaria, ndipo mshitakiwa wa pili, Nedelcheva, alinyosha mkono na kuiambia mahakama hiyo kwamba hawana imani na mkalimani huyo (jina tunalihifadhi kwa sababu za kiusalama).

Nedelcheva alidai kuwa wamefikia uamuzi wa kumkataa mkalimani huyo kwa sababu haifahamu vyema lugha ya Bulgaria na kwamba hata walipokamatwa hivi karibuni, mkalimani huyo aliletwa polisi na wakati wakihojiwa, alikuwa akitafsiri lugha yao isivyostahili.

“Mheshimiwa hakimu, mkalimani huyu hatumtaki, atafutwe mkalimani mwingine kwa sababu hatuna imani naye kwa kuwa hata tulivyokamatwa na kuchukuliwa maelezo na polisi, alikuwa akitafsiri tofauti na maelezo yetu tuliyokuwa tukiyatoa kwa lugha yetu ya Bulgaria,” alidai Nedelcheva ambaye alijifunga kanga aliyopewa na wasamaria wema baada ya kutinga mahakamani hapo akiwa na kaptula fupi iliyokuwa ikionyesha maungo yake.
Aidha, Hakimu Lema alisema amesikia ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Julai 27, na kuamuru washitakiwa hao wakahifadhiwe kwenye mahabusu ya polisi.

Mapema wiki hii, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, aliwaambia waandishi wa habari kwamba wanawashikilia watuhumiwa wakiwa na kadi maalum zilizowawezesha kuiba kwenye ATM ya benki ya Barclays.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Julai 24,2009

No comments:

Powered by Blogger.